KATIKA kauli ambazo zitawashitua watawala, Waziri Mkuu wa zamani, Jaji Joseph Warioba, amesema nchi ina viongozi dhaifu, umma unanyonywa, rushwa imeongezeka, wezi wa fedha za EPA waanikwe na Rais Msitaafu,
Benjamin Mkapa akajibu tuhuma zake mahakamani.
Katika mahojiano maalumu na Raia Mwema, Warioba amesema kuna dalili ya kuwapo watu wakubwa nyuma ya kashfa ya fedha zilizopotea katika sakata la EPA na kwamba yaliyotokea ni wizi wa hali ya juu na baadhi
wameghushi na kwamba hatua za kisheria ni lazima zichukue mkondo wake.
JAJI Warioba
"Niliyosoma hasa kutokana na taarifa ile ya Serikali, ukiisoma kwa makini unaona kuwa
haukuwa ununuzi wa madeni, huo ulikuwa ni wizi wa fedha za umma," anasema Jaji Warioba.
Anasema kwa mujibu wa taarifa ya Serikali, baadhi ya madeni si madeni bali kuna watu
wametumia ulaghai kuchukua madeni ambayo yamekwisha kulipwa na wao kufanya udanganyifu kuyadai.
"Wapo ambao wamefanya hivyo kwa kughushi. Sasa kuna makosa mawili hapo.
Wizi na kughushi, ni makosa mazito, na kama nilivyosema wakati ule ilipotoka mara ya kwanza, ukiona makampuni ambayo yametajwa si
makampuni makubwa na mengi yake yaliundwa kwa kazi hii tu," alisema katika mahojiano ambayo sehemu yake ya kwanza imechapishwa katika kurasa za 12 na 13 za toleo hili.
Akionyesha kuwapo kwa watu wakubwa nyuma ya wizi wa fedha za EPA, Warioba anasema biashara ya kununua madeni inataka mtu mwenye fedha na mwenye ujuzi wa biashara hiyo lakini makampuni yaliyoorodheshwa na serikali mengi yanamilikiwa na watu wa kawaida kabisa wasio na uwezo huo.
"Kampuni hizi ni ndogo, watu wenye kampuni hizi wameandikwa watu wenye majina ya kawaida. Kwa mtu yeyote mwenye busara atajua hii ni hadaa tu. Wanaoshughulika hawakujiandika kwenye kampuni hizi, wamechukua watu wengine tu. Kwa hiyo, kuna kazi, kuna kazi ya kuwatafuta hawa wazito waliokuwa wanahusika.
Na kama ni wazito na wameingia katika wizi wa mali ya Taifa na kughushi, suala hili ni zito kuliko tunavyoliona," anasema na kuongeza;
"Mimi naamini kama kweli tunaishughulikia kwa nguvu zote, EPA ni kubwa kuliko Richmond, kuliko haya yaliyotokea. Kwa hiyo tutangojea matokeo. Na hapa kwa kuwa walau ushahidi wa kawaida upo, taarifa zinasema zile nyaraka zilizowezesha madeni hayo kununuliwa ni za kughushi, basi unaanzia hapo. Ukihakikisha kwamba ni za kughushi, kwamba haya madeni hayakuwapo, ukithibitisha kwamba hili deni halikuwapo sasa huyo aliyechukua fedha hizo alitumia wapi?"
Alisema akiwa kama raia mwema wa Tanzania anasubiri kwa makini kuona matokeo ya EPA, na kuongeza kwamba kama kweli nia ya kusafisha ipo,
ni lazima waliofanya makosa wapatikane na kushughulikiwa na si wale waliotangulizwa.
"Mimi sijui utaratibu wanaotumia.
Lakini kwa utaratibu wa kawaida, mimi nilikuwa Mwanasheria Mkuu wa nchi, kwa suala hili la jinai unalishughulikia linakwenda mahakamani. Adhabu inatolewa pamoja na kurudisha hizo fedha, hilo ndilo nalitarajia," anasema.
Anasema kwa kawaida hatua za kisheria ni lazima zichukuliwe na kwamba unapokwenda mahakamani unaweza kutumia sheria kurudisha fedha zilizoibwa hata ikibidi kufilisi wahusika.
Hivi karibuni timu iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete kushughulikia waliochukua fedha za EPA ilieleza wazi kwamba imekua ikipokea fedha kutoka kwa watuhumiwa kwa kile kilichoelezwa kwamba ni kuepuka kupoteza fedha hizo huku wanaozirejesha wakiendelea kuwa siri.
Timu hiyo ya Rais inaongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika, akisaidiana na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Saidi Mwema, na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Edward Hosea, wote wakisaidiwa na maofisa kutoka ofisi zao na kutoka asasi nyingine za umma.
Akizungumzia kitendo cha viongozi hao wa juu wa dola kufanya mazungumzo na watuhumiwa, Jaji Warioba anasema; "Kwamba hawa ndio kweli viongozi wa ngazi ya juu wa vyombo vya dola vinavyoshughulika na uhalifu wanafanya kazi hiyo. Imani yangu ni kwamba hawatapinda sheria.
Wakipinda sheria tutakuwa tumeleta madhara makubwa sana kwa nchi hii. Kwa sababu wananchi lazima kwa upande wa sheria waamini ofisi ya Mwanasheria Mkuu, ni lazima waamini ofisi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi, lazima waamini ofisi ya TAKUKURU."
Warioba anasema watendaji hao wa dola wakipinda sheria, imani ya wananchi itapungua na hivyo ni jukumu lao ni kubwa, na kwamba yeye ana imani kwamba hawatapinda sheria.
Akizungumzia hali ya kisiasa ya nchi kutokana na kukwama kwa mambo mengi ikiwamo muafaka wa kisiasa Zanzibar na kuibuka kwa wimbi kubwa la tuhuma za ufisadi, Jaji Warioba anaonekana kutokua na imani na hali hiyo na anakiri kuwapo kwa udhaifu katika uongozi wa juu wa kitaifa.
"Kama nilivyosema, kila mtu ni kuzungumzia ufisadi, hata mafisadi wenyewe, maana ukiona wote hawa wanaozungumzia, huwezi kusema ni watu safi, pamoja na vyombo vya habari, navyo haviwezi kujisifu.
Wengine wanaoandika juu ya ufisadi ndio hao hao waliokuwa wakichukua fedha za hawa, wanawaandika kuwa ni wazuri wakati wa uchaguzi. Walikuwa wakiwapamba. Kwa hiyo kuna wengine ni unafiki tu, ama ni ufisadi na wenyewe," anasema.
Warioba anapongeza juhudi zinazofanywa na vyombo vya habari na wabunge katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi lakini anaonya vita hiyo isitumike kufunika madhambi yaw engine ama kuwaumiza baadhi yao.
"Sina hakika kama wote wamezinduka hivi. Jana walikuwa wanasema hakuna rushwa, hakuna ufisadi. Leo ndiyo wako msitari wa mbele wanatafuta mafisadi na ukiangalia zaidi ni viongozi. Na hasa wabunge ndio wanaongoza vita hii. Ni vizuri Bunge liongoze lakini je, tunawaamini wote? Kwamba nia yao hasa ni kumaliza ufisadi au kuna sababu nyingine?
"Ikifika mahali tuwaulize hawa ambao sasa wanaonekana wana uchungu sana na ufisadi. Mwaka 2005 tuliona yaliyotokea. Hivi ni wangapi ambao wako safi? Mwananchi akimwuliza mbunge wake, na hii inawezekana kwa zaidi ya nusu ya wabunge, kwamba mbona wewe ulikuja na fedha nyingi sana kwenye uchaguzi na wewe si tajiri, ulizipata wapi?" anahoji Jaji Warioba.
Anasema wamo wengi ambao ni sehemu ya uongozi, na hivyo isije tokea mapambano ndani ya uongozi yakageuzwa kuwa ni vita ya kweli kumaliza ufisadi.
"Mimi nataka niwe na uhakika tukifika mwaka 2010 tuweze kuchagua viongozi safi, tusipate viongozi ambao katika mchakato wa uchaguzi watakwenda na takrima kwa sababu kama wanakwenda na takrima wamezipata fedha hizo kwa ufisadi," anasema.
