Bishop Hiluka
JF-Expert Member
- Aug 12, 2011
- 7,140
- 14,678
Na Bishop Hiluka
(Mwandishi wa stori za kusisimua zilizowahi kuchapishwa hapa JF za Kizungumkuti!; Laiti Ningejua!; Hekaheka!; Hadi Lini! na nyinginezo)
0685 666964
SAA 1:35 asubuhi, Samuel Kambona alishuka kutoka ndani ya gari aina ya Toyota Alphard la rangi ya bluu katika viunga vya maegesho ya magari vya majengo ya hoteli ya Udzungwa Beach Resort, iliyopo katika ufukwe wa Oystebay, jijini Dar es Salaam.
Gari lile lilikuwa na nembo ubavuni iliyokuwa na maandishi ya Udzungwa Beach Resort.
Samuel maarufu kama Sammy, alikuwa kijana mtanashati mwenye umri wa miaka 35 na msomi wa Shahada ya Umahili ya Biashara za Kimataifa na Lugha (M.A in International Business with Languages), aliyoipata kutoka Chuo Kikuu cha Warwick nchini Uingereza,
Alikuwa mrefu na mweupe mithili ya chotara wa kizungu, mwenye sura ya tabasamu muda wote. Urefu, mwili wake wa kimazoezi, utanashati na asili ya ngozi yake nyeupe ni vitu vilivyowavutia wasichana wengi aliokutana nao.
Ukiongezea na ndevu nyingi alizopenda kuzinyoa katika mtindo wa circle beard au kama wengi walivyozoea kuita “O”, vilimfanya azidi kuwa mvuto mkubwa kwa walimbende pindi walipomtia machoni.
Siku ile ilikuwa Ijumaa, kama kawaida yake, Sammy alikuwa katika mwonekano maridadi kabisa, akiwa amevalia shati zuri la rangi ya samawati la kitambaa brandi ya Barba ndani ya suti nyeusi ya aina ya Dunhill, tai ya rangi ya bluu shingoni na viatu ghali vya ngozi halisi kutoka nchini Switzerland.
Pia alikuwa amevaa saa ya mkononi aina ya Cartier iliyokuwa na nakshi ya madini ya dhahabu na kujipulizia manukato ghali aina ya Dolce & Gabbana. Mkononi alikuwa amebeba mkoba wake mdogo wa kiofisi aina ya Pad & Quill wa rangi ya hudhurungi.
Wakati akishuka kutoka kwenye gari manyunyu mepesi ya mvua yalikuwa yakianguka ardhini, lakini bado hayakumzuia Sammy kutembea taratibu akikatisha kwenye viunga vya maegesho ya magari na kuelekea mbele ya jengo la mbele la ile hoteli ya kitalii yenye hadhi ya nyota tano.
Wakati akitembea macho yake yaliangaza huku na kule kana kwamba alikuwa akitafuta kitu. Alipishana na askari mmoja wa ulinzi kutoka kampuni ya ulinzi ya Spark K7 aliyekuwa akilinda eneo lile la viunga vya maegesho ya magari.
Eneo lile lilikuwa pana likiwa na uwezo wa kuruhusu magari madogo hadi 100 kuegeshwa kwa wakati mmoja, na lilikuwa limepandwa miti mirefu ya kivuli aina ya ‘Quercus virginiana’ na ‘Arecaceae’ iliyojulikana pia kama ‘coconut palms’.
Pia eneo lile lilipandwa nyasi nzuri laini aina ya ‘Citronella’ na kulikuwa na bustani ya maua ya kupendeza yaliyotoa hewa safi ya upepo wa asili baina ya sehemu moja ya maegesho ya magari na sehemu nyingine, ndani ya uzio wa yale majengo ya hoteli.
Kwa yeyote aliyefika Udzungwa Beach Resort angeweza kubaini mara moja kuwa majengo ya hoteli hiyo yalijengwa kwa ufanisi wa hali ya juu.
Kulikuwa na majengo makuu mawili, moja lilikuwa mbele na la pili lilikuwa nyuma na kila moja lilikuwa na ghorofa saba za juu na mbili za chini, zilizotumika kwa ajili ya kumbi za burudani, kumbi za mikutano na migahawa ya kisasa ya chakula cha kitanzania na cha kimataifa. Pia kulikuwa na maduka na ofisi za utawala kwenye orofa ya chini nay a kwanza ya jengo la mbele.
