Trilioni za makinikia pasua kichwa

saidoo25

JF-Expert Member
Jul 4, 2022
602
1,407
Mwanza. Swali la Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina limewasha upya moto wa ahadi ya malipo ya mabilioni ya shilingi kutokana na malimbikizo ya kodi kutoka kampuni ya Barrick Gold.

Maswali ya waziri huyo wa zamani wa mifugo na uvuvi bungeni, yameibua mjadala uliolenga kupata majibu ya Serikali iwapo fedha za makinikia zililipwa, huku wengine wakipendekeza suluhisho la kudumu la suala hilo.

Katika swali la msingi alilouliza bungeni wiki iliyopita, Mpina alihoji kwa nini kesi 1,067 za kodi zenye thamani ya Sh360 trilioni na Dola za Marekani 181.4 milioni hazijaamuliwa hadi sasa.

Na katika swali lake la nyongeza, mbunge huyo alihoji kwa nini Serikali ilikubali kupokea malipo ya Sh700 bilioni kutokana na kesi ya malimbikizo ya kodi ya makinikia, badala ya malipo halali ya Sh360 trilioni.

Licha ya maswali hayo kujibiwa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Hassan Chande akisaidiwa na waziri wake, Dk Mwigulu Nchemba, majibu yao hayakumridhisha Mpina, aliyeungwa mkono na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson.

Kutokana na hilo, Spika Ackson aliiagiza Serikali kupeleka bungeni majibu mapya kulingana na swali lenyewe.

Hata hivyo, akizungumza jana na gazeti hili, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba alisema kama ambavyo makubaliano yalikuwa ya kulipa Dola milioni 100 mwaka wa kwanza na nyingine baadaye wamekuwa wakilipa. “Mwaka wa kwanza (Barrick) walilipa dola milioni 100.”

“Katika miaka mitano mingine, wakakubaliana kuwa wanalipa dola milioni 40 kila mwaka, wamekuwa wanalipa kila mwaka,” alisema.

Katibu mkuu huyo alisema, “lakini kuna mambo mengi ambayo walijadiliana wakati ule, CSR (uwajibikaji wa kampuni kwa jamii) fedha zinaendelea kutolewa, ujenzi wa barabara zinaendelea kutolewa na kuna vitu vingi vilijadiliwa wakati ule ambavyo utekelezaji wake unaendelea, ikiwemo Serikali kupewa hisa asilimia 16.”

Oktoba 19, 2017, Barrick ilikubali kuwa italipa dola 300 milioni (Sh660 bilioni) kwa ajili ya kuonyesha uaminifu. Kampuni hiyo ilifikia uamuzi huo baada ya majadiliano baina yake na Serikali.

Sakata hilo lilianza wakati Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli alipopiga marufuku usafirishwaji wa mchanga wa madini nje ya nchi kwa ajili ya kuchenjua kupata madini ya aina mbalimbali.

Baadaye, Rais aliunda kamati iliyochunguza biashara ya madini na kutoka na matokeo yalionyesha udhaifu katika sheria, mikataba na utendaji wa watumishi wa Serikali uliosababisha nchi kutonufaika na rasilimali hizo.

Kamati hiyo pia ilibaini kampuni ya Acacia ilikuwa ikifanya kazi bila usajili rasmi na baadaye Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ikabaini kuwa kampuni hiyo haikulipa kodi iliyofikia dola 190 bilioni za Marekani ikichanganywa na riba.

Vilevile, ripoti ya Tume ya kuchunguza makinikia, iliyoongozwa na Profesa Abdulkarim Mruma ilibainisha kuwa Tanzania ilipoteza takriban Sh188 trilioni (dola bilioni 84 za Marekani) katika kipindi cha miaka 19 kati ya mwaka 1998 na mwaka 2017 kupitia usafirishaji wa makinikia ya dhahabu na shaba.

Februari 20, 2019, baada ya majadiliano baina ya Rais Magufuli na ofisa mwendeshaji mkuu wa Barrick anayeshughulikia Afrika Mashariki na Kati, Dk Willem Jacob, umma ulielezwa kampuni hiyo ilikubali kulipa mabilioni hayo.

Hata hivyo, hakukuwa na taarifa za mara kwa mara kuhusu kinachoendelea kuhusu malipo hayo hadi Mpina alipoibua tena suala hilo bungeni.



Wachumi, wanasheria

Kufuatia hali hiyo, wachumi, wanasheria na wanasiasa waliozungumza na Mwananchi wametaja usiri katika mikataba ya madini, ukosefu wa uongozi, utashi wa kisiasa na utawala bora kuwa kiini cha matatizo hayo.

