Miss Zomboko
JF-Expert Member
- May 18, 2014
- 4,501
- 9,280
Na Ezekiel Mtonyole, Dodoma.
Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) kinataraji kuanza kutoa Mitihani ya Kimataifa ya Ujuzi wa Lugha ya Kiswahili kwa lengo la kuhakikisha lugha ya kiswahili inakuwa zaidi
Hayo yamebainishwa jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk.Leonard Akwilapo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mitihani hiyo ambayo inatarajia kuanza kufanyika kuanzia mwaka 2020.
Amesema hiyo inalenga juhudi zinazofanywa katika kuikuza na kuieneza Lugha ya Kiswahili ulimwenguni kote kwa kuhakikisha kuwa ni miongoni mwa lugha 10 zenye wazungumzaji wengi duniani.
“Mtakumbuka kwamba Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alishafanya jitihada kubwa sana na za kuiendeleza na kuieneza Lugha ya Kiswahili pamoja na kusimamia ubora wake ndani na nje ya nchi halikadhalika na waliofuata" amesema Dkt Akwilapo.
Amesema mitihani hiyo itakuwa ikifanyika mara sita kwa mwaka ikiendana na kipindi cha masomo ya Kiswahili kwa kila ngazi na itafanyika kwa njia za kielektroniki katika vyuo na vituo mbalimbali vya Kiswahili duniani ambavyo tayari kuna makubaliano maalumu.
“CKD(UDSM), kinakuwa ni Chuo Kikuu cha kwanza duniani kutunga mitihani hii na kusimamia utahini na usahihishaji wake na kutoa Cheti cha Kimataifa kinachoonesha kiwango cha ujuzi wa mtahiniwa,”amesema.
Amebainisha kuwa Chuo hicho kimechukua na jukumu la kuanzisha mitihani ya Kimataifa ya Ujuzi wa Lugha ya Kiswahili sanifu na ili lugha ya kimataifa ipate nguvu zaidi hutungiwa mitihani ili wanaojifunza lugha hizo waweze kutathminiwa na kupata vyeti.
Amesema tayari kuna makubaliano baina ya walimu wa Kiswahili wa Chuo kikuu Dar es saalam na walimu wanaofundisha Kiswahili katika vyuo vya nje kuhusiana na mitihani hiyo ambayo itaanza kutolewa mwakani.
“Chuo kikuu Cha Dar es saalam kimejiandaa kuhakikisha kuwa mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano iko madhubuti kuwezesha mitihani hii kufanyika kwa ufanisi na kwa viwango vya kimataifa kwani kuna wahitaji ambao watafanyia mitihani hii wakiwa katika nchi zao, sio lzima wasafiri na kuja kufanyia mitihani yao hao Tanzania,”alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili, Prof.Aldin Kai Mutembei, amesema mitihani hiyo itakuwa ikiitwa kwa jina la MKUKi.
“Kuna wanafunzi wengi wanasoma Kiswahili huko nje na walitamani kuja kwenye nchi zinazozungumza Kiswahili lakini wangependa wawe na utambulisho kuwa wanajua Kiswahili hawa ndio tunaowalenga,”amesema.
Amebainisha kuwa Chuo kikuu Cha Dar es saalam, kitahakikisha kinakuwa wawakilishi wazuri wa serikali katika kukuza na kuendeleza lugha ya kiswahili.