Bashungwa Amataka Mkandarasi Barabara ya Nanganga - Ruangwa Kuelekeza Nguvu Ujenzi wa Madaraja

Stephano Mgendanyi

JF-Expert Member
May 16, 2020
1,897
941
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameutaka Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Lindi kuhakikisha wanamsimamia Mkandarasi wa Kampuni ya China Railway 15 Bureau Group anayejenga barabara ya Nanganga – Ruangwa (km 53.2) kwa kiwango cha lami, kuelekeza nguvu katika ujenzi wa Daraja la Lukuledi ili kuwezesha magari na wananchi kupita eneo hilo ambalo limekuwa likijaa maji na kusababisha barabara kufunga.

Bashungwa ametoa agizo hilo mkoani Lindi wakati alipoambatana na Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Deo Ndejembi kukagua ujenzi wa miradi ya maendeleo na miundombinu ya barabara na Madaraja iliyoathiriwa na mvua.

“Nimefika na nimejionea changamoto ya mawasiliano ya barabara, kwa kuwa ujenzi wa madaraja unachukua muda mrefu hivyo Mkandarasi hakikisha unaelekeza nguvu katika ujenzi wa daraja hili ili kuruhusu shughuli za kimaendeleo kwa wananchi kuendelea kufanyika”, amesema Bashungwa.

Bashungwa amefafanua kuwa ujenzi wa madaraja ukikamilika utasaidia wananchi kuendelea kutumia barabara wakati Mkandarasi akiendelea kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami ambayo kwa sasa imefikia asilimia 78.

Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa Serikali imekwishasaini mkataba wa ujenzi wa barabara ya kuanzia Ruangwa – Nachingwea - Nanganga yenye urefu wa kilometa 106 kwa kiwango cha lami ambapo muda wowote kuanzia sasa Mkandarasi ataanza kupeleka vifaa vya ujenzi katika eneo la mradi.

Vilevile, Bashungwa ameitaka TANROADS kujipanga kikamilifu kukamilisha ujenzi wa barabara hizo kwa awamu zote mbili bila ya kuingiliana katika utekelezaji wake na hivyo kukabidhi kwa wananchi ambao wamekuwa wakiisubiria kwa muda mrefu.

“Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa barabara hiyo kwa Awamu ya Pili ili Mkandarasi huyo atakapokuwa anendelea kuikamisha ujenzi wa barabara hiyo sehemu ya Nanganga-Ruangwa aanze na utekelezaji wa Awamu ya Pili”, amefafanua Bashungwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainabu Telack, ameishukuru Serikali kwa jitihada zinazoendelea kufanyika katika mkoa huo ambapo baadhi ya maeneo yameshakarabatiwa na kufanyiwa matengenezo ya barabara katika maeneo yaliyoathiriwa na mvua inayoendelea kunyesha.

Pia, Zainabu amewataka wananchi kuwa na Subra katika kipindi hiki ambacho mvua zinanyesha nyingi na Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuchukua hatua katika kila maeneo ambayo yametokewa na changamoto.

Akitoa taaarifa ya miundombinu ya barabara, Meneja wa TANROADS, Mkoa wa Lindi, Eng. Adrea Kasamwa ameeleza kuwa utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya Nanganga – Ruangwa (km 53.2) kwa kiwango cha lami umefikia asilimia 78 na mkandarasi amekwishaomba kuongezewa muda wa utekelezaji kutokana na changamoto za Mvua nyingi zitakazopelekea kuchukua muda kwenye ujenzi wa madaraja.

WhatsApp Image 2024-03-05 at 11.15.31.jpeg
WhatsApp Image 2024-03-05 at 11.15.32.jpeg
WhatsApp Image 2024-03-05 at 11.15.32(1).jpeg
WhatsApp Image 2024-03-05 at 11.15.33.jpeg
WhatsApp Image 2024-03-05 at 11.15.33(1).jpeg
WhatsApp Image 2024-03-05 at 11.15.35.jpeg
 
Back
Top Bottom