Tatizo la Kukosa Usingizi (Insomnia) na tiba yake

Pape

JF-Expert Member
Dec 11, 2008
5,488
79



Wana JF, kuna ndugu yangu yaani yeye asipokunywa chai kabla hajalala basi atakesha akihesabu 'kenchi' na kuna siku alikosa chai akanywa kahawa na matokeo yake 'alikesha', je, hali hiyo ya kutopata usingizi bila kunywa chai ni ugonjwa?

Kuna namna ya kuepukana nayo?

Tatizo la Ukosefu wa Usingizi
UKOSEFU wa usingizi ni hali ya kushindwa kupata usingizi wakati wa usiku, kushindwa kulala kwa muda wa kutosha au kushindwa kurudia kulala pale ambapo umeamka.

Watu wenye tatizo la ukosefu wa usingizi, hulala kwa muda mfupi au hawalali usingizi mzuri pamoja na kuwepo kwenye mazingira yanayoruhusu kupata usingizi mzuri.

Ukosefu wa usingizi huambatana na hali ya mwili kuwa mchovu wakati wa mchana.

Idadi ya saa ambazo mtu huwa amelala, sio kipimo cha ukosefu wa usingizi kwa kuwa saa za kulala hutofautiana kati ya mtu na mtu na kati ya watu wa umri tofauti.

Ukosefu wa usingizi ni tofauti na kulala saa chache kwa sababu wapo watu ambao wanaweza kulala saa chache na kuamka asubuhi mwili ukiwa umepumzika vizuri na wakaendelea na shughuli bila shida yoyote.

Ukosefu wa usingizi unakuwa tatizo, pale ambapo unaambatana na kuwa mchovu siku inayofuata.

Vilevile, kuna tofauti kati ya ukosefu wa usingizi na kupungua kwa saa za kulala. Ikiwa ukosefu wa usingizi umesababishwa na kupungua kwa saa za kulala, mazingira yanaporuhusu kulala muda mrefu, mtu anaendelea kupata usingizi kama kawaida. Kukosa uzingizi ni mojawapo ya sababu za watu, kuhudhuria hospitali.

Karibu kila mtu hupatwa na hali ya ukosefu wa usingizi kwa wakati fulani kutokana na sababu mbalimbali na mara nyingi hali hiyo haijirudii. Ukosefu wa usingizi unakuwa tatizo, endapo hali hiyo inatokea mara kwa mara au inaendelea kwa muda mrefu.

Dalili ambazo zinaashiria kuwa mtu ana tatizo la ukosefu wa usingizi ni pamoja na kushindwa kupata usingizi wakati wa kulala usiku, au kulala kwa muda mfupi, ambayo inaambatana na kuwa mchovu au kusinzia wakati wa mchana; kuwa na hali ya usahaulifu au kushindwa kufanya kazi na kuwa na hali ya wasiwasi.

Kwa watu walio wengi ukosefu wa usingizi kwa muda mrefu, husababisha matatizo kazini, hasa kwa sababu ya kupunguza ufanisi wa kazi, na pia husababisha matatizo katika mahusiano.

Hali ya ukosefu wa usingizi, huleta hofu ambayo pia inaongeza tatizo la kupata usingizi, hivyo kuendelea kuongeza ukubwa wa tatizo.

Yapo mambo mengi ambayo yanasababisha ukosefu wa usingizi, baadhi ni ya muda mfupi na mengine ni ya muda mrefu.

Mambo yanayoleta ukosefu wa usingizi kwa kipindi kifupi ni mabadiliko ya mazingira ya kulala (mfano sehemu yenye kelele, hali ya hewa ya joto sana au baridi sana, mwanga n.k); kutumia au kuacha kutumia kahawa au dawa zinazoathiri usingizi; kuwa na msongo wa mawazo au wasiwasi hasa baada kupata shida kama vile za kufiwa, kutalikiwa, au kupoteza kazi; au kuwa na maumivu ya kuugua.

Vilevile, mabadiliko ya saa za kulala yanaweza kuleta ukosefu wa usingizi, mfano kusafiri kwenye maeneo yenye tofauti kubwa ya saa au kubadili saa ya kazi.

Ukosefu wa usingizi kwa muda mrefu, unaweza kusababishwa na mambo mbalimbali, kama vile ugonjwa ambao unaleta maumivu au hali ya msongo wa mawazo au matumizi ya dawa ambao zinaathiri usingizi.

Hata hivyo, ukosefu wa usingizi unaweza kutokea bila kuwa na sababu yoyote, ambapo kunakuwa na historia ya ukosefu wa usingizi kwenye familia na tatizo huanza wakati wa utoto.

