UJUMBE WA WAZI WA ASKOFU KWA SPIKA WA BUNGE, DKT. TULIA ACKSON MWANSASU
Hongera Dkt. Tulia! Sasa wewe ndiye Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Waandishi wa Habari wanasema umewashinda washindani wako 8 kwa kupata kura zote na wao wameambulia patupu. Lakini sisi tunajua kuwa wewe haukuwa na mshindani kama jinsi ambavyo hakuna upinzani ndani ya Bunge.
Katika Theologia kuna dhana za predestination na preordination! Dhana hizi mbili zinaeleza wazo moja. Kwamba umeufikia wakati kama huo sio kwa uweza, elimu, ujanja, utendaji, mikakati au hata uadilifu wako! Bali umeufikia wakati kama huo kwa sababu ya predestination na preordination kuchukua mkondo wake. Kwamba hizo predestination na preordination ndizo zilizopelekea kuanguka kwa aliyekuwa Spika Job Ndugai, lisikutoke katika fikra zako!
Tunachoweza kukushauri sisi tulio Askofu ni kwamba uipokee nafasi hiyo kwa kutetemeka huku ukijua kuwa hatima ya predestinationa na preordination haibagui. Wewe ni shahidi wa jinsi ambavyo hatima hiyo iliyowatupa kando baadhi ya miamba iliyowahi kuwepo na kuvaa kiburi, majivuno na kujimwambafai! Wengi wao wamezama na kumbukumbu zao zinaendelea kufutika kama vile 'amatebhe' yaani maji ya mvua yanavyokauka haraka!
Ukipokea kijiti kutokana na mazingira ya nguvu ya predestination na preordination, unatakiwa kuwa makini na kunyenyekea. Katika uso wa dunia, wapo watu ambao walipoonywa, badala ya kupokea maonyo kwa unyeyekevu na upole, walitumia mamlaka na madaraka waliyokuwa nayo katika kuwatweza, kuwanyamazisha na hata ikibidi kuwapoteza wengine. Hatima yao haikuwa ndefu na dunia haijakosa mifano ya watu wa aina hiyo.
Lakini sisi Askofu tunao ujasiri wa kukueleza wewe hayo na wewe unaelewa fika kuhusu ujasiri huo na sababu zetu. Ukiyafuata hayo na kujitenga na kiburi pamoja na mitandio yake, hatima itakupeleka mbali na ukiyapuuza na kujipamba na kiburi pamoja na mitandio yake, hatima itakupa kisogo (Ezekieli 33:1-20).
Mwana Kondoo Ameshinda! Tumfuate!
Askofu Emmaus Bandekile Mwamakula