Uchambuzi: Kuvuja kwa mazungumzo ya siri ya kamanda wa Ujerumani, Russia yaonyesha kuwa ipo juu katika medani ya ujasusi duniani, NATO washangaa

Richard

JF-Expert Member
Oct 23, 2006
14,939
20,400
Balozi wa Ujerumani alieko nchini Uingereza bwana Miguel Berger aliitwa katika ofisi za wizara ya mambo ya nje ya Uingereza ili atoe maelezo kuhusu kuvuja kwa rekodi ya mazungumzo ambayo kamanda wa jeshi la anga la Ujerumani alisikika akikiri kuwepo kwa vikosi vya jeshi la Uingereza nchini Ukraine.

Luteni Jenerali Ingo Gerhartz ambae ni mkuu wa jeshi la anga la Ujerumani, aliingia ofisini kwake na na kama kawaida alikuwa na mazungumzo ya siri kati yake na viongozi wengine wa kijeshi kupitia simu ya video yaani "teleconferencing". Lakini mwanajeshi huyo wa cheo cha ngazi za juu hakuwa makini na "app" ambayo ingefaa kwa matumizi ya simu hiyo ya video na akaamua kutumia Webex ambayo ni "app" ya majadiliano ilobuniwa na kampuni ya kimarekani ya Cisco na inofanya kazi sawa na App zingine kama WhatsApp, Zoom na Telegram.

Hivyo luteni jenerali huyo akaanza mazungumzo na viongozi wenzie lakini wakiwa kwenye njia ya simu ya video ambayo haikufungwa kiusalama yaani "insecure line" na pia hakukuwa na protokali ya kuhakikisha mazungumzo hayavuji kwenda sehemu ingine yaani "encryption". Mazungumzo hayo yalichukua dakika 38 na yalihusu namna ambavyo Ujerumani ingeweza kusaidia kupeleka Ukraine makombora aina ya Taurus. Pia walizungumzia kuhusu Ufaransa na Uingereza kupeleka makombora aina ingine yaani "cruise missiles".

Hapohapo wakazungumzia kuhusu makombora hayo ya Taurus kutumiwa na Ukraine kudungua daraja la Kerch ambalo launganisha Russia na rasi ya Crimea. KIongozi wa ujerumani Scholz tayari hapo awali alikataa kutuma makombora hayo ya Taurus kutokana na uwezo wake wa hali ya juu na teknolojia ambayo yatumia hivyo kungekuwa na ulazima wa kutuma majeshi yake ili yaweze kuyatumia kutokana na uwezo mdogo wa kiufundi wa majeshi ya Ujerumani.

Lakini wakati hayo yote yakifanyika majasusi wa Russia nao hawakuwa mbali na eneo la tukio kiasi cha kuyarekodi mazungumzo hayo ambayo baadae waliamua kuyatoa kupitia katika mtandao wao wanoupenda wa telegram. Ni katika kampeni inoendelea ya vita vya habari na propaganda yaani "information war and propaganda". Russia imeonekana kuwa juu katika vita hiyo hadi sasa kwa kuonyesha uwezo wake wa kuyadukua mazungumzo hayo pamoja na operesheni zake kadhaa ambazo zimekuwa zikisemwa kwamba zafanywa na majasusi wake.

Jambo hilo la kuvuja kwa siri hizo kumezua taharuki barani Ulaya huku ujerumani ikishutumiwa kwa kutokuwa makini ya utunzaji wa siri za kijeshi na uimara wa usalama wa vyombo vyake vya mawasiliano, kiasi cha kuambiwa nchi hiyo imeleta dhihaka na mafedheheko.

Katika kuonyesha jinsi Russia ilivyojizatiti katika tasnia hii ya ujasusi khasa katika majukwaa ya kimataifa na katika vita yake inoendelea nchini Ukraine, Russia imefanya mambo kadhaa katika ardhi za nchi za barani Ulaya jambo ambalo hadi sasa limevifanya vyombo kadhaa vya kijasusi wa ndani katika nchi hizo kuwa macho masaa yote.

