Taxi - (152)
“Joyce, najua unayo maswali mengi sana kichwani kwako na hili tulilokwambia limekuzidishia mkanganyiko badala ya kujibu maswali yako. Naomba ufahamu kuwa mimi ndiye mama’ako, nilipata ujauzito wako nikiwa kidato cha nne, nikakatisha masomo na mambo fulani yakatokea, nilipokuzaa nikakuacha na baba’ako Jengo,” Madame Norah alisema kwa sauti ya kutetemeka huku machozi yakianza kumtoka.
“Huwezi kuamini, kwa miaka yote hii nimekuwa nikikutafuta sana, ilifikia kipindi nikaamini kuwa wewe na baba’ako mlikufa kwenye ajali ya moto ulioteketeza nyumba mliyokuwa mkiishi eneo la Ngamiani Tanga. Baada yah apo sikujua ningewapata wapi hadi jana nilipokutana na baba’ako pale hospitali. Nisamehe sana binti’angu, najua sikukutendea haki lakini itoshe tu kusema kuwa najutia sana kitendo changu, kwani tangu wakati huo nimekuwa nikiishi maisha ya huzuni kubwa na majuto mengi ingawa watu wakiniangalia hudhani labda nina furaha...”
Maneno yale yalizidi kumuumiza Joyce, hakujua aseme nini. Hata hivyo, aliendelea kuwa kimya kabisa. Alihisi labda akili yake ilikuwa haifanyi kazi sawasawa. Aliendelea kumtazama Madame Norah kwa makini. Kikatokea tena kitambo kirefu cha ukimya.
Haikuwa rahisi kwa Joyce kuipokea taarifa ile. Ilikuwa ni taarifa ngeni kabisa masikioni mwake na akili yake ilikataa kuikubali. Siku zote alikuwa akimchukulia Madame Norah kama mfano wa mwanamke mwenye mafanikio, akitamani siku moja kufikia japo nusu ya mafanikio yake, hakuwahi kudhani kama angeweza kuwa mama’ake mzazi.
Japo alitaka kuamini lakini akili yake likataa, ila alipowatazama wale wanawake wawili alikiona kitu kwenye macho yao na nyuso zao, kitu kilichomhakikishia kuwa yote aliyoyasikia yakisemwa juu yake yalikuwa kweli kabisa!
Baada ya kitambo kirefu hatimaye Joyce aliwataka wamwache kwanza, kwani alihitaji muda wa kuwa peke yake ili aweze kutafakari kabla hajaamua lipi la kufanya. Hata hivyo, kabla hajajitenga aliomba afahamishwe ni wapi ilipokuwa familia yake. Madame Norah alimtaka kuwa jasiri huku akijitahidi kuifanya sauti yake iwe za kawaida.
Kisha walimweleza Joyce yote kuhusu nyumba yao kushambuliwa na bomu lililotegwa kwenye gari na watu wasiojulikana, wakati huo Sammy na Jengo wakiwa ndani ya nyumba hiyo. Wakamweleza kuhusu majeraha waliyoyapata na Sammy kulazwa Muhimbili, na kwamba hali yake ilikuwa inaendelea vizuri.
* * * * *
Mr. Oduya aliwasili katika jengo la makao makuu ya ofisi za
The Splendid Group lililopo barabara ya Bagamoyo, eneo la Kijitonyama. Alikuwa akitokea
Paradise Club alikokwenda kuonana wa mshirika wake mkubwa, Kamishna Omalla, Mkuu wa Kamisheni ya Intelijensia wa Jeshi la Polisi.
Kama mtu mkubwa, Mr. Oduya alitumia lifti maalumu ambayo ilimfikisha katika ghorofa ya saba ilikokuwa ofisi yake na kuutumia mlango maalumu ili kuingia ofisini kwake bila kubughudhiwa na mtu mwingine. Alipoingia alijibwaga juu ya kiti chake na kuitazama saa yake ya mkononi, ilionesha kuwa ilishatimia saa nne na nusu asubuhi. Mr. Oduya alishusha pumzi na kupandisha miguu yake juu ya meza na kuinyoosha, akatulia akitafakari.
