Uhakiki wa shairi: Kuku zinduka akili

Dotto C. Rangimoto

JF-Expert Member
Nov 22, 2012
1,985
1,282
1472542601520.jpg



MHAKIKI: Dotto Rangimoto Chamchua.

REJEA TENA SHAIRI.

KUKU ZINDUKA AKILI.

Kuku kwa lako umbile, huwezi liona hili,
Hukuumbwa na machale, kuyaepuka makali,
Halali yetu tukule, Mola katupa kibali,
Kuku zinduka akili, mgeni hali tembele.

Kuku kucha niparule, uchunike wangu mwili,
Upige nyingi kelele, sitatoka kwenye reli
Waja kurudi ulale, hivyo natulia tuli,
Kuku zinduka akili, mgeni hali tembele.

Kuku wajitia kele, kutinga kila mahali,
Pale ulapo mchele, wajiona kwelikweli,
Kumbe ni mtego vile, mgeni ataka wali,
Kuku zinduka akili, mgeni hali tembele.

Kuku una uchechele, leo nakupa ukweli,
Mchana si wa milele, usiku yake badili,
Utanaswa kichewale, tayari kwa maakuli,
Kuku zinduka akili, mgeni hali tembele.

Kuku ninakupa shule, sema na zako akili,
Jifunze kuona mbele, uwate na ufedhuli,
Mtana hila zitele, kizani huwa jahili,
Kuku zinduka akili, mgeni hali tembele.

Kuku 'kisikia lele, ni ngoma sio zikili,
Waja waweke tungule, basmati pishi mbili,
Pembeni pana uzile, masala na filifili,
Kuku zinduka akili, mgeni hali tembele.

Kuku sikia kengele, zichunge zako shughuli,
Fahamu yajayo ndwele, ya sasa yakiwa nduli,
Jikage japo kwa chale, mambo yawe bulibuli,
Kuku zinduka akili, mgeni hali tembele.


MAANA YA SHAIRI KWA UJUMLA.

Mgeni ni nani??

Mgeni ni UCHAGUZI MKUU ambaye huja kwetu mara moja kila baada ya miaka mitano.

Mwenyeji ni nani?

Mpiga kura ambaye yeye SIKU ZOTE YUPO akifuga kuku na kutumia bidhaa zake.

Kuku ni nani?

Kuku ni vyama vyote vya siasa, serikali iliyo madarakani na wanasiasa wote.

Kuchinjwa maana yake nini??

Kushindwa kwa chama na mwanasiasa katika uchaguzi, baada ya kukosa kura za kutosha kutangazwa mshindi.

Kuepuka kuchinjwa maana yake nini?

Kushinda uchaguzi kwa chama na mwanasiasa. Hii ni baada ya chama au mgombea kupata kura za kutosha kutangazwa mshindi.

Makali maana yake nini?

Ni kisu chenye makali, na hapa nimemaanisha kiparata (kadi ya mpigia kura). Kama mtakumbuka tulikiita kichinjio.

Mchana maana yake nini?

Ni siku zote zile za bunge jipya hadi pale bunge hilo kutakapo vunjwa. Muda huu walio shinda na walioshindwa wanaendeleza maisha yao kisiasa huku wakijindaa na uchaguzi ujao.

Usiku maana yake nini??

Kipindi chote cha mchakato wa uchaguzi kuanzia ndani ya vyama hadi siku ya uchaguzi mkuu.

Banda maana yake nini?

Sanduku la kura, jimbo la uchaguzi, kata ya uchaguzi na hali ya nchi ikiwa katika uchaguzi.

Kuku kurudi kulala/bandani maana yake nini?

Ni kwa chama na wanasiasa kwenda kuomba kura kwa wapiga kura.

Kuku kula mchele maana yake nini?

Ni kitendo cha chama kuongoza nchi, manispaa, kata, Au mwanasiasa kutumikia wadhifa wake alio upata baada ya kushinda uchaguzi.

Kuku usiniparue maana yake nini?

Rejea huko juu, kuku mwanasiasa au chama,,

Kama kashinda uchaguzi anatakiwa kutimiza ahadi zake, kushindwa kwake ndio KUNIPARUA, yaani ananiumiza kwa kushindwa kutimiza matarajio yangu.



HIYO NDIO MAANA YA JUMLA YA SHAIRI HILO KWA KIFUPI.

Madhui

Dhamira

1. Umuhimu wa kupiga kura

2. Viongozi kuetekeleza ahadi na ilani zao,

3. Mamlaka ya kuongoza nchi yanatakiwa kuwekwa na kutolewa na wananchi wenyewe.

4. Wananchi wafuatilie utekelezaji wa ilani na ahadi za chama au mgombea aliyeshinda, asiishie kupiga kura tu.

5. Mamlaka haitolewi kwa vurugu na pia haiwekwi kwa vurugu. Kwanini USHIRIKI UKUTA uvunjwe miguu, wakati kuku atarudi bandani tu? Kwanini uende vuchakani kusaka kuku wakati jioni hana pa kwenda isipokuwa katika banda lako?

Falsafa.

Mimi kama mtunzi wa shairi hili naamini kuwa umma ndio una sauti ya mwisho juu ya matumizi na magawanyo wa rasimali za nchi kwa kupitia mamlaka yao ya kuchagua viongozi watakao fanya hayo kwa niaba yao.

Pindi viongozi hao wakifanya vizuri wanaweza kupewa tena nafasi na kama wakifanya vibaya wanaweza kufukuzwa kazi na yote haya yanafanyika chini ya mwavuli wa uchaguzi ulio huru, wa haki na wa kweli.

KUHUSU FANI.

Ni shairi la kimapokeo lilofuata kanuni za utunzi wa kimapokeo.

Lugha.

Lugha ya picha.

Nimechanganya lahaja zaidi ya moja, lakini kiunguja kimetia fora.

MWISHO.

Kama mshairi kujihakiki mwenyewe kwa kazi aloifanya ni mwiko, basi mimi nimevunja mwiko huo kwa kuhakiki kazi yangu.

Nimefanya hivyo baada ya kupokea kauli za vitisho(si kutoka serikalini) kuwa nimemtukana rais Magufuli kwa kumuita kuku, na baadhi ya makundi ya facebook na majukwaa mengine walifikia hatua ya kufuta shairi langu na makala yangu ambayo shairi hili nililiambatanisha katika makala hiyo.

Nimefanya hivi kwa kusudi la kujitoa shubuhani ama makosani ambako baadhi ya wapenzi wa mashairi yangu bila kuelewa walijaribu kunipeleka huko.

Dotto Rangimoto Chamchua(Njano5)
Call/whatspp 0622845394 Morogoro.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom