Suluhu katika elimu yetu si kukwepa ukweli

Undava King

JF-Expert Member
Aug 11, 2017
3,205
5,333
Kumekuwa na sintofahamu kubwa juu ya uelekeo wa elimu yetu. Katika siku za hivi karibuni hatuitaji utafiti wowote kujua kama elimu yetu imeshuka.

Baadhi ya dalili za elimu yetu kuporomoka ni kama hizi

1. Watoto kufahulu kwenda kidato cha kwanza wakiwa hawajui kusoma wala kuandika mpaka wazazi wanaona aibu kupoteza pesa zao kuwaripotisha shuleni.

2. Kuwa na mitahala mibovu na isiyo tengeneza wasomi bali wategemezi, kuanzia shule za misingi mpaka vyuo vikuu.

3. Uhaba wa miundombinu, walimu na vifaa vya kujifunzia.

4. Kukosekana kwa sera nzuri ya kudhibiti ubora na kuboresha mazingira ya elimu nchini.

5. Maslahi madogo kwa walimu, muda mrefu wa masomo kila siku aghalabu 11 hadi 12 na mfululizo wa wanafunzi kusoma mpaka wakati wa likizo pasipo mapumziko lakini matokeo ni yale yale.

6. Elimu kuchukuliwa kuwa ni adhabu kwa watahiniwa hivyo kurahisishwa kila mwaka hili kupata ufaulu mkubwa.

7. Wasomi kutoajirika wala kuonekana kuwa na mchango katika jamii zao tofauti na wale ambao hawajasoma n.k

Nini chanzo

1. Tumeacha misingi imara tulikuwa nayo katika elimu natukabakia katika matukio na utandawazi

2. Umasikini wa taifa umeongezeka maradufu ikiwemo ongezeko kubwa la watu ambao wanazaliana lakini hawawezi kumudu mahitaji yao sababu ya kukosa kipato, hivyo utegemezi unaielemea hata serikali yenyewe.

3. Kukosa vipaumbele kama taifa, hasa suala la elimu kuwa ni kitu cha ziada kwa kuwa akileti pesa ya moja kwa moja haraka kama utalii na madini ambavyo si vitu vya kudumu au kutegemewa sana kwa muda mrefu.

4. Kukosekana kwa sera bora ya elimu na mfumo wa mabadiliko ya mara kwa mara katika mitahala sababu ya kuigaiga au mitizamo binafsi ya viongozi na siyo taaluma n.k

Nini kiachwe
1. Tuache tabia za kulazimisha mambo yawe mazuri wakati ukweli unaonesha sivyo.

Mfano kumkamata mzazi aliyegoma kumpeleka mwanaye shule baada ya kugundua kahitimu ila hajui kusoma wala kuandika, kumchapa mwalimu viboko mbele ya kadamnasi au wanafunzi kisa kashindwa majukumu yake kwa kuwa alienda kujitengenezea kipato chake kwa kuendesha boda boda katika muda wake wa halali jioni ambapo wewe mwajiri unahitaji aendelee kufundisha mpaka full time yako ya saa moja usiku na haumlipi n.k

2. Tuache kuitumia elimu kisiasa au kutafutia huruma au kuaminiwa na umma. Kumbuka rasilimali watu ndiyo uti wa mgongo wa taifa lolote lile lililofanikiwa.

3. Tuache tabia za kujifanisha kana kwamba matatizo ya elimu yameshakomaa na hivyo hayatatuliki, hivyo tuaminishane kuwa tunahitaji muda mrefu na bajeti kubwa mno kurekebisha makosa yetu.

4. Kuogopa ushindani na sekta binafsi kwa kisingizio kuwa ukiwatangaza kuwa wamekuzidi katika ufahulu na mazingira yakujifunzia utawapaisha kibiashara n.k

Kitu ambacho hakipo kiuhalisia isipokuwa unajaribu kuyaficha madhaifu yako nakuhisi hiyo ndiyo njia pekee ya kukiepuka kivuli chako.

Nini Kifanyike

1. Elimu ya Awali (chekechea) iwe ni lazima katika ngazi ya chini yaani elimu ya msingi na walimu wake waajiriwe kwa wingi kulingana na uhitaji.