Huko nchini Uingereza mwezi Februari mwaka huu watu wapatao sita na raia wa Bulgaria waliwekwa chini ya ulinzi kwa tuhuma za kuwa ni majasusi wa Russia. Wiki chache kabla ya hapo aliekuwa rubani wa ndege za kijeshi wa Russia Makzim Kusminov alikutwa amekufa kwa kupigwa risasi nyingi mwilini nchini Hispani katika kitongoji cha Benidorm.

Kusmikov alikuwa ametorokea nchini Hispania baada ya kulipwa fedha na Ukraine kwa kitendo chake cha kuisalimisha ndege ya kivita ya Russia.

Na katika wiki hizohizo mjini Paris nchini Ufaransa kuligunduliwa tovuti zipatazo 193 ambazo zimetayarishwa kwa ajili ya kuharibu shughuli za uchaguzi na katika bunge la Ulaya mbunge wa kutoka Latvia anachunguzwa kwa tuhuma za kuwa jasusi wa Russia.

Lakini kubwa ya haya yote ni kuvuja kwa mazungumzo ya maofisa hawa waandamizi wa jesho la anga la Ujerumani ambako ndiko kulikopelekea mie kujadili hili kwa kuchambua khasa nini kiko nyuma ya uwezo huu mkubwa wa Russia katika medani za ujasusi.

Kuvuja huko kwa mazungumzo hayo kulikuja baada ya raisi Vladmir Putin kutoa hotuba ya taifa siku ya jumanne tarehe 27 mwezi ulopita ambapo alisema nchi za NATO zimekuwa zikijiandaa kupeleka majeshi yake nchini Ukraine kupigana na Russia na akatoa onyo kwamba vita hiyo itaingia hatua ingine ya hata kutumia silaha kali za kinyuklia ambazo Russia pia inazo.

Lakini tukirudi nyuma kabisa ambapo Russia ilianza kampeni yake ya operesheni maalum ya kijeshi nchini Ukraine mwezi februari mwaka 2022 kwa kupeleka vifaru mjini Kyiv, nchi nyingi za Ulaya khasa NATO zilianza kuchukua hatua kadhaa zikiwemo kuweka vikwazo vya kiuchumi, kufukuza maofisa wa kibalozi wa Russia ambao walituhumiwa kuwa ni majasusi na pia mawakala pamoja na watu wasokuwa na vibali vya kuishi katika nchi za Ulaya walikusanywa na kurudishwa kwao Russia (deportation).

Baada ya zoezi hilo majeshi la Russia yakaanza kupata shida kusogea zaidi nchini Ukraine na hapo ndipo raisi Putin alipokusanya makamanda wake na majasusi waandamizi kutambua tatizo lipo wapi.

Ndani ya wiki chache maofisa waandamizi wa kijasusi wa idara ya kijasusi ya FSB na makamanda wa jeshi wakawekwa chini ya ulinzi kwa kushindwa kuweka sawa mikakati ya kushinda vita na kukosea mahesabu ya uwezo wa Ukraine kukabiliana na Russia. Hilo la Ukraine kuwa na uwezo wa kukabiliana na Russia lilitokana na maandalizi ya kutosha pamoja na taarifa za kijasusi za mipango ya kijeshi ya Russia kuvuja na kuwa wazi kwa nchi za NATO na Ukraine.

Russia baada ya kujipanga upya wakaja na matumizi ya njia zingine mpya yaani "modus operandi" ambayo ni pamoja na kutafuta majasusi ambao ni raia wa nchi zingine au "proxy intelligence actors". Hapo mwanzo ilikuwa rahisi kwa majasusi wa nchi za Ulaya na marekani kukabiliana na majasusi ambao ni raia wa Russia, lakini zama hizi zilobadilika jambo hilo limekuwa ni kinyume na sasa wapambana na majasusi tofauti kutoka nchi tofauti ambao ni mawakala wa SVR au GRU idara za usalama wa nje za Russia.

