Mkuu karibu JF kwa hii ID yako mpya.... Ivi watanzania hatujifunzi tu...??? Hwa jamaa wataacha lini huu wizi? Nakubaliana na Johnson Mbwambo hapa chini... Msome...
Tafakuri Jadidi
Baba fisadi, mtoto fisadi, mjukuu fisadi!
Johnson Mbwambo
Toleo la
253
8 Aug 2012
SASA ni dhahiri mwezi hauwezi kupita bila nchi yetu kutikiswa na skandali kubwa ya ufisadi. Unaweza kusema kila mwezi una aina yake ya skandali ya ufisadi.
Mwezi uliopita (kwa mfano) ilikuwa ni skandali ya mafisadi (wakiwemo viongozi wastaafu) waliojilimbikizia mabilioni ya shilingi katika benki za Uswisi.
Mwezi huu ni skandali ya ufisadi wa ununuzi wa mafuta iliyoikumba Tanesco, skandali ambayo pia inawahusu wabunge kadhaa wanaotuhumiwa kuhongwa fedha za rushwa na makampuni ya mafuta.
Sina hakika mwezi ujao ni skandali ya aina gani itaitikisa tena nchi yetu, lakini nina hakika kwamba itakuwepo tu; maana hii sasa inaonekana kuwa ndio staili ya maisha yetu tuliyojichagulia.
Sijui wenzangu mnaitafsiri vipi hali hii ya kusikitisha ya nchi yetu, lakini kwangu mimi hali hii inaashiria jambo moja kubwa; nalo ni kwamba tumeanza kuwa sugu katika masuala ya ufisadi. Na hii si ishara njema hata kidogo kwa nchi yetu.
Nasema tumeanza kujenga usugu kwa sababu skandali hizi za ufisadi hufuatana – moja baada ya nyingine, na hiyo maana yake ni kwamba kufichuliwa kwa skandali moja hakuwatii hofu mafisadi wengine kukamilisha (au kusuka) zao.
Na hali hii imeanza kuwa ni ya kukatisha tamaa kwa sababu wabunge (watunga sheria (zikiwemo za kupambana na ufisadi) sasa ndio vinara wa uovu huo.
Kwa maneno mengine, wabunge ambao ndio tegemeo la wananchi katika kuiwajibisha serikali ipambane vyema na ufisadi ndio sasa wamegeuka kuwa vinara wa ufisadi.
Tena wanaufanya ufisadi huo katika hali inayodhalilisha uwezo wa kufikiri wa wananchi; hususan wapiga kura wao. Wale wabunge ambao walionekana wakali bungeni wakiichachafya serikali kuhusu ufisadi huu na ule kumbe wenyewe ndio vinara wa ufisadi.
Wabunge hawa watatema cheche ndani ya bunge, lakini wakitoka nje ya bunge wanazifuata halmashauri za wilaya au mashirika ya umma (mfano Tanesco) au kampuni za mafuta au madini kuomba rushwa ili "watetee" hili na lile ndani ya bunge, na wasipopewa hutisha kuwa "watawawashia moto" ndani ya bunge!"
Kwa hiyo, naweza kusema ya kuwa sasa vita dhidi ya ufisadi katika Tanzania haina tena wapiganaji au majemadari wakuaminika. Wale tuliowadhania ni majemedari wa vita hiyo kumbe ilikuwa ni "danganya toto" tu.
Sasa imedhihirika kwamba, wakipiga kelele dhidi ya ufisadi si kwa sababu wanauchukia kweli kweli au si kwa sababu wao ni watu waadilifu; bali ni kwa sababu wanataka wasikike na waogopwe ili waweze kuzitisha halmashauri, mashirika ya umma, makampuni ya madini, makampuni ya mafuta, makampuni ya utalii nk. ili waweze kukatiwa pesa za rushwa!
Katika siku za karibuni, kwa mfano, tumesikia habari za mbunge kijana aliyedhaniwa ni mwadilifu na machachari akitumiwa kupoza skandali ya ufisadi katika Tanesco.
Aidha, tumesikia habari za wabunge kadhaa walioziendea halmashauri za wilaya na kuziomba rushwa! Mmoja tayari ana kesi mahakamani kwa kuomba rushwa ya Sh. milioni moja.
