SoC01 Taka kama fursa kiuchumi, utunzaji mazingira na umuhimu wake

Stories of Change - 2021 Competition

Golden Eagle

New Member
Jul 14, 2021
2
0
UTANGULIZI.

Mazingira ni nyenzo muhimu sana katika Maisha ya Mwanadam hasa ikichukuliwa kwamba kila kiumbe chenye uhai hutegemea Mazingira (asili) ikiwemo udongo, maji na hewa. Hii yote hudhihirishwa hata katika masimulizi ya uumbaji ndani ya vitabu vyote vya Dini.

Kabla ya Maisha ya Mwanadamu na viumbe vingine hai Mwenyezimungu aliumba Mazingira kwanza kwa siku sita (Mwanzo 1:1-25 na Qur an 50:38), uumbaji wa Mazingira ulilenga kumwezesha Mwanadam kuishi vizuri pamoja na viumbe vingine hai.

Mazingira yakitunzwa vizuri na kuwa safi na salama huchangia kwa 100% Maisha ya Mwanadam na viumbe wengine hai juu ya uso wa Dunia kuwa endelevu hasa kwa kuhakikisha upatikanaji wa chakula, maji, matunda na hewa safi.

Mbali na umuhimu mkubwa wa Mazingira safi kwa Mwanadam, Mazingira yetu yanakumbwa na changamoto kubwa ya uharibifu hususani kutokana na taka zinazozalishwa nyumbani na viwandani ambazo zimekuwa tishio si kwa Mazingira tu bali hata kwa viumbe hai vipatikanavyo juu ya uso wa Dunia na vile viishivyo ndani ya maji.

Tangu mwanzoni mwa Karne ya 20 mpaka leo hii pamekuwa na ongezeko la uzalishaji taka katika makazi yetu na viwandani ambapo ongezeko hili limechangiwa sana na ongezeko la idadi ya watu. Taka za aina mbalimbali za taka ikiwemo taka laini (aghalabu mabaki ya chakula) ambazo huoza kwa haraka ambazo mara nyingi huzalishwa nyumbani na sokoni, pia kuna taka ngumu ambazo huchukua muda mrefu sana kuoza na mara nyingi taka hizi hujumuisha plastiki zinazozalishwa Viwandani.

Mazingira yetu kwa kiasi kikubwa yameathiriwa na taka hizi hali ambayo inatishia uwepo wa viumbe hai mbalimbali waishio juu ya uso wa Dunia na ndani ya Maji. Lakini pia taka hizi zinachangia sana katika uzalishwaji wa hewa ya ukaa ambayo inaathari kubwa katika anga hewa na kupelekea baadhi ya maeneo kukumbwa na ongezeko kubwa la joto, theluji kuyeyuka, kina cha bahari kuongezeka na hata mmong’oyoko wa udongo, hali hii itokanayo na uharibifu wa Mazingira huitwa Mabadiliko ya Tabia Nchi.

MADHARA YA KUTOKUTUNZA MAZINGIRA.

Mabadiliko ya Tabia Nchi ni hali ambayo si ya kawaida iipatayo Dunia na kuharibu asili yake ya Kimazingira. Hali hii hupelekea ongezeko la joto, theluji kuyeyuka, mvua nyingi, mafuriko, mioto ya msituni, kutoweka kwa viumbe hai pamoja na mmong’onyoko wa udongo.



Mabadiliko ya tabia Nchi huambatana na athari mbalimbali kama ilivyo orodheshwa hapo juu, lakini athari zake kubwa huonekana katika ardhi hasa pale mvua zinaponyesha kupita kiasi na kusababisha mafuriko ambayo humong’onyoa udongo na kuacha mashimo katika barabara zetu pia kubebwa kwa udongo wenye rutuba na kupelekea uzalishaji kupungua.

Picha ifuatayo inaonesha namna Mazingira yalivyoharibiwa baada ya mvua zisizo za kawaida kunyesha Mkoani Tabora, Kata ya Chemchem, mtaa wa Baruti.
1627542220453.png





Mabadiliko haya ni matokeo ya kuzagaa kwa taka mbalimbali katika Mazingira yetu ambazo zimeshindwa kudhibitiwa vyema na mwisho kuleta athari hasi katika Mazingira yetu.