NB: Napendekeza waajiriwe walimu waliobobea katika taaluma hii ya elimu ya Awali kwa watoto na mahitaji maalumu na vilevile tusiwabague hawa waliopo mtahani ila kiwango chao cha elimu ni kidogo ila ni wazoefu na wanawasaidia watoto wetu kujua kusoma na kuandika kwa kiswahili na kiingereza huko tuisheni, tuwape nafasi watuandalie kizazi kijacho.

2. Mtoto aingie darasa la kwanza akiwa tiyari anajua kusoma na kuandika, daraja hili liwe ni la kujifunza kujua kuandika vizuri (imla,mwandiko na uchoraji) hesabu, lugha, sayansi na stadi za kazi kama tulivyokuwa Awali.

3. Mitihani ya kujipima ufahulu wetu irudi kama Awali na itiliwe mikazo kuanzia darasa la nne na la saba, pia kidato cha pili na cha nne, mwanafunzi yeyote ambaye hajapikwa vyema asivuke hatua hizi pasipo kuzimudu.

4. Masomo ya shule ya msingi yarudishwe yote katika muundo wa zamani wa Hisabati, kiswahili,kiingereza, sayansi, maarifa ya jamii na stadi za kazi.

Hata hivyo ningependekeza ibadilike kuanzia darasa la pili na kuwa stadi za maisha hili liwe ni somo ambalo ni la lazima na liwe na maksi zote katika mtihani wa mwisho,

Somo hili lijumuishe mafunzo ya nadharia na vitendo(inapowezekana) na litajumuisha mambo yote yanayohusu maadili, tamaduni, afya, majanga, shughuli halisi za kiuchumi na uzalishaji mali katika jamii mfano kilimo cha bustani,ufugaji, useremala,uchimbaji visima na mabomba,ujenzi,utengenezaji magari,ususi,upishi,muziki, sanaa, nadharia ya awali ya kompyuta, michezo n.k

Hili somo likifundishwa vyema hata kama ni kwa nadharia litamwandaa mwanafunzi kisaikolojia kung'amua wajibu na shughuli ya kufanya endapo hata akikomea katika elimu ya msingi lakini litamsaidia pia kujua anachotaka kubobea hapo baadae katika ngazi za juu za elimu yake au hata atakapohitaji kujiunga VETA.

5. Katika elimu ya sekondari masomo yabakie kuwa yalivyo isipokuwa kuwepo na ongezeko la masomo ya biashara, ujasiriamali, kompyuta(nadharia na vitendo)na stadi za maisha (life skills for adult)

6. Elimu ya kidato cha sita kwa mtizamo wangu upande wa nadharia iko sawa isipokuwa elimu ya vitendo kwa shule zetu zote za TECHNICAL ifufuliwe upya kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita, mazingira ya kujifunzia yakiwemo makarakana, mitahala ya masomo, walimu na vifaa ni duni na ni kama sehemu ya elimu yetu ambayo tumeshaitelekeza.

7. Tujenge shule kadhaa za watu wenye mahitaji maalumu, (siyo mbaya kuanza na sehemu zenye uhitaji mkubwa) na tutoe vifaa vinavyohitajika pamoja na kuajiri walimu wenye taaluma hii wa kutosha.

8. Tuwe na vipaumbele katika kozi tunazopitisha kama mapendekezo kwa vyuo vikuu na vidogo vinavyoakisi uhalisia wa mahitaji ya soko la ajira tulilonalo nchini.

9. Tujitahidi kuboresha na kujenga miundombinu hitajika, kuajiri, kutengeneza upya mitahala yetu, vifaa vya kujifunzia na kuandaa mazingira bora ya elimu kwa wakati uliopo na kwa baadae hata kama uwezo wetu kama taifa ni mdogo kikubwa ni nia na kuipa elimu yetu kipaumbele kikubwa.

10. Tuje na sera nzuri shirikishi kwa jamii katika elimu na siyo suala la michango tu, ikiwemo kuhimiza uzazi wa mpango na malezi mazuri kwa watoto wetu, tuimarishe na sekta nyingine za kiuchumi,afya na uzalishaji mali hili jamii iweze kuwa na mchango wa moja kwa moja katika kuboresha mazingira ya elimu yao.
 
Back
Top Bottom