Wengi wetu bado tunazikumbuka habari za Katibu Mkuu wa zamani wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, aliyewakatia wabunge posho za rushwa ili waitetee wizara yake wakati wa mawasilisho ya bajeti!
Kwa ufupi, tumesikia kila aina ya ripoti za skandali za ufisadi zilizowahusu wabunge wetu. Na kama nilivyoeleza mwanzo, kufichuliwa kwa moja hakukuwatia hofu wabunge wengine kuendelea na zao!
Nje ya Bunge - yaani katika serikali, makampuni ya umma na binafsi, NGOs, sekta za madini, utalii nk, hali ndio mbaya zaidi. Na tena huko ndio kwenye rushwa kubwa kubwa.
Nisisitize tena kwamba vita hii dhidi ya ufisadi sasa haina wapiganaji wa kweli wala majemedari wa kweli. Kwa hakika, sasa naanza kupata shaka kama kweli vita hii ilipata kuwanao baada ya Mwalimu Nyerere na Edward Sokoine kututoka.
Hawa wa sasa waliojitokeza katika miaka ya karibuni na tukawaamini kuwa ni wapambanaji wa kweli wa vita hii, imedhihirika kuwa walichokuwa wakifanya ni "danganya toto" tu.
Chukulia mfano wa jemadari mkuu kabisa, Rais Jakaya Kikwete. Huyu hatujamsikia kwa muda mrefu akifungua kinywa chake kukemea ufisadi huu mkubwa au hata kuchukua hatua zozote kubwa (maamuzi magumu) kupambana na hawa tunaowaita mafisadi papa.
Hatukumsikia Kikwete akifungua kinywa chake hata pale ripoti ya benki kuu ya Uswisi ilipoitaja Tanzania kuwa ni moja ya nchi ambayo viongozi wake wameficha mabilioni ya fedha kwenye akaunti za benki za nchi hiyo.
Kwa hiyo, ninaposema ya kuwa vita hii dhidi ya ufisadi katika Tanzania haina wapiganaji wa kweli wala majemedari wa kweli, maana yangu ni hiyo.
Kwa upande mwingine, hata Takukuru nayo imeshindwa kuushawishi umma kama inapigana kweli kweli vita hii. Masra nyingi imeisdhia kupambana na vijidagaa wa ufisadi na si mafisadi papa ambao ndio kansa inayolitafuna taifa hili.
Miezi kadhaa iliyopita niliandika katika safu hii kwamba Takukuru haina uwezo wa kufuatilia na kuwafikisha mahakamani mafisadi hao walioficha mabilioni ya fedha katika benki hizo za Uswisi. Nilishauri kitafutwe chombo cha nje (mathalan
Interpol) kutufanyia kazi hiyo.
Lakini bosi mkuu wa Takukuru, Dk. Edward Hoseah, hakufurahishwa na kauli yangu hiyo, na katika mahojiano na televisheni moja alinishutumu kwamba sielewi vyema utendaji wa asasi hiyo na kunitaka nifike ofisini kwake ‘anielemishe'.
Katika mahojiano hayo, Dk. Hoseah aliwapa matumaini Watanzania kwamba asasi yake itahitimisha vyema suala hilo la mapesa yaliyofichwa Uswisi. Hata hivyo, mpaka sasa miezi miwili imeshakatika na bado hakuna ripoti yoyote ya maendeleo ya suala hilo ambayo imetolewa kwa umma na Takukuru!
Na ndio maana msimamo wangu ni ule ule kwamba asasi yetu hiyo haina ubavu wa kulishughulikia suala hilo zito la ufisadi wa kimataifa na kufikia mwisho mwema!
Kama asasi hiyo ingekuwa na uwezo huo, pengine ingekuwa tayari imefikia mwisho mwema katika suala lile la kashfa ya ufisadi wa rada ambalo limefikia hata hatua ya kuandikiwa kitabu na mchunguzi mmoja wa kimataifa!
Nionavyo mimi, Takukuru husikika zaidi pale tu skandali kubwa zinapoibuliwa na wengine na si yenyewe kuwa ya kwanza kuziibua skandali hizo.
