Karamagi aitosa serikali
2008-07-09 09:21:44
Na Jackson Kalindimya, Dodoma
Uamuzi wa kuongeza muda wa mkataba wa Kampuni ya Tanzania International Container Terminal Services (TICTS) kwa miaka 15 zaidi kufanya kazi ya kupakua mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam, ulifanywa na Baraza la Mawaziri, Bunge limeelezwa.
Spika wa Bunge, Bw. Samuel Sitta, amekiambia kikao cha Bunge kinachoendelea mjini hapa jana, kuwa amepokea ushahidi toka serikalini unaothibitisha kwamba uamuzi wa kuongeza muda wa mkataba wa TICTS ulifuata taratibu za maamuzi ya serikali.
Bw. Sitta aliliambia Bunge kuwa Bw. Nazir Karamagi, aliwasilisha barua yenye kumbukumbu na TYC/A/400/386 ya Oktoba 25, 2005 iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bw. Peniel Lyimo kwenda kwa Ofisa Mtendaji wa TICTS, ambayo pamoja na mambo mengine ilithibitisha kuwa, serikali ilikubali kuongeza muda wa kufanya kazi kwa miaka 15 hadi mwaka 2025.
Alisema pamoja na barua hiyo, Ofisi ya Spika pia ilipokea barua nyingine ya Juni 18, mwaka 2008 kutoka kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Bw. Gray Mgonja, yenye kichwa cha habari `Ushahidi wa kuwa Mkataba wa TICTS ulijadiliwa na Baraza la Mawaziri`.
Barua hiyo inanukuliwa kuandikwa ``Naandika kuthibitisha kwamba, uamuzi wa kuongeza muda wa mkataba wa kampuni ya TICTS ulifuata taratibu za maamuzi Serikali``.
Bw. Sitta aliliambia Bunge kuwa, baada ya kutafakari maudhui ya maelezo yaliyomo kwenye barua hizo mbili, ameridhika kwamba ushahidi uliotolewa na Bw. Karamagi umekidhi matakwa na masharti ya Kanuni ya 63(6) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, toleo la 2007 yaliyomtaka kuthibitisha ukweli wa maelezo yake aliyoyatoa Bungeni kwa kiwango cha kuliridhisha Bunge.
Ufafanuzi huo unamnusuru Mbunge wa Bukoba Vijijini (CCM) Bw. Karamagi, kuchukuliwa hatua kwa kuzingatia kanuni kuhusiana na kulidanganya Bunge kufuatia matamshi aliyoyatoa Aprili 25, mwaka huu, wakati akichangia hoja binafsi ya Bw. Geofrey Zambi, kuhusu utendaji usioridhisha wa kampuni ya TICTS ambapo alidai kuwa mkataba wa kampuni hiyo uliokuwa wa miaka 10 uliongezwa muda wake kwa miaka 15 zaidi kabla ya kuisha kwa muda wake na Baraza la Mawaziri.
Kufuatia matamshi hayo, Mbunge Anna Abdallah (CCM- Viti Maalum), aliomba mwongozo wa Spika kwa kuzingatia kanuni ya 68(7) kumtaka Bw. Karamagi taarifa aliyozungumza kama kweli iliamuliwa na Baraza la Mawaziri.
Spika Sitta alimtaka Mbunge Karamagi aseme na kudhihirisha kama ana ushahidi wa Baraza la Mawaziri vingineyo arekebishe taarifa yake.
Bw. Karamagi alikataa kufuta usemi wake na kuliambia Bunge kuwa ana ushahidi wa waraka toka Baraza la Mawaziri alioupata wakati yakifanyika majadiliano na Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC).
Spika Sitta, alimpa muda wa siku moja awasilishe ushahidi huo ambao hadi muda aliopewa ulipofika hakuwa amewasilisha na badala yake, akaongezewa muda wa wiki moja zaidi ili awasilishe ushahidi na hatimaye akafanya hivyo.