SoC03 Tujenge utamaduni wa kujali vipaji ili tutanue wigo wa maendeleo

Stories of Change - 2023 Competition

Enigmatic_

Member
May 12, 2023
16
13
Kipaji ni mtaji pekee ambao kila binadamu huzawadiwa na asili. Kila mtu anauwezo wa kipekee kufanya jambo au kitu Fulani. Na, ili uwezo huo (kipaji/kipawa) uweze kukua na kuendelezwa na kuleta matokeo chanya kwa mhusika na jamii, mazingira yana mchango mkubwa.

Kama ilivyo kwa punje ya muhindi, ili iweze kuota na kukua vizuri inahitaji maji, udongo wenye rutuba, hewa na mahitaji mengine, vivyo hivyo kipaji. Ni rahisi sana kwa mtu mwenye kipaji cha uchoraji kukuza kipaji chake kama familia yake (watu wa karibu) na jamii yake wanathamini kile anachokifanya. Kinyume na hapo wengi hukata tamaa. Wachache hufanikiwa ‘kutoboa’ kwenye mazingira magumu kwao.

Nchini kwetu (Tanzania), suala la kuzingatia vipaji vya watu bado linasuasua. Hii ni kwa sababu hatuna utamaduni huo na inaonekana bado hatujaona umuhimu. Sio kwamba watanzania hawana vipaji. vipo sana. Ni mara ngapi imeripotiwa mtu kafanya uvumbuzi Fulani au kitu Fulani cha kipekee na bado jambo likachukuliwa kawaida? Sio bahati mbaya. Ukweli ni kwamba hatujawa na utaratibu wa kuthamini kile ambacho mtu anaweza kukifanya tofauti na tunavyoweza. Nchi za wenzetu mambo hayapo hivyo. Kipaji cha mtu kinathaminiwa. Kinaatamiwa. Mpaka tunakuja kusikia kwenye vyombo vya habari kwamba mtu Fulani kafanya kitu Fulani, mambo mengi yanakuwa yamefanyika.

Tujaribu kuwaza wale wanafunzi wanaochukuliwa kila mwaka kwenye UMISETA/UMITASHUMTA huwa hatma yao ni ipi baada ya kumaliza shule na kutopata bahati ya kuendelea na masomo? Wengi wao huishia mtaani. Kuna binti alikuwa bingwa wa mbio za mita 400 kwenye UMISETA lakini hakufanikiwa kuendelea na masomo kidato cha tano. Kwa sasa, usimuulize tena kuhusu ubingwa wake kwenye mbio za mita 400. Atakwambia “familia nimuachie nani!” Kinaochooneka ni kwamba shughuli za mashindano ya michezo zipo kukamilisha ratiba tu. Si kwa ajili ya kuibua, kukuka na kuendeleza vipaji.

Lakini pia upande mwingine, mashindano ya UMISETA/UMITASHUMTA mara nyingi hayazingatii vipaji vyote. Mara nyingi yamejikita kwenye michezo tu, nayo sio yote. Vipengele vingine kama uandishi wa insha na utunzi, uchoraji, uchongaji, muziki na vingine huwa vinaachwa na hivyo kuwanyima fursa wanafunzi wenye vipaji kwenye maeneo hayo.

FAIDA ZA KUJENGA UTAMADUNI WA KUTHAMINI VIPAJI

-Tutatengeneza raia wanaoijiamini;

-tutapunguza idadi ya wahitimu wanaoachwa na mfumo rasmi wa elimu;

-Ni rahisi kuongeza kipato kwa mtu binafsi na taifa;

-Ni namna nzuri ya kuondoa utegemezi kwenye chanzo kimoja cha mapato. Hii ni kwa sababu hakutakuwa na ulazima wa kila mtu kufanya kilimo ili afanikiwe. Anaweza kukitumia kipaji chake vizuri na akafanikiwa.

-watu wenye vipaji wanaweza kuwa mabalozi wazuri katika kuitangaza nchi, hivyo kuvutia watalii na wawekezaji.

-Tunaweza kupunguza gharama za uzalishaji na kupunguza utegemezi endapo wabunifu kwenye sekta ya sayansi na teknolojia ‘wataatamiwa’ vizuri.

TUNAWEZAJE KUTENGENEZA UTAMADUNI HUU?

Ili kufanikiwa kujenga utamaduni wa kuthamini vipaji, kuna mambo mengi ambayo inatakiwa yafanywe na wadau mbalimbali, ambao ni wazazi/walezi, jamii na serikali.

