THE OTHER HALF
EPISODE 1
Kwa miaka kadhaa hakuna aliyeamini kuwa itatokea. Hata dalili zote zilipoonyesha kwamba iko karibu kutokea, watu walipuuza na kuendelea na mambo mengine kana kwamba hawauoni uhalisia. Kila mtu akiamini haitotokea.
Ndio sababu baada ya kutokea, kitu ambacho kilikuwa kimeonyesha dalili ya kutokea miaka mingi, kiliathiri kila mtu na kila nukta ya pembe ya Dunia.
Mwaka 2038: Nachingwea, Lindi
Ilikuwa tayari inakaribia saa tisa na nusu alasiri, kikosi cha wataalamu wa masuala ya vinasaba, bailojia na mtaalamu mmoja wa akiolojia walikuwa wanajitahidi wamalize zoezi la ukusanyaji sampuli katika Anabelle mpya iliyotokea takribani wiki mbili zilizopita.
Kama ilivyo katika Anabelle nyinginezo, joto lilikuwa juu kiasi cha sentigredi 30 za selsiasi, kimya kilikuwa ni kikubwa kana kwamba mji wote haukuwa na kiumbe hata kimoja chenye kujongea. Sauti pekee iliyokuwa inasikika ilikuwa ni sauti ya upepe uliokuwa unavuma kwa sauti kama ya mluzi hafifu masikioni na kutimua vumbi lililofunika lami na majengo.
Majengo yote yalikuwa na muonekano mkuu kuu kana kwamba labda mji huo haujakaliwa na binadamu kwa karne kadhaa, na vumbi lilikuwa limetuama kwenye majengo na hata barabara kiasi kwamba lami ilikuwa haionekani. Vumbi hili lilikuwa jingi kiasi kwamba, ukikanyaga chini kwenye barabara ukiinua mguu unaacha alama ya kiatu chako kwa ufasaha mkubwa kabisa.
Jambo la ajabu ni kwamba, japokuwa kulikuwa na uchakavu wote huu na vumbi lote hili linalotoa hisia kuwa labda mji umetekelezwa kwa karne nyingi, ukweli ni kwamba mji huu wiki mbili tu zilizopita ilikuwa na wakazi wapatao laki moja unusu na uliitwa Nachingwea kwa miaka yote nyuma.
Eneo hili la mji wa Nachingwea kwa sasa ulipewa jina la Anabelle 23 likimaanisha kwamba, eneo hili lilikuwa ni mji wa 23 duniani katika mfululizo wa kuchukuliwa kwa miji katika mazingira yenye utata na aina mpya ya viumbe wasiojulikana na kisha kupotea kwa wakazi wote, yaani population nzima iliyokuwamo kwenye miji hiyo inapotea kusikljulikana.
Timu hii ya wataalamu ilikuwa imebakiza nusu saa tu kwa siku ya leo kukusanya sampuli kabla ya kufika saa kumi jioni muda ambao wakazi wapya wa Anabelle 23 walikuwa 'wanaamka'.
Wataalamu hawa wote walikuwa wamevalia nguo za 'overall' rangi nyeupe na usoni wakiwa wamefunika nyuso kwa vizuizi vya gesi (gas mask) kwa tahadhari ya kujikinga na uwezekano wa vimelea hatarishi ndani ya mji huu.
Timu hii ya watu watano ilikuwa inaundwa na mtaalamu wa vinasaba Shafii Mwaisela kutoka kituo cha Utafiti cha Ifakara (Ifakara Medical Research Institute), Magdalena Odinga mtaalamu wa kemikali ya kibaiolojia (biochemist) kutoka chuo kikuu cha Kenyatta nchini kenya, Goodluck Hokororo mtaalamu wa masuala ya forensic kutoka makao makuu ya jeshi la polisi, mwanamama Dr. Cindy Wheaton mtaalamu wa akiolojia kutoka chuo kikuu cha Stanford nchini Marekani na Salim Kawambwa mchambuzi wa intelejensia za mashambulio ya kibaolojia kutoka Idara ya Usalama wa Taifa ya Tanzania.
Kwa dakika hizi chache zilizokuwa zimebakia walikuwa wanamalizia kwa haraka kuokota vipande vidogo vidogo vya sampuli mbali mbali na kuziweka kwenye vifuko vidogo vya plastiki ili waweze kuvifanyia uchunguzi baadae.
"Dakika kumi na tano... Muda wa kuondoka.!" Salim Kawambwa afisa wa TISS ambaye ndiye kiongozi wa timu hii akawajulisha wenzake.
