Taarifa ya kifo cha Sheikh Abdallah Rashid Sembe May 1999

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,915
30,259
TAARIFA YA KIFO CHA SHEIKH ABDALLAH RASHID SEMBE MAY 1999

Nimeweka hapa historia ya dua iliyofanywa Mnyanjani mwaka wa 1958 ka ajili ya kutaka msaada wa Allah katika tatizo kubwa lilikokuwa linaikabili TANU katika Uchaguzi wa Kura Tatu.

Kisa chote kile cha dua hii ya Mnyanjani kuanzia Mwalimu Nyerere kwenda Tanga akiongozana na Amos Kisenge hadi mkutano wa siri waliofanya ambao Mwalimu aliomba Tanga waunge mkono TANU kushiriki katika uchaguzi ule wa Kura Tatu.

Historia hii alinieleza Sheikh Sembe hadi makubaliano yao ya kupambana na wanaopinga kushiriki uchaguzi na kufikia kuamua kufanya dua kwa kutaka msaada wa Allah yote aliinieleza.

Katika walioshiriki katika dua ile nilimtaja Sheikh Abdallah Rashid Sembe.

Tulikuwa tumekaa nyumbani kwake Barabara ya 14 Ngamiani kaniwekea soda nakunywa taratibu lakini akili yangu yote iko katika kalamau, ''note book,'' yangu na kumsikiliza yeye.

Sheikh Sembe alifurahi sana kuwa nataka kuandika historia ya kupigania uhuru wa Tanganyika.

Sheikh Sembe alinieleza kila kitu hadi jinsi mkutano ulivyokwenda ndani ya Parish Hall, Tabora.

Huu ulikuwa mwaka wa 1987 niko katikati ya utafiti wangu.

Kifo cha Abdallah Rashid Sembe kilitokea Hospitali ya Bombo, Tanga tarehe 22 Mei, 1999.

Siku ya pili yake, Jumapili asubuhi kwa wale waliokuwa wanasikiliza Radio One walisikia katika matangazo ya vifo Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akiarifiwa msiba ule.

Kisha jina lililofuata likawa la Rais wa Zanzibar Dk. Salmin Amour na baadae mtangazaji akasema habari za msiba ziwafikie ndugu na jamaa wote.

Hili halikuwa tangazo la kifo la kawaida.

Si kila siku wananchi wanapata bahati kama hiyo ya kusikia Mwalimu Nyerere akitangaziwa taarifa ya kifo kwenye radio.

Ni wazi kuwa wananchi wengi walikuwa wamepigwa na mshangao. Pana uhusiano gani kati ya Sheikh Abdallah Rashid Sembe na Mwalimu Nyerere kiasi ya kifo cha Sheikh aarifiwe.

Kubwa ni kuwa watu hawakuwa wanamjua huyo Sheikh Abdallah Rashid Sembe ni nani na ana umuhimu gani?

Wengi hadi leo hawamfahamu Sheikh Abdallah Rashid Sembe na wengi wataendelea kutomjua hadi hapo wana-historia na CCM yenyewe itakapoamua kuandika upya historia yake na kuwaenzi wale wote waliopigania uhuru wa Tanganyika.

Hata pale makaburini Msambweni katika makaburi ya Sharif Haidar alipozikwa Sheikh Sembe, CCM walipokuwa wakieleza habari za mchango wa Sheikh Rashid Sembe katika kuasisi TANU na kupigania uhuru wa Tanganyika habari zilizotolewa zilijaa makosa matupu.

Msomi maarufu na makini, Juma Mwapachu katika taa'zia aliyomwandikia marehemu Dossa Aziz katika gazeti la The African mwaka wa 1998 kwa uchungu alisema kuwa, wakati mwingine inakuwa aibu na fedheha unapowasikia viongozi wa CCM wakijaribu kwa shida sana kueleza mchango wasiojua wa mzalendo mpigania uhuru alipofariki aliyefariki dunia.

Juma Mwapachu akamaliza katika makala ile kwa kumwuliza Mwalimu Nyerere kuwa hadi lini atanyamaza kimya bila ya kuwataja wenzake aliokuwa nao katika kupigania uhuru wa Tanganyika?

Hali kadhalika akawauliza wasomi wazalendo kwanini hadi leo hakuna juhudi ya kutafiti na kuandika historia ya kweli ya uhuru wa Tanganyika?

Ukweli ulikuwa kwa wakati ule kuwa hadi hapo Mwalimu Nyerere atakapofungua kinywa chake kuwaeleza wananchi habari za mashujaa wenzake aliokuwa nao katika harakati za kudai uhuru, wananchi na hasa kizazi cha hivi karibuni kitakuwa kinamtukuza yeye pekee kama shujaa wa uhuru wa Tanganyika.

Screenshot_20220217-183202_Facebook.jpg
 
Back
Top Bottom