T.B. Joshua amebeba siri gani kifuani, anatumika

Rubawa

JF-Expert Member
Dec 25, 2015
2,055
3,239
Na Ahmed Rajab

T.B. Joshua ni mtu wa ajabu. Kuna wasemao kwamba mzalia huyu wa Nigeria si binadamu wa kawaida. Wanaamini kwamba yeye ni nabii. Wengine wanasema kuwa ni mtume kamili aliyepewa wahyi na miujiza ili aweze kuwahubiria watu na kuwalingania.

Na kuna wanaokana. Wanasema kwamba T.B. Joshua hana unabii wala utume wowote ila yeye ni afiriti, mwana wa ibilisi, shetani anayewaghilibu watu.

Serikali ya Cameroon iliwahi kuliweka jina lake kwenye orodha ya watu wabaya wasiotakikana nchini humo. Na ikawaonya wananchi wake wenye kufunga safari kwenda kumtembelea Lagos, Nigeria, wawe na hadhari wasighilibike.

Serikali ya Zambia nayo iliwahi kuwaonya raia zake wasimwendee Joshua kwa sababu fedha zikiwaishia hukwama huko Nigeria.

Naawe awavyo, apendwe asipendwe, T.B. Joshua hakosi wenye kumfuata. Ana wafuasi wengi miongoni mwa walio katika tabaka aali la watu wenye uwezo katika jamii katika takriban ukanda mzima wa Afrika ya Magharibi. Watu husafiri kila mwaka kutoka sehemu mbalimbali za Afrika kwenda Lagos kulizuru kanisa lake.

Wasiojiweza huuza hata nyumba au mashamba ili wapate fedha za safari. Wanatoka Liberia, Ghana, Sierra Leone, na hata kutoka nje ya Afrika ya Magharibi.

Nakumbuka safari moja nikiwa uwanja wa ndege wa Murtala Muhammed, jijini Lagos, nilikumbana na kikundi cha watu zaidi ya hamsini waliowasili kutoka Nairobi. Wote walikuwa wamevaa fulana za T.B. Joshua. Walikuwa wanaelekea mtaa wa Egbe, huko Lagos, kwenye kanisa la The Synagogue, Church of All Nations (Sinagogi, Kanisa la Mataifa Yote), kwa ufupi SCOAN. Hapo ndipo penye makao makuu ya madhehebu hayo ya kikristo aliyoyaanzisha T.B. Joshua. Hili ni kanisa kubwa Afrika kwa idadi ya wafuasi wake na linazidi kukua.

Septemba 12, 2014 jengo la ghorofa sita la kanisa hilo huko Lagos liliporomoka. Watu wasiopungua 116 walikufa katika ajali hiyo, 85 kati yao walitoka Afrika Kusini. Jamaa wa marehemu hadi leo wanataka kujua nini hasa kilitokea na nani wa kuwajibika. Mwaka 2015 Joshua alifunguliwa kesi ya jinai, yeye pamoja na wahandisi wawili na wadhamini wa kanisa. Bado kesi haijamalizika kwa sababu Joshua amekuwa akikwepa kwenda mahakamani.

Ni wazi kwamba mchungaji huyo na mwinjilisti wa televisheni anaifahamu Afrika na anawafahamu vilivyo Waafrika wenzake, hasa wasomi miongoni mwao. Anafahamu namna akili zao zinavyofanya kazi na jinsi anavyoweza kuzichezea.

Rais wa zamani wa Ghana, marehemu Profesa John Attah-Mills baada ya kushinda uchaguzi alimshukuru kwanza Mungu na halafu akamshukuru T.B. Joshua kwa kumsaidia kushinda uchaguzi huo. Attah-Mills aliwahi kusema hadharani kwamba Joshua alitabiri kweli ya kuwa baada ya kushiriki katika chaguzi tatu ndipo ataposhinda uchaguzi wa urais wa Ghana.

Attah-Mills alikuwa na mazoea ya kumtembelea Joshua kwenye kanisa lake. Alikuwa akenda mara kwa mara kufanya maombi kabla hajawa rais na baada ya kuwa rais. Marais wengine wa zamani wa Kiafrika waliowahi kumzuru Joshua walikuwa Andre Kolingba (Jamhuri ya Afrika ya Kati), Frederick Chiluba (Zambia), Profesa Pascal Lissouba (Congo-Brazzaville), Joyce Banda (Malawi) na Omar Bongo (Gabon).