Kabla ya saa kumi kamili walikuwa wanatakiwa wawe walau kilomita kumi na tano kutoka eneo la Anabelle kwa sababu za kiusalama. Japokuwa kwa muda huu kabla ya kutimia saa kumi jioni, mji mzima ulikuwa umezizima kwa ukimya wa kutisha lakini mara tu ikitimia saa kumi, viumbe vilivyouteka na kuubadili mji huu 'wanaamka'.
Baada ya Salim kutoa amri hii wote wakaweka sampuli zao kwenye vihifadhi kama brieface na kupanda kwenye gari waliyopaki pembezoni kabisa linapoishia eneo la Anabelle na kuondoka.
Wakaendesha gari kama mwendo wa kama dakika kumi na mbili hivi mpaka eneo la karibu na msitu wa Namala, takribani kilo mita kumi na tano kutoka Anabelle 23.
Hapa walikuwa wameweka kambi ya muda ya mahema.
Pamoja nao mahali hapa kulikuwa na kikosi maalumu cha kijeshi ambacho kiliundwa mahususi na Amiri jeshi mkuu kwa ajili ya zoezi hili. Kikosi hiki kilipewa jina la Team 5C na kilikuwa na wanajeshi kumi na tano wa weledi wa hali ya juu.
Baada ya kufika na wote kubadili nguo za kazi na kuvaa nguo za kawaida, wataalamu wote watano wakakusanyika kwenye hema la Salim, afisa kutoka Usalama Wa Taifa.
"Kuna yeyote ana la kitushirikisha wengine?" Salim akafungua maongezi baada ya wote kuketi.
"Vile tungekuwa labda tunajua nini tunatafuta.. Labda ningekuwa na cha kuongea.. Lakini tumekuwa hapa kwa siku mbili na sijui nini au niangalie wapi.. Niko nafuata maelekezo tu.!" Magdalena Odinga akaongea kwa lafudhi yake ya kikenya.
"Naunga mkono hoja.!" Goodluck na Shafii wakajikuta wameongea kwa pamoja.
Salim akageuka kumuangalia Dr. Cindy Wheaton..
"Cindy.. Sote hapa tunafahamu kuhusu matukio yanayoendelea duniani kote kuhusu wakazi wa miji mbali mbali, population nzima kupotea katika mazingira ya kutatanisha… lakini lazima ufahamu kuwa baada ya tukio hili kutokea, nchi yetu imeunda hii timu kwa dharura, kwahiyo wengi hapa hawafahamu kiundani kuhusu hili suala.. Kwa faida ya wenzangu labda ungetupa maelezo ya kina ambacho wenzetu mmekifahamu mpaka sasa.!" Salim akaongea huku anamtazama Dr. Cindy Wheaton.
"Nadhani tulikubaliana kuchukua sampuli tu na tukirudi makao makuu ndio tupeane maelezo.!" Cindy akajibu akiwa ameshangaa kidogo.
"Cindy tumebakiza siku moja tu ya kesho.. Huwezi jua kama ukitupatia mwanga walau kidogo inaweza kusaidia vipi kwenye kukusanya sampuli kesho.!"Magdalena akadakia haraka haraka.
" Tupe japo kwa muhtasari tu.. Nini kinaendelea?? Hili suala limefikia vipi hapa?" Salim akaendelea kusisitiza.
Cindy akavuta pumzi ndefu ndani na kushusha…
"OK..!" Akaongea huku anainuka.
Baada ya kuinuka, akageza laptop yake kuelekea upande mmoja wa hema na kuwasha projector kisha akaanza kuongea.
"Chanzo cha haya yote kinatupeleka kwenye nchi ya Maldives mwezi May mwaka……"
"Oohh sorry nadhani wote tunajua hiyo stori, unaweza kutueleza vitu vya kitaalamu ambavyo hatuvijui maana hilo ndilo swali letu.?" Magdalena akamkatisha Dr. Cindy kabla hajamaliza alichokuwa anakiongea.
"Magdalena tafadhali kuwa mtulivu.. Acha Cindy aongee" Salim akaongea kwa busara na utulivu kutuliza mukali zilizoanza kuinuka.
Dr. Cindy akamkata Magdalena jicho la hasira na kukereka, kisha akaendelea tena kuongea huku akitumia picha kwenye projector zilizokuwa zinarushwa kwenye 'ukuta' wa hema.
