Tanzania Tuitakayo competition threads

Tanzanized S

New Member
May 3, 2024
3
3
Tanzania iko katika wakati muhimu sana katika safari yake ya maendeleo. Kama Taifa ni muhimu kuandaa ramani ambayo itakuwa muongozo wetu kwa miaka 20 ijayo, ramani ambayo itagusa sekta zote muhimu katika ustawi wa nchi. Katika makala hii nimeelezea mpango wa maendeleo tunaoweza kuutumia;

Screenshot_20240504-030023~2.jpg

Ramani ya Ukanda wa Afrika Mashariki ikionesha uelekeo wa Kimbunga Hidaya katika pwani ya Tanzania. Source: Zoom Earth

Afya: Katika sekta ya afya serikali ilenge kuwapatia raia wote bima ya afya ya msingi kabla ya mwaka 2044.

Ihakikishe kwamba huduma bora za afya zinawafikia wananchi wote, mijini na vijijini. Hili litafanikishwa kwa kuimarisha miundombinu ya afya, kutoa mafunzo hitajika kwa wahudumu wa afya na kupeleka wataalamu zaidi katika maeneo ya vijijini.

Aidha, hatua za kinga ya afya zipewe kipaumbele kwa kutekeleza kampeni za chanjo kwa magonjwa yanayozuilika kwa chanjo, bila kusahau kipaumbele kwenye afya ya uzazi na watoto kwa ustawi wa vizazi vijavyo.

images (3).jpeg

JP Magufuli akikagua mashine ya kupiga picha za viungo ndani ya mwili (MRI Scan). Source: MNH Mloganzila

Elimu: Kufikia mwaka 2044, Tanzania iwe na mfumo imara wa elimu utakaohakikisha upatikanaji wa elimu kwa raia wote bila kujali tofauti zao za kiuchumi.

Pamoja na suala la elimu bure kwa shule za msingi mpaka sekondari, serikali ifanye uwekezaji katika miundombinu ya elimu kwa kujenga shule za kisasa na vituo vya elimu ya ufundi katika maeneo yenye uhitaji.

Aidha, Mtaala wa elimu ufanyiwe marekebisho yatakayosaidia kukuza uwezo wa kufikiri kwa kina na kutatua matatizo bila kusahau kuwajengea wanafunzi ujuzi wa kidijitali ili kuwaandaa kwa changamoto za soko la ajira la karne ya 21.


images (5).jpeg

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Pamba wakijisomea wenyewe kwenye chumba maalum cha kompyuta. Source: pambasec.blogspot.com

Mazingira: Udhibiti wa mazingira upewe kipaumbele katika ajenda ya maendeleo ya Tanzania.

Ili taifa letu liweze kuhifadhi urithi wake wa asili na kuurithisha kwa vizazi vijavyo tunapaswa kudhibiti uwiano kati ya shughuli za kiuchumi na uhifadhi wa mazingira.

Pamoja na juhudi za kupanda miti, serikali ihamasishe matumizi ya nishati jadidifu ili kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa.

IMG_20240504_155527_820~2.jpg

Matumizi ya Nishati safi ya gesi kupikia

Teknolojia: Katika kipindi cha miaka 20 ijayo, inawezekana kabisa kwa Tanzania kuwa kitovu cha Afrika Mashariki na kati katika suala zima la teknolojia na uvumbuzi.

Hilo litatimia kama tu serikali itaamua kwa nia ya dhati kabisa kuwekeza katika kuboresha miundombinu ya mawasiliano ili kurahisisha upatikanaji wa intaneti katika maeneo yote nchini.

Serikali iongeze uwekezaji katika tafiti na kuboresha sera za uwekezaji katika teknolojia ili kuchochea uanzishwaji wa kampuni za kidijitali.

Matumizi ya teknolojia yataimarisha utoaji wa huduma katika sekta mbalimbali kama vile kilimo, fedha, na utawala hivyo kurahisisha maisha.

download.jpeg

Kiwanda cha kutengeneza magari aina ya Toyota. Source: Bloomberg

Uchumi: Ili kukuza uchumi wa taifa na mtu mmoja mmoja serikali ihamasishe wafanyabiashara kuwekeza katika Viwanda vidogo vidogo na vya kati kwa kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji.