Madhara ya ukosefu wa usingizi, yamegawanyika katika makundi makuu mawili ambayo ni madhara ya muda mfupi na madhara ya muda mrefu. Madhara ya muda mfupi ni kupunguza ufanisi wa kufanya kazi wakati wa mchana, kuumia au kupata ajali.

Ukosefu wa usingizi kwa muda mrefu, husababisha madhara ya kiafaya kama vile kisukari, magonjwa ya moyo, unene kupita kiasi na kupungua uwezo wa kufikiri. Hatua ya kwanza katika matibabu ya ukosefu wa usingizi ni kutambua endapo kuna chanzo.

Matibabu ya ukosefu wa usingizi, hufanywa na wataalamu wa afya kwa kuzingatia historia na mazingira, ambayo yamesababisha ukosefu wa usingizi. Endapo ipo sababu maalumu, mara chanzo kitakapoondoka hali ya usingizi huimarika.

Usingizi bora huletwa na mambo mbalimbali, ambayo yanatakiwa kufanyika wakati wa mchana, usiku kabla ya kulala, wakati wa kulala na wakati usingizi umepotea.

Wakati wa mchana: Mazoezi ya mara kwa mara, hata dakika 20 yanachangamsha mwili, hata hivyo kwa wenye ukosefu wa usingizi, mazoezi yasifanyike wakati wa jioni.

Kutolala wakati wa mchana, na endapo ni lazima kulala, basi muda wa kulala usiwe zaidi ya nusu saa.

Kabla ya kulala: Kutotumia vilevi, kahawa au sigara jioni au usiku kabla ya kulala; kupunguza utumiaji wa vitu vya maji maji na kuzima luninga angalau saa moja kabla ya kulala. Wakati wa kulala: Ni vizuri kwenda kulala na kuamka asubuhi wakati uleule hata kama ni siku za wikiendi.

Ikiwa ni lazima kula kitu wakati wa kwenda kulala, vitu vizuri vya kutumia ni pamoja na maziwa ya moto au ndizi. Chumba cha kulala kitumike kwa matumizi ya kulala na sio kusoma, kuangalia luninga au kufanya kazi.

Ni vizuri kulalia upande ambao mara nyingi huamkia asubuhi (mfano kama mara nyingi mtu anaamka asubuhi akiwa amelalia upande wa kushoto, huu ndio upande mzuri wa kuanza kulala).

Ni muhimu kwenda kulala wakati mmoja na mwenza.

Wakati wa ukosefu wa usingizi: Endapo baada ya kuingia kitandani kulala usingizi haujaja kwa dakika 15, ni vema kutoka kitandani na kutafuta kitu cha kufanya kama vile kusikilliza muziki kwenye chumba kingine, au kusoma vitabu mpaka usingizi utapokuja.

Hatua hii inaweza kurudiwa mpaka usingizi utakapopatikana.

Zipo dawa ambazo zinatumika kuleta usingizi kwa watu wenye shida ya kupata usingizi.

Dawa hizi japokuwa zinapatikana kwenye maduka ya dawa, ni vizuri zitumike baada ya kushauriwa na daktari tu na zisitumike kwa muda mrefu.

BAADHI YA MAJIBU YALIYOTOLEWA NA WADAU:
---
---
 
Huyo nadhani ameathirika kisaikolojia kwa kujiwekea imani kuwa chai ndo njia pekee ya kumpatia usingizi. Cha muhimu mshauri ajilazimishe kutokunywa chai kabla ya kulala, ingawa mwanzoni atapata tabu kupata usingizi, lakini akili itajizoesha na hatimaye ataweza kulala bila ya chai. Huo ni mtazamo wangu.
 
Wajameni nasikia mtu unaweza kumpenda mtu kiasi cha kukosa usingizi hivi inawezekana vipi?,kwani siku hizi naona hakuna kupendana zaidi ya kutamaniana hebu pls nijuzeni
 
Hulali unafanya nini sasa wakati una mtu unayempenda na anayekupenda? duh!
 
Sipati picha kwani kuna mtu amenishtakia kusema kua hana raha kwa kukosa usigizi kwa kumfikiria mtu anaempenda kuliko sasa sielewi kabisa.
 
Ndio maana nikauliza kwani usingizi wako anao mwengine au unakuaje?,tena basi shuti kakonda
 
Nami nilikuwa nikisikia hivyo nikawa siamini. Mpaka na mimi nilipokuja kupenda,nilipenda kwa kweli usingizi ulikuwa wa tabu,na imagine nae kila sehemu. na nikilala huwa namuota yeye karibu kila siku,na nikishtuka usiku ooh,akili inarudi kwake.

Nikiongea nae kwenye simu,sitaki simu aikate.kama sijawasiliana nae siku moja tu,basi nakuwa kama sichanganyi vizuri. usiombe ukapenda,bora upende juu juu tu kwani sometimes ni kama mateso fulani hivi.
 
