JUMAMOSI, OCTOBA 13, 2012 08:58 BENJAMIN MASESE NA ZITHA KANNONYELE, DAR ES SALAAM
WAZIRI Mkuu mstaafu, Fedrick Sumaye ameshambulia Serikali ya awamu ya nne, akidai imekiuka misingi ya uongozi iliyoasisiwa na baba wa taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Sumaye alisema Serikali imeshindwa kusimamia usawa, maendeleo ya watu, uzalendo, maadili, mfumo wa kujitegemea, na demokrasia shirikishi vilivyoachwa na Mwalimu Nyerere.
Sumaye aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana katika mdahalo maalumu uliondaliwa na Chuo cha Kumbumbuku ya Mwalimu Nyerere na kuhudhuriwa na wageni mbalimbali.
Sumaye alikuwa mgeni rasmi na mchokaza mada katika mdahalo huo kwamba nini kifanyike katika kumuenzi Mwalimu Nyerere, ikiwa ni sehemu ya kumbu kumbu ya miaka 13 baada ya kifo chake.
Sumaye alisema kuwa kauli za Mwalimu Nyerere kuhusu rushwa zimepuuzwa na kwamba rushwa sasa ndiyo inayotumika kuwapeleka watu Ikulu.
RUSHWA
Akizungumzia rushwa Sumaye alisema rushwa imekuwa janga kubwa Tanzania na Afrika nzima huku jambo ambalo alisema ni hatari katika suala la amani na usalama wa nchi.
"Mwalimu Nyerere aliwahi kusema mtu yeyote anayeonekana anapenda kwenda Ikulu na hata yuko tayari kununua kura ili kufika Ikulu ni wa kumkwepa kama ukoma.
"Leo hali ikoje? kauli zote za mwalimu zimepuuzwa na rushwa ndiyo inayotumika kuwapeleka watu Ikulu tena vitendo hivi vinafanywa mchana kweupe bila haya.
"Leo Ikulu imefikia hatua ya watu kuitumia katika biashara yao, sasa swali la kujiuliza na kujitafakari wote hapa ikitokea miujiza Mwalimu Nyerere akafufuka ni wangapi watajitokeza kwenda kumlaki?
"Tuseme ukweli kwamba asilimia kubwa ya viongozi wa sasa watakimbilia katika mapango ya wakoloni na wachache ambao hawamfahamu na hawakulelewa na Mwalimu ndiyo watakaomlaki," alisema.
Sumaye alisema kuwa Mwalimu Nyerere alikaa katika uongozi kwa miaka mingi bila kuihusisha familia yake na Ikulu na kwamba hata watoto wake walisoma na kula chakula ambacho Watanzania wengine walikuwa wanakula.
"Isitoshe hakutaka kujenga wala kujilimbikizia mali pia alikuwa mtu wa maono ya mbali na kuchukua hatua na alipinga ubepari.
"Lo tunashuhudia Serikali imeshindwa kukemea mabaya na kuendeleza mazuri ya mwalimu, watoto wa viongozi wanapewa madaraka na elimu yao ni tofauti.
"Tunapokuwa tunafanya maadhimisho ya kifo cha Mwalimu Nyerere kila mmoja ajitafakari anachofanya, anachotamka mbele ya jamii na kukifananisha na kile ambacho mwalimu alikipinga kama vina uhusiano," alisema.
Sumaye ambaye alikuwa waziri mkuu kwa miaka 10 alisema kiongozi yeyote aliyefanya kazi na Mwalimu Nyerere wakati wa uhai wake leo hii anashikwa na kigugumizi kulingana na mambo yalivyo.
ELIMU
Akizungumzia elimu, Sumaye alisema asilimia kubwa ya vijana wamefikia elimu ya sekondari ambayo haina manufaa kwao kutokana na kutoandaliwa katika misingi ya kujiajiri.
"Hali katika shule nyingi za binafsi ni tofauti na ufaulu wa wanafunzi wa shule za Serikali jambo ambalo ni hatari, sasa tujiulize kwanini unatokea utofauti, jibu ni kwmaba kumeibuka matabaka ya wenye fedha na masikini.
‘Hali hii isipozuiliwa mapema italeta matabaka ingawa hakuna wa kuizuia kutokana na kupuuza misingi tuliyoachiwa, sisi sote ni mashahidi ndani ya jamii yetu wamekuwa hawajali wengine kutokana na umaskini kuongezeka.
"Leo Tanzania iliyoachwa na Mwalimu Nyerere imefikia hatua ya kufuta elimu ya kujitegemea ambapo vijana wengi wamemaliza shule hawana ajira kutokana na Serikali kushindwa kuanzisha viwanda vya kusindika
Katika hatua nyingine Sumaye alisema moja ya ugonjwa uliopo sasa ni wa viongozi kukubali kuwa na udhaifu na kutokiri kukosea kama alivyokuwa Mwalimu Nyerere.
"Nyerere alikubali kukosolewa na akalazimika kuanzisha kitabu cha tujisahihishe, kitabu kilitumika kurekebisha pale walipokuwa wakikosea.
"Lakini leo hakitumiki na kila kiongozi sasa anatumia siasa kuongeza, nisema wazi tusipiorudi katika misingi tuliyoachiwa hatutafanikiwa.
"Watu wanasema mdomoni kwamba wanamuenzi mwalimu na kulinda misingi bora ya utawala lakini moyoni wanachofikiwa ni kitu kingine.
"Viongozi wa Serikali wa leo wamefikia hatua ya kutumia ushirikina kutafuta madaraka na pia wananchi wanapouliza maswali magumu wao hutoa majibu rahisi, hili ni tatizo katika uongozi.
"Wameshindwa kusimamia ushupavu, usomi, busara, kupenda maendeleo, haki, msimamo na mambo mengine kama hayo ambapo hivi sasa wamejigeuza na kujiita waheshimiwa badala ya ndugu,"alisema.
Akizungumzia uchumi wa nchi alisema anaipongeza Serikali kusimamia ukuaji wa uchumi lakini akaongeza kwamba uchumi huo hauonekani dhahiri katika mabadiliko chanya.
"Katika maisha ya mwalimu alisimamia upande wa wanyonge na aliwatetea maisha yake yote lakini kutokana na mtawanyiko wa mali hivi sasa katika nchi yetu hautupi tena tumaini la amani na utulivu la muda, hivyo kwa faida ya wote ni vema marekebisho yatakafanya bila kuchelewa,"alisema
Sumaye alisema Tanzania itarudi katika hali yake ya kimaadili na utu ikiwa viongozi watarejea misingi ya uongozi iliyoasisiwa na Mwalimu Nyerere.
"Watanzania tuwe kama familia moja bila kujali cheo na nafasi ya mtu kula chakula kinachofanana, elimu yenye mazingira na ubora unaolingana, kupewa adhabu inayofanana bila upendeleo na kutoa ajira kwa usawa," alisema.
Naye Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Dk. John Magoti alisema mdahalo alisema lengo la kufanya mdahalo huo ni kupima na kutathmini misingi na maadili ya Mwalimu Nyerere yanavyoenziwa.