TUENDAKO:Sitta aibu, JK fedheha | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

TUENDAKO:Sitta aibu, JK fedheha

Discussion in 'Celebrities Forum' started by Pdidy, Aug 5, 2009.

 1. Pdidy

  Pdidy JF-Expert Member

  #1
  Aug 5, 2009
  Joined: Nov 22, 2007
  Messages: 33,158
  Likes Received: 5,589
  Trophy Points: 280
  Sitta aibu, JK fedheha
  [​IMG]


  Absalom Kibanda

  [​IMG]
  WIKI iliyopita ilikuwa ni wiki ya Tanzania Daima. Kwa hakika ilikuwa ni wiki njema kwa wahariri na wafanyakazi wote tunaofanya kazi katika gazeti hili.
  Ilikuwa ni wiki njema kwa sababu, kama gazeti, tuliweza kutimiza ipasavyo jukumu letu la kihabari, kwa kuipasha jamii ya Watanzania kuhusu kuwapo kwa taarifa za kweli ambazo kwa hakika zinaonekana kuzigusa vilivyo taasisi kuu mbili za dola: Bunge na Serikali.
  Nikiwa Mhariri Mtendaji wa gazeti hili, ninaona fahari kubwa kuandika bayana kwamba habari na makala ambazo zimekuwa zikiandikwa na gazeti hili kwa wiki kadhaa sasa ‘zikifichua’ mwenendo binafsi wa viongozi wakuu wawili wa taasisi hizo, hatimaye ziliwagusa vilivyo vigogo hao hata kulazimika kuzitolea majibu.
  Ni jambo la bahati mbaya kwamba viongozi wote wawili walioguswa na taarifa sahihi zilizoandikwa na gazeti hili, Spika wa Bunge, Samuel Sitta, na Rais Jakaya Kikwete, walitoa majibu wakitumia hoja za kibabe, kebehi na wakati mwingine vitisho kwa sababu tu ya kutimiza malengo yao binafsi na ya kisiasa.
  Usahihi ninaouzungumzia katika habari na makala zilizoandikwa ambazo zote zimeonekana kuwasonga na kuwakera viongozi hao wawili, unatokana na ukweli kwamba ziliandikwa kutokana na kuwapo kwa taarifa zilizotolewa na mamlaka zenye dhamana au watu ambao kwa vyombo vya habari wanazo sifa zote za kuwa vyanzo sahihi vya habari (sources of news).
  Tukio la kwanza lilikuwa ni lile lililokuwa likimgusa Sitta; lilikuwa ni lile linalomhusisha na tuhuma za ufisadi unaogusa ofisi yake na wakati mwingine yeye binafsi.
  Habari ya mwisho, ambayo ilipewa uzito wa juu kabisa katika gazeti hili, iliyomgusa yeye ilichapishwa Alhamisi ya wiki iliyopita.
  Kabla ya kuandikwa kwa habari hiyo, mwandishi wa gazeti hili, ambaye alikuwa yuko bungeni mjini Dodoma, alifanya juhudi za kumfikia Sitta mwenyewe ili kusikia kile alichokuwa akikifahamu kuhusu waraka wenye tuhuma zake hizo ambao wakati huo ulikuwa umevujishwa katika mtandao wa intaneti kwa namna ileile ilivyoanza kwa sakata la EPA.
  Katika majibu yake, Sitta alimweleza mwandishi wetu huyo na wenzake aliokuwa ameongozana nao kuwa alikuwa amezisoma tuhuma hizo katika intaneti alizoziita za kipuuzi.
  Hakuishia hapo, alikwenda mbele zaidi na kuwaeleza waandishi hao kuwa nyuma ya waraka huo walikuwapo maadui zake ambao siku zote wamekuwa wakitaka kuona akiliongoza Bunge kilegelege akitumia maneno ‘Bunge Poa.’
  Siku moja baada ya Sitta kutoa matamshi hayo, ikiwa ni pamoja na yeye mwenyewe kukiri kuwa alikuwa amezisoma tuhuma hizo mtandaoni, Tanzania Daima liliandika taarifa hizo likieleza kile kilichomo katika waraka huo, sambamba na kurejea majibu rasmi yaliyotolewa na yeye mwenyewe (Tanzania Daima Toleo namba 1,700, Julai 30, 2009).
  Katika hali iliyonishangaza na kunishtua mimi binafsi, wakurugenzi, wafanyakazi na wasomaji wa Tanzania Daima, siku habari hizo zilipochapishwa, Spika Sitta akiwa katika kiti chake kikuu cha uspika alisimama na kuziponda taarifa hizo na akaenda mbele zaidi kwa kulituhumu gazeti hili kuwa miongoni mwa magazeti manne aliyosema yamekuwa yakitumiwa na maadui zake kwa malengo ya kumdhoofisha kisiasa.