Kwa mfano, ilipoibuliwa skandali ile ya Jairo, Takukuru iliibuka na kusema kuwa itachunguza. Lakini pia mawaziri kadhaa walipong'olewa uwaziri baada ya wabunge kuwatuhumu kuhusika na rushwa, ndipo Takukuru ilipotoa tamko kwamba itawahoji kwa lengo la kuwafikisha mahakamani wale ambao ushahidi dhidi yao ni mzito. Mpaka sasa hakuna aliyefikishwa mahakamani.
Na hata majuzi ilipoibuliwa hii skandali ya ufisadi ya ununuzi wa mafuta katika Tanesco ndipo tumeisikia Takukuru ikitamka kuwa itachunguza suala hili kwa kuwahoji watuhumiwa.
Kwa mwenendo huo, mtu unashawishika kujiuliza kuwa Takukuru inakuwa wapi muda wote huo na ishindwe kuwa ya kwanza kuibua skandali hizo? Kwa nini inajitokeza tu kuchunguza pale skandali hizo zinapoibuliwa na wengine? Na mbona pia umma hauoni mwisho mwema au matokeo mema ya uchunguzi wao huo?
Si nia yangu kuilaumu Takukuru. Kwa hakika, kuilaumu Takukuru kwa utendaji usioridhisha katika nchi ambayo imeota usugu wa ufisadi hadi vyombo vya juu vya maamuzi, ni kutoitendea haki.
Tumeukumbatia utamaduni wa ufisadi kwenye kona zetu zote za maisha, na tumeikumbatia tabia ya kutowashitaki mafisadi
(impunity culture) kiasi kwamba tatizo hili sasa limekuwa dubwana kubwa linaloelekea kutushinda nguvu.
Jamii imeoza kuanzia ngazi ya familia: Baba fisadi, mtoto fisadi na mjukuu fisadi! Hakika, baba fisadi hatamuuliza kijana wake amepata wapi fedha za kununua gari la kifahari aina ya
Hammer.
Na mtoto naye mwenye
Hammer hatamuuliza mtoto wake amepata wapi fedha za kununua
Range Rover new model au
Vogue katika miaka yake michache tu kazini!
Vivyo hivyo mtawala aliyeingia madarakani kwa njia za ufisadi hawezi kukasirika akisikia waziri wake anashiriki vitendo vya kifisadi. Na wala kope zake haziwezi kupepesa akisikia wabunge kutoka chama chake wanapita huku na kule kuomba rushwa kwenye makampouni ya mafuta, madini nk!
Ndio maana ufisadi umekita Tanzania. Hakuna aliye msafi wa kumkemea mwenzake. Na tusipozinduka, ufisadi ndio utakuwa urithi wetu kwa vizazi vijavyo; maana kibaya kamwe hakizai chema.
Katika injili ya Luka Mtakatifu (6:43-44) imeandikwa hivi:
"Mti mwema huzaa matunda mema, na mti mbaya huzaa matunda mabaya, wala mti mbaya hauwezi kuzaa matunda mema."
Ndio maana siku zote ninasema kuwa taifa hili halitakuwa tena na waadilifu kama tutarithishana hulka hizi za kifisadi kuanzia kwa baba, mwana, mjukuu hadi kwa kitukuu. Na hayo ndio maangamizi tunayoyaandaa kwa jamii ya Watanzania.
Nihitimishe safu yangu kwa kusema hivi: Kwa mambo yanavyokwenda hivi sasa, kila mwezi utakuja na skandali zake kubwa za ufisadi lakini
kombe litafunikwa na
mwanaharamu atapita, na watu wataendelea kunywa bia zao bila wasiwasi; huku wakisubiri tena mwezi ujao……wakisubirii skandali nyingine tena iibuliwe ili nayo izimwe kwa staili ile ile ya kisanii ya kuunda tume nk!
Ndugu zangu, nyumba yetu (Tanzania) ni chafu, na inahitaji kufagiliwa. Sina hakika kama mchafuzi (CCM na serikali yake) ndiye huyo huyo anayeweza kuifagia na ikawa safi kweli kweli!