Kufanya hivyo kutasaidia kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira jambo litakalosaidia kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na kuondoa utegemezi wa bidhaa kutoka nje huku mauzo ya bidhaa zilizoongezewa thamani nje ya nchi yakiliongezea taifa mapato na fedha za kigeni.

Pamoja na sekta ya uzalishaji viwandani, serikali ihakikishe sekta nyingine zinazoliingizia taifa fedha za kigeni zinafanyiwa uwekezaji utakaochochea ukuaji wake zaidi.

Katika Utalii kwa mfano; pamoja na ujenzi wa barabara za lami, serikali ijenge viwanja vya ndege katika maeneo yote ya kitalii nchini ili yaweze kufikika kwa urahisi.

Tail_of_a_Boeing_737_of_ATC_in_1995.jpg
Mkia wa ndege ya ATC aina ya Boeing 737 mwaka 1995. Source: Wikipedia


Miundombinu mingine ya utalii kama ujenzi wa hoteli ichangamkiwe na wawekezaji wa ndani ili pesa wanazotumia watalii katika hoteli hizo zibaki hapa nchini.

Sekta nyingine ya muhimu kwa uchumi wetu ni Kilimo. Katika kilimo serikali ihakikishe upatikanaji wa pembejeo ni wa uhakika katika maeneo yote nchini.

Ikibidi, gharama inayotumika kuweka ruzuku kwenye mbolea ielekezwe katika ujenzi wa viwanda vya kuzalisha mbolea hapa nchini ili kuokoa fedha zetu.

Sekta ya kilimo ikisimamiwa vizuri, si tu kwamba tutakuwa na uhakika wa chakula nchini lakini pia tutakidhi mahitaji ya malighafi katika viwanda vyetu.

Usalama: Kwa kutambua umuhimu wa amani na usalama katika maendeleo ya nchi, ndani ya miaka 20 ijayo Tanzania iimarishe mfumo wake wa ulinzi ili kuwa tayari kudhibiti matishio ya amani yanayoweza kujitokeza. Mfano; Ugaidi, Uvamizi wa kimataifa, na mashambulizi ya kimtandao.

800px-FIB-training-22_(9311333487).jpg

Wanajeshi wa Tanzania wakiwa kwenye mafunzo maalum kwa ajili ya mission ya MONUSCO chini ya UN. Source: Wikipedia

Hii ijumuishe kuimarisha uwezo wa kutekeleza sheria ili kudhibiti matukio ya uhalifu yanayotokea mara kwa mara nchini.

Pia serikali iwekeze katika ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa za kijasusi, na kuimarisha zaidi sera yetu ya mambo ya nje kwa kukuza ushirikiano wa kikanda katika kushughulikia changamoto za kiusalama katika nchi jirani zinazoweza kuvuka mipaka.


Kwa kuhitimisha, Dira ya maendeleo kwa miaka 20 ijayo ilenge kuwa na taifa lenye maendeleo kiuchumi na jamii yenye ustawi inayoishi kwa amani bila hofu za kiusalama.

Kwa kuweka kipaumbele katika sekta hizo na nyingine ambazo sijazigusa kama Madini, Uchumi wa Blue n.k, Tanzania inaweza kupiga hatua kubwa mno kimaendeleo na kuwa miongoni mwa mataifa 5 tajiri zaidi barani Afrika.

Ili yote hayo yatimie tunahitaji Uongozi thabiti utakaoweza kusimamia utekelezaji wake bila kuyumbishwa.

MWISHO!
 
Afya: Katika sekta ya afya serikali ilenge kuwapatia raia wote bima ya afya ya msingi kabla ya mwaka 2044.
Swali hili ninamuuliza kila anayeitaka bima ya afya.

Je mpango wa kuchangia gharama (cost sharing) na mpango wa bima upi una mashiko zaidi kwa tabia za watanzania na afya zao. Mimi nahisi kuchangia gharama papo kwa hapo huongeza uwajibikaji wa mtu binafsi kwa afya yake, wewe una maoni gani mtoa mada??