"OK! Nilikuwa nasema kwamba chanzo kabisa cha hizi Anabelle kinatupeleka mpaka kwenye nchi ya Maldives mwaka juzi mwezi May.. Kwa kuwa mnasema mnafahamu historia hii kwahiyo sitazama ndani sana nitaenda moja kwa moja kwenye masuala ya kitaalamu.." Akanyamaza kidogo na kuwaangalia.
"Eleza kila kitu tafadhali.. Tunaweza kupata kitu kingine kipya.!" Salim akaongea tena kwa hekima.
"OK asante! Mwezi May mwaka juzi 2037, nchi Maldives.. Kama ambavyo wote tunafahamu kuwa Maldives ni kanchi kadogo kenye visiwa vidogo vidogo vipatavyo elfu moja mia moja tisini na mbili katika bahari ya Hindi kusini mwa bara la Asia.. Mwaka juzi 2037 mwezi huo May, wavuvi wawili alfajiri wakiwa kwenye shughuli zao wakiwa wanatoa nyavu walizotega, wakakuta samaki wengi tu, lakini pamoja na hao samaki kulikuwa na chupa ya rangi ya kahawia ambayo ilikuwa juu mdomoni imezibwa na kipande cha mti cha mviringo na ndani yale kulikuwa na kipande cha karatasi.. Sasa nadhani wote hapa mnafahamu Meldives ni nchi yenye tamaduni gani?"
Cindy akauliza huku anawaangalia kuona ni nani labda anajua kile alichouliza.
"Ni moja ya nchi chache ambazo serikali yake inatambua masuala ya kiroho na uchawi." Shafii akamjibu.
"Kabisa.. Kwahiyo kutokana na mazingira ya kupatikana hii chupa baharini na wavuvi, ikabidi ipelekwe kwa Gavana wa jimbo.. Kumbuka nimesema hapo Maldives kuna visiwa vidogo vidogo vipatavyo elfu moja mia moja tisini na mbili. Hivi visiwa vimegawanywa kwenye mafungu ishirini na sita na kila fungu moja linahesabika kuwa ni jimbo na linaongozwa na Gavana.. Sasa baada ya chupa hii kufikishwa kwa Gavana na wazee wa kimila wa Maldives kuitwa, ikaamuliwa kuwa ifunguliwe.. Kwa taarifa ambazo wenyewe watu wa Maldives wametupatia... Inasemekana kwamba, walipoifungua tu hii chupa ulitoka moshi na karatasi ya ndani ikawa kama inaungua.. Ndipo hapo wale wazee wa mila wakaamuru chupa ifungwe kuzuia moshi zaidi usitoke.."
Cindy akanyamaza kidogo, kisha akawaangalia. Akabadili badili picha kwenye projector ukutani mpaka zilipofika picha alizokuwa anazitaka. Kisha akaendelea na maelezo.
"Mwezi mmoja baadae ndipo masahibu yakaanza.. Akina mama wote wajawazito katika visiwa vya Maldives watoto walikuwa wanajifungua walikuwa wanatoka mwili nzima wana manyoya kama paka.! Yaani wanakuwa ni vitoto vichanga binadamu kabisa lakini mwili mzima unakuwa imefunikwa naanyoya ya paka.! Jambo la ajabu zaidi likaja, ilikuwa ikifika siku ya saba tu wale watoto wanapotea hawaonekani tena.. Yani huyu mama mzazi, siku ya saba akiamka asubuhi yule mtoto wake mchanga mwenye manyoya kama paka anakuwa hayupo.!"
Cindy akanyamaza tena kuwatazama. Akaona jinsi walivyosisimuka na wote wakimsikiliza kwa umakini mkubwa. Akaendelea..
"Sasa baada ya tatizo kuwa kubwa sana.. Maana kwa mwezi mmoja tu wa May walizaliwa watoto zaidi ya elfu tano wakiwa na manyoya na wote hao wakapotea.. Na mwezi wa pili vivyo hivyo.. Kwa hiyo serikali yetu ya Marekani ikaingilia kati maana tulikuwa na wasi wasi hili tatizo linaweza kuenea sehemu nyingine mbali mbali duniani.. Kwahiyo serikali ikatuma timu ya wataalamu kwenda Maldives kuchukua sampuli za damu za wakazi wake pamoja na ile chupa iliyookotwa na wavuvi.. Sampuli za damu zilivyoletwa Marekani na kufanyiwa uchunguzi tuligundua kitu cha ajabu sana.!"