  Kiongozi huyo wa Bunge ambaye hivi karibuni alisikika akiwaasa wanasiasa wenzake kuwa na ngozi ngumu wakati wanapotuhumiwa, alikwenda mbele zaidi na kumuomba Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kumuongezea ulinzi kutokana na kuhofia usalama wake.
  Nikiwa Mhariri Mtendaji wa gazeti hili, tamko hilo la Sitta alilolitoa huku akijua fika kwamba alikuwa akisema uongo wa wazi lilinishtua na kwa kiwango kikubwa lilininyima sana raha.
  Moja ya sababu iliyonifanya nikose raha ni ukweli kwamba Sitta alitoa maneno hayo ya kejeli na ya kutuvunjia heshima wakati akijua kuwa gazeti hili limekuwa likiandika taarifa nyingi kuhusu hatua mbalimbali anazochukua katika kupigania maendeleo ya taifa hili.
  Aidha, niliguswa na taarifa hizi baada ya kukumbuka kwamba wakati fulani mwaka jana kiongozi huyo alilazimika kuniomba radhi mimi binafsi kutokana na kupata kutoa matamshi dhidi ya gazeti hili baada ya kuandika taarifa ambazo hazikumfurahisha.
  Tatu nilikosa raha kwa sababu kejeli zake dhidi yetu zilikuja ikiwa ni zaidi ya wiki mbili tangu mtu mmoja ninayemheshimu alipofika ofisini kwangu na kunieleza kuwa alikuwa na ujumbe muhimu kutoka kwa Sitta au mtu wake wa karibu wa kujaribu kuniasa nizuie kuruhusu kuchapa taarifa zozote zinazomhusu kiongozi huyo.
  Mtu huyo alipofika alinieleza namna Sitta alivyokuwa akisononeshwa kwa kiwango kikubwa na taarifa mbalimbali zilizokuwa zikiandikwa na gazeti hili na kumhusisha na tuhuma za matumizi mabaya katika ofisi yake.
  Mjumbe huyo alikwenda mbele zaidi na kunieleza kuwa upande uliomtuma kuniletea taarifa hizo ulikuwa uko tayari kuona nikikutanishwa na kiongozi huyo wa Bunge ili kutafuta muafaka wa namna ya kusitisha kuandika habari zinazomhusu ambazo alinieleza bayana kwamba zilikuwa zinaweza kumharibia ubunge wake.
  Alipofika ofisini kwangu mtu huyo, nilimueleza bayana kwamba Sitta akiwa kiongozi aliyetangaza yeye mwenyewe kujitoa mhanga kupambana na vitendo vya ufisadi alikuwa akipaswa kuwa mfano bora wa matendo na maneno ili kuepuka hatari ya kuingia katika tuhuma za namna hii.
  Mbali ya hilo, nilimueleza mjumbe huyo kwamba nikiwa mhariri wa gazeti hili, nilikuwa nina kila sababu ya kuunga mkono jitihada zote zinazoongozwa na spika huyo katika kuhakikisha kuwa Bunge linajijengea heshima inayostahili katika kusimamia utendaji wa kazi za serikali kwa maslahi ya taifa.
  Hata hivyo, nilimsisitizia waziwazi kwamba Tanzania Daima haliwezi kamwe kuruhusu tabia iliyoanza kuonyeshwa na Spika Sitta na wanasiasa wenzake kadhaa wa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao sasa wamefikia hatua ya kuamua kuvitumia vita dhidi ya ufisadi kama kichaka cha kuficha tuhuma za ufisadi zinazoelekezwa kwao.
  Kwa sababu hiyo, nilimwambia mjumbe huyo wa kundi la Sitta kuwa akiwa kiongozi mwenye dhamana ya kuwatumikia wananchi kwa uaminifu, alikuwa akipaswa kuja na majibu sahihi kuhusu malipo ya dola 8,000 (zaidi ya shilingi milioni 10) ambazo inadaiwa kuwa zinalipwa na Bunge kumpangishia nyumba kwa mwezi.
  Katika hili nilimshauri amfikishie Sitta ujumbe kwamba Tanzania Daima lilikuwa likitaka kupata maelezo ya kina kutoka kwake na katika Ofisi ya Bunge kuhusu madai mengine kwamba alikuwa ameagiza gari jingine aina ya Mercedes Benz lenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 300.
