Mchakato wa kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 umeendelea kugubikwa na tuhuma za ukiukwaji wa kanuni, ambapo safari hii Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Bi. Zainabu Shomari amejikuta katika hali ya utata baada ya kuhusishwa na vitendo vinavyotafsiriwa kuwa ni upendeleo wa wazi na kugawa rushwa.
Bi. Shomari, ambaye ni mmoja wa viongozi wa kitaifa wa chama hicho, anadaiwa kuonekana wazi akiwapa maelekezo wasimamizi wa uchaguzi wa ndani ya chama katika Jimbo la Kiembesamaki, Zanzibar. Taarifa kutoka kwa mashuhuda wa tukio hilo zinaeleza kuwa maelekezo hayo yalikuwa na lengo la kumpendelea mgombea Wardat Nassir Ali ambaye pia ni mtoto wake katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya Uwakilishi katika jimbo hilo.
Aidha, Bi. Shomari pia ametajwa na mashuhuda wakisema alionekana nje ya ukumbi wa mkutano akigawa fedha kwa wajumbe waliokuwa wamezingira gari lake, huku wajumbe hao wakiwa ndiyo wapiga kura katika mchakato huo. Kitendo hicho kimeibua taharuki na malalamiko miongoni mwa wagombea wengine waliokuwa wanashiriki kura za maoni katika jimbo hilo.
Baada ya taarifa hizo kusambaa na waandishi wa habari kumfuata kwa ajili ya maelezo, Bi. Shomari alitoweka ghafla kutoka eneo la tukio. Juhudi za kumpata kwa njia ya simu pia hazikufanikiwa, kwani hakujibu wito wala kutoa kauli yoyote kuhusu tuhuma hizo nzito.
Baadhi ya wagombea waliokuwa wakishiriki mchakato huo wameeleza kusikitishwa kwao na hatua ya kiongozi wa kitaifa wa chama kushiriki vitendo vinavyokwenda kinyume cha misingi ya chama, huku wakiahidi kuwasilisha malalamiko rasmi kwenye vikao vya chama ili hatua stahiki zichukuliwe.