Cindy akanyamaza tena kidogo na kuwaangalia.
"Mligundua nini?" Goodluck akauliza kwa shauku.
"Idadi kubwa ya wanawake wa Maldives walikuwa wameambukizwa moja ya kirusi adimu na ambacho akijaonekana juu ya uso wa Dunia kwa maelfu ya miaka, Mollivirus Sibericum.!"
Akawaangalia jinsi ambavyo wote walishtuka kwa mshangao juu ya taarifa hii.
Akaendelea tena.
"Nadhani wote hapa tunafahamu HERVs, Human Endogenous Viruses.. Aina ya virusi ambavyo tunaamini kuwa walikuwepo maelfu ya miaka iliyopita na kuwaathiri mababu zetu na kusababisha kuacha sampuli zao za ribonucleic acid (RNA) katika DNA zetu binadamu mpaka Leo hii.. Sasa huyu kirusi
Mollivirus Siberium ambaye tulimgundua kwenye sampuli za damu za wakazi wa Maldives, ni moja wapo ya hao virusi aina ya HERVs na hii ni mara ya kwanza ndani ya miaka elfu thelathini anaonekana tena juu ya uso wa Dunia.. Najua ni ngumu kuamin! Hata sisi siku ya kwanza tulipigwa na bumbuwazi kama ninyi hivi Leo!"
Akanyamaza tena na kutoa tabasamu ambalo walikuwa la utani.
"Mlichukua hatua gani?" Salim akauliza.
"Serikali ikatoa kandarasi kwa kampuzi ya madawa ya CORBO BioTech itengeneze haraka iwezekanavyo chanjo ya kukidhibiti kirusi hicho kisiendelee na kisilete madhara zaidi. Na ndani ya mwezi mmoja CORBO walikuwa wamefanikiwa kupata chanjo na ikaenda kutolewa kwa raia wote Maldives.. Baada ya chanjo kutolewa.. Ile hali ya watoto kuzaliwa na manyoya ya paka ikaisha na maisha yakaendelea kama kawaida.. Lakini ilipofika mwaka jana mwezi june kila mama ambaye mototo wake mwenye manyoya ya paka alipotea mwaka juzi, mtoto huyo alirudi katika mazingira ambayo ni ya utatanishi kama walivyopotea mwaka juzi.. Jambo la ajabu ni kwamba watoto hawa japo walikuwa na umri wa mwaka mmoja lakini walikuwa wana uwezo wa kuongea!! Na walikuwa wanaongea sentesi mbili tu, ya kwanza,
"Mama usiogope, nilienda safari!", na sentesi ya pili walikuwa wanauliza
, "Mama kwanini umeua ndugu zetu?"
Cindy akanyamaza tena kidogo. Maelezo haya yalikuwa yanawafanya Salim na wenzake wasisimke mpaka vinyweleo vinasimama.
Cindy akaendelea kutoa maelezo.
"Kwa kadiri ya tafiti zetu tunadhani kwamba hili swali la pili 'mama kwanini umeua ndugu zetu?' lilikuwa na maana ya chanjo iliyofanyika nchini Maldives na kusababisha wasizaliwe tena watoto wenye manyoya.. Ndio hii tunadhania wale watoto walikuwa wanasema ndugu zao wameuwawa.!"
Cindy akameza mate kidogo, kisha akaendelea.
"Sasa wiki moja, yaani siku saba baada ya wale watoto kurudi ndipo likatokea tukio la kwanza la mji wa kwanza kuchukuliwa.. Ndipo ilipotokea Anabelle 01.. Siku hii ya saba, kulipokucha asubuhi, population yote ya wakazi wa Maldives walikuwa wamepotea wote hawajulikani walikoenda.. Ndani ya siku moja tu kulipokucha mji mzima ulikuwa umebadilika.. Miji ulikuwa umechakaa na vumbi kila mahali kana kwamba kwa karne kadhaa hakuna binadamu aliyeishi hapo.. Mji wote ulikuwa na ukimya uliotisha.! Ndipo hapa tukafanya kosa la kwanza tukapeleka timu ya wataalamu ndani ya Anabelle 01.. Na kosa kubwa walilolifanya ni kuingia ndani za zile nyumba na majengo.. Hakuna yeyote aliyetoka mpaka leo.. Tukapeleka timu nyingine, hawa wakaepuka kuingia ndani ya majengo.. Wakawa wanakusanya sampuli tu na uchunguzi mwingine lakini ilipotimia saa kumi jioni wakiwa ndani ya Anabelle 01 wote wakapotea na mpaka leo hawajarudi.. Kwa hiyo tukajifunza mambo mawili hapo.. Kwanza ukiwa ndani ya Anabelle, hutakiwi kuingia ndani ya Jengo lolote, na pili usikae ndani ya Anabelle mpaka kufikia saa kumi jioni.!"