  Mara baada ya kuachana na mjumbe huyo, kwa makusudi nilifanya mawasiliano na wana habari wenzangu walio karibu na Sitta na nikaenda mbele zaidi kwa kufanya mawasiliano na baadhi ya wanasiasa hususan wabunge, marafiki na maadui wa mwanasiasa huyo.
  Jambo la ajabu ni kwamba wabunge na wanasiasa wa CCM na hata wale wa upinzani, niliozungumza nao kuhusu masuala haya yanayohusu uadilifu binafsi wa spika Sitta, wote walionekana kukosa imani naye, japokuwa hakuna aliyeonyesha kuwa na jeuri ya kuanika kile wanachokijua.
  Katika hali ya kushangaza, baadhi ya wabunge niliozungumza nao nilipowauliza ni kwa nini basi walikuwa wameamua kulifumbia macho hili, wote hao, wakizungumza kwa lugha tofauti, walionyesha dhahiri kuhofia kumpinga hadharani, wakisema kufanya hivyo kungeweza kuwamaliza kisiasa kwani kiongozi huyo tayari alikuwa ameshajijengea uhalali mkubwa miongoni mwa wananchi kutokana na namna anavyoonekana kuliongoza Bunge katika kuchukia kwa dhati vitendo vya rushwa.
  Kwa kutambua hilo basi, sisi wa Tanzania Daima tukijua fika kwamba Sitta ni mmoja wa majabali waliojitoa mhanga kupambana na ufisadi hata kujijengea heshima ya pekee katika jamii, tuliamua kufanya kile ambacho vyombo vingine vya habari na wanasiasa wa pande zote wamekuwa wakikiogopa. Kumuonyesha Sitta kwamba hatumhofii yeyote, yeye akiwamo.
  Kwa makusudi na kwa nia safi kabisa, huku tukitambua kwamba tunao wajibu wa kuandika ukweli hata kama ukweli huo utakuwa mchungu kwa kiwango gani, tukakubaliana kujitoa mhanga kufichua tuhuma za wazi ambazo zimekuwa zikimkabili Spika Sitta.
  Tulifanya hivyo tukitambua kwamba, zaidi ya mwaka mmoja uliopita, gazeti hili ndilo lililokuwa mstari wa mbele kuandika tuhuma nyingine za namna hiyohiyo zilizokuwa zikielekezwa kwa Sitta ambazo baada ya kuziponda kwa kuziita ‘siasa za majitaka’ na kuagiza Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali kuzichunguza, hadi hivi leo ofisi yake imeamua kuatamia matokeo yake.
  Ni jambo la kusikitisha kwamba leo hii, Sitta, ambaye ni bingwa wa kuona vibanzi katika macho ya wenzake, anakuwa mkali kwelikweli wakati baadhi ya watu wenye nia njema au mbaya wanapomweleza wazi kuwa anayo boriti ndani ya jicho lake.
  Tukiachana na hilo la Sitta, wiki hiyohiyo ya jana, Tanzania Daima kwa ujasiri uleule wa kutomuonea haya yeyote, hasa katika masuala yanayohusu mustakabali wa taifa letu, tukamvaa jemedari wetu, na kiongozi tunayemheshimu kwa dhati, Rais Kikwete.
  Hili la Kikwete lilianza kwa habari iliyomkariri Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, ambaye Julai 11 mwaka huu alinukuliwa akimtaja Rais kuwa na mkono katika kuiruhusu kampuni ya kitapeli ya Richmond kushinda zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura hapa nchini.
  Kama ilivyokuwa kwa habari ile ya Sitta, kauli hiyo ya Lipumba, iliyotolewa katika mkutano wa hadhara jijini Mwanza, ama haikuripotiwa kabisa kwenye baadhi ya vyombo vya habari au ikafinyangwafinyangwa na kuliacha gazeti hili pekee likiipa uzito mkubwa na wa juu.
  Siku habari hiyo ilipochapishwa gazetini, Julai 13 mwaka huu, vituo vya redio na televisheni, ambavyo kwa kawaida husoma vichwa vyote vya habari vya magazeti ikiwa ni pamoja na kusoma kwa muhtasari habari kubwa, kwa hofu ya kuogopa ‘kumchafua’ Kikwete, vikagwaya kulisoma gazeti hili. Huku ni kupindua meza ya uhuru wa habari!