Japokuwa alipaswa kufurahia kazi nzuri iliyofanywa na Robert Kamau ya kumsababisha ajali ya gari Inspekta Abel, mtu aliyeanza kuwa tishio kwake, huku akihakikishiwa kuwa asingeweza kuamka tena na kama angefanikiwa kuamka basi angekuwa mlemavu maisha yake yote, lakini Mr. Oduya alishangaa kuona kuwa bado hakuwa na furaha wala amani kabisa moyoni.
Alijihisi kama yupo uchi kabisa kwa Tunu na hilo halikuwa na mjadala. Kwanza binti huyo alikuwa amefanikiwa kuepuka mitego yote aliyomtegea kwa miaka mitatu na kusababisha vifo vya watu wake muhimu sana kwenye harakati zake, huku Victor akiwa mahututi akipigania roho yake hospitali, na pili alishagundua mambo yao mengi.
Mr. Oduya alidhani kuwa ili kuwa salama alipaswa kuhakikisha anammaliza Tunu kabla jua halijatua. Hata hivyo jambo la ajabu, hadi wakati huo hakuna yeyote miongoni mwa watu wake aliyejua Tunu alikuwa wapi. watu wote aliowapa jukumu la kumfuatilia Tunu hawakujua alikuwa wapi, tangu alipookolewa na watu wake usiku wa kuamkia siku ile. Alianza kuingiwa na mawazo kuwa huenda alikufa kwenye ile ajali.
Alijikuta akianza kupata furaha moyoni ingawa hakupendaa kuamini, alitoa maagizo kwa watu wake wote kuwa makini sana na kuhakikisha wanafuatilia kila taarifa na maeneo yote waliyodhani huenda Tunu angeweza kuwepo. Maeneo kama Hospitali ya Amana, Muhimbili au katika mgahawa wa kisasa wa Elli’s ambako Tunu aliliacha gari lake.
Muda huo Mr. Oduya alikuwa mchovu aliyechoshwa na fikra nzito. Aliwasha kiyoyozi ndani ya ofisi yake kilichojaribu kuupooza mwili wake. Kisha alianza kumezwa na fikra nzito mpaka pale alipokuja kushtushwa na simu yake ya mkononi iliyoanza kuita kwa fujo. Mr. Oduya aliichukua ile simu na kuitazama kwa makini, akaachia tabasamu baada ya kuliona jina la Kamishna Omalla. Aliipokea ile simu na kuipeleka sikioni.
“Hallo, poti!” Mr. Oduya alisema kwa sauti tulivu huku akibana pumzi zake.
“Ni nini hiki umefanya?” sauti nzito ya Kamishna Omalla ilisikika ikimuuliza Mr. Oduya pasipo kujuliana hali.
“Kwani ulitarajia nini, poti?” Mr. Oduya aliuliza huku akiminya midomo yake kuzuia kicheko kilichotaka kumtoka. “Vipi, amekufa?”
Kamishna Omalla hakujibu mara moja, alibaki kimya kwa kitambo kirefu hadi Mr. Oduya akadhani labda alikuwa amekata simu. Alipotaka kuita akamsikia Kamishna Omalla akikohoa kidogo kusafisha koo lake.
“Oduya, hii tabia ya kutaka kuua watu wote unaodhani ni tishio kwako inabidi uipunguze, imezidi sasa!” Kamishna Omalla alisema kwa sauti ya majonzi. Ilionekana wazi kuwa alikuwa haipendi tabia ile ya mauaji, aliamini kama yangeendelea basi mwisho wake si Mr. Oduya tu ambaye angetiwa hatiani bali hata yeye, endapo angegundulika kuwa ni mshirika wake mkubwa.
“Kamishna, najua huwezi kunielewa,” Mr. Oduya aliongea kwa sauti ya chini, “Ulimwengu huu haupo sawa kama unavyodhani. Muda mwingine yatupasa kufanya hivyo kabla hatujafanyiwa hivyo sisi wenyewe!” Mr. Oduya alisema na kumfanya Kamishna Omalla agune.
“Nakuelewa, lakini nilidhani tulikubaliana nilipokwambia suala hilo nitalishughulikia. Hukupaswa kufanya ulichokifanya,” Kamishna Omalla alisema na kushusha pumzi za ndani kwa ndani. “Hata hivyo, ngoja nione itakavyokuwa.” Kamishna Omalla alisema na kukata simu.
Usichoke kufuatilia simulizi hii ili kuujua mwisho wake...
NB:
Litro 👩