Aidha, hatua za kinga ya afya zipewe kipaumbele kwa kutekeleza kampeni za chanjo kwa magonjwa yanayozuilika kwa chanjo, bila kusahau kipaumbele kwenye afya ya uzazi na watoto kwa ustawi wa vizazi vijavyo
Sawa sawia, sambamba na elimu ya kinga. Ahsante.

Pamoja na suala la elimu bure kwa shule za msingi mpaka sekondari, serikali ifanye uwekezaji katika miundombinu ya elimu kwa kujenga shule za kisasa na vituo vya elimu ya ufundi katika maeneo yenye uhitaji.
Ninarudi tena kwenye kukazia swali. Je hatuoni kwamba ile kitendo cha mzazi kumwambia mwanae "Ninakulipia ada, sasa ole wako uchezee elimu.." au "Nyie watoto, wazazi wenu wamewalipia ada halafu mnafanya nini mtaani saa hii?" Inasaidia katika uwajibikaji.?.??
Ni nini kinatuvutia kwenye bure lakini watanzania?


Serikali iongeze uwekezaji katika tafiti na kuboresha sera za uwekezaji katika teknolojia ili kuchochea uanzishwaji wa kampuni za
Ninakubali, taifa lazima liendeshwe kisomi.
Mada nzuri sana mtoa mada
 
Je mpango wa kuchangia gharama (cost sharing) na mpango wa bima upi una mashiko zaidi kwa tabia za watanzania na afya zao. Mimi nahisi kuchangia gharama papo kwa hapo huongeza uwajibikaji wa mtu binafsi kwa afya yake, wewe una maoni gani mtoa mada??
Lengo kuu la bima ya afya ni kuwahakikishia wananchi uhakika wa matibabu hata pale wanapokuwa na hali mbaya kiuchumi.

Tabia ya watu kusubiri wakumbwe na ugonjwa mbaya ndipo waende kutibiwa imegharimu maisha ya Watanzania wengi. Ugonjwa hauna hodi, watu wanakumbwa na maradhi yanayohatarisha uhai wakati hawana uwezo wa kugharamia matibabu. Lazima utakubaliana na mimi kwamba watu wengi wanapoteza maisha, si kwa sababu magonjwa yao hayatibiki, ila kwa sababu wameshindwa kumudu gharama za matibabu.

Mimi nadhani bima ya afya itawajengea watu mazoea mazuri ya kuchunguza afya zao mara kwa mara kwa kuwa haitawalazimu kutumia pesa kila wanapohitaji kufanya hivyo. Kwa namna hiyo magonjwa yatagundulika mapema jambo litakalorahisisha matibabu na kuokoa maisha ya watu wetu.

Kila nikilitazama suala la bima ya afya naona faida tu kuliko hasara. Taifa linakuwa na watu wenye afya ambao pia wana uhakika wa kupatiwa matibabu muda wowote afya zao zinapodhoofika.

.
 
Je hatuoni kwamba ile kitendo cha mzazi kumwambia mwanae "Ninakulipia ada, sasa ole wako uchezee elimu.." au "Nyie watoto, wazazi wenu wamewalipia ada halafu mnafanya nini mtaani saa hii?" Inasaidia katika uwajibikaji.?.??
Ni nini kinatuvutia kwenye bure lakini watanzania?
Ni kweli kwamba kulipia elimu kunachochea uwajibikaji kwa sababu wazazi wanakuwa na uchungu na pesa zao jambo linalowafanya wawakazie wanafunzi kuhusu kuwa makini na masomo.

Lakini naamini kwamba wazazi wanawatakia mema watoto wao, kwahiyo sidhani kama wataacha kuwahimiza kusoma kwa bidii kisa tu serikali imewasaidia kugharamia ada.

Hata hivyo, lengo kuu la elimu bure ni kuhakikisha kila mtoto anapata haki yake ya msingi ya kuelimika bila kisingizio chochote.

Kwa kuondoa kisingizio cha hali mbaya ya kiuchumi, serikali inapata haki ya kumburuza mahakamani mzazi anayejaribu kumnyima mwanae haki ya kuelimika either kwa kutaka kumuozesha au vinginevyo.

.
 
Back
Top Bottom