Hali hii inapelekea kuwepo kwa uhitaji wa maarifa ya msingi ya namna ya kutenganisha na kudhibiti taka ili kuweza kupunguza na kuondoa kabisa uzagaaji wa taka katika Mazingira yetu. Jamii zetu bado zina nafasi kubwa ya kuweza kukusanya na kudhibiti taka kwa kuzigeuza taka hizo kuwa fursa endapo tu maarifa sahihi juu ya udhibiti taka yatatolewa kama ifuatavyo;

MAPENDEKEZO JUU YA NAMNA YA KUTUNZA MAZINGIRA.

Moja, Jamii inaweza saidiwa kupatiwa maarifa ya namna ya kuandaa mpango maalumu wa kudhibiti taka ili kupunguza taka katika maeneo yanayowazunguka. Mpango huu unaweza husisha uandaaji wa maeneo maalumu kwa ajili ya kukusanya na kutenganisha taka kwa aina zake ili iwe rahisi kwa taka zinazoweza kutumika kama malighafi kuchukuliwa na kutumika tena na zile zinazohitaji kuteketezwa ziweze kuteketezwa kwa urahisi na kwa njia zisizokuwa na athari kubwa katika Mazingira yetu.


1627542130869.png

Mfano wa kifaa kinachopaswa kuwepo katika kituo cha ukusanyaji taka cha Kijamii.



Vilevile kwa taka zinazozalishwa nyumbani na sokoni. Jamii inaweza shauriwa kwanza ikiwa taka nyingi za nyumbani zinatokana na mabaki ya chakula, basi wanajamii waelemishwe na kushauriwa kuandaa chakula kinachotosha wanajamii waliopo ili kuepuka uzalishwaji wa mabaki ya chakula, na ikiwa mabaki yatazalishwa basi njia nzuri ya kutumia mabaki hayo kama malighafi kwa ajili ya kutengeneza aidha chakula cha mifugo au mbolea (mboji) basi ziweze kutumika ili kuepusha kuzagaa kwa mabaki hayo na kuleta athari hasi katika Mazingira. Pia taka zinazozalishwa sokoni zaweza kutumika katika uzalishaji wa funza kama chakula cha mifugo hususani Kuku na Samaki. Picha chini ni taka za nyumbani na sokoni.





1627541843648.jpg


Takataka za plastiki hususani zile zitokanazo na matumizi ya maji zinaweza tumika pia kama malighafi za ujenzi au vifaa vya kutengenezea bustani ya mbogamboga na maua badala ya kuyatupa na kuyaacha yazagae mtaani na kuwa ni uchafu katika Mazingira yetu.



1627541843777.jpg
1627542391400.png


Ukusanyaji taka za Plastiki. Kuziandaa chupa za Plastiki kwa matumizi mengine.



1627541843908.jpg
1627542275736.png


Ujenzi wa kibanda cha biashara kwa kutumia Chupa za Plastiki. Kibanda kilicho kamilika kwa malighafi ya chupa za Chupa za Plastiki.

Vilevile ili kudhibiti taka zisilete athari katika Mazingira yetu, ni muhimu na lazima pawepo na vyombo maalumu kwa ajili ya kukusanyia taka mbalimbali kwa aina zake ili ziweze kutumika tena au kuteketezwa pasipo kuleta madhara hasi katika Mazingira yetu. Vyombo hivi vyaweza kuwa Mapipa maalumu yanawekwa katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa kama vile sokoni, vituo vya mabasi, vituo vya garimoshi, hospitali, shuleni, katika viwanja vya michezo pamoja na maeneo ya minada ambapo huchukua watu wengi kwa wakati mmoja. Hili laweza kufanywa na watu binafsi, Serikali kupitia Halmasahuri za Manispaa lakini pia Taasisi pamoja na wadau mbalimbali wa Mazingira.