Katika eneo lile kulikuwa na duka kubwa la bidhaa mbalimbali maarufu kama “supermarket”, duka kubwa la vipodozi na nguo za kisasa (boutique), na duka la kubadilishia fedha za kigeni maarufu kama “Bureau de Change” na vyumba viwili vidogo vyenye Mashine za ATM
Pia kulikuwa na jengo maalumu la klabu iliyojulikana kama Paradise Club, ambayo ilikuwa kwenye jengo la nyuma iliyowakutanisha mabilionea na baadhi ya vigogo serikalini na ilikuwa na ulinzi mkubwa sana, nje na ndani ya klabu.
Walioruhusiwa kuingia ndani ya klabu hiyo ni wanachama tu waliokidhi vigezo na kusajiliwa, ambao walilipa kiasi kikubwa cha ada ya uanachama kila mwaka.
Ndani ya majengo yote ya hoteli hiyo kulikuwa na kamera za usalama (CCTV) kila kona, viyoyozi vilivyosambaa kila mahali, na kutoka ghorofa moja kwenda nyingine kulikuwa na ngazi za kawaida na vyumba maalumu vya lifti za kisasa. Pia kulikuwa na ngazi iliyoendeshwa kwa umeme.
Yale majengo yalijengwa katika eneo tulivu mno lisilo na bughudha la ufukwe wa Oysterbay, jirani kabisa na ofisi za kibalozi na makazi ya watu wenye ukwasi, takriban kilomita tatu tu kutoka katikati ya jiji la Dar es Salaam.
Kwa watu wengi wenye ukwasi, Udzungwa Beach Resort ilikuwa ndiyo sehemu nzuri na tulivu zaidi ya kwenda kujipumzisha na kufurahia maisha, kwani ilikuwa imezungushiwa uzio madhubuti wenye ulinzi na kamera za usalama ulioifanya kuwa mahali patulivu zaidi na pa usalama wa uhakika.
Asubuhi ile kulikuwa na magari machache madogo na mabasi mawili ya wanafunzi wa vyuo vikuu vya Cape Town cha nchini Afrika Kusini na Chinhoyi cha nchini Zimbabwe yaliyokuwa yameegeshwa katika viunga vya maegesho ya magari.
Pia kulikuwa na malori mawili makubwa ya kubebea watalii wa masafa marefu aina ya Mercedes Benz, yaliyokuwa yameegeshwa mwisho kabisa wa yale majengo.
Mbele ya ile hoteli katika jengo la mbele Sammy aliipita milingoti saba iliyokuwa na bendera za Afrika Mashariki, Marekani, Uingereza, India, China, Afrika Kusini na bendera yenye nembo ya Udzungwa Beach Resort, zilizokuwa zinapepea taratibu.
Kulikuwa na mlango mkubwa wa vioo mbele ya jengo na varanda pana yenye ngazi iliyofunikwa kwa kofia nzuri ya zege ikiwa na sakafu nzuri yenye marumaru iliyonakshiwa kwa maandishi ya “Udzungwa Beach Resort”.
Kijana mmoja askari wa kampuni ya ulinzi ya Spark K7 alikuwa amesimama kikakamavu kwenye ile varanda pana akiwa kando ya ule mlango mkubwa wa vioo wa kuingilia ndani. Yule askari wa ulinzi aliyeitwa Fred Luvanda alimuona Sammy na kumpokea kwa tabasamu la kirafiki lililokuwa na bashasha zote kwenye uso wake.
Endelea kufuatilia...
SEHEMU 2
Taxi - (2)
“Habari za asubuhi, Boss!” Fred alimsalimia Sammy wakati alipokuwa akizikwea zile ngazi za ile varanda.
“Salama tu, Fred,” Sammy alijibu huku naye akiachia tabasamu na kuusogelea ule mlamgo mkubwa wa kioo ambao ulijifungua wenyewe kwa vioo vyake kujisogeza pembeni ili kumruhusu aweze kuingia ndani.
