Tamasha la Mwaka Mpya wa jadi wa China linalorushwa na CMG lazidi kujibebea umaarufu duniani

Yoyo Zhou

Member
Jun 16, 2020
72
111
Tamasha la Mwaka Mpya wa jadi wa China (CCTV Gala) ama kwa jina jingine linajulikana kama Chunwan, ni tamasha maalum la Mwaka Mpya wa jadi wa China linalotayarishwa na Shirika Kuu la Utangazaji la China, (CMG). Tamasha hili ambalo hutangazwa kila mwaka katika mkesha wa Mwaka Mpya wa China sio tu linaangaliwa kupitia televisheni ya CCTV-1 ya China, bali pia nchi nyingine duniani huangalia tamasha hili kupitia Mtandao wa Televisheni wa Kimataifa wa China (CGTN).

chunwan.jpg


Tamasha hili lina watazamaji wengi zaidi likilinganishwa na kipindi chochote cha burudani duniani, na linatambuliwa na Rekodi za Dunia za Guinness kama kipindi cha televisheni kinachotazamwa zaidi duniani. Kipindi cha tamasha hili kilichorushwa kwenye mkesha wa Mwaka Mpya wa jadi wa China mwaka 2018, kilivutia watazamaji zaidi ya bilioni moja. Safari hii gala ama tamasha hili lilioneshwa tarehe 9 Februari mwaka 2024, ambayo ndio ilikuwa siku ya mkesha wa mwaka mpya hapa China. Kabla ya kuoneshwa kwa tamasha hili maandalizi makubwa hufanyika yanayogharimu kiasi kikubwa cha fedha.

Mwaka huu, kwa bahati nzuri, nilishiriki kwenye maandalizi ya kurikodi tamasha la opera ambalo pia ni kama tamasha endelezo la tamasha la mwaka mpya wa mkesha huko Deyang, mkoani Sichuan. Wasanii mbalimbali wa opera walifika huko kwa takriban wiki moja kabla ya kurikodiwa. Hii ni mara ya pili kwa tamasha hili kufanyika mkoani Sichuani, kwasababu imezoeleka kwamba mara kwa mara huwa linafanyikia Beijing. Mambo yanayooneshwa kwenye kipindi cha tamasha hili ni pamoja na muziki, dansi, vichekesho, maonesho ya maigizo na mambo mengine mengi.

chunwan123.jpg


Nikiwa miongoni mwa washiriki wa maandalizi ya tamasha hili la opera, nilifunga safari kutoka Beijing kwenda Deyang, Sichuan, nikiambatana na timu ya wafanyakazi wenzangu wa CMG kwenda kushuhudia maandalizi yanavyofanyika hadi siku ya kilele ambayo ni siku ya kurikodiwa. Likiwa ni tamasha linalooneshwa mara moja tu kwa mwaka, ni nafasi adimu kabisa kwa sisi wageni kushuhudia kwa macho yetu mchakato mzima wa maandalizi yake. Labda kabla ya kuendelea mbele wacha nikudokeze kwa ufupi tu historia ya tamasha la mwaka mpya wa jadi wa kichina kwa ujumla..

Katika nyakati za kale, unapofika wakati wa mkesha wa mwaka mpya, watu wa China walikuwa wakicheza ngoma ya simba, ngoma ya dragon, na aina nyingine za sarakasi. Hata hivyo tangu yafanyike mageuzi na ufunguaji mlango, maisha ya watu wa China yakaanza kuboreka hatua kwa hatua na kufanya maisha yao ya kitamaduni kuwa tunu kubwa.

Wakati maisha yanazidi kuwa bora, watu walikuwa na burudani chache sana, na kwa kuwa familia nyingi zaidi za Wachina ziliweza kumudu televisheni katika miaka ya 1980, kuandaa sherehe ya kitaifa kwenye TV likawa ni jambo linalowezekana. Kwa hiyo mwaka 1983, CCTV ilitangaza tamasha lake la kwanza la Mwaka Mpya moja kwa moja. Tangu wakati huo, kila inapofika siku ya mkesha wa Mwaka Mpya wa China, tamasha hili likawa linatangazwa kuanzia saa 2:00 usiku, na kuendelea kwa saa 4.50. Ikumbukwe kwamba Mwaka Mpya wa China ni kipindi ambacho familia zinajumuika pamoja. Hivyo Gala la Mwaka Mpya linalooneshwa na CCTV linabeba jukumu muhimu katika sikukuu hii maalum.

Mimi safari hii nikiwa mshiriki wa tamasha la opera, nilivaa mavazi mbalimbali ya kale ambayo yanaoneshwa kwenye opera, huku uso wangu ukiwa umerembwa na kuonekana kama wachezaji wa opera. Mavazi hayo ni pamoja na vazi la hakimu, vazi la malkia, vazi la jenerali mwanamke na pia vazi la kale la wasichana.

Nikiwa shabiki mkubwa wa mila na desturi za kale za China, ambazo nyingi nimezijua kupitia tamthilia za kihistoria zinazoonesha hadithi mbalimbali za uhalisia zilizowahi kutokea katika enzi mbalimbali za China, ilikuwa ni furaha isiyo na kifani kwangu kuweza kuyaishi maisha ya kale japo kwa dakika mbili tatu. Ndio maana waswahili waliposema kwamba “vya kale ni dhahabu” hawakukosea hata kidogo.

Mbali na mimi binafsi kupata uzoefu wa tamasha hili, pia niliweza kutangamana na wasanii mbalimbali wakubwa, wakiwemo wa filamu zinazorushwa kwenye televisheni na opera. Waigizaji wengi wa Chunwan wamejibebea umaarufu mkubwa nchini China kwa sababu ya kuonekana kwao mara kwa mara kwenye tamasha hili. Kwa hiyo kama nilivyosema awali kwamba hii ni fursa adimu kuipata, kwasababu kwa kipindi chote nilichoishi China takriban miaka 16 sasa, hii ni mara yangu ya kwanza kujionea maandalizi ya tamasha hili na kutangamana na wasanii wakubwa wa China.

Kwa kuwa kipindi hiki kinatazamwa na Wachina wengi zaidi kuliko vipindi vingine vyovyote, sio tu ndani ya China yenyewe bali pia Wachina wa ng'ambo na watazamaji wa nchi za nje kupitia chaneli za kimataifa za CCTV, maonesho katika Gala la Mwaka Mpya yanaweza kuibua jina lisilojulikana la msanii wa China na kuwa mtu mashuhuri duniani. Msanii huyu ana uwezekano wa kupanda hadhi ya kimataifa na kupata umaarufu kwenye mitandao ya kijamii mara moja.

Sentesi hizi “Xin Nian Kuai le” na “Guo Nian Hao” zenye maana ya “Heri ya Mawaka Mpya” ni sentensi maarufu sana katika kipindi hiki cha sikukuu. Watu kwenye tamasha hili huanza kuhesabu sekunde kadhaa kabla ya saa sita usiku, na inapotimia saa sita kamili za usiku watu wote waliohudhuria tamasha hili pamoja na watazamaji husikika wanazitamka kwa pamoja kuashiria kwamba mwaka mpya umeingia. Nami nisiwe na hiyana niseme tu Xin Nian Kuai le! ama Guo Nian Hao!
 
Ni vizuri kulinda utamaduni.

wachina mnaupiga mwingi katika kulinda utamaduni sisi wacha tuendelee kufukuza na kuonea maasai
 
Back
Top Bottom