Doctor Mama Amon
Platinum Member
- Mar 30, 2018
- 2,311
- 3,490
Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro
Mheshimiwa Waziri,
Nimeshangazwa na ombi la baadhi ya makuhani kwa Rais Samia wakitaka awape nafasi za ubunge wa kuteuliwa kutokana na kofia zao za kidini.
Nataka kulipinga ombi hili kwa kutumia hoja inayosindikizwa na ushahidi usiokanushika.
Kama unavyojua, tangu mwaka 1648 kwenye mkutano wa Westaphalia, ni kanuni ya kimataifa kwamba, vyombo vya dola ambayo ni Jamhuri ya Kikatiba na Kidemokrasia havipaswi kuwatumikia miungu wa aina yoyote.
Hivyo, nimeirejea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Sura ya 02 ya Sheria za Tanzania) ili kuthibitisha ukweli huu katika mazingira ya Tanzania.
Kwa mujibu wa ibara ya 3(1) ya nakala ya Katiba ya Kiingereza, niliyoipakua kutoka kwenye tovuti rasmi ya Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Fedha za Serikali (NAOT), tunasoma kwamba:
“The United Republic [of Tanzania] is a democratic, secular and socialist state which adheres to multi-party democracy.”
Kwa mujibu wa tafsiri yangu, kwa Kiswahili ibara hii inapaswa kusomeka kama ifuatavyo:
“Jamhuri ya Muungano [wa Tanzania] ni nchi ya kidemokrasia, isiyo na dini rasmi, ya kijamaa na yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa.”
Lakini, nilipotaka kunukuu maneno rasmi kutoka kwenye nakala ya Katiba ya Kiswahili nikakwama, nikakwazika na kushangaa sana.
Nimekuta kwamba kuna mtu au watu wamefuta maneno "isiyo na dini rasmi ," yaani, "secular" kutoka kwenye nakala ya Kiswahili ya Katiba ya Tanzania (1977).
Yaani, chini ya ibara hii ya 3(1) ya Katiba ya Kiswahili tunasoma kwamba:
“Jamhuri ya Muungano [wa Tanzania] ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamaa, yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa.”
Kuondolewa kwa maneno hayo huenda ni mkakati wa kimya kimya wa kutenegeneza dirisha la kuunganisha kazi za dola na kazi za dini kwa kiwango kinachoweza kutikisa umoja wa Taifa kwa sababu za kidini.
Kama tunavyojua, katika mambo ya ujasiriadola na usalama wa nchi, maneno ya Kiingereza "state organs," ni kisawe cha maneno ya Kiswahili "vyombo vya dola."
Kwa upande mmoja, maneno haya yanamaanisha mtu mmoja mmoja ambaye ni mtumishi wa umma, wakiwemo watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama.
Na kwa upande mwingine, yanamaanisha taasisi za kijamii kama vile serikali, mahakama na Bunge, ambazo ni sehemu ya mamlaka ya nchi.
Kwa sababu hii kutaka kuingiza dini serikalini, kuchomeka dini mahakamani na kueneza dini bungeni, kama wanavyotaka kufanya makuhani hawa ni utovu wa umakini wa hali ya juu.
Na jambo la ajabu zaidi ni kwamba, nakala ya Katiba ya Kiswahili iliyochakachuliwa ndio nimeikuta kwenye tovuti zifuatazo:
- Tovuti ya Tume ya Haki za Binadamu,
- Tovuti ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, na
- Tovuti ya Wizara ya Katiba na Sheria.
- Tovuti ya wanasheria ya Tanzania ya www.tanzlii.org
- Tovuti Rasmi ya Rais.
- Tovuti Kuu ya Serikali.
- Tovuti ya Bunge.
- Tovuti ya Mahakama Kuu ya Tanzania.
Yote haya ni maajabu yanayoashiria kwamba huenda kuna nia ovu ndani ya mfumo wa kiutawala inayopaswa kukabiliwa kwa kutumia kasi na nguvu kubwa.
Tabia za wanasiasa matapeli kuhamisha magoli ya kanuni zilizobuniwa na waasisi wa Taifa letu kwa ajili ya kulinda umoja wa Taifa hazipaswi kuvumiliwa.
Nafahamu kuwa, ibara ya 84 ya "Sheria Inayofafanua Lugha ya Sheria (Interpretation of Laws Act, Chapter 01)" inatamka kwamba, pale sheria inapokuwa imeandikwa kwa Kiswahili na Kiingereza, na ikatokeo tofauti ya kimaudhui au mashaka kuhusu maana iliyokusudiwa katika maneno yaliyotumika, basi toleo la Kiingereza litatumika kama marejeo rasmi.
Lakini sina uhakika kama mwongozo huu unaihusu Katiba ya nchi pia.
Hivyo, kabla sijaendelea na utafiti wangu naomba Waziri wa Katiba na Sheria unisaidie kujibu maswali haya mawili:
- Pale nakala ya Kiswahili ya Katiba ya nchi na nakala ya Kiingereza ya Katiba ya nchi zinapotofautiana, nakala ipi inapaswa kutumika kama marejeo rasmi?
- Nani amechakachua ibara ya 3(1) katika nakala ya Kiswahili ya Katiba ya nchi yetu, amefanya hivyo kwa lengo gani, na hatua gani zinapaswa kuchukuliwa ili kuondoa dosari hii?
Naomba nipatiwe majibu kabla ya ukomo wa masaa ya kufunga ofisi za serikali kesho.
Na hapa chini naambatanisha nyaraka zifuatazo kwa ajili ya kukuonyesha tatizo ninaloliona kwa njia ya ushahidi usiokanushika:
- Nakala ya Katiba ya Kiswahili (1977).
- Nakala ya Katiba ya Kiingereza (1977).
- Video ya viongozi wa dini wakiomba kupewa Ubunge (2025).