TANROADS Kutumia Teknolojia Mbadala Ujenzi wa Barabara Nchini

Stephano Mgendanyi

JF-Expert Member
May 16, 2020
1,898
943

TANROADS KUTUMIA TEKNOLOJIA MBADALA UJENZI WA BARABARA NCHINI

Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), imefanya majaribio ya awali ya matumizi ya teknolojia mbadala katika ujenzi wa Barabara kwa baadhi ya maeneo na inaendelea kutathmini ufanisi wake kwenye mazingira kwa kutumia teknolojia hizo mpya za kisasa zinazotumia gharama nafuu.

Hayo yameelezwa Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa Februari 6, 2024 wakati akijibu swali la Mbunge wa Busekelo Atupele Mwakibete aliyetaka kujua Je, Serikali haioni haja ya kutumia teknolojia mpya ya kisasa na gharama nafuu katika ujenzi wa Barabara nchini.

Waziri Bashungwa amesema Mtaalam wa ujenzi kwa kutumia teknolojia hizo amepatikana na majaribio yatafanyika katika Barabara ya Chamwino Ikulu – Babalo – Itiso (km1.1) mkoani Dodoma kwa kutumia teknolojia ya Geopolymer Stabiliser na Barabara ya Mtwara – Mnivata (km 12) mkoani Mtwara kwa kutumia teknolojia ya Amarseal Surface Rejuvenator.

Amfafanua kuwa teknolojia hizo zimeanza kutekelezwa na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) ambapo wataalamu wameeleza zimekuwa na manufaa katika Barabara ambazo zinapita magari yasiyo na uzito mkubwa.

Aidha, akijibu swali la Zainab Katimba Mbunge wa Viti Maalum aliyeuliza Je, ni lini upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mkoa wa Kigoma utakamilika ambapo Bashubgwa amesema Mradi wa Upanuzi na Ukarabati wa Kiwanja cha Ndege cha Kigoma unatekelezwa na Mkandarasi M/S China Railway Engineering Construction Group Co. Ltd kwa gharama ya Shilingi Bilioni 46.6.

Amesema Mkandarasi alianza kazi tarehe 05 Septemba, 2023 na anatarajia kukamilisha utekelezaji wa mradi huo tarehe 05/03/2025 kwa mujibu wa Mkataba.
 
Back
Top Bottom