Tafadhali Thread hii wasisome wanawake ni kwa wanaume tu.

GAZETI

JF-Expert Member
Feb 24, 2011
5,126
2,000
NIMEITOA MAHALI KAMA ILIVYO KUTOKA KWENYE TIMELINE YA RAFIKI YANGU

NAOMBA 'MWANAMKE' YEYOTE ASISOME UJUMBE HUU.
Waraka huu ni mahsusi kwa wanamume tu. Nipotumiwa kwa mara ya kwanza, ulikuwa kwa lugha ya kigeni, lakini sasa nimeuleta katika Kiswahili ukiwa na ziada ya nasaha zangu ili ujumbe ufike mbali.
Ukichunguza utagundua kwamba, kumekuwepo na kasumba kwa watoto wengi kuwatii na kuwajali zaidi mama zao kuliko baba zao. Hali hii imezoeleka kiasi cha kuonekana ni jambo la kawaida kabisa.
Baada ya kushuhudia akina baba wengi wakivuja machozi, jasho na damu kwa kufanya kazi za sulba karibu maisha yao yote ya ujana ili tu kuwahudumia mke na watoto, na mwishowe wakiishia kudhalilika uzeeni na kufa kwa vihoro, nimeona niwafunulie pazia kubwa mpate kufumbua fumbo hili. Hivyo, kama wewe ni baba au baba mtarajiwa, makinika na ujumbe huu kwa mustawa wa maisha yako uzeeni.

Ewe baba, kumbuka, miaka kadhaa ijayo mkeo atakuacha nyumbani kwako (si kwa talaka), na kuanza kuruka leo kwa bintiye huyu, kesho kwa mwanaye yule. Atakwambia ati huko anakwenda kupumzika. Lakini wewe kama mume (baba), licha ya kuwa na haki na wanao, hautoweza kufanya hivyo. Utabaki ukilinda nyumba yako na kuisubiri siku isiyo na jina, ambayo mkeo ataamua kurudi.

Sasa jitambue, wewe ni kama 'mhudumu' tu ndani ya hiyo familia unayoiita ni ya kwako. Hiyo nyumba uliyopambana kuijenga si yako - ni mali ya watoto wako na mkeo. Hata kuiuza tu huruhusiwi. Mume ni kama trekta lijengalo barabara nzuri na imara, lakini mara baada ya ujenzi wa barabara kukamilika, litaletwa gari maalumu kuja kulibeba trekta juujuu na kuliondoa barabarani - kwa madai kuwa likipita hapo litaiharibu barabara. Yaani, trekta haliruhusiwi kupita kwenye barabara liliyoitengeneza lenyewe. Hivyo ndivyo hututokea akina baba. Tunajikusuru, tunasulubika, tunaingia madeni, tunavaa nguo chakavu, nk, ili tu kuwaridhisha watoto wasome vizuri. Lakini wakishahitimu na kuanza kujitegemea, hapo ndipo umuhimu wa baba unapomalizika na umakini wao huegemea kwa mama zao. Yumkini ni mama zao ndiyo huwapandikiza chuki vichwani mwao, kwa sababu wewe umekuwa ukiwahudumia bila kuwakaririsha jitihada zako lakini mama amekuwa akitumia mdomo kuhodhi sifa zote.

Ikifikia mahala unasikia zile kauli za akina mama wengi: "Isingelikuwa mimi, usingekwenda shule!" Au "baba yako alichojua yeye ni pombe na wanawake wakati mimi nikitaabika kukuleeniu!" Ujue ule muda wa kuondolewa lile trekta lililojenga barabara umewadia.

Kimsingi, mtoto atakapoanza kufanya kazi, baba huwa amekwishastafu na mategemeo yake hubaki kwa watoto. Lakini huyo mtoto aliyefanikiwa, anapofika kutembelea familia baada ya mwaka mzima, masikini baba ataambulia shilingi elfu ishirini tu - tena mbele ya mkewe, ilhali mkewe (mama) atapewa hata laki moja akiwa peke yake jikoni. Kisanga kitaanza mtoto akishaondoka. Mama atamtaka baba atoe pesa kwa ajili ya matumizi (si aliziona wakati unapewa!?). Usipotoa, utaambulia uji usio na sukari. Na ukitoa, mtatumia nyote ndani. Lakini mama yeye ataamua ale bata atakavyo, kwakuwa maamuzi juu ya pesa aliyopewa faraghani ni siri yake na shetani wake. Hii ni moja kati ya sababu za akina baba wengi kufa mapema kwa vihoro (kwani hujaona mtaani wajane ni wengi kuliko wagane?).

Kwenye maisha ya uzeeni, kila uchao mama huruka kwenda kula bata na watoto wake huko ughaibuni ilhali baba hubaki nyumbani akitafuna mihogo na kunywa ukungu. Baada ya muda mrefu kupita, mama aliyenawiri kwa kupetiwa na watoto, akirudi nyumbani huanza kumshangaa baba aliyesawajika kwa kukosa uangalizi na usaidizi. Ikifikia hapo, usishangae kusikia watoto wako wametafutiwa 'anko'. Ndiyo - mume mwenziyo.

Nakutahadharisha ewe baba mwenzangu, dunia hii iliyojaa ghururi na hadaa haina huruma kwa waume-wazee ambao hawakujiandalia mazingira ya kujinufaisha walipokuwa vijana. Sasa basi, ukijenga nyumba yako, hakikisha kila mmoja anaelewa kuwa pale ni kwako - na si kwao. Jenga biashara mapema itakayokuja kukufaa uzeeni. Simika nguzo madhubuti utakazokuja kuegemea bila kutetereka huko uzeeni. Jenga mahusiano mema na marafiki watakaokufariji kipindi wanao watakapokuwa ubavuni mwa mama yao. Kipindi hiki cha ujana ndiyo sahihi kujishirikisha kwenye jumuiya na nyumba za ibada ambako utapata matumaini na msaada wa Muumba wako kipindi uzee utakapobisha hodi.

Uzee ni mzigo mzito kubebeka kwa akina walioendekeza kuwaandalia maisha watoto pekee kuliko kujihadhari na hatma za maisha yao ya baadaye. Kuchacha mfukoni na kukosa wafariji wema kati ya marafiki zako kipindi cha uzeeni, ni kama hukumu ya kifo chako. Ni suala la kusubiri tu saa ya ufu.

Zingatia haya makundi makuu matatu muhimu, utakayoyahitaji kadri unavyozeeka: familia (nduguzo), waumini wenziyo wa dini na marafiki zako wa ujanani (shuleni, kazini na mtaani).

Ewe baba mwenzangu, kubali au kataa, ukishagonga miaka 60 kwenda juu, upweke ndiyo kitu cha kwanza kitakachohatarisha uhai wako, kwani muda huo watoto uliowapigania kwa udi na uvumba, watakuwa busy kujenga familia zao kama tufanyavyo sisi hivi sasa. Ni muda huu ndipo utakapoanza kuona umuhimu wa makundi matatu niliyoyataja hapo juu.

Cha kufanya, pamoja na ugumu wa ratiba zako, tenga muda wa kwenda kusalimiana na kupiga soga walau kidogo tu na wale watakaokuja kuwa matabibu wako wa msongo wa mawazo wakati wa uzeeni. Usipowaandaa leo, hawatopatikana kesho. Wanaoshuhudia jitihada zako hivi leo, ni marafiki hawa wa ujanani - hao ndiyo watakaokuja kukutetea kwa kusadikisha ukweli dhidi ya hila na ngendembwe kwamba uliendekeza kuuchapa ulabu na wanawake badala ya familia.
Maendeleo mazuri ya wanao yasikuhadae ukaanza kujipiga kifua, mbele ya jumuiya na marafiki ambao siku si nyingi utawahitaji kukufariji kipindi hao wanao watakapokuwa busy kujenga familia zao - ilhali muda mchache watakaobakia nao wakiutumia kwa mama zao.

Popote mlipo akina baba wote gongeni cheers huku mkisambaza ujumbe huu kama sehemu ya kwanza ya maandalizi.
 

J.wawatu

JF-Expert Member
Dec 20, 2013
244
500
Ukitaka raha ya uzee ni kweli unapaswa kujiandaa kipindi cha ujana,
Na wengi wetu huwa tunakosea sana wakati wa kuoa tu!
Ila ukitaka raha ya uzee, usikubali kutofautiana sana na mwanamke angalau mpishane miaka miwili au mitatu uzee wako utafaidi sana!

Lakini unakuta mwanaume una miaka 35 unaoa binti wa miaka 25 au 23 hapo jua tu utapata tabu sana!
 

tremendous

JF-Expert Member
Aug 12, 2016
3,247
2,000
Wewe si una wazazi je unawapenda na kuwajali wote, watoto kama unao si unawajali na uko karibu nao? Kama jibu ni ndiyo basi ondoa shaka watoto watakutunza tu .

Mawazo kama haya huwezi kusikia kwa tycoons.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom