Muda umewadia sasa kwa chama tawala kuvirudisha viwanja vyote vya michezo ilivyojimilikisha, ili viwe chini ya serikali. Ni ukweli usiopingika ya kwamba utaratibu uliotumika katika kuvimiliki haukuwa mzuri hata kidogo, na unaacha maswali mengi sana juu uhalali wa CCM wa kuvimiliki kama mali binafsi, huku kimsingi ukweli ni kuwa hivi ni mali ya umma.
Viwanja hivi, mathalani Kirumba - Mwanza, Sokoine- Mbeya, Samora - Iringa, Mkwakwani - Tanga, Sheikh Amri Abeid - Arusha, Ali Hassan Mwinyi - Tabora, n.k. vyote vilijengwa kupitia nguvu za wananchi wenyewe, katika maeneo ya serikali yaliyotengwa mahususi kwa ajili hiyo, lakini tu katika kipindi cha utawala wa chama kimoja cha kidola. Kwa hiyo hakuna hoja yoyote ile ya msingi ya CCM ya kuzidi kung'ang'ania kuvimiliki kama mali binafsi katika mazingira ya sasa ya uwepo wa vyama vingi.
Ukiachilia mbali suala la uhalali wa kuvimiliki, lakini jambo lingine ni dhahiri pia kuwa CCM imeshindwa kuviendeleza ili vikidhi mahitaji ya sasa ya maendeleo ya vijana kwa michezo mbalimbali. Viwanja vyote vya kisasa huwa na miundombinu bora ambayo huchochea maendeleo ya michezo yote kwa ujumla, na pia ndiyo kichocheo kingine cha kuzalisha ajira nyingi kwa vijana katika soko la ndani na hata lile la kimataifa.
Kwa sasa hali ya viwanja hivi ni mbaya na hairidhishi hata kidogo kutokana na ufinyu wa bajeti wa kutenga fedha za kuviendeleza, ama pia mapato kiduchu yanayopatikana ili kuweza kuviboresha ili viwe na muonekano wa kisasa sambamba na miundombinu bora na ya kisasa. Jambo ambalo litakuwa ni rahisi kulifanyika endapo vitakuwa chini ya manispaa za miji ama majiji.
Uongozi wa CCM Taifa uwiwe kufanya maamuzi yenye tija kwa Taifa letu, wapate busara ya kuona kuna kila aina ya haja, na pia ni takwa la wakati la kuvirudisha viwanja hivi viwe ni mali ya wananchi wote chini serikalini. Ni vyema njia za kistaarabu zikatumika kwa sasa kuvirudisha kwa hiyari kuliko kusubiri aibu ya kuja kunyang'anywa kwa nguvu siku za mbeleni, ambazo kwa akili ya kawaida kabisa zinaonyesha kuwa wala hazipo mbali kutoka hivi sasa.
Ndiyo! Ajenda ya kuwa katiba mpya na tume huru ya uchaguzi ni maana sana, lakini vyama vya upinzani pia vinapaswa pia kupaza sauti zao juu ikiwa ajenda nyingine pia inayopaswa kupelekwa kwa wananchi kwa ajili ya maslahi mapana ya nchi yetu. Na mwisho ni vyema michakato ya kufungua shauri la kisheria ili kupata tafsiri, na hata kuhoji uhalali ma utaratibu uliotumika kwa CCM kujimilikisha baadhi ya mali zake ikiwemo hivi viwanja katika kipindi cha kuanzishwa kwa utawala wa vyama vingi.