  Huku tukikumbuka wajibu wetu wa kusema kweli daima, wiki iliyopita, wakati Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu ilipotoa taarifa ya kukanusha habari yetu iliyokuwa ikimhusisha Kikwete na tamko la serikali kuhusu Richmond, gazeti hili likairejea tena kauli ile ya Lipumba kuhusu kuhusika kwa Kikwete katika sakata hilo zima.
  Kitendo cha gazeti hili kulirejea tamko hilo la Lipumba, kikaonekana dhahiri kuikera Ikulu na pengine Rais Kikwete mwenyewe na siku tatu tu baada ya kuandika hivyo, Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, akatoa tamko la kumsafisha Kikwete akionyesha dhahiri kulenga taarifa za gazeti hili na namna serikali ilivyokuwa ikikerwa na jinsi tamko la Lipumba lilivyokuzwa. Huo ukawa ushindi wa pili kwa Tanzania Daima.
  Kwa muhtasari tu, Luhanjo akatoa tamko akisema eti Kikwete hakuhusika katika mchakato mzima ulioipa ushindi kampuni ya Richmond.
  Katika hali inayodhihirisha wazi kwamba Ikulu ilifanya hivyo ikiepuka fedheha iliyokuwa ikimnyemelea Kikwete kwa kuhusishwa na uchafu wa Richmond kwa gharama za kukiuka hata misingi ya uwajibikaji wa pamoja ambao serikali inapaswa kuheshimu na kuutekeleza, Luhanjo akasema kiongozi huyo alihusika tu katika eneo moja la kuzuia kuidhinisha malipo kwa ajili ya kampuni hiyo.
  Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba kwa sababu hiyohiyo ya vyombo vya habari kuogopa kumfedhehesha rais kama wanavyohofia kumtia aibu Spika Sitta, vikaamua kulibeba juujuu tamko hilo la Ikulu, ilhali akili za kawaida kabisa zikithibitisha pasipo shaka kwamba, alihusika kwa namna moja au nyingine katika mchakato mzima ulioipa ushindi kampuni ya Richmond, hasa kama wanakiri kwamba alizuia malipo. Hiki ni kichekesho.
  Wakati ikulu ikifanya mzaha huu wa wazi, kumbukumbu zinaonyesha kuwa katika taarifa yake bungeni mwaka jana, Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza Richmond ilisema bayana kwamba Waziri wa Nishati na Madini alikuwa akiwasilisha katika vikao vya Baraza la Mawaziri, vilivyokuwa vikiongozwa na Rais Kikwete, taarifa za maendeleo ya mchakato mzima ambao hatimaye uliipa ushindi Richmond. Jitihada hizi za Ikulu kujaribu kumsafisha Kikwete hata katika masuala ambayo serikali ilipaswa kuwa imechukua hatua za tahadhari muda mrefu kabla Bunge halijaiadhibu, zinakuja wakati huu baadhi yetu tunapokumbuka namna Rais mwenyewe alivyolazimika (kwa matakwa yake au kwa ushauri wa akina Luhanjo) kuibadili hotuba aliyopanga kuitoa mjini Musoma, Siku ya Ukimwi Duniani, ikiwa na maneno mazito kuhusu na dhidi ya Richmond. Si vyema kuandika mengi pengine ni vyema tu kusema kwamba iko siku huko tuendako hulka za namna hii, za kina Kikwete na Sitta kujaribu kujitakasa hata katika matatizo ambayo wao wenyewe wamechangia kwa sababu tu ya kutaka kuficha aibu au fedheha, zitasababisha wapoteze nafasi zao katika jamii au heshima ambayo wanajaribu kujijengea leo wakitumia vibaya madaraka waliyonayo.
   
 2. S

  Silas A.K JF-Expert Member

  #2
  Aug 5, 2009
  Joined: Apr 23, 2008
  Messages: 807
  Likes Received: 16
  Trophy Points: 35
  Binafsi nafikiri hili suala la Richmond,Ikulu wameamua kulikuza. Ingekuwa busara wangeacha tu kauli ya Lipumba ipite kama upepo wa msimu na wao waendelee na mambo mengine nyeti yanayolikabili taifa.
   
 3. Gama

  Gama JF-Expert Member

  #3
  Oct 17, 2011
  Joined: Jan 9, 2010
  Messages: 9,224
  Likes Received: 1,411
  Trophy Points: 280
  666666666666666666666666666
   
Loading...