Miongoni mwa Waafrika mashuhuri waliovutwa na simaku yake ni Prince Johnson na Rais George Weah (wote wawili kutoka Liberia). Kutoka Tanzania ni Edward Lowassa na Rais John Magufuli. Kutoka Zimbabwe Morgan Tsvangirai, kutoka Malawi Sam Mpasu na Walter Nyamilandu, Rais wa Jumuiya ya Soka ya Malawi (FAM).

Kutoka Afrika Kusini Julius Malima, Winnie Mandela, Goodwill Zwelithini (mfalme wa Wazulu), pamoja na waimbaji Yvonne Chaka Chaka na Sechaba.

Hata Gavana-Mkuu wa Bahamas, Sir Orville Turnquest alimpokea Joshua alipomtembelea 2001.

Jambo linalonihangaisha ni ushawishi mkubwa alionao mchungaji huyo kwa baadhi ya viongozi wa Kiafrika. Unaweza ukautafsiri ushawishi huo kwa walau njia mbili. Ama amewateka na kuwatia mikononi viongozi hao au hao viongozi wamemkinai vya kutosha kiasi cha kuwa tayari kumuamini na siri zao ambazo pia huenda zikawa siri za serikali.

Mgeni kuwa na nguvu za aina hizo katika nchi za watu wengine si jambo la maskhara la kuchukuliwa kijuujuu, hasa kwa mtu ambaye dhamira na ajenda zake za kisiasa si bayana. Si jambo la kufumbiwa macho. Hatujui huwa anafanya nini au hutaka kujua nini anapowatembelea viongozi katika Ikulu zao.

Huenda akawa anatumiwa, ama kwa kujua au bila ya kujua. Kwa mfano, tunajua kwamba ana uhusiano mzuri na serikali ya Israel, nchi ambayo amekuwa akiizuru mara kwa mara na ambako amekuwa akionana na wakubwa wake.

Tuijuavyo Israel na weledi wake wa kuelea katika mikondo ya chini kwa chini katika siasa za kimataifa, nadhani ni halali tukiuliza kwa kiasi gani Israel imeweza kumtumia T.B. Joshua kuwafanya baadhi ya viongozi wa Kiafrika wabadili misimamo ya nchi zao kuhusu Israel?

Israel, taifa la majungu lisilopoteza fursa yoyote itayoweza kuinufaisha kimataifa, itakuwa imepoteza moja ya sifa zake kuu lau haikumtumia Joshua kwa maslahi yake. Israel haitokuwa Israel ikiwa haikujaribu kufanya hivyo.

Wenye kuifuatilia mitandao ya wahalifu wa kimataifa wana wasiwasi kwamba huenda kanisa lake la SCOAN likatumiwa, hata bila ya mwenyewe kujua, kuzisafisha fedha chafu zilizopatikana kwa njia za haramu.

La hatari zaidi ni kwamba yeye mwenyewe T.B. Joshua huenda akawa hatari kwa usalama wa taifa kwa kujulishwa mambo na wenye kuendesha nchi au na walio karibu nao, mambo ambayo hastahiki kuyajua.

Yote hayo tunayasema kwa hadhari tu kwani huenda akawa anawachezea akili tu viongozi wa Kiafrika bila ya kuwa na madhara kwa mustakbali wa nchi zao. Hatujui. Lakini hayo ni baadhi ya maswali nyeti yanayostahiki kuulizwa kuhusu ushawishi wake kwa viongozi wa baadhi ya serikali za Kiafrika.

Tatizo lililopo ni kwamba mtu atapokuwa anajaribu kuyauliza maswali hayo atakuwa anayaingilia mambo ya kiroho na ya imani za watu. Hili ni tatizo kubwa. Kuna hatari kwamba katika kuulizauliza kwako ukadhaniwa kwamba unapinga ukristo au unampinga Yesu Kristo. Kosa kama hilo la kuziingilia imani za watu liliwahi kufanywa na Kwame Nkrumah, rais wa kwanza wa Ghana.