Pia shughuli hizo za kijasusi za Russia zatumia majasusi wa kukodi kutoka nyanja kama za siasa, biashara na makundi ya wahalifu ya kupangwa yaani "organised crime" khasa yake ya kutoka katika nchi kama Albania ambayo yasifika barani Ulaya kwa kuwa na wahalifu wa kiwango cha juu. Kwa mfano wahalifu hawa wa Albania ambao pia hujihusisha na uporaji mali kutoka katika majumba ya matajiri barani Ulaya, walitumika kumtorosha raia wa Russia Artem Uss ambae alikamatwa nchini Italy kwa tuhuma za kuuza silaha za kiteknolojia za Marekani kwa Russia na ambae ana uhusiano wa karibu na Kremlin.

Jambo la kuangalia hapa ni kwamba majasusi hawa wa kukodi mara nyingi huwa hawafahamu kwamba wafanya kazi za kijasusi za Russia na ni pale linapotokea jambo ndipo huja kutambua.Mfano wa hili ni mauaji ya kijana rubani Kusmikov ambae baada ya kufika Hispania na kupata sehemu ya kulala alianza kuwa na urafiki na watu kadhaa pale Benidorm. Lakini Benidorm ni sehemu yenye raia kutoka nchi mbalimbali barani Ulaya na wengi wakiwa wahalifu ambao wamekimbia nchi zao. Hivyo bila kugundua Kusmikov akaanza kuwasiliana na rafiki yake wa kike ambae alimwacha Russia.

Bila kugundua chochote yule msichana kule Moscow akawa afuatiliwa hali kadhalika na Kusmikov ambae alilipwa fedha nzuri na Ukraine za kuanzia maisha Benidorm nae akawa chini ya uangalizi ambapo mwisho wa maisha yake ulihitimishwa na risasi kadhaa alopigwa kifuani na sehemu zingine za mwili na wauaji wasifahamike hadi leo.

Njia ingine ambayo Russia yatumia kutimiza malengo yake ya kijasusi ni kuwatumia kwa kuwashinikiza raia wake ambao wengi walikimbia baada ya vita na Ukraine kuanza. Njia hii imekuwa ikitumiwa na wakuu wa vyombo vya usalama vya Russia kuhakikisha ndugu za wale walokimbilia nje wanakuwa wanafahamika na kujenga mawasiliano nao ili kuwashinikiza raia walio nje kusaidia kampeni za kijasusi kwa Russia.

Majasusi hawa wa kuazima wamekuwa wakisaidia kazi za kijasusi kama vile kuiba taarifa za siri za kibiashara, kuanzisha biashara ambazo aitasaidia kuepuka vikwazo vya kiuchumi ilivyowekewa Russia na kupenyeza program kadhaa za kompyuta ili kupata taarifa kwa kutumia kijiti cha USB tu.

Kwa mfano mwaka 2021 nchini Norway majasusi wa ndani ya nchi hiyo walimkamata msomi kutoka Brazil bwana Jose Assis Giammaria ambae alipata kazi ya kufundisha katika chuo kikuu cha Norway lakini akiwa ni jasusi (undercover agent) wa Russia na hadi sasa asubiri kesi yake mahakamani.

Mfano mwingine ni wa Sergey Cherkasov ambae mwaka huu amefikishwa mahakamani nchini Marekani kwa tuhuma za kuwa jasusi na kuiba siri za kidiplomasia za sera za nje za Marekani. Cherkasov amekuwa akitumia uraia wa Brazil na kupata jina la Victor Muller Ferreira tangia mwaka 2012. Cherkasov alihamia nchini Marekani mwaka 2018 na kujiunga na chuo kikuu cha Columbia kusoma.

Ntamuelezea zaidi Cherkasov katika mada ingine ijayo juu ya namna majasusi wa kigeni wanovoajiriwa.

Lakini taasisi ya Royal United Service Institute (RUSI) inoshughulika na tafiti, imesema kwa kuwa majasusi hawa wa kukodi wamekuwa wakati mwingine ni shida kuwadhibiti, idara za GRU imeripotiwa kuanza kuajiri majasusi wapya kabisa ambao hawana rekodi yoyote ya kijeshi ambao wataweza kuingia katika nchi lengwa ili kupata taarifa za kijasusi huku wakiwa wanaripoti moja kwa moja kwa mwakilishi wa GRU alieko karibu katika nchi jirani.

Matumizi ya vituo maalum katika ofisi za kibalozi. Mkataba wa Vienna bado umeruhusu maofisa wa kibalozi wa Russia kutumia mwanvuli huo au "diplomatic cover" kufanya shughuli zao katika nchi za Ausrtia na Switzerland kwenye miji ya Vienna na Geneva na pia katika nchi zilo nje ya eneo la schengen la Ulaya kama katika nchi za Uturuki na UAE ambazo zina uhusianowa karibu na Russia hivyo kuweza kutoa nafasi kwa Russia kufanya shughuli zake za kijasusi barani Ulaya kutokea katika nchi hizo.

Nchi ya Serbia ambayo bado ina uhusiano wa karibu na Moscow nayo imekuwa ni mwenyeji wa majasusi karibuwote walofurumushwa kutoka katika nchi mbalimbali za Ulaya nasasa wameweka kituo chao mjini Belgrade.

Vita ya Ukraine imesababisha nchi nyingi za Ulaya khasa NATO kuiwekea vikwazo mbalimbali Russia na njia kadha wa kadha za kijasusi kukabiliana na majasusi wa Russia. Lakini kwa nyakati kadhaa Russia kwa kutumia majasusi wake imeweza kufanikiwa kuwashinda majasusi wa nchi za Ulaya na Marekani. Mwaka 2021 majasusi wa Russia waliweza kufanya mashambulizi kwenye mitandao ya internet yaani "cyber attack" Pentagon ambapo mitambo umeme wa upepo (Solar Wind) iliingiliwa na kushindwa kufanya kazi.

Na mfano wa juzi kwa kuingilia mawasiliano ya maofisa waandamizi wa jeshi wa Ujerumani na kuyavujisha pia kumeonyesha uwezo wa hali ya juu wa majasusi wa Russia katika kufanya operesheni kabambe iitwayo kwa lugha ya kijasusi "stupendoulsy cool".

Katika uchambuzi ujao ntaeleza namna jasusi Sergey Cherkasov alivyoweza kukamatwa kwa msaada wa shirika la ujasusi la Uholanzi ambalo ndilo kwa sasa linoaminika kwa umahiri wa kazi zake barani Ulaya.
 
Wewe unasema kuwa mfuko haikuwa secured alafu bado unasema kuwa Russia wako vizuri kwenye nini!! Kwahiyo uwezi kujiuliza kwanini hawakuifanyia security.
 
Kama namuona jinsi huyo Balozi alivyokuwa anaenda kujielezea baada ya mazungumzo kuvuja😆
NAPEZZ.png
 
Kama namuona jinsi huyo Balozi alivyokuwa anaenda kujielezea baada ya mazungumzo kuvuja😆View attachment 2926766
Mkuu, hapa twajadili watu kutegwa mazungumzo yao kitaalam. Yaani majasusi nao waliweza kuingia kwenye mazungumzo wakijifanya nao ni sehemu ya wahudhuriaji bila kugundulika.

Hiyo unosema ni ile kampuni ya simu kuambiwa itoe recording ya mazungumzo ya wateja wake.

Kwahiyo mazee wao huingia Voda au air tel na kudai recordings.
 
Ukweli katika SMO hii ndio nimeweza kupata uhakika kua Urusi Iko juu sana kiintelijensia.

