Kichwa cha Yohana kwanza kinatakiwa kwenye huo upinzani ambao unatakiwa ndio uwe rejea mbadala ya Taifa.
Huwezi kutaka mambo makubwa wakati huna maono ya kuyafanikisha mambo hayo.
Wewe huwezi kuona umuhimu wa standard gauge leo hii, lakini itakapokamilika treni ya umeme kutoka Dar mpaka Burundi, hao wanaoishi kando kando yake watawasimulia wajukuu au watoto zako juu ya umuhimu wa usafiri huo.
Flyover zinao umuhimu ambao wakati huu wa ujenzi huwezi kuuona. Hayo mataifa makubwa ambayo waafrika tunaona fahari kwenda kuishi, hayakujengwa ndani ya miaka 56 ya uhuru wao.
Ujerumani ilianza kujengwa upya baada ya vita kuu ya pili. Japan ilipigwa bomu zito pale Hiroshima. Marekani mwaka jana imefikisha miaka 240 ya uhuru.
Hatuhitaji kichwa cha Yohana, kwa sababu hakuna short cut ya kutufikisha kwenye nchi ya ahadi.
Kuifikia nchi hiyo ni mchakato wa miaka mingi, pengine sisi wa kizazi cha sasa turidhike tu na ule ukweli kwamba watakaokuja kuiona Tanzania yenye neema ni wale watakaoishi miaka mingi kutoka leo hii.