Historia ya Sheikh Suleiman Takadir kama nilivyoipokea kutoka kwa Sheikh Haidar Mwinyimvua

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,921
30,265
HISTORIA YA SHEIKH SULEIMAN TAKADIR KAMA NILIVYOIPOKEA KUTOKA KWA SHEIKH HAIDAR MWIMYIMVUA

Baada ya zaidi ya miaka 60 leo Sheikh Suleiman Takadir anatajwa.

Lakini imekuwaje atajwe ilhali Sheikh Suleiman Takadir alifutwa katika historia ya kupigania uhuru wa Tanganyika?

Katajwa lakini anaemtaja wala haijui historia ya Sheikh Suleiman Takadir.

Anaeleza kwa kubahatisha.
Hana moja analolijua.

Mimi nimemleta hapa Sheikh Suleiman Takadir baada ya kusoma kejeli kuwa Waislam walipinga uhuru kupitia AMNUT na wakaandamana.

Nimeomba ushahidi wa maandamano ya AMNUT leo siku ya pili hakuna jibu.

Aliyeandika haijui historia ya AMNUT ndipo nilipoingia kueleza sababu zilizosababisha kuundwa kwa AMNUT nikianza na ugomvi uliotokea baina ya Sheikh Suleiman Takadir na Nyerere mwaka wa 1958 kufuatia Kura Tatu.

Yote haya leo yanazungumzwa baada ya kitabu kuandikwa na watu kuanza kusoma upya historia ya uhuru wa Tanganyika.

Vinginevyo tungebakia na historia ya TANU na uhuru wa Tanganyika ambayo si ya kweli.

Historia ya Sheikh Suleiman Takadir nimesomeshwa na Sheikh Haidar Mwinyimvua aliyekuwa rafiki wa Sheikh Takadir wakati wa kupigania uhuru wa Tanganyika, urafiki ulikatizwa baada ya Sheikh Takadir kufukuzwa TANU na kususwa na jamii.

Sheikh Takadir akafa akiwa mpweke.

Barza ya wana TANU iliyokuwa nyumbani kwake Mtaa wa Msimbazi moja ya barza kubwa za wanachama wa TANU Kariakoo ikakimbiwa na kila mtu.

Iddi Tulio akachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU.

Lakini kabla ya kufukuzwa TANU iliundwa kamati ya watu watatu waende kwa Sheikh Suleiman wapate kauli yake kwa nini alitoa maneno yale dhidi ya Nyerere.

Wajumbe wa Kamati hii walikuwa Iddi Tulio, Jumbe Tambaza na Iddi Faiz Mafungo.

Huyu Iddi Faiz Mafungo alikuwa Mweka Hazina wa TANU na Mweka Hazina wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika.

Sheikh Takadir hakubadilisha kauli yake aliyarudia maneno yale yale kama alivyoyatamka mara ya kwanza.

Kilichofuatia ikawa yeye kufukuzwa TANU.

Katika kitabu cha Abdul Sykes nimehitimisha historia ya Sheikh Suleiman Takadir kwa maneno hayo hapo chini:

‘’Wanachama wa TANU walikuwa wakikutana kwa Sheikh Takadir kunywa kahawa, kupoteza wakati na kujadili siasa.

Baada ya yeye kufukuzwa kutoka TANU mahali hapo palihamwa na hakuna aliyekwenda pale kama ilivyokuwa mazoea hapo siku za nyuma.

Sheikh Takadir alipokwenda sokoni Kariakoo kununua mahitaji yake hakuna mfanyabiashara aliyegusa fedha zake au hata kule kumtizama tu.

Alipotoa salam hakuna aliyemwitikia.

Sheikh Takadir alisuswa na jamii yake na TANU.

Sheikh Takadir aliuhisi khasa uzito kamili wa kupigwa pande na jamii.

Biashara yake ikaanza kuanguka na vivyo hivyo afya yake ikaanza kuathirika.

Akawa mpweke sana na mtu mwenye fadhaha.

Enzi zile alipokuwa akisoma Surat Fatha na kusoma dua kabla ya kumtambulisha Nyerere kwa watu wa Dar es Salaam katika mikutano ya awali ya TANU katika viwanja vya Mnazi Mmoja zilikuwa zimepita.

Yalikuwa ya kale wakati Sheikh Takadir akijenga vyema taswira ya Nyerere akimkweza hadi kufikia kiwango cha kumnasibisha na mtume.

Haukupita muda mrefu Sheikh Takadir alifariki.

Lakini kabla ya kufariki Sheikh Takadir aliwaachia usia.

Kikundi cha Waislam walikuwa wamekwenda nyumbani kwake kumdhihaki, wakimtukana na kumkebehi, wakipiga makele huku wakiimba kwa sauti kubwa mwimbo, ‘’Takadir mtaka dini!''

Kikundi hiki kilivamia nyumba yake baada ya kutoka mkutanoni ambako Nyerere alitoa hotuba ya kumshambulia Sheikh Takadir.

Sheikh Takadir alitoka nje ya nyumba yake kuwakabili wale Waislam na akawaambia, ‘’Iko siku mtanikumbuka.’’