“Kinachotangulia katika uvunaji na matumizi ya rasilimali ya Taifa kuanzia madini, misitu, wanyamapori, ardhi na hata maji ni kuwa na uongozi bora unaopatikana kwa Taifa kuwa na katiba bora; hili ndilo tatizo letu, ni moja ya mambo yanayofanya Katiba mpya kuwa jambo muhimu na la lazima,” alisema Wakili Method Kimomogoro.

Alisema licha ya kuunda taasisi imara na huru, Katiba hiyo itaweka masharti ya kulinda rasilimali za Taifa.

“Wenzetu Ghana katiba yao imeweka masharti ya mikataba yote ya uvunaji wa rasilimali zote za Taifa kupelekwa bungeni. Lakini hapa kwetu mikataba hiyo ni siri kati ya Serikali na wawekezaji,” alisema.

Kwa upande wake, Profesa Haji Semboja, mhadhiri wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema muda umefika wa kufanya mabadiliko ya kisheria katika umiliki, ulinzi, uvunaji na biashara zote zinazohusisha rasilimali za Taifa.

“Siku zote natofautiana na wengi kuhusu sheria zetu katika umiliki, kuongoza na kuendesha taasisi na makampuni yanayovuna rasilimali za Taifa kwa sababu tunajielekeza kwenye faida ndogo ya kodi, ushuru, tozo na ajira huku wawekezaji ambao wengi ni wa kigeni wakichukua faida yote,” alisema.

“Tubadilishe sheria na mfumo wa uvunaji wa rasilimali za Taifa kuwezesha umma kumiliki, kuvuna na kuendesha shughuli zote zinazogusa rasilimali zetu bila kugombana na wawekezaji waliopo.

Kufanya hivyo, alisema kutalihakikishia Taifa mapato na faida zaidi, kuimarisha uchumi ili kuongeza mzunguko wa fedha.



Tulisema sana jambo hili

Akizungumzia mjadala uliobuka kuhusu fedha za makinikia, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu alisisitiza hoja zake alizozitoa bungeni wakati wa mjadala wa taarifa za kamati mbili za Profesa Mruma na Profesa Osoro.

Akitumia video ya mchango wake bungeni wa Juni 13, 2017, Lissu alisema “nilishatoa miaka mitano iliyopita. Watu hawakutaka kuangalia facts (hoja), kwa sababu walikuwa wanaogopa consequences (matokeo yake). Walikuwa tayari kufarijiwa na uongo kuliko kuumizwa na ukweli.”

Mwanasiasa huyo anayeishi uhamishoni nchini Ubelgiji alisema tatizo linaloitafuna nchi katika sekta ya madini kuanzia kwenye mikataba ni ubovu wa sheria ya madini, kodi na uwekezaji ambayo alisema lazima irekebishwe iwapo kuna nia na utashi wa kushughulikia matatizo ya sekta hiyo.

Alisema Serikali imeunda tume na kamati mbalimbali kuchunguza na kasoro za sekta ya madini, lakini mapendekezo ya kamati na tume hizo hayajafanyiwa kazi.

Baadhi ya tume na kamati hizo ni ya Jenerali Robert Mboma (2002), Dk Jonas Kipokola (2004), Dk Enos Bukuku (2005), Lawrence Masha (2006), Jaji Mark Bomani (2008) pamoja na kamati za Profesa Mruma na Profesa Osoro za 2017.

Hata hivyo, Dk Mutahyoba Baisi alisema japo hajafuatilia kwa karibu mjadala uliobuka kutokana na maswali yaMpina, anaamini fedha hizo zikilipwa na kuingizwa kwenye mzunguko kwa njia yoyote ile, ikiwemo utekelezaji wa miradi na shughuli nyingine za Serikali zitaleta matokeo makubwa na chanya kwenye uchumi wa Taifa.

“Siwezi kuzungumzia hili kwa undani zaidi kwa sababu hadi sasa sifahamu kama zimelipwa au la; ingawa pia nina wasiwasi kama zitalipwa,” alisema Dk Baisi ambaye ni mchumi na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Nyongeza na Bakari Kiango


SOURCE MWANANCHI: THURSDAY SEPTEMBER 28 2022
 

Attachments

  • Fdt7SuAXEAIhav4.jpg
    Fdt7SuAXEAIhav4.jpg
    98.2 KB · Views: 3
Back
Top Bottom