"Kitu gani kingine mme jifunza?" Shafii akauliza kwa udadisi.
"Tumejifunza pia dalili za mji kabla ya kuchukuliwa!" Cindy akajibu kwa mkato.
"Inakuwaje?" Shafii akauliza tena.
"Linapita tetemeko dogo la ardhi lisilo maadhara yoyote na likiisha pita tetemeko masaa sita baadae mji unatwaliwa na hao viumbe.. Pia baada ya tetemeko, mwisho kabisa mwa mji kunatokea ufa wenye upana kama wa kama hatua moja, hii ni alama ya mpaka wa Anabelle na Dunia iliyobaki.!" Cindy akaeleza.
"Vipi kuhusu ile chupa iliyookotwa na wavuvi mliyoichukua na kuipeleka Marekani?" Magdalena akamuuliza Cindy.
"Tunaamini kuwa kile kirusi kilichosababisha watoto wazaliwe na manyoya kilitoka kwenye chupa hii, kwasababu baada ya kuipima maabara tumeikuta ina kiwango kikubwa sana wa hao virusi wa Mollivirus Sibericum..!" Cindy akajibu tena kwa ufupi.
"Na ile karatasi?" Magdalena akauliza tena.
"Sorry??"
"Namaanisha ile karatasi ambayo ilikiwa ndani ya chupa na ilipofunguliwa kwa mara ya kwanza moshi ukatoka na karatasi kuungua!"
"Oooh! Tuliitoa kwa vizuri tu.. Uzuri iliungua lakini bado ilikuwa imeshikana.. Ni kama ukichoma moto gazeti au karatasi ngumu alafu ikibaki imeshikana, unaweza bado hata kusoma kilichoandikwa.. Ndivyo ilivyokuwa kwenye hii karatasi.. Tuliitoa kwa uzuri tu na kunakili pembeni kilichoandikwa.. Kilikuwa kimeandikwa kilatini, lakini ni kilatini kikongwe mno kiasi kwamba mpaka sasa hatujapata tafsiri sahihi.. Ni sentesi moja tu ndio timefanikiwa kuitafsiri kwa usahihi kabisa.!"
"Sentesi gani?" Salim na Magdalena wakajikuta wameuliza kwa pamoja kwa shauku.
"Kichwa chake cha habari.. Kimeandikwa
'Novus Ordo Sedorum'."
"Novus Ordo Sedorum?? Ina maana gani?" Salim akauliza.
"Novus Ordo Sedorum, ikimaanisha
'The New Order Of Ages'." Cindy akajibu huku amewakazia macho.
"The New Order Of Ages!" Salim akajikuta ameorudia sentesi kuitamka kwa mshangao.
"Kwa hiyo hizo nilizowaeleza ndivyo vitendawili vilivyopo mbele yetu tunavyopaswa kuvitegua.. Kwa namna miji inavyochukuliwa, tunakadiria kwamba kama hali itaendelea hivi basi mpaka kufikia miaka mitatu ijayo, yaani mwaka 2041 dunia yote itakuwa imechukuliwa.. Na huo unaweza ukawa mwisho wa binadamu juu ya uso wa Dunia maana hatujui mpaka sasa miji ikishachukuliwa ni nini kinachoendelea huko ndani.!?" Cindy akaongea kwa kumaanisha huku anaweka sawa laptop yake na kuzima projector.
Kwa dakika kadhaa hakuna ambaye aliweza kuongea. Kila mmoja alikuwa amezama kwenye mawazo akitafakari haya maelezo yote aliyoyasikia hapa. Hakika vitendawili vilivyopo mbele yao vilikuwa vinaonekana havina majawabu, lakini walipaswa wapate majawabu, na kazi iliyokuwepo mbele yao ilikuwa ni nzito lakini pia walipaswa kuubeba mzigo huo mabegani mwao.
Wakiwa bado wanaendelea kutafakari, Mara simu ya Salim, ikaita.
"Hallo Mkuu…nakusikia Mkuu…ndio, sawa Mkuu.. Aisee.. Mmehakiki lakini? Aisee… sawa Mkuu.. Sawa.. Nashukuru kwa taarifa Mkuu! Asante!" Kisha akakata simu.
