SoC04 Tanzania ya Kesho itajengwa na betting?

Tanzania Tuitakayo competition threads

Mrs Jucbreezy

New Member
May 3, 2024
2
1
BETTING KUUA TAIFA LA KESHO
Michezo ya kubahatisha maarufu kama 'kubet' ndiyo habari ya mjini kwa sasa. Ukiacha aina mbalimbali za michezo hiyo zilizokuwepo kwa miaka mingi na katika maeneo maalumu kama vile kasino, hivi karibuni imeibuka ile ya kutabiri michezo na mashine za kutumia sarafu ambayo imesambaa maeneo mengi nchini, pia kukithiri kwa michezo ya kubahatisha kwenye mechi za mpira wa miguu imekuwa kama ya ajira ya kwanza kwa kijana wa kitanzania lakini pia imekuwa chanzo cha pili cha mapato kwa waajiriwa wa serikali na taasisi binafsi.

Michezo hii ya kubahatisha ilikuwa ikitangazwa kwa wingi kwenye mitandao ya kijamii, lakini kwa hivi sasa matangazo ya michezo ya kubahatisha yameshamiri katika chaneli za televisheni, redio, kwenye kompyuta na hata kwenye simu za mkononi.

Michezo ya kubahatisha imekuwa uraibu mpya kwa vijana ukiachana na ule uraibu wa madawa ya kulevya, pombe na sigara. Kwa mujibu wa ripoti ya Bodi ya Michezo ya Kubahatisha nchini (GBT) zinaonyesha watu wanaokumbwa na uraibu wa michezo ya kubahatisha nchini si zaidi ya 10 kwa mwaka, wengi wao ni vijana wanaocheza michezo hiyo kwenye Kasino. Mwaka 2020 watu 10 walitambulika kuwa na uraibu wa michezo ya kubahatisha (betting), mwaka 2021 walikuwa saba, wote ni wanaume na vijana, hasa wale wanaobahatisha kwenye michezo (mpira wa miguu), hususani za mitandaoni.

Kwa sasa michezo ya kubahatisha nchini Tanzania imekuwa sehemu ya chanzo cha mapato ya serikali kwani kwa mujibu wa ripoti ya Bodi ya michezo ya kubahatisha (GBT) mwaka wa fedha 2020/2021 mzunguko wa fedha katika sekta ndogo ya michezo ya kubahatisha ulikuwa ni miamala yenye thamani ya Tshs 3.17 trilioni na makusanyo ya Serikali yalikuwa Tshs 132 bilioni.

Pamoja na faida hiyo ambayo serikali inapata kupitia michezo hii ya kubahatisha kwangu naliona hili ni tatizo kwa taifa la kesho, vijana wamekuwa waraibu wa michezo hii na sio tu vijana sasa hivi si kusikia mzee amestaafu kazi na mafao yote yamepotelea kwenye betting. Serikali inajaribu kuwalinda watoto wadogo dhidi ya michezo hii lakini ni kama kumtuma mtoto sigara dukani halafu umzuie kutumia lazima atahitaji kujua kuna siri gani kwanini azuiliwe kutumia. Serikali imezuia matumizi ya pombe na sigara kwa watoto wadogo kwani hawatumii? Kwa mujibu wa vifungu namba 47 na 70 vya sheria ya michezo ya kubahatisha ni kosa kwa mtu yeyote aliyejuu ya miaka 18 kuruhusu au kusababisha mtoto wa chini ya umri huo kushiriki kwenye michezo ya kubahatisha. Lakini kwa sasa watoto wanamiliki simu za mkononi wanatazama matangazo haya ya betting kupitia televisheni ambazo yanaelezea hatua ya kwanza hadi ya mwisho jinsi ya kucheza michezo hii, je hawajifunzi?

Serikali inashiriki kwa asilimia 100% kuharibu taifa la kesho kwani mtu hujifunza kwa kuona, kusikia na hata mazoea ya hali ya maisha ya kila siku. Kwa sasa channel kubwa maarufu hapa nchini zimejaa matangazo ya betting na sio tu matangazo ya kampuni za michezo ya kubahatisha bali channel zenyewe zinaendesha bahati nasibu wakati wa vipindi muhimu ikiwemo taarifa ya habari. Kama serikali umeruhusu vyombo vya habari ambavyo ndivyo chachu ya mabadiliko kubeba agenda ya michezo ya kubahatisha kuwa kipaumbele cha chanzo cha mapato kwa vijana tutarajie nini kwa Tanzania ya kesho. Sasa hivi ukiwasha televisheni utakuwa ITV inaendesha Mchezo Supa, ukienda Clouds TV utakutana na Mchongo Pesa, ukienda WASAFI TV utakutana na WASAFI BET, akili ya vijana muda wote inalishwa mbinu mpya za betting.

Vijana wengi wa vyuo vikuu ambao ndio wasomi wanaotegemewa na taifa kusoma na kuleta mabadiliko chanya kwa taifa ndio waraibu wakuu wa michezo hii ya kubahatisha, nimeshuhudia vijana wa vyuo vikuu wakiacha masomo kwa sababu wameshinda bahati nasibu za michezo hii, lakini pia wapo waliopoteza ada na boom kwenye betting na kushindwa kuendelea na masomo. Na sio vijana wa mjini tu, michezo hii haijawaacha nyuma hata vijana vijijini ambapo karibia vijiji vyote nchini vina mashine za kichina za kuchezesha sarafu maarufu kwa jina la bonanza, ambapo vijana wa vijijini pesa zao za pembejeo za kilimo zinapotelea huko.
IMG_7684.png
IMG_7684.png


Kama serikali imeshindwa kuvitumia vyombo vya habari kuhamasisha mambo muhimu kwa vile ujasiriamali, utunzaji wa mazingira, kupinga ukatili, kupinga madawa ya kulevya na kuhamasisha kilimo tutarajie taifa la watu wavivu wasio na uwezo wa kufikiri bali kutarajia utajiri wa haraka haraka bila kufanya kazi. Vyombo vya habari ni silaha kubwa sana katika kuangamiza au kujenga taifa kesho kama tutaruhusu vyombo vya habari kuwafundisha vijana na watoto wetu waendelee kujifunza kubet kupitia vipindi na muda muhimu (prime time) tutarajie hasara kubwa kwa siku za usoni kwani hata vijana tunaowasonesha hawatalisaidia taifa. Mwaka 2019 Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania ilizuia kwa muda urushaji wa matangazo ya michezo hiyo kupitia redio na televisheni, matangazo ambayo yalielezwa kukithiri. Lakini je, katazo hilo liliishia wapi na mbona ni kama bodi hiyo ilichochea moto wa matangazo haya. Hata hivyo kasi ya vijana kujihusisha na michezo ya kubahatisha imeleta hofu kiasi cha baadhi ya serikali za nchi za Afrika Mashariki ikiwemo Uganda kupiga marufuku michezo hiyo. Nchi yetu ya Tanzania haijaliona hili kama tatizo kwa taifa au kuna viongozi wanaonufaika na michezo hii wakati taifa likiteketea, tumepoteza vijana waliojiua kwa kupoteza pesa zao kwenye betting lakini bado serikali hailioni hili kama tatizo?

Kwa kujenga Tanzania tuitakayo ndani ya miaka 25 ijayo michezo ya kubahatisha ipigwe marufuku na serikali iangalie agenda muhimu za kutembea nazo ili kujenga taifa, kama ambavyo tulitembea na kauli mbiu ya Tanzania ya kijani ili kulinda mazingira tukahamasishana kupanda miti. Tunaweza pia kutembea na agenda ya kilimo, viwanda, biashara, uvuvi na nyingine tukajenga uchumi wa nchi na sio kuhamasishana kubet.​
 
Kwa sasa michezo ya kubahatisha nchini Tanzania imekuwa sehemu ya chanzo cha mapato ya serikali kwani kwa mujibu wa ripoti ya Bodi ya michezo ya kubahatisha (GBT) mwaka wa fedha 2020/2021 mzunguko wa fedha katika sekta ndogo ya michezo ya kubahatisha ulikuwa ni miamala yenye thamani ya Tshs 3.17 trilioni na makusanyo ya Serikali yalikuwa Tshs 132 bilioni
Duh, asee ni biashara kubwa.

Kama serikali imeshindwa kuvitumia vyombo vya habari kuhamasisha mambo muhimu kwa vile ujasiriamali, utunzaji wa mazingira, kupinga ukatili, kupinga madawa ya kulevya na kuhamasisha kilimo tutarajie taifa la watu wavivu wasio na uwezo wa kufikiri bali kutarajia utajiri wa haraka haraka bila kufanya kazi​
Yaani ni masikitiko, haifai kuwa na taifa linaloamini katika kupata pasipo kufanya kazi yoyote ya kueleweka kwa jamii.

Pesa inatakiwa kumfikia yule mtu ambaye amefanya kitu kwa jamii -kipato cha shughuli halali...... au basi anaenda kifanua kambo la kuifaidisha jamii - kapewa mkopo akaanzishe mradi.

Lakini hii ya mtu kukizwa mazingira ambayo haioni juhudi ikileta matokeo sio mfumo bora wa kijamii. Italeta mpasuko ambao kama hautarekebishwa basi sijui.

Unegusia jambo nyeti sana, kwa kuangalia mbali zaidi serikali ilizingatie. Na sio kutazama tu pafupi (kodi za fasta) zitatugharimu.


Kwa upande mwingine, linaweza kukaa kama jopo na kuuiba huu mfumo wa kutoa pesa za kubahatisha (national lotto) lakini chini ya sheria kwamba ni lazima anayezipata akafanyie kazi biashara aliyoainisha katika mpango wake wa biashara (bussiness plan)
 
a kujenga Tanzania tuitakayo ndani ya miaka 25 ijayo michezo ya kubahatisha ipigwe marufuku na serikali iangalie agenda muhimu za kutembea nazo ili kujenga taifa, kama ambavyo tulitembea na kauli mbiu ya Tanzania ya kijani ili kulinda mazingira tukahamasishana kupanda miti. Tunaweza pia kutembea na agenda ya kilimo, viwanda, biashara, uvuvi na nyingine tukajenga uchumi wa nchi na sio kuhamasishana kubet.
Kubeti, kuwe kama sigara kwa baadhi ya nchi, isitangazwe sana kuvutia watu kisaikolojia. Ibaki kama mchezo tu sio kazi ya kupigiwa upatu
 
Back
Top Bottom