Yaani Kisukari umenikumbusha mbali sana. Tulipokuwa shule FV na VI alikuwepo kijana mmoja akimpenda sana msichana ambaye ni rafiki yetu (sote tulikuwa darasa moja). Sasa ilikuwa balaa, yule binti akiongea tu na mvulana mwengine yule kijana huanguka na kuzimia! Binti wa watu alikosa amani kabisa na unajua tena vijana walivyo wachokozi. Wavulana wengine wakimwona karibu yule mwenzao anaependa basi hujifanya kama wanaongea na yule binti kwa makusudi. Masikini kijana wa watu puuuu!

Tulivyomaliza FVI alijaribu kwenda nyumbani kwao kupeleka posa lakini hiyo tena ilikuwa issue nyingine.

Siku moja tulionana baada ya miaka kidogo. Katika maongezi tukaongea kuhusu kipindi kile. Aliniambia hakumbuki alifikwa na mikasa gani hata ikawa anampenda yule binti kiasi kile, alikuwa hali vizuri, akilala hapati usingizi anamuwaza na kila analofanya picha ya yule binti ilikuwa kwenye brain yake. Ndio maana alikuwa anabehave namna ile. Ila baadae viliondoka wenyewe tu.

Kuna wimbo unasema hivi:
Usinione nakonda ukadhani kwetu sili
Nala mchele kibaba na nyama kilo mbili
Ninakukondea wewe punda usie fadhili
 
Ndio maana nikauliza kwani usingizi wako anao mwengine au unakuaje?,tena basi shuti kakonda

Mawazo yanaweza kukufanya ukose usingizi.

imagine unampenda mmeo /mkeo boyfriend /G/friend lakini kila kukicha anaboronga inakuwa kero.

Ukipanda kitandani unatawaliwa na mawazo tele juu ya nini ufanye unajikuta tayari jogoo anawika.

Unampenda mtu hakupendi ..mawazo mawazo.

umekataliwa na umpendae mawazo mawazo.

Kuna wengine wanabugiaUlabu mradi umsaidie kidogo
 
Mpenzi,
Salaam, ama baada ya salamu mimi ni mzima.
Dhumuni (Disco) la barua hii ni kutaka kukujulisha kuwa nimezama kwwenye lindi la mapenzi.
Nikinywa maji nakuona kwenye glasi, usingizi sipati, nakuota wewe malaika wangu.
Naomba unitunukie tunu ya mahaba na penzi lako maridhawa.
Wako mtiifu, mnyenyekevu, mvumilivu na mwaminifu penzi.
Cool Sumba.
Hizo zilikuwa enzi zetu zilee tukibonga vishtobe.
Akikukubali ugumu unakuja kwa kumpeleka kutoa jalamba.
 
Hebu fafanua kisukari hua hulali kabisa au usingizi unakupitia bila kujijua?.
 
Habari madoctor,
mimi ni mama zaid ya miaka 32 na chini ya 36, naomba kufahamu juu ya hili.

Wakati wa kulala nisipopaka mafuta miguuni mpaka unyayoni na kwenye lips za midomo sipati usingizi kabisa, hata kama nimechoka sana usingizi hauji kabisa ntakaa macho nilipolala mpaka kunakucha, lakin nikipaka mafuta hasa haya mazito ,mfano vaseline,bodyline au vestiline na mengineyo mazito, miguuni mpaka unyayoni ,kwenye lips za midomo halafu ndiyo nalala.

Nalala usingizi mzuri saaaana (kama alalavyo mtoto mchanga, kwa wale wenye watoto wachanga watanilewa kuwa ni usingizi wa aina gani),hata nikiamka asubuhi naamka nikiwa na siha njema kabisa.sipaki mafuta mengi napaka kawaida tu.hivyo ni lazima kilasiku nipake mafuta usiku sehemu hizo ili niweze kupata usingizi mzuri na tulivu.mimi nimeligundua hili tangu nilipoanza kujitambua japo wazazi wangu wanasema hili ni tatizo tangu nilipozaliwa.

Halinikeri sana,lakin ninapenda kufahamu kwanini inakuwa hivi, kwa sababu kuna watu wengine mfano wanangu,rafiki zangu,ndugu zangu wao wakioga na kulala pasipo kupaka mafuta wanapata usingizi bila wasiwasi.

Kuna uhusiano gani kati ya mafuta na usingizi kwa baadhi ya watu kama sisi?

Nategemea kupata majibu toka kwenu, asanteni.
 
Mmm!! Klorokwin, ina maana wanafunzi wa mzumbe tu ndy wenye majibu ya hilo swali??
 

Similar Discussions

Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…