Baada tu ya kukata simu sura yake ilikuwa inasema kila kitu bila kuongea chochote kile. Uso wa Salim ulikuwa umejaa woga na huzuni kubwa. Ni mara chache sana kwa Afisa Nguli wa Usalama wa Taifa uso wake kuonyesha hofu kubwa kiasi hicho.
"Hao walikuwa makao makuu wamenipigia!" Salim akaongea kwa unyonge huku anaweka simu mezani.
"Wanasemaje?" Gooluck akauliza.
"Wanasema tetemeko kimepita mahali.. Kuna dalili ya mji mwingine kutwaliwa masaa machache yajayo..!" Salim akaongea huku anajiinamia kuficha machozi yalikuwa yanaanza kumtoka.
"Mji gani?" Shafii akauliza kwa woga na hofu iliyosikika mpaka kwenye sauti yake.
"Dar es Salaam.!!" Salim akajibu bila kuwaangalia wenzake.. Sauti yake ilidhihirisha kuwa alikuwa ameanza kulia.
Taarifa hii ikawaacha wote vinywa wazi, wasijui wasemeje au wafanyaje.
Wakati huo huo..
RABAT, MOROCCO
Kuna kipindi ambacho kila mtu anakuwa amekata tamaa lazima wainuke watu wa kuibeba dunia mabegani na kuifanya isonge mbele. Lakini pia sio kila muda unapoona wameinuka watu basi wanakuwa na nia ya kuibeba mabegani, wengine wanainuka ili kuikimbia dunia wasizame nayo pale itakapozama! Kuna wengine watainuka na kuibeba mabegani mwao, lakini haimaanishi kwamba wanatapeleka mbele, wengine nia yao ya kuibeba mabegani ni ili waiinue juu zaidi ili watakapoibwaga ipasuke vipande vipande kisisalie kitu.
Kila dunia inapozama, kila atayeyeinuka ana nia yake, na kila atayeibeba mabegani kuna mahali anapotaka kuipeleka. Mtihani mkubwa huja pale ambapo, tukiibeba dunia pamoja lakini hatukubaliani mahali kwa kuipeleka.
Huu ulikuwa ni usiku wa karibia saa saba usiku, ndipo muda ambao watu sita, walivalia majoho marefu myeusi yenye kofia za kufunika vichwa na wakiwa hawana viatu miguuni, walikuwa wamewasili katika pwani ya Morocco na mashua wakitokea nchini Hispania kwa kuvuka bahari.
Walikuwa wameshashusha mzigo wao mmoja tu waliokiwa nao na sasa walikuwa wameubeba na wakitokomea kutoka hapo pwani.
Leo hii walikuwa wanatarajia kuhitimisha safari yao ya karibia miezi miwili kwa mguu, kutokea Italia, na baadae Hispania na hatimaye kuvuka bahari kwa mashua.
Licha ya majoho yao meusi ya kufanana, na licha ya wote kufanana kwa kuwa peku peku, lakini pia walifanana alama iliyopo shingoni mwao wote ambao ilikuwa ni tatoo ya neno,
'Sancta Sedes'.
Mzigo wao pekee waliokuja nao ulikuwa ni sanduku kubwa mfano wa jeneza ambalo lilihitaji walau watu wanne ili kuweza kulibeba.
Kwahiyo walikuwa wamelibeba mabegani kila upande wa sanduku mtu mmoja, na mmoja ametangulia mbele na mwingine nyuma.
Sanduku hili kuu kuu linaloonekana la siku nyingi mno na pengine lilikuwa limefukiwa chini kwa miaka mingi, juu yake lilikuwa na maandishi yaliyofifia lakini bado yaliweza kusomeka.. Yalikuwa yameandikwa,
"Novus Ordo Sedorum " (The New World Of Ages).
Japokuwa watu hawa walikuwa wamechoka haswa kwa safari hii ya miezi miwili, kiasi kwamba nyayo zao zilikuwa zimepasuka kiasi zilikiwa zinakaribia kutoa damu kwasababu ya kutembea umbali mrefu kwa miezi miwili mfululizo, lakini waliona faraja mbele yao, safari yao ilikuwa imefikia ukingoni, walikuwa wamebakisha kilomita tano tu kuingia mji wa
Rabat.
Ulimwengu unapozama, lazima wainuke watu wa kuubeba mabegani… lakini je wakishaubeba, ni wapi wataupeleka??
ITAENDELEA…