Tabora: Madiwani wamkataa Meneja RUWASA kwa madai ya kuwa na dharau

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,377
8,121
Baraza la madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua limeazimia kutofanya kazi na Mapambano Mashini ambaye ni kaimu meneja wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini na Vijijini (Ruwasa) wilayani Kaliua kwa madai ya kulidharau baraza hilo.

Uamuzi huo umesomwa kwa niaba yao na mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Kaliua, Japhael Lufungija baada ya kumjadili na kufikia uamuzi huo ulioungwa mkono na wote.

Katika kikao hicho, baraza lilikuwa linataka kusikiliza na kutoa maoni kuhusu rasimu ya bajeti ya Ruwasa kama utaratibu unavyotaka na kaimu meneja huyo baada ya kuulizwa amejipangaje kuhusu kuwasilisha bajeti hiyo ili madiwani waweze kutoa maoni yao, alijibu hana cha kufanya na kwamba mwenye uamuzi ni bodi ya Ruwasa Taifa.

Ruwasa na taasisi nyingine za serikali kama Tarura na Tanesco nazo zilikuwa zinawasilisha rasimu zao za bajeti katika baraza hilo ambalo pia linajadili rasimu ya bajeti yake kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Mashini alipoulizwa kama kauli yake ina maana baraza hilo halina maana kwake, haliwajibiki kuhusu mambo ya Ruwasa na yeye hawajibiki kwa baraza, alikubali na kuwafanya madiwani kushangaa.

Kutokana na kauli yake hiyo, Lufungija alimtaka aendelee na shughuli zake kwani kwenye baraza atakuwa anapoteza muda.

"Kwa vile umesena huwajibiki kwenye baraza hili basi tunakuruhusu uendelee na majukumu yako mengine maana sisi hututambui," amesema Lufungija na kisha Mashini alisimama na kutoka katika kikao hicho cha baraza la madiwani.

Wakimjadili kaimu meneja huyo, madiwani wamemweleza kama mwenye dharau na kiburi wakieleza hata akipigiwa simu huwa hapokei au kutoa ushirikiano.

Walieleza kuwa hali ya upatikanaji wa maji katika Wilaya ya Kaliua hairidhishi na mhandisi huyo sio mtu wa kutoa ushirikiano kwa madiwani na ndio maana hawajashangaa kauli yake hiyo.

Alipoulizwa kuhusu uamuzi huo, Mashini aliwaomba radhi madiwani, "kama niliwakosea kwa kuteleza kutokana na kauli yangu kwenye baraza, nawaomba wanisamehe na uamuzi waliochukua ni mkubwa sana."

MWANANCHI
 
Back
Top Bottom