“Vipi, kesho utaenda Uwanja wa Taifa?” Fred alimtupia swali Sammy kabla hajaingia ndani ya lile jengo na kumfanya asimame na kugeuza shingo yake kumtazama.
“Kesho lazima niende, safari hii tumejipanga kweli kweli, nyie Simba msubiri kipigo tu,” alisema Sammy kwa msisitizo huku akiangua kicheko hafifu.
“Aa wapi, kwa timu ipi mtufunge sisi?” alisema Fred aliyeonekana kuwa shabiki kindakindaki wa timu ya Simba na aliiamini mno timu yake.
“Basi kesho usizime simu, mpira ukiisha tu nitakutafuta… safari hii hamtoki salama pale kwa Mchina. Tunawapiga hizi!” Sammy alisema kwa kujiamini huku akimuonesha Fred ishara ya vidole vitatu.
“Thubutuu… mumpige nani tatu, labda kama unaongea kinyume chake!” Fred alisema huku akiachia kicheko hafifu, na kuongeza, “Nyie ni vibonde wetu tu.”
“Ningekwambia tuwekeane dau lakini najua utaliwa tu, sisi ndio mabingwa wa kihistoria bwana!” Sammy alisema huku akiingia ndani, na kumwacha Fred akiwa anatabasamu.
Ndani ya lile jengo Sammy alipokewa na mhudumu mmoja wa kiume aliyekuwa amevaa shati jeupe lenye kola ya rangi ya samawati, suruali ya rangi ya samawati, koti la suti la rangi ya bluu, tai ndogo ya rangi ya bluu na kofia ya bluu kichwani.
Yule mhudumu alimsalimia Sammy kwa bashasha zote huku akionesha tabasamu la kirafiki kwenye uso wake. Sammy aliitikia salamu yake na kumpita huku akitembea taratibu kupita juu ya zulia nene la rangi nyekundu, akatokea katika eneo la mapokezi.
Eneo lile la mapokezi lilikuwa pana lenye mazingira yaliyoashiria ustaarabu, yakiwa masafi na yenye mandhari yenye kuvutia kiasi cha kutoa liwazo kwa mgeni yeyote aliyeingia, huku likizungukwa na meza nzuri ya kaunta yenye umbo la nusu duara iliyotengenezwa kwa mbao za mninga, na ilikuwa ikitazamana na makochi mawili makubwa ya ngozi laini ya sofa.
Pembeni ya kidogo pia kulikuwa na makochi mengine manne madogo ya ngozi laini ya sofa yaliyopangwa kwa ustadi mkubwa na mbele yake kulikuwa na meza fupi za vioo zilizokuwa katika mpangilio uliovutia.
Ukutani kulikuwa na madirisha makubwa ya vioo yaliyoruhusu mwanga kutoka nje kuingia mle ndani na yalikuwa na mapazia marefu yenye rangi nzuri za kupendeza yaliyobanwa vizuri pembeni yake. Ukutani kulikuwa na runinga kubwa ya bapa iliyokuwa ikionesha kipindi cha mitindo kilichorushwa na kituo cha runinga cha Nuru.
Pia kulikuwa na kitufe kikubwa chekundu cha kengele ya hatari pembeni ya mitungi miwili mikubwa ya gesi ya kuzimia moto wa dharura.
Sammy alishusha pumzi za ndani kwa ndani huku akilakiwa na hewa safi ya ubaridi iliyokuwa ikisambazwa na viyoyozi vikubwa vilivyokuwa kwenye kona mbili za eneo lile, kutokea juu dari ya gypsum iliyonakshiwa vyema.
Sammy aliwatupia macho watu wachache waliokuwa wameketi kwenye yale makochi ya sofa katika eneo lile la mapokezi: miongoni mwao kulikuwa na Wazungu wawili walioonekana kuwa wapenzi kutokana na mkao wao.
Mwanamume alikuwa mrefu na mwembamba akiwa amevaa fulana nyeupe, suruali nyeusi ya jeans na raba miguuni, na mwanamke alikuwa mrefu kiasi na alivaa gauni fupi jeusi la kukata mikono lililolichora vyema umbo lake na kuyaacha mapaja yake wazi.