Ujasusi kiuchumi.
Inaonekana majasusi wa Urusi walishasoma mchezo mapema kua watawekewa vikwazo ndipo wakaweka mipango mapema kabisa ya kuvishinda.
Leo hii Rubo imeimarika zaidi kuliko hat kabla ya SMO.
Gesi inauzwa na bidhaa za kilimo Urusi zimeongezeka

Kidiplomasia
Majasusi walishasoma mapema kabisa mchezo napo wakajipanga,kidiplomasia ni n hi za west TU ndio zimejaribu kuitenga urusi.nchi nyingine zote za duniani bado ziko vizuri kabisa na Urusi na Tena mahusiani yameongezwkanmara dufu.
Sasa hivi nchi nyingi sana za Afrika ,Arab na Asia zimeongeza uhusiano.hebu fikiria hata Saud Arabia Leo anammkataa Marakani.

Vifaa vya kijasusi.
Ndio huo udukuzi unaoungelewa .
Huko angani Kuna satellite nyingi sana za kilaia na za kijeshi zote kwa umoja wao zinapambana na satellite za Urusi peke yake.
Ingekua satellite za west zimezishinda za Urusi nadhani Leo hii vita ingekuabimeisha kwa Urusi kushindwa vibaya.

Ulinzi wa mipaka.
Amini usiamnini mipaka ya Urusi Urusi upande wa Magharibi mwa Urusi Iko kwenye mashinikizoakibwa sana,NATO wanatamani na kujaribu kuingiza majasusi wao na waharibifu kijeshi saboters lakini wanashindwa.


Ndani ya uwanja wa mapambano.
Huko ndo usiseme kabisa.majasusi wa kijeshi wa pande zote mbili yaani wa ukraine wakisaidiwa na majasusi wa NATO wanapambana na majasusi wa Urusi peke yake.
Lakini kama unavyoona Warusi Wanakamata majimbo Kila siku.
Walichofanikia NATO ni kupunguza spidi ya Urusi tu.
Hapa ni kama mlivyosikia hivi majuzinkua Majasusi wa Ukraine wamekua wakifundishwa na CIA toka mwaka 2014 na Kuna vituo ya CIA visivyopungua 11 nchi Zima na vingije viko underground.


Usalama wa ndani.
Nadhani lengo mojawapo la vikwazo,mbali na kuuangusha uchumi wa Urusi lakini pia ni kuleta machafuko nchini humo na Kupelekea Putin kupinduliwa.
Lakini majasusi wameweza kuituliza Hali ya usalama wa Urusi na maisha ni Salama salmon kabisa.

Mambo ni mengi ila ukweli kama Urusi isingekua na majasusi imara ni zamani sana Ingekua imeishaanguka.
 
Mjadala mzuri.
Kiasi flani ni kama umejadili au umetafsiri ile taarifa iliyochapishwa na Financial Times(FT) kuhusu kuogezeka au kukua kwa uwezo wa kijasusi wa Urusi.
 
Nadhani lengo mojawapo la vikwazo,mbali na kuuangusha uchumi wa Urusi lakini pia ni kuleta machafuko nchini humo na Kupelekea Putin kupinduliwa.
Hili deputy secretary of state wa Marekani Bi Victoria Nuland ameshakiri wazi Jambo usemalo.
Kasema nia yao ni kumweka madarakani kiongozi wa Urusi atakaye fuata matakwa ya watu wa magharibi.
Lakini amekiri wameshindwa katika hili.
 
anyway,
hapa duniani kwa sasa ni nchi mbili tu ndio zina uwezo mkubwa kijeshi, na kijasusi..... Russia na US...... hawa wana uwezo, uzoefu na ujuzi wa kila mbinu kwenye uwanja wa vita!

akina China bado sana, sijui itachukua miaka mingapi maana hajawahi pigana vita hata moja
 
Back
Top Bottom