Mwafrika, gazeti la kila wiki chini ya uhariri wa Heri Baghdelleh na Robert Makange, lilichapisha habari za Sheikh Suleiman Takadir katika ukurasa wake wa mbele likitangaza kufukuzwa kwake kutoka TANU kwa wino mzito, picha yake akiwa amevaa kanzu na kofia ya mkono akikodoa macho ikachapishwa gazetini.

Picha ya Sheikh Takadir iliwekwa pale ili wote wauone uso wa ‘’msaliti’’ anaetaka kuchelewesha uhuru kwa kutaka Waislam wapewe uthibitisho wa hali yao ya baadae kwa sababu ya mchango wao katika harakati za kudai uhuru.

Mtu mmoja tu ndiyo aliyejitokeza kumuunga mkono Sheikh Takadir na huyo alikuwa Ramadhani Mashado Plantan.

Akiandika katika gazeti lake la Zuhura alihoji ile haraka ya Nyerere kuwatumbukiza wananchi ndani ya Uchaguzi wa Kura Tatu ingawa ilikuwa wazi kuwa yale masharti ya kupiga kura yalikuwa ya kuchukiza na ile haraka ambayo kwayo Sheikh Takadir alifukuzwa kutoka TANU.’’

Bwana Kamara Kusupa hii ndiyo historia ya Sheikh Suleiman Takadir niliyoipokea kutoka kwa Sheikh Haidar Mwinyimvua.

Historia ya sheikh anaihadithia sheikh na wote walikuwa TANU mstari wa mbele pembeni ya Baba wa Taifa Julius Nyerere.

Umeshapata kujiuliza ingekuwaje kama Mohamed Said asingeandika historia hii?

Sheikh Haidar Mwinyimvua picha yake hiyo hapo chini.

Mengine,
Siku nyingine,
In Shaa Allah.

1697690081157.png

Sheikh Haidar Mwinyimvua
 
TANU ilianza ukaburu uliokuja kurithiwa na CCM.

Ubaguzi dhidi ya waliopinga fikra za Nyerere ulikuwa dhahiri na seems uliungwa mkono ionekane jambo jema.

Unafiki wa viongozi na kufukia historia ya uhuru wa Tanganyika vina mizizi mirefu sana sana.
 
Nyerere nae alikuwa hataki kupigwa, nishawahi sikia baadhi ya visa dhidi ya takadir.
Aligombana na OSCAR KAMBONA hivyo hivyo ye anajiona ni kila kitu.
Hauwezi kuwa sahihi muda wote wape nafasi wezio,wasikilize vyenye maana beba.
 
Sasa nani wa kuyathibitisha hayo madhila aliyokua anafanyiwa huyo mzee ? Kwa sababu we umesimuliwa tu 'hearsay'
 
Hizi historia za mashehe si mkasomeane misikitini huko?
Ava...
Historia hiyo ya masheikh inatoka katika ofisi ya African Association mwaka wa 1929 ilipoasisiwa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika (Umoja wa Waislam wa Tanganyika) mwaka wa 1933 kuitia nguvu African Association mpaka baina ya vyama hivi viwili ukawa mwembamba sana.

Angalia hii kama ya TAA Political Subcommitee: Dr. Vedasto Kyaruzi (President), Abdul Sykes (Secretary) (baba yake Kleist Sykes ndiye aliyeasisi hivyo vyama viwili hapo juu na Abdul Sykes kasoma Al Jamiatul Ismaiyya Muslim School), Mufti Sheikh Hassan bin Ameir, Sheikh Said Chaurembo Liwali wa Mahakama ya Kariakoo (hawa wanachama wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika), Steven Mhando na John Rupia.

Mkutano wa kwanza wa TANU August 1954 ulihudhuriwa na watu wasiozidi 20 miongoni mwao Abdul na Ally Sykes vijana wa Al Jamiatul Islamoyya, Iddi Faiz Mafungo na nduguye Iddi Tosiri wanachama wa Al Jamiatul Islamiyya.

Safari ya Nyerere UNO mkusanyaji fedha za safari alikuwa Iddi Faiz Mafungo Mweka Hazina wa Al Jamiatul Islamiyya na Mweka Hazina wa TANU.

Naamini kwa maelezo haya umeelewa uhusiano katika ya TANU Waislam.
Leo huitaki historia hii ielezwe hapa ipelekwe msikitini.

Historia hii bado ipo sana msikitini ila hapa JF mimi ndiyo nimeleta kiasi cha miaka 10 iliyopita na inapendwa sana.

Fuatilia uzi huu angalia watu wangapi wanausoma.
 
Sasa nani wa kuyathibitisha hayo madhila aliyokua anafanyiwa huyo mzee ? Kwa sababu we umesimuliwa tu 'hearsay'
Mpaji...
Kisa cha Sheikh Takadir ni maarufu katika historia ya TANU.

Unaweza kusoma historia ya Sheikh Suleiman Takadiri katika magazeti haya mawili hapo chini yapo Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, East Africana:

Mwafrika, 11 th October, 1958.
Zuhra, 14 th November, 1958.

Wahariri wa Mwafrika alikuwa Rashid Kheri Baghdelleh na Robert Makange.
Mhariri wa Zuhra alikuwa Ramadhani Mashado Plantan.
 
Back
Top Bottom