Mbali na wale Wazungu, kulikuwa na Waafrika watatu, mwanamume mmoja wa makamo, mrefu na alikuwa na ndevu nyingi zilizokizunguka kidevu chake, alivaa suti maridadi nyeusi na miwani ya macho, pia kulikuwa na vijana wawili walioonekana ni wapenzi au mume na mke waliotoka kufunga ndoa na sasa walikuja kwa ajili ya fungate.
Yule kijana wa kiume alikuwa mrefu na maji ya kunde, alivaa shati la bluu lenye mistari myeupe na suruali nyeusi, na muda wote alikuwa anatabasamu. Mwenzi wake alikuwa msichana mrembo mrefu kiasi, alikuwa amevaa gauni la kitambaa cha bazee lililoshonwa na kudariziwa vizuri na kichwani alikuwa amevaa kilemba.
Mbele ya meza kubwa ya mapokezi kulikuwa na watu wazima wawili wenye asili ya Kiasia waliokuwa wamesimama na mabegi yao, na ilionekana kuwa walikuwa ni mke na mume walioishi maisha marefu ya ndoa yenye furaha na walifika hapo kwa ajili ya mapumziko.
Nyuma ya ile meza kubwa ya mapokezi kulikuwa na wahudumu wawili vijana, mmoja wa kiume na mwingine wa kike, waliokuwa katika sare nadhifu za kazi: mashati meupe yaliyokuwa na kola za rangi ya samawati, suruali za rangi ya samawati na makoti ya suti ya rangi ya bluu iliyokolea, na shingoni wakiwa wamevaa tai ndogo za samawati zilizowakaa vizuri.
Mhudumu wa kiume aliyeitwa Abbas Saleh alikuwa anazungumza na wale wenzi wenye asili ya Kiasia, na yule mhudumu wa kike aliyefahamika kwa jina la Rose Mahenge alikuwa akiongea na simu huku akiweka vizuri mazingira ya pale mezani.
Alikuwa msichana mrembo sana mwenye uso wa umbo duara, akiwa na umbo kubwa lililovutia mno lenye kiuno chembamba lakini imara, kilichoshikilia minofu laini ya mapaja yake makubwa, na hakuwa amezidi miaka therathini.
Rose alimuona Sammy wakati akipita katika eneo lile la mapokezi na haraka aliishusha ile simu na kuacha kazi aliyokuwa akiifanya, uso wake ukachanua kwa tabasamu pana lenye bashasha lililovifanya vishimo vidogo mashavuni kwake vichomoze haraka.
Japokuwa alikuwa amevaa sare za kazi lakini bado uzuri wake haukujificha kabisa. Alikuwa na macho mazuri malegevu lakini yaliyoonekana kuwa makini kuliko hata simba jike anayewinda.
Alikuwa mrefu wa wastani na mweupe kwa rangi ya ngozi iliyokuwa na mng’aro wa aina yake na mvuto wa kipekee, na hakuhitaji vikorombwezo vya aina yoyote kuinakshi ngozi ile
Sammy alimpiga ukope huku akipunga mkono wake kumsalimia, tabasamu kabambe la aina yake lilichanua usoni kwake na kumfanya Rose ajikute akiachia kicheko hafifu kilichowafanya watu wote wageuke kumtazama Sammy kwa makini, na baadhi yao walijikuta wakiachia tabasamu.
“The guy is so handsome… ni mpole, mcheshi, mchapakazi na zaidi ya yote ana moyo wa upendo na huruma,” Rose aliwaza huku akiendelea kumtazama Sammy kwa tabasamu.
Kwa kuwa Sammy hakuwa akipenda kutazamwa na kugeuka kivutio alishusha pumzi za ndani kwa ndani na kuzitupa hatua zake haraka haraka kulivuka eneo lile akielekea eneo zilipokuwa ngazi za lile jengo la hoteli za kuelekea juu. Alipoaliacha eneo lile la mapokezi aliupita mlango wa kuingia kwenye kaunta kubwa ya vinywaji.
Itaendelea...
SEHEMU YA 3
Taxi - (3)
Kisha alielekea upande wa kushoto na mbele yake akauvuka ukumbi mkubwa kiasi wa kisasa wa chakula, uliokuwa na meza nyingi za kulia chakula zenye umbo mstatili zilizozungukwa kwa viti nadhifu vyenye foronya laini.
