Ni kweli kabisa hapa kuna kivuli fulani kama makala ya gazeti la Raiamwema lilivyochambua changamoto za Milenia:
Na Padri Privatus Karugendo
Gazeti la Raiamwema
MIRADI ya Changamoto za Milenia, kwa walio wengi, na hasa mijini (wasomi na waelewa) inajulikana kama Miradi ya Bush au Fedha za Wamarekani. Miradi hii ni ya barabara, maji, afya, elimu, umeme nk. Kiasi kikubwa miradi hii iko katika hatua za utekelezwaji. Vijijini miradi hii inajulikana kama Miradi ya Mheshimiwa Jakaya Kikwete; maana wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2010 aliahidi vitu vingi ambavyo alijua kwa uhakika vitatekelezwa na mfuko wa miradi ya Changamoto za Milenia. Mashabiki wa CCM wanaamini miradi hii ni utekelezaji wa sera nzuri za chama chao.
Tatizo letu kubwa hapa Tanzania na nchi nyingi za dunia ya tatu (AFRIKA) ni kufumbwa macho na upole wa njiwa. Anayeleta msaada ana lengo lake; hivyo ni muhimu anayepokea msaada awe na matumaini na malengo ya muda mrefu pia! Bila kuumizana, anayetoa na anayepokea wanufaike sawa au kwa kupishana kidogo.
Tanzania Bara mradi huu utatekelezwa katika mikoa sita ya Tanga, Morogoro, Mbeya,Iringa, Dodoma na Mwanza. Na sasa hivi ninapoandika makala hii mradi huu umefikia hatua ya kuandaa fidia kwa mali za wananchi zitakazoathiriwa na mradihuu wa kukarabati na uwekaji wa miundombinu mipya ya kusafirisha umeme. Wananchi ambao mazao yao yataguswa na njia ya umeme watalipwa fidia na wale ambao nyumba zao zitabomolewa watalipwa fidia au watajengewa nyumba nyingine.
Tanzania Bara mradi huu utatekelezwa katika mikoa sita ya Tanga, Morogoro, Mbeya,Iringa, Dodoma na Mwanza.
Nimezungukia mikoa yote sita na kupitia karibia vijiji vyote vitakavyonufaika na mradi huu. Swali langu kubwa kama mchambuzi wa masuala ya kijamii ni: Ni vigezo gani vilitumika kuichagua mikoa hii sita kunufaika na mradi huu? Je ni serikali ya Tanzania iliichagua mikoa hii (kwa vigezo gani?) au Wamarekani wenyewe waliichagua mikoa hii?
Baada ya kuzunguka katika mikoa yote sita, jibu nililolipata si la ni nani alichagua mikoa, wilaya na vijiji kwa vigezo gani; bali kwa mtizamo binafsi. Ni kwamba vijiji vyote vitakavyonufaika na mpango huu wa kusogeza huduma ya umeme vimesheheni madini na raslimali nyingi. Ardhi ya vijiji hivi ina rutuba na nzuri kwa uwekezaji wa kilimo, uwindaji, utalii na viwanda.
Mfano, wilaya ya Morogoro vijijini, Kata ya Matombo itanufaika na huduma hii ya umeme. Kata ya Matombo inajulikana kwa uzalishaji wa matunda na mazao mengine mengi. Inaaminika kwamba msitu wa asili ya Kimboza umesheheni madini ya kila aina. Njia ya kwenda Matombo ni njia ya utalii na kuna uwezekano wa kuipanua njia hii kwa siku za usoni.
Je, inawezekana Mfuko wa Changamoto za Milenia unatumika kutengeneza miundombinu ya wawekezaji kutoka Marekani? Wakija kuwekezawakute umeme? Kwao iwe ni rahisi kuvuta na kuutumia jinsi watakavyo? Ni msaada au ni upole wa njiwa na ujanja wa nyoka?
Dodoma, itanufaika na mradi huu! Sote tunajua kwamba mkoa huu umesheheni madini muhimu sana. Wilaya ya Mpwapwa tayari ina machimbo yanayoendelea. Inawezekana zoezi zima la kusogeza umeme vijijini ni kuandaa miundombinu ya wawekezaji? Katika vijiji vya Tubugwe na Hogoro, wilaya ya Kongwa, asilimia tisini (90) ya wanavijiji walisema hawana uwezo wa kuuvuta umeme kuingiza kwenye nyumba zao. Mradi wa kuziboresha nyumba zao ungekuwa muhimu zaidi ya umeme. Na wale waliosema wanaweza kuuvuta, hawakuwa na uhakika wa kulipa bili kila mwezi.
Wilaya ya Geita nako vijiji vingi vyenye machimbo ya dhahabu vitanufaika na mradi huu. Nyumba nyingi za wananchi hazina ubora wa kuunganisha umeme. Ni wazi huduma hii imewalenga wawekezaji zaidi ya wananchi.
Haiwezekani Wamarekani wakatusaidia sisi bila wao kuwa na malengo yao; ni wapole kama njiwa, lakini wajanja kama nyoka. Wito wangu ni kwamba na sisi tusipokee msaada bila kuwa na malengo yetu. Wao wanasogeza umeme kwenye maeneo yenye madini na yenye uwezekano wa kuwekeza kwenye mambo mbalimbali, na
hawana mpango wa kuanzisha vyanzo vipya vya kuzalisha umeme; basi, sisi tuanze mkakati wa kusambaza umeme vijijini na kutoa elimu juu ya matumizi ya umeme sambamba na kuanzisha vyanzo vipya ya kuzalisha umeme. Kwa njia hii Wamarekani watanufaikana sisi tutavuna vya kutosha!
Soma makala nzima ktk link hapa chini:
Source: Raiamwema Toleo namba 175 tarehe 2, Machi 2011
Utata wa miradi ya umeme ya Changamoto za Milenia[Hao pia ni wezi wamebadirisha umiliki wa kampuni]