Tukaona wageni wakiitawala miji ya wenyeji wao

Aldonia

Member
Sep 13, 2016
20
14
Tafakuri na....

Na ule mti ulivyokatwa shina, tukaona wazee waliokosa hekima. Tukaona wazazi waliokosa heshima, tukaona mafundi waloshindwa pima, madaktari walioshindwa kutibu watu kwa kukosa pesa na bima. Mahakimu waliopinga haki kwa kukosa takrima. Tukaona wajomba walioshindwa kutunza na kuwalinda yatima na wafungwa waso hatia gerezani wakilala wima.

Tukaona makaburi ya watoto yakiongeza idadi na vijana wadogo wadogo wakiitana dadi, na majumba ya ibada yaliyojaa waumini na wachungaji mafisadi. Tukaona utu wa watu ukivuliwa kwa midadi.

Tukaona taswira za watu wema zikifutika kwa maji. Waliokuja kusaidia masikini kugeuka kwa dhamira zao na kuwa wapigaji. Tukaona visima vilokauka maji. Tukaona vitabu vilokosa dibaji, wenye tamaa, wahalifu na wenye wivu wa nafasi wakigeuka na kuwa majaji.

Tukaona wakubwa wakihimiza vijana juu ya utafutaji, wakati nafasi zao kwenye ofisi kubwa za umma toka wadogo ni kama samaki na maji.

Kutokuwa na thamani ya shule tukaona nafasi ya vipaji na hamasa zikafanywa samadi kisha vipaji vya vijana wa mtaani vikatoa Ulaji. Tukaona mitaa iliyojaa degree na ma GPA. Tukaona mabinti kwa mabinti wakiitana hey, na watu wa misuli na nguvu wakijiita sinapei.

Mwenye makosa kwa kujiamini akisema sikosei. Tukaona milango iliyokosa vitasa, zile kelele tulizohisi ni yowe kumbe ni anasa na Barabara zilojaa mashimo, na adhabu zilokosa vipimo na mashamba yakipinga kilimo. Maadui na Marafiki wakipatana kwa wino.

Yale makosa na madhambi ya vipindi yakigeuka kuwa desturi na wale walioshindwa kutenda vema wakitoa ushauri. Nyumba za ibada zikigeuka kuwa miradi ya kila sampuli na wanyama wakiwa juu ya binadamu wenye viburi. Tukaona ukubwa wa pesa na mali.

Tukaona tulowaamini na kuwategemea wakiilamba asali. Tukaona ugumu wa kukosa majibu ya maswali na mali zilopotea bila habari kisa daftari.

Tukaona wahudumu wakishindana kuumiza wateja wao na wakiamini kushindwa kwao siyo makosa yao, na tathmini zikifanywa kwa milengo yao, ya kulinda maslahi na matakwa ya mabosi zao huku wakikalia taaluma na ujuzi wao.

Tukaona wasomi wakiendeshwa na hisia zao, tukaona wachungaji wakiongozwa na wanyama wao. Tukaona ma house girls wakimiliki nyumba za mabosi zao, na wale wake wakibakia na majina tu ya waume zao. Tukaona nguvu ya mitandao ya kijamii, ikiharibu malezi na familia kwa kufanya watu wajihisi wako free.

Tukaona baraka za mungu zikitafutwa kwa watu, na Watu walo hai wakitembea kama wafu. Mikutano ya kimazingira, wakihimiza usafi na usiku Barabarani wakitupa mipira, wakihusia watu waache zinaa au wafanye kwa uangalifu, wakati uhalisia wa mambo kwa vijana ni ubabaifu.

Wakaficha pesa za bando wakaoffer WiFi, wakabana na passwords wakaulizwa why? Wakasema ni maagizo toka juu usoni wakifurahi. Tukaona tabasamu ziloficha chuki vichwani na misamaha iliyoicha visasi kwa ndani, na ukarimu uliyoficha dhamira mbovu na hatari kwa majirani, majungu na kejeli za kweli zilofichwa kwenye Utani.

Tukaona wageni wakiitawala miji ya wenyeji wao na wakiwataka kubadili mila na desturi zao, na wachawi waliovaa suti na tai, na wale wezi wa mikataba wakibaki na nafasi zao licha ya ukweli wa wazi ya kuwa hawafai!
 
Back
Top Bottom