Katika ule ukumbi wa chakula kulikuwa na watu wachache waliokuwa wakijipatia stafustahi katika meza zilizokuwa zikimefunikwa kwa vitambaa visafi vya rangi nyeupe na juu yake kuliwekwa kadi ngumu za kupendeza zenye orodha ya vyakula na vinywaji vilivyokuwa vinapatikana katika hoteli ile.
Mbele kidogo Sammy alipishana na wazungu watatu, wanawake wawili na mwanamume mmoja waliokuwa wanaelekea kwenye ukumbi wa chakula. Sammy aliwasalimia na kuifuata korido ndefu iliyokuwa upande wake wa kulia na kisha akavivuka vyumba viwili vya lifti za kuelekea ghorofa za juu za lile jengo la hoteli.
Katika eneo lile, kulikuwa na wahudumu wawili wa ile hoteli waliokuwa wakisubiri lifti ya kuelekea juu, na wakati huo huo mlango wa chumba kimoja cha lifti iliyokuwa imefika sehemu ya chini ya jengo ulifunguka na kuwaruhusu watu kadhaa kutoka ndani yake, huku wakiwapisha wale wahudumu kuingia.
Sammy alielekea mbele zaidi akaupita mlango mkubwa wa kuelekea kwenye ukumbi wa mazoezi, na juu ya mlango ule kulikuwa na kibao cheusi chenye maandishi meupe yaliyokuwa yakisomeka ‘GYM’, yaani Ukumbi wa mazoezi.
Upande wa kushoto wa eneo lile kulikuwa na mlango mwingine uliokuwa unaelekea sehemu ya maliwato na hatua chache mbele yake, mwisho kabisa wa ile korido kulikuwa na mlango mkubwa wa vioo uliokuwa na maandishi juu yake yaliyoandikwa “Administration”, na upande wa kulia kulikuwa na ngazi za kuelekea juu ya lile jengo la hoteli.
Sammy alizikwea zile ngazi hadi ghorofa ya kwanza, akaufikia mlango mwingine mkubwa wa vioo uliokuwa na maandishi juu yake yaliyoandikwa “Administration”.
Aliusukuma ule mlango na kutokea kwenye korido pana iliyokuwa na ofisi kadhaa, ofisi yake ilikuwa mkono wa kulia mara baada ya kuingia katika eneo lile. Juu ya kizingiti cha mlango wa ile ofisini kulikuwa na kibao cheusi kilichokuwa na maandishi meupe: “Event Manager”. Ulikuwa ni mlango mkubwa na imara wa mbao ngumu za mninga.
Sammy alitoa kadi ngumu ya kielektroniki, mfano wa kadi ya benki, kutoka kwenye mkoba wake na kuipitisha juu ya kile kitasa maalumu cha mlango ule na kuusukuma ule mlango. Ukafunguka na kumruhusu kuingia ndani.
Ilikuwa ofisi kubwa na nzuri iliyokuwa na mandhari tulivu kama ilivyo kwa ofisi yoyote ya kisasa yenye vitu vyote muhimu. Sammy aliwasha swichi ya kiyoyozi makini aina ya Boss kilichoanza kusambaza hewa safi ya ubaridi mle ndani.
Alishusha pumzi za ndani kwa ndani na kukatisha katikati ya kile chumba kukielekea kiti chake, kisha akavua koti lake na kulitundika kwenye “henga” maalumu ya kutundikia koti.
Aliminya midomo yake, akaitia mikono yake mifukoni kwa utulivu akionekana kutafakari jambo kwa kitambo kifupi, kisha alisogea kwenye dirisha pana la kioo, lililokuwa limefunikwa kwa mapazia mawili mepesi na marefu ya rangi ya bluu, kando ya meza yake kubwa ya ofisi.
Aliyasogeza yale mapazia pembeni na kuruhusu mwanga wa jua upenye mle ndani kupitia ukuta msafi wa kioo cha lile dirisha. Kwa dakika kadhaa alitulia pale dirishani huku akiyatazama mandhari ya lile jengo la hoteli kwa upande ule wa nyuma, kana kwamba alikuwa akiyaona kwa mara ya kwanza.