Wajibu wa wazazi/walezi:- hawa ni wa wadau wa kwanza katika kutambua vipaji vya watoto. Kutokana na ukaribu walionao, wanauwezo wa kujua kipaji cha mtoto kwa kuangalia uwezo wake kwenye mambo mbalimbali. Hata hivyo, ili kujenga utamaduni wa kuthamini vipaji, wazazi/walezi wanatakiwa:

-kutenga muda wa kuchunguza watoto na kuongea nao kuhusu uwezo na ndoto zao

-kutoa msaada wa vitu na wa kimawazo kwa watoto kwenye mambo yanayohusiana na vipaji vyao. Kwa mfano kama mzazi anaona kabisa mtoto ana kipaji cha uchoraji, basi anaweza kumnunulia vifaa kama ubao wa kuchorea, rangi na vingine. Pia anaweza kumtafutia vitabu/vyanzo vingine vya maarifa vinavyohusiana na kipaji chake.

-kusema vitu chanya kwenye vipaji vya watoto. Mzazi anapaswa kusifia kazi ya mtoto na kutoa mapendekezo kwa ajili ya maboresho. Hii inajenga hisia chanya kwa mtoto kwani anaona ni kwa kiasi gani watu wa karibu yake wanamjali.

-kutoa taarifa kwenye mamlaka kuhusu kipaji cha mtoto wake. Wazazi/walezi wanapaswa kupeleka taarifa kwa walimu, au wadau wa serikali kuhusu vipaji ili kupata msaada wa kifedha, kimawazo na msaada mwingine wowote ambao unaweza kusaidia kipaji cha mtoto kukuzwa.

-kuweka urafiki na watoto na hivyo kurahisisha mawasiliano kati yao na watoto. Mzazi/mlezi anapokuwa mkali anatengeneza mazingira ya kuogopwa na watoto, hivyo mawasiliano kati yao yanakuwa magumu.

Wajibu wa jamii:- utamaduni haujengwi na mtu mmoja; ni kazi ya watu mbalimbali. Katika ujenzi wa utamaduni wa kujali vipaji, wadau kama walimu, wasanii wakubwa, vyombo vya habari, viongozi wa dini na siasa na taasisi mbalimbali wana mchango katika kufanikisha hili. Jamii ina wajibu wa:

-kutengeneza mtazamo chanya kuhusu elimu na vipaji. imejengeka kwenye jamii kwamba ili mtu afanikiwe basi aachane na vitu ambavyo ‘sio vya darasani’. Kwa hiyo unakuta mtoto ana kipaji cha muziki lakini anaonekana ‘mhuni’ na hivyo hapati msaada. Kipaji chake kinakufa. Jamii ibadilike katika hili.

-kutoa msaada: Kuna wazazi wanatamani sana vipaji vya watoto wao viendelezwe, lakini hawana uwezo. Hapa jamii inaweza kutoa msaada wa kifedha ili kuhakikisha kipaji cha mtoto husika kinastawi.

-jamii pia ina kazi ya kumtia moyo mtoto mwenye kipaji.



Wajibu wa serikali:- serikali ndiye mdau mkubwa katika kutengeneza utamaduni huu kwa kushirikiana na wazazi/walezi na jamii. Wajibu wa serikali ni pamoja na:

-kuanzisha vituo vya mafunzo kwa watu wenye vipaji mbalimbali ambavyo vinaweza kuambatana na mfumo rasmi wa shule, kama ilivyo kwa shule za ufundi. Vituo hivi vinaweza kujengwa kikanda ili kuepusha gharama za kujenga kuanzia ngazi ya kata.

-kuanzisha kampeni mbalimbali za kuhamasisha vipaji, ambazo zitaambatana na mashindano na utoaji wa tuzo na zawadi kwa washindi.

-kuanzisha madawati na vitengo mbalimbali mashuleni ambavyo vitapokea taarifa kutoka kwa wazazi na kuratibu mienendo ya watoto shuleni.

-kutoa ufadhili kwa watoto wenye vipaji mbalimbali. Wizara mbalimbali zitatakiwa kuweka fungu kwa ajili ya kuwafadhili watoto. Kwa mfano wizara ya utamaduni, Sanaa na michezo inaweza kuweka fungu kwa ajili ya watoto wenye vipaji vinavyohusiana na michezo na burudani.

-kutengeneza mazingira ya uhuru wa kujieleza. Uhuru wa kujieleza ni kichocheo kikubwa cha ubunifu. Kwa kulitambua hilo, serikali inatakiwa iendelee kutengeneza mazingira wezeshi ili tuweze kuchuma hazina ya vipaji na kuleta maendeleo kwa mtu mmoja mmoja na kwa taifa kwa ujumla.

Kwa ufupi, kuna makaburi mengi ya vipaji na ndoto ambayo yapo kwa watanzania wengi tunaoishi. Lakini hata hivyo bado hatujachelewa. Kama wazazi/walezi, jamii na serikali tukichukua hatua ya pamoja, tunaweza kupunguza tatizo la ajira na kujenga jamii iliyoendelea katika Nyanja zote.
 
Back
Top Bottom