SoC03 Tathimini ya taratibu za uendeshaji wa shughuli za biashara nchini Tanzania

Stories of Change - 2023 Competition

Hamza Nsiha

JF-Expert Member
Jul 25, 2022
208
191
Habari! Ndugu wana JamiiForums, ni matumaini yangu kuwa sote tu bukheri wa afya. Leo hii ninapenda kuwashirikisha katika uzi huu unaoangazia tathimini yenye madhumuni ya kuibua njia madhubuti ambazo zinaweza kuchochea matokeo chanya katika shughuli mbalimbali za biashara kwa maendeleo ya taifa letu na watu wake kwa ujumla.

Nchini Tanzania, asilimia kubwa ya watu wake hupenda kujihusisha katika shughuli mbalimbali za uzalishaji mali kama vile kilimo, biashara n.k.

La hasha! Hata watu walioajiriwa bado hupenda pia kuongeza wigo wao wa mapato kupitia shughuli mbalimbali kama vile biashara na shughuli zinginezo. Hivyo, biashara ni moja ya nguzo kuu ya uchumi kwa taifa na raia wake kwa ujumla.

Mpaka sasa, kuna aina nyingi za biashara ambazo wananchi wamekuwa wakijihusisha nazo kulingana na mitaji yao. Mfano; biashara za vyakula, maduka ya nguo, vifaa vya umeme, usafirishaji n.k.

Je! Ni kitu gani muhimu kinachohitajika ili kuwezesha uanzishaji wa biashara?
Ni ukweli usiopingika kuwa, ili kuanzisha biashara nchini Tanzania ni muhimu kukamilisha taratibu mbalimbali zilizowekwa ili kuhalalisha biashara hiyo.

Labda tukumbushane pamoja, Ili kuwezesha biashara kuna mamlaka ambazo unahitaji kuzipitia kulingana na aina ya biashara na mahitaji yako maalumu kama vile;
  • BRELA (Business Registrations and Licensing Agency): Unapaswa kusajili biashara yako na kupata cheti cha usajili. BRELA inahusika na usajili wa biashara na kutoa vibali vya uendeshaji.
  • TRA (Tanzania Revenue Authority): Unahitaji kujiandikisha na TRA kupata namba ya utambulisho wa mlipa kodi (TIN) na kusajiliwa kwa VAT (Value Added Tax) ikiwa biashara yako inastahili kutoza ushuru wa VAT.​
  • SUMATRA (Surface and Marine Transport Regulatory Authority): Ikiwa una nia ya kuanzisha duka la kutoa huduma za usafirishaji, unahitaji kuzingatia sheria na kanuni zinazosimamiwa na SUMATRA.​
  • TFDA (Tanzania Food and Drugs Authority): Ikiwa unapanga kuanzisha duka la kuuza bidhaa za chakula, dawa, au vinywaji, unahitaji kusajiliwa na TFDA na kuzingatia kanuni zao za usalama na ubora wa bidhaa.​
  • TBS (Tanzania Bureau of Standards): Ikiwa unapanga kuuza bidhaa zilizosanifishwa au zinazohitaji viwango, unahitaji kuzingatia viwango vya TBS na kupata vibali vya leseni vinavyohitajika.​
  • NEMC (National Environment Management Council): Ikiwa biashara yako inaathiri mazingira, unahitaji kuzingatia kanuni za NEMC na kupata vibali vinavyohitajika kwa shughuli yako.​
  • OSHA (Occupational Safety and Health Authority): Ikiwa unaajiri wafanyakazi, unapaswa kuzingatia sheria na kanuni za OSHA na kuhakikisha mazingira salama kazini.​

Je! Usambazwaji wa taarifa muhimu kuhusiana na uanzishaji wa biashara mbalimbali upo katika kiwango gani?
  • Licha ya serikali kutoa miongozo mbalimbali kuhusiana na masuala mbalimbali ya biashara nchini, ukweli ni kuwa bado haijafikia kiwango kikubwa katika kuwafikia raia wake kuhusiana na taarifa mbalimbali muhimu zinazohusiana na mambo ya uanzishaji wa biashara mbalimbali nchini.​
Watu wengi hususani wajasiriamali wamekuwa wakianzisha biashara pasipo kuwa na taarifa muhimu juu ya taratibu zilizowekwa na mamlaka husika hivyo huishia kupata changamoto mbalimbali ambazo kwa namna moja au nyingine zinaweza kukwamisha biashara zao.


Je! Watu wenye uelewa juu ya taratibu au hatua zinazohusika katika zoezi la kuanzisha biashara zao hukumbwa na changamoto gani?
  • Kama ilivyoainishwa hapo juu, kuhusiana na baadhi ya mamlaka muhimu zinazohusika katika usimamizi wa shughuli za biashara, baadhi ya wananchi wamekuwa wakikumbwa na changamoto mbalimbali kama vile matumizi ya muda mwingi katika kufuatilia vibali kutokana na uwepo wa mamlaka nyingi ambazo kila moja hufafanya kazi kwa kujitegemea.​
Mfano; Mtu anaweza kutumia siku ya kwanza kufuatilia kibali katika mamlaka moja, kisha kibali kingine katika mamlaka nyingine kwa siku itakayofuata, hivyo mpaka kukamilisha mamlaka zote hujikuta ametumia muda mrefu katika kukamilisha mlolongo wa zoezi husika.

Hivyo, baadhi ya watu hukata tamaa au kuamua kutumia njia za mkato ili kukwepa mlolongo wa utaratibu uliowekwa.

MAPENDEKEZO;​
  1. Serikali kupitia mamlaka zake husika zinaweza kuongeza mbinu madhubuti katika kuhakikisha wananchi wake wanapata uelewa wa kutosha kuhusiana na masuala mbalimbali ya uendeshaji wa shughuli za biashara kupitia uboreshwaji wa kitengo cha utoaji habari kupitia magazeti, matangazo ya Televisheni pamoja na kufanya makongamano mbalimbali yenye lengo la kutoa elimu ya kina kwa wananchi wake.​
  2. Kuweka mfumo yakinifu utakaorahisisha uratibu wa mamlaka mbalimbali ili kupunguza muda unaotumika katika kukamilisha zoezi zima kwa ujumla. Serikali inaweza kutengeneza mfumo wa taarifa utakaojumuisha mamlaka zote zinazohusika kwa kutengeneza muundo wa ushirikiano baina ya mamlaka moja na mamlaka nyingine kama vile namna rahisi ya kubadilishana taarifa.​
  3. Kuboresha kituo cha utatuaji migogoro: Serikali inaweza kuboresha kituo cha usuluhishi au bodi ambayo inashughulikia migogoro au masuala yanayohusiana na biashara. Kituo hicho kinaweza kusaidia katika kung'amua changamoto mbalimbali zinazo wakumba wafanyabiashara wake hivyo kusaidia kuleta mamlaka mbalimbali pamoja katika kutafuta suluhisho la pamoja.​
  4. Kuongeza au kuboresha zaidi ushirikiano baina ya mamlaka husika na raia wake. Hii itasaidia kuongeza uhuru wa kuripoti changamoto mbalimbali zinazowakumba katika shughuli za biashara hivyo kuibua njia madhubuti zitakazosaidia kuleta matokeo chanya.​
  5. Pia, ikipendeza zaidi, kuna umuhimu wa Serikali kuonesha nia dhahiri ya kuwaunga mikono wananchi wake wenye nia dhahiri ya kuanzisha biashara zao kwa kufuata utaratibu maalumu uliowekwa na mamlaka husika. Mfano; kuwafanyia ofa mbalimbali kama motisha wa kuonesha nia dhahiri yenye lengo la kuinua uchumi wa taifa kwa ujumla. Lakini pia, kutoa adhabu stahiki kwa wote watakaobainika na makosa ya kughushi au kutofuata taratibu zilizowekwa.​
Hivyo basi, serikali inaweza kuchukua baadhi ya hatua hizi na zingine nyingi ili kupunguza changamoto zinazowakumba wananchi wenye nia ya kuanzisha biashara mbalimbali. Kwa kufanya hivyo, inawezekana kukuza ujasiriamali, kujenga ajira, na kukuza uchumi wa nchi.

Kwa ujumla, nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipotoa pongezi zangu za dhati kwa mamlaka zinazohusika na masuala mbalimbali ya uendeshaji wa shughuli za biashara kwa utendaji kazi wake.

Hivyo, andiko hili halina dhumuni la kupinga au kupotosha utendaji kazi wa mamlaka husika bali lina nia ya dhati ya kukumbusha baadhi ya vipengele muhimu ambavyo vinahitaji kutiliwa mkazo ili kuinua uchumi wa taifa letu kwa pamoja. Kwani mimi na nchi yangu tunahitaji kuwajibika katika kutengeneza taifa lenye uchumi unaovutia na kung'aa Afrika na ulimwenguni kote.​
 
Kiukweli kuna mamlaka bado hazijajipambanua kwa mapana niliwahi sikia BRELA kwa mtu ndipo akaanza kunipatia majukumu yake, tunahitaji nguvu zaidi wananchi wetu waelewe.
 
Back
Top Bottom