Upande ule wa nyuma kulikuwa na bustani nzuri ya nyasi laini aina ya ‘Citronella’ zilizokuwa zimekatwa vizuri na kupendeza, huku mandhari yake ikipambwa na aina mbili za maua mazuri: ‘Magnolia grandiflora’ ya rangi ya maziwa na maua aina ya ‘lotus’ yenye mchanganyiko wa rangi nyeupe, pinki na zambarau.
Katika eneo lile kulikuwa na sehemu za kupumzika zenye viti na meza chini ya miamvuli mikubwa yenye rangi za kupendeza na mabwawa makubwa ya kuogelea, sehemu zenye viti maalumu vya kupumzikia chini ya miti mizuri aina ya coconut palms pamoja na vibanda vidogo vya faragha.
Kwa utulivu huku akiwa bado ameweka mkono wake wa kushoto mfukoni na mkono wa kulia akiwa ameuegemeza pale kwenye kioo cha dirisha, alijikuta akivutiwa kuwaangalia wazungu wawili, mwanamke na mwanamume waliokuwa wameketi chini ya lile ghorofa kwenye vibanda vidogo vya faragha wakiongea huku wakipapasana sehemu mbalimbali za miili yao kwa mahaba.
Kama mtu aliyekumbuka jambo, alishusha pumzi za ndani kwa ndani kisha akaenda kuketi kwenye kiti chake kikubwa cha ngozi halisi cha kiofisi cha kuzunguka na chenye magurudumu madogo yaliyokiwezesha kusogea.
Mbele yake kulikuwa na meza kubwa ya ofisini ambayo juu yake kulikuwa na kompyuta mpya aina ya iMac Pro, mashine ndogo ya kuchapa barua (printing machine) aina ya HP LaserJet na ‘trei’ mbili zilizokuwa na maandishi ya ‘IN’ ikimaanisha kazi zilizoingia na ‘OUT’ ikionesha kazi zinazotoka, huku lile trei la kazi zilizoingia likiwa tupu.
Pia juu ya ile meza mbele yake kulikuwa na kibao kidogo kilichokuwa na maandishi ya “Samuel Komba - Event Manager”, simu ya mezani, majalada kadhaa, vitabu, kidau cha wino, mhuri na kichupa kidogo chenye wino mweupe wa kufutia maandishi.
Kando ya ile meza jirani na lile dirisha pana la kioo, kulikuwa na rafu kubwa ya vitabu na majalada mbalimbali yaliyopangwa kwa ustadi wa hali ya juu.
Mbele yake kulikuwa na seti moja ya makochi madogo ya ngozi laini ya sofa yaliyoizunguka meza fupi ya kioo yenye umbo la yai na chini ya meza ile kulikuwa na magazeti na majarida kadhaa tofauti.
Ukutani kulikuwa na picha kubwa mbili, moja ya Rais wa Tanzania na ya pili ilikuwa ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, na sakafu ya ofisi ile ilifunikwa kwa zulia maridadi jekundu.
Sammy alipotaka kuwasha kompyuta yake simu yake ya mkononi ikaanza kuita kwa fujo, Sammy aliichukua ile simu na kuangalia namba ya mpigaji lakini hakuweza kumtambua kwani ilikuwa ngeni. Akaipokea.
“Hello!” Sammy alisema mara baada ya kuiweka ile simu kwenye sikio lake.
“Hallo…” sauti nyororo ya mwanamke ilisikika kutoka upande wa pili wa ile simu. Mara kukazuka ukimya uliomshangaza kidogo Sammy.
“Ndiyo!” Sammy alisema huku akijaribu kusikiliza kwa makini.
“Nani mwenzangu?” ile sauti nyororo ya kike ilisikika ikiuliza kwa mshangao na kumfanya Sammy akunje sura yake.
“Kwani wewe ulikusudia kumpigia nani?” Sammy naye aliuliza kwa mshangao.
“Sina uhakika…” ile sauti nyororo ya kike ilijibu na kumfanya Sammy aachie kicheko hafifu.
“Nadhani utakuwa umekosea namba,” alijibu huku akilamba midomo yake.
“Inawezekana!” ile sauti nyororo ya kike ilisema.
“Huwa inatokea… usijali sana,” Sammy alisema na kukata simu.
Itaendelea...