Waumini wa T.B. Joshua wanaiona imani yao juu yake kuwa ni sahihi. Kwa hivyo, hawaoni ubaya wowote kwa viongozi wa serikali zao pia kumfuata. Hawa ni watu ambao wanapomuona T.B. Joshua anafanya maombi kwenye vipindi vyake vya televisheni vya Emmanuel TV huugusa uso wa televisheni ili wapate “baraka” zake. Huna cha kuwaambia watu kama hao.

Ikiwa viongozi wa Kiafrika wana itikadi kama hizo basi nchi zao zimekwisha.

Kwa kiwango gani viongozi hao huwa wanamshirikisha wanapokata maamuzi yao. Na yeye huwashauri nini na kwa mantiki gani?

Ni nani hasa huyu T.B. Joshua? Alikwendakwendaje akaibuka kuwa na wafuasi alionao hata katika Ikulu za baadhi ya nchi za Kiafrika? Na ushawishi wake hauko Afrika tu, umevuka bahari ya Atlantiki na umesukumwa na pepo hadi Amerika ya Kusini, ingawa ushawishi huo haukufika bado katika Ikulu za huko.

Hata hivyo, lukuki na lufufu ya watu walihudhuria ibada zake alizozifanya miaka ya hivi karibuni Colombia, Mexico, Peru na Paraguay. Aliziita ibada hizo “vita vya msalaba” au “vita vitakatifu”

Ziara aliyoifanya Paraguay 2017 ilizusha mjadala mkubwa nchini humo, pale bunge la huko lilipoidhinisha atunukiwe nishani ya “Orden Nacional del Merito”. Hiyo ni nishani ya hadhi ya juu kabisa nchini humo na hutunukiwa raia wa Paraguay tu.

Kuna waliokuwa wakihoji kwamba “el profeta” (mtume) Joshua alistahiki nishani hiyo kwa “kuwaponesha” watu waliokuwa na magonjwa makubwa kama saratani au UKIMWI. Inasemekana pia kwamba aliwapunga wenye kudai kwamba walikuwa na mashetani kichwani.

Joshua amechuma fedha chungu nzima kutokana na ziara zake hizo, pamoja na michango na ada anazolipwa na wafuasi wake. Alionyesha ukarimu wake Julai 2014 alipokuwa ziarani mjini Cali, Colombia, ambako watu wasiopungua laki moja walihudhuria mkusanyiko wake aliouita “Muujiza wa Vita vya Msalaba”.

Baada ya kumaliza ibada aliwapa polisi wa huko Cali dola za Marekani laki moja ($100,000) kuwasaidia wanafamilia wa polisi waliouliwa au waliojeruhiwa wakiwa kazini. Fedha hizo ni kama ndururu tu ukizingalisha na utajiri wake binafsi unaokisiwa kuwa si chini ya dola za Marekani milioni 15.

Kwa mtu asiyependa kusafiri Joshua amesafiri sana kwani amewahi pia kuzuru Tanzania, Korea, Singapore, Indonesia na Australia.

Joshua anadai kwamba mazazi yake yalitabiriwa miaka mia moja kabla. Kuzidi kuonesha kwamba yeye si binadamu wa kawaida anadai pia kwamba alikuwa tumboni mwa mama yake kwa muda wa miezi 15 kabla ya mama yake kujifungua Juni 1963.

Jina lake kamili ni Temitope Balogun Joshua, ingawa alipokuwa anasoma skuli akijulikana kwa jina la Balogun Francis.

Masomo yake rasmi ya skuli hayakupindukia ya sekondari ambayo hakuyamaliza. Mwenyewe anasema alivutiwa na masomo ya Biblia tangu akiwa mdogo. Baada ya kumaliza masomo yake ya msingi alifanya kazi mbalimbali za vibarua ikiwa pamoja na kubeba mavi ya kuku katika shamba la kuku.

Anasema mambo yalimfungukia alipoamriwa mbinguni aanzishe kanisa lake. Lakini je, ushawishi wake kwa viongozi wa Kiafrika unamalizika kwa kuwazingua na kuwapunga pepo tu? Au kunaya ziada?


Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter: @ahmedrajab



images.jpeg
unnamed.jpeg


Sent using Jamii Forums mobile app
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom