Parabolic
JF-Expert Member
- Dec 3, 2013
- 2,743
- 2,601
Geneva, Uswisi. Tanzania imeangazia juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan, katika kuimarisha uwajibikaji, maridhiano na kuendelea kuzijenga taasisi za umma kupitia kuundwa kwa Tume Huru ya Uchunguzi kuhusu vurugu zilizohusishwa na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Hayo yaliwasilishwa katika tukio maalumu lililofanyika sambamba na Kikao cha 61 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa (UNHRC), mjini Geneva, Uswisi.
Katika uwasilishaji huo, ilielezwa kuwa Tume hiyo ni chombo muhimu cha kitaifa kilichoanzishwa kwa lengo la kuweka wazi ukweli kuhusu matukio ya vurugu, uharibifu wa mali na madai ya vifo vilivyotokea wakati na baada ya uchaguzi huo.
Pia, inalenga kuimarisha imani ya umma na kusaidia juhudi za taifa katika kukuza uwajibikaji, maridhiano na utawala wa kidemokrasia.
Akizungumza katika tukio hilo, Mkurugenzi Msaidizi wa Taarifa za Haki za Binadamu Wizara ya Katiba na Sheria, Beatrice Mpembo,
alisema Tume hiyo iliundwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Novemba 18, 2025 kwa mujibu wa Sheria ya Tume za Uchunguzi, Sura ya 32, kwa lengo la kuchunguza matukio hayo na kuishauri Serikali kuhusu hatua stahiki zinazopaswa kuchukuliwa.
Alieleza kuwa, Tume hiyo ni chombo huru, maalumu na cha muda cha uchunguzi kinacholenga kubaini chanzo cha vurugu hizo, kuchambua matukio yaliyofuata baada ya uchaguzi na kutathmini hatua zilizochukuliwa katika kurejesha utulivu.
Aidha, kazi ya Tume inalenga kuimarisha uwajibikaji na kusaidia kurejesha imani ya wananchi kwa taasisi na mifumo ya kitaifa.
Tume hiyo inaongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman, ambaye ni mtaalamu wa sheria anayeheshimika kwa mchango wake katika uadilifu wa mifumo ya sheria, haki za binadamu na sheria ya kimataifa ya jinai.
Anasaidiwa na makamishna wanane wengine, wakiwemo wanawake wawili na wanaume sita wenye uzoefu katika maeneo ya utawala bora, sheria na usalama, maendeleo pamoja na utawala wa umma.
Kwa mujibu wa uwasilishaji huo, majukumu ya Tume ni pamoja na kuchunguza visababishi vya msingi vya vurugu hizo, ikiwemo malalamiko ya vijana na nafasi ya vitendo vya upinzani; kutathmini hatua zilizochukuliwa na vyombo vya usalama katika kurejesha utulivu; kupendekeza hatua za kuimarisha maridhiano na mshikamano wa kijamii; kuchunguza uwezekano wa uwepo wa ufadhili kwa waliohusika katika vurugu hizo; pamoja na kupendekeza mageuzi yatakayosaidia kuzuia vurugu za uchaguzi zijazo na kuimarisha taasisi za kidemokrasia.
Aidha, Tanzania ilisisitiza kuwa uwazi na ushiriki wa wananchi ni msingi muhimu wa utekelezaji wa kazi za Tume hiyo.
Kwa lengo hilo, tovuti ya umma ilianzishwa kutoa taarifa kuhusu muundo wa Tume, hadidu za rejea na njia ambazo wananchi wanaweza kushiriki katika mchakato huo kupitia barua, simu na mitandao ya kijamii.
Tume hiyo pia ilifanya mkutano na vyombo vya habari uliorushwa kitaifa Desemba 1, 2025, uliowakutanisha wahariri na wawakilishi wa vyombo vya habari.
Baadaye, ilifanya vikao vya hadhara na vya faragha vilivyowahusisha mawaziri, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, watumishi waandamizi wa umma, wananchi, wasomi pamoja na wawakilishi wa asasi za kiraia.
Katika uwasilishaji huo, ilielezwa pia kuwa Tume hiyo inatarajiwa kuchangia si tu katika uwajibikaji, bali pia katika maridhiano mapana ya kitaifa na mageuzi ya muda mrefu.
Kufuatia matokeo ya Tume hiyo, Serikali imependekeza kuanzishwa kwa Mpango wa Kitaifa wa Maridhiano utakaolenga kurejesha amani na utulivu, kuponya mipasuko ya kijamii, kuhimiza ukweli na majadiliano, kushughulikia malalamiko ya kihistoria, kuzuia migogoro ya baadaye na kuimarisha utawala wa kidemokrasia pamoja na umoja wa taifa.
Tanzania pia ilieleza hatua nyingine zilizochukuliwa na Serikali baada ya uchaguzi huo, ikiwemo kutoa msamaha kwa vijana 1,787 waliobainika kuwa na makosa madogo yaliyohusiana na matukio ya vurugu.
Aidha, Serikali ilitangaza kuanzishwa kwa Wizara ya Vijana chini ya Ofisi ya Rais tarehe Novemba 17, 2025, kwa lengo la kushughulikia changamoto za ajira kwa vijana, maendeleo ya ujuzi, uwezeshaji na ushiriki wao katika maendeleo ya taifa.
Awali Tume hiyo ilipewa muda wa siku 90 kukamilisha kazi yake, lakini baadaye muda huo uliongezwa kwa siku 42 kutokana na mwitikio mkubwa wa wananchi.
Inatarajiwa kuwasilisha ripoti yake mwezi Aprili 2026.
Tanzania imesema kuwa Tume hiyo inaakisi dhamira pana ya nchi katika kuimarisha haki, uwajibikaji, haki za binadamu na utawala shirikishi, huku ikiweka msingi wa amani endelevu, taasisi imara na mshikamano wa taifa wa muda mrefu.