Akizungumzia muafaka kati ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF), Jaji Wariona anasema tatizo kubwa ni mgawanyiko katika uongozi. Anasema wapo ambao hawataki muafaka wanaona njia ni kusema tupate maoni ya wananchi wakitarajia kwamba wananchi watakataa.
Kuhusu wanaotishia kurejea kwenye Afro Shirazi Party (ASP) kuliko kuingia katika Muafaka na CUF, Warioba anasema hivyo ni vitisho visivyo na maana katika mazingira ya sasa kwani hata wakiachwa hawana uwezo huo na kwamba tatizo kubwa ni udhaifu wa viongozi.
"Zaidi wanaosema warudi ASP ni watu wa Zanzibar, lakini nadhani pia kuna udhaifu katika viongozi Bara. Wakiisha kusikia madai hayo ya ASP, wanasema jamani waachieni mambo yao! Lakini haya si mambo yao, ni mambo ya nchi. Zanzibar ni sehemu ya Tanzania, likitokea tatizo Zanzibar ni tatizo la Tanzania. Hawa wanaosema waachieni haya ni mambo yao ni viongozi dhaifu," anasema na kuongeza;
"Hilo ni suala muhimu, hapo ndipo uongozi unapohitajika. Huwezi kukwepa.
Uongozi kazi yake ni kuamua mambo mazito, na wakati wote unaweza kuwa na wasiwasi, lakini unaamua kwa maslahi ya taifa. Hata kama katika kuamua huko unahisi kuwa kuna baadhi watakulaumu. Usiogope lawama, dira yako iwe kuwa hii ni kwa manufaa taifa ama hapana. Manufaa ya Taifa sasa hivi ni kumaliza mpasuko wa Zanzibar. Lolote linalohitajika kumaliza mpasuko huo ni vizuri viongozi wakachukua uamuzi, utakuwa ni mgumu lakini ni wajibu wao kuchukua uamuzi."
Pamoja na kuonekana kukwepa kumshutumu Rais Mstaafu Mkapa,
Jaji Warioba anasema kinga waliyonayo viongozi akiwamo rais ni ya kisiasa tu, na hivyo kwake yeye suala la kinga ya kisheria si tatizo bali ukweli na uhakika wa tuhuma zinazomgusa kiongozi husika na kwamba ni mahakama inayoweza kutoa uamuzi wa haki.
"Nimeona wanaandika na nimeona mjadala mkubwa tu unaolenga kwenye
immunity. Mimi nafikiri suala hilo si la msingi kwa sasa hivi. Na mjadala unalenga kwamba aseme, naona si la msingi. Kwa sababu hatutaki kwamba huyu awe tried na vyombo vya habari. Maana hapa naona kama ni trial kwenye vyombo vya habari.
"
Waseme ni kosa gani, amefanya kwa msingi wa sheria gani, sasa waendelee. Sasa mengi wanayosema ni ya kisiasa. Yakisemwa ya kisiasa unataka mtu awajibike kisiasa. Kama ni kosa la jinai, waseme amevunja wapi sheria, lakini kusema kweli mimi sioni kwa vyombo vya habari kusema yote haya na wanachotaka ni kwamba ajitetee, ajitetee wao ndio wamekuwa Mahakama?" anahoji Jaji Warioba ambaye amewahi kufanya kazi kwa karibu na Mkapa.
Warioba anasema vyombo vya habari vinataka kuwa Mahakama na akashauri kwamba kama kuna kosa alilofanya Mkapa ni vyema wakasubiri
afikishwe mahakamani ambako atakuwa na nafasi ya kujitetea na kueleza upande wake.
"
Immunity nasema sasa hivi siyo issue. Sema kosa lililotendeka. Anashitakiwa lakini wanasema hatuwezi kuendelea kwa sababu kuna
immunity. Bila kusema kosa huwezi kufika kwenye
immunity. Huwezi kuanza na
immunity bila kuwa na kosa, kwa hiyo mimi sitaki kujiingiza katika mjadala wa
immunity. Hii ni ya kisiasa tu," anasema.