Pia sehem maalumu zaweza kutengwa kwa ajili ya uchimbaji wa mashimo maalumu ya kufukia taka (landfill) hususani zile zenye madhara ya moja kwa moja kwa Wanadam na Viumbe hai vingine. Mfano taka za vioo vilivyovunjika, vimiminika vya sumu pamoja na taka zinazotokana na bidhaa za chakula zilizokwisha muda wake wa matumizi au ambazo hazijakidhi ubora wa viwango vya matumizi ya Binadam au Viumbe hai vilivyolengwa.

Pia taka zinaweza dhibitiwa vyema kwa kuzirejeshea tena thamani yake na kutumika tena kama bidhaa, rasilimali au vyombo kwa matumizi mengine. Kama ilivyoainishwa hapo juu, taka nyingi ambazo huzalishwa nyumbani na sokoni hutokana na mabaki ya chakula na matnda ambayo huoza kwa haraka sana hivyo taka hizi zaweza kurejeshewa thamani kwa kuozeshwa na kutumika tena kama mbolea au mboji. Pia taka za plastiki toka viwandani mbali na kutumika kama malighafi za ujenzi, zinaweza kuchakatwa na kutumika tena katika kuzalisha bidhaa zingine kwa ajili ya matumizi mbalimbali.



1627541844069.jpg


Taka za Plastiki zinazosubiri kuchakatwa. Uokotaji wa taka toka mto Kenge,Chemchem,

Manispaa ya Tabora.



FAIDA ZA UTUNZAJI MAZINGIRA.

Utunzaji wa Mazingira una faida kubwa sana katika kuhakikisha Dunia yetu inakuwa sehem salama kwa Maisha ya Binadam na Viumbe wengine walio hai waishio juu ya uso wa Dunia na ndani ya maji kma ifuatavyo;

Utunzaji wa Mazingira huhakikisha shughuli za Kiuchumi zinakuwa endelevu kwa ustawi wa Maisha ya Binadam wakati wote. Mfano shughuli za Kilimo huwa za uhakika pale tu Mazingira yetu yanapotunzwa na kuwa salama ili kuwepo na upatikanaji mzuri wa ardhi yenye rubuta pamoja na maji ya kutosha kwa ajili ya kutawisha mazao. Hii pia itasaidia sana kuchangia katika Malengo ya Maendeleo endelevu ya Dunia hasa lengo namba 2 lisemalo kutokomeza njaa (Zero hunger).

Pia utunzaji Mazingira huhakikisha Maisha endelevu kwa viumbe waishio ndani ya maji kama inavyoainishwa katika Malengo ya Maendeleo endelevu ya Dunia hasa lengo namba 14 (Life below water) kwani maji ni moja kati ya maeneo ya Mazingira linaloharibiwa kwa kasi na kupelekea hata mazao yatokanayo na Maji kupungua na mengine kutoweka kabisa. Hivyo kwa kutunza Mazingira tutakuwa na uhakika wa ongezeko la mazao ya majini hususani samaki na kuchochea uvuvi ambao ni sehemu kubwa ya shughuli za Kiuchumi.

Vilvile utunzaji Mazingira huhakikisha Maisha juu ya uso wa Dunia yanakuwa endelevu kama inavyoainishwa katika Malengo ya Maendeleo endelevu ya Dunia kama inavyoainishwa katika lengo namba 15 (Life on Earth). Maisha juu ya uso wa Dunia huathiriwa sana na Mazingira yetu, hivyo Mazingira yanapotunzwa vizuri Dunia inakuwa salama kwa ajili ya Maisha endelevu kwa viumbe hai ikiwemo mimea, binadam na wanyama.

Pia utunzaji Mazingira husaidia sana tuweze kupata maeneo mazuri kwa ajili ya mapumziko ikiwemo maeneo na fukwe za bahari na maeneo mengine yenye kuvutia yakiambatana na hewa safi.

Mwisho Mazingira yakitunzwa vyema, Maisha huwa mema…tumerithi Mazingira yetu nasi tuwarithishe Watoto wetu kwa ajili ya Maisha endelevu.


NB: Picha zote zilizotumika ni kwa hisani ya (Chanzo) Mwandishi.
 
Back
Top Bottom