Tundu Lissu: Tusipoyasema haya juu ya kifo cha Ruge Mutahaba, mawe yatasema

Francis12

JF-Expert Member
Sep 30, 2016
7,533
22,276
KIFO CHA RUGE MUTAHABA: TUSIPOYASEMA HAYA, MAWE YATASEMA!!!

Ruge Mutahaba amefariki dunia nchini Afrika Kusini alikokuwa akitibiwa. Ruge alikuwa mmojawapo wa wakurugenzi wa Clouds Media Group, mojawapo ya vyombo vya habari vikubwa hapa nchini.

Inaelekea huu ni msiba mkubwa sana kwa taifa letu. Viongozi wa Serikali, vyama vya siasa, taasisi mbali mbali na wananchi wa kawaida wamejitokeza hadharani kutoa salamu zao za rambi rambi kwa ndugu, jamaa na marafiki zake marehemu Ruge.

Hii ni sawa sawa, kwani Ruge Mutahaba hakuwa mtu mdogo kwenye jamii yetu. Hivyo, na mimi naungana na waombolezaji wengine kumuomboleza kijana huyu.

Naomba nikiri mapema: mimi sikumfahamu sana Ruge. Nilikutana naye mara mbili au tatu aliponifuata Bungeni mwaka 2012 (kama sikosei) ili nisaidie kumpatanisha yeye na baadhi ya wanamuziki wa kizazi kipya, wakiongozwa na Mh. Joe Mbilinyi 'Sugu.' Nilifanya hivyo.

Zaidi ya hapo, nilimfahamu kwa juu juu kama mmoja wa wakurugenzi wa Clouds Media Group.

Kwa hiyo siwezi kumzungumza sana kwa mema au kwa mabaya yake. Siyafahamu sana. Ninachotaka kukizungumzia ni haya maombolezo ya kifo chake.

Sikujua kwamba kumbe Ruge Mutahaba alikuwa "... kada wa CCM... aliyejijengea heshima na ukubalifu..." kwa Chama hicho. Sikujua kwamba CCM ilimtumia Ruge sana wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Haya yote nimeyafahamu kufuatia kifo chake. Nimeyafahamu kwa sababu ya salamu za rambi rambi za Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole.

Kwenye hili kuna fundisho kubwa sana.

Mapema ya mwaka 2017, ofisi za Clouds Media Group zilizoko Mikocheni, Dar Es Salaam, zilivamiwa usiku na watu wenye silaha na sare za Jeshi la Polisi, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na wengine wakiwa wamevalia kiraia.

Watu hao waliongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Paul Makonda alias Albert Bashite. Watu hawa walifanya uhalifu mbali mbali wa kijinai kwa mujibu wa sheria za nchi yetu.

Kwa bahati nzuri, tukio hilo lilirekodiwa kwenye kamera za video za ulinzi (CCTV), ambazo marehemu Ruge na wafanyakazi wa Clouds Media Group walizisambaza mitandaoni. Kwa hiyo hadithi ya 'watu wasiojulikana' haikuwezekana kwenye tukio hilo la kihalifu.

Kwa sababu ya kelele na shinikizo kubwa la umma, Waziri wa Habari, Michezo na Utamaduni wakati huo, Mh. Nape Nnauye, aliunda Kamati ya Uchunguzi wa tukio hilo. Jukwaa la Wahariri (TEF) na Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT) nao waliunda Kamati za Uchunguzi.

Wachunguzi wote hawa walithibitisha pasina shaka yoyote kwamba Mkuu wa Mkoa Makonda aliongoza uhalifu huo. Kwa hiyo ukweli wa uhalifu huo haubishaniwi.

Hata hivyo, mara baada ya kupokea taarifa ya Kamati ya Uchunguzi aliyoiunda, Waziri Nape Nnauye alifukuzwa kazi na Rais Magufuli.

Na alipojaribu kufanya mkutano wa waandishi habari kuelezea tukio hilo, alizuiliwa kufanya hivyo kwa mtutu wa bastola ya maafisa wa Idara ya Usalama wa Taifa na Ujasusi (TISS).

Na hii nayo haina ubishi maana ilifanyika mchana kweupe na picha za video za tukio zilisambazwa mitandaoni.

Jeshi la Polisi halikuchukua hatua yoyote ya kisheria dhidi ya Mkuu wa Mkoa Makonda na wavamizi wenzake wa Clouds Media Group, wala maafisa wa usalama wa taifa waliomtishia Nape Nnauye kwa bunguki. Rais Magufuli naye hakuchukua hatua zozote dhidi ya mteule wake Makonda.

Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), kupitia kwa Baraza lake la Uongozi, lilitoa kauli ya kulaani vikali uhalifu uliofanywa na Mkuu wa Mkoa Makonda na wavamizi wenzake. TLS iliazimia kufungua mashtaka ya jinai ya binafsi dhidi ya wahalifu hao, lakini hilo halikufanyika kufuatia kushambuliwa kwangu kwenye jaribio la mauaji la Septemba 7, 2017.

Kwa vyovyote vile, tukio la uvamizi wa Clouds Media Group halikushughulikiwa kwa mujibu wa sheria za nchi yetu.

Ni heshima kwa marehemu Ruge Mutahaba kwamba, licha ya shinikizo kubwa la kumnyamazisha, alipiga kelele kubwa hadharani.

Licha ya kuwa 'kada mkubalifu' wa CCM, hakukaa kimya mbele ya uovu uliofanywa dhidi ya Clouds Media Group na wafanyakazi wake. Aliwataja wale waliomfanyia yeye na Clouds Media Group na wafanyakazi wake uhalifu.

Hata hivyo, wale aliowasaidia kupata madaraka ya kisiasa kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita walimsaliti Ruge Mutahaba.

Rais Magufuli aliingilia kati kwa upande wa Mkuu wa Mkoa Makonda na wavamizi wenzake. Rais Magufuli alimfukuza kazi Waziri Nape Nnauye aliyejaribu kuingilia kati kwa niaba ya Clouds Media Group, Ruge Mutahaba na wafanyakazi wake.

Jeshi la Polisi halikuingilia kati. Liliangalia upepo uliokuwa unavuma kutoka Ikulu ya Magogoni likaamua kukaa kimya.

Chama cha Mapinduzi nacho halikuingilia kati wala kutoa kauli yoyote ya kumuunga mkono. Kiliangalia mwelekeo wa Mwenyekiti wake na kunyamaza kimya.

Sasa Ruge Mutahaba amefariki dunia. Sasa hatasema tena. 'Dead people tell no tales.' Sasa ni salama kwa wabaya wake kujitokeza hadharani na kumlilia machozi ya mamba.

Rais Magufuli amemwita 'kijana wake.' Wakati Ruge na Clouds Media Group walipovamiwa, Rais Magufuli alisimama upande wa wavamizi na 'kijana wake' mwingine, Paul Makonda aliyeongoza uvamizi huo.

Sasa Mkuu wa Mkoa Makonda, kiongozi wa wavamizi, anamtaja mvamiwa kama "... kijana mchapakazi, mwenye nidhamu na mzalendo wa kweli."

Sasa Chama alichokisaidia kupata madaraka halafu kikamkimbia wakati wa shida yake kinadai Ruge alikuwa na 'ukubalifu' ndani ya Chama hicho. Dead people tell no tales.

Sasa ni wakati wa wanafiki kujitokeza hadharani, na wachawi kulia kwa uchungu kuliko waliofiwa.

Ni lazima tuyaseme haya sasa na hadharani. Tusipoyasema, hata mawe yatasema.

Mwenyezi Mungu ampe marehemu Ruge Mutahaba mapumziko ya amani. Na Mwenyezi Mungu atupe sisi tulio hai nguvu na ujasiri wa kusimama na kupaza sauti zetu kwa niaba ya akina Ruge waliopo na wale wajao.

Tundu Lissu, UZ Leuven, Gasthuisberg, Leuven, Ubelgiji, 27 Februari, 2019
 
Sasa kama hukujua kuwa Ruge alikuwa kada wa CCM... aliyejijengea heshima na ukubalifu basi hata suala la Ruge na Makonda huwezi kulijua jinsi lilivyotatuliwa kwa ndani!

Ndio maana wenye hekima na busara husema, ndugu wakigombana chukua jembe ukalime...

Mambo ya kushabikia na kujihusisha na ugomvi wa ndugu wakati hata hujui vizuri mahusiano yao ni kukosa hekima na busara!

Wapinzani huwa wananishangaza na kunichekesha pale wanaposhabikia ugomvi wa wanaCCM bila kujua kuwa ugomvi wao ndio unawaimarisha zaidi katika vita vya kisiasa.

Hili la Ruge kuwa kada wa CCM aliyejijengea heshima liwe ni funzo kuwa CCM ina mizizi mirefu ambayo wale wanadhani wanaweza kuing'oa kwa makelele bila mbinu makini ni kupoteza muda na nguvu zao ndogo walizonazo.

Masuala kama haya kwa mtu mwenye akili pana akisikia CCM wanaposema wataendelea kuwa chama tawala atajua huwa hawatanii bali wanamaanisha!
 
Back
Top Bottom