Stori ya kusisimua - Taxi

Stori ya kusisimua - Taxi

Taxi - (153)

ILIPOISHIA

“Oduya, hii tabia ya kutaka kuua watu wote unaodhani ni tishio kwako inabidi uipunguze, imezidi sasa!” Kamishna Omalla alisema kwa sauti ya majonzi. Ilionekana wazi kuwa alikuwa haipendi tabia ile ya mauaji, aliamini kama yangeendelea basi mwisho wake si Mr. Oduya tu ambaye angetiwa hatiani bali hata yeye, endapo angegundulika kuwa ni mshirika wake mkubwa.

“Kamishna, najua huwezi kunielewa,” Mr. Oduya aliongea kwa sauti ya chini, “Ulimwengu huu haupo sawa kama unavyodhani. Muda mwingine yatupasa kufanya hivyo kabla hatujafanyiwa hivyo sisi wenyewe!” Mr. Oduya alisema na kumfanya Kamishna Omalla agune.

“Nakuelewa, lakini nilidhani tulikubaliana nilipokwambia suala hilo nitalishughulikia. Hukupaswa kufanya ulichokifanya,” Kamishna Omalla alisema na kushusha pumzi za ndani kwa ndani. “Hata hivyo, ngoja nione itakavyokuwa.” Kamishna Omalla alisema na kukata simu.

ENDELEA...

Mr. Oduya aliachia tabasamu pana kwa namna fulani ya kujipongeza kwa kuandaa mkakati mzuri wa kumwondoa yule inspekta wa polisi ‘mwenye kiherehere’ aliyetaka kuwa tishio kwenye harakati na maslahi ya Mr. Oduya. Hata hivyo, hakuona kama tabasamu lilitosha, aliamua kungua kicheko. Kisha aliona kicheko hakitoshi, akainuka na kuliendea jokofu dogo lililokuwa katika pembe moja ya kile chumba kikubwa cha ofisi yake. Alilifungua lile jokofu na kutoa chupa kubwa ya mvinyo ghali kutoka Italia, aina ya Gaja Barbaresco na bilauri moja.

Akaifungua ile chupa na kujimiminia mvinyo wa kutosha kwenye ile bilauri kisha akainyanyua juu na kupiga funda kubwa la mvinyo huku akifumba macho yake na kusisimkwa mwili huku akiusikilizia ule mvinyo ukisafiri toka kwenye koo lake hadi tumboni.

Alikuwa na kila sababu za kusherehekea kwani aliamini kuwa haikupata kutokea kwa mtu yeyote au kwenye mpango wowote aliouandaa ukashindwa kumletea mafanikio. Ni mtu mmoja tu aliyetaka kumharibia rekodi yake, Tunu Michael. Hata hivyo, hakuwa na shaka tena kuwa wakati wowote angepewa taarifa njema kuhusu kifo cha Tunu, taarifa ambazo zingezidisha furaha yake mara dufu. Kwani watu wake walimhakikishia kuwa walikuwa na fununu kuhusu mahali ambapo Tunu angeweza kuwa amejificha na tayari walikwisha anza safari ya kuelekea eneo hilo ili kummaliza. Mr. Oduya alijikumbusha kuwa ili aendelee kufanikiwa katika harakati zake alikuwa na mambo mawili tu: ama kufa akipambana au kushinda vita.

* * * * *

Ni dhahiri kwa yeyote aliyemtazama machoni Naibu Kamishna Mamboleo asingeshindwa kubaini kwamba alikuwa hajapata usingizi wa kutosha kwa siku kadhaa. Mambo mengi yalikuwa yamemkabili kichwani kiasi cha kumpokonya hata hamu ya kula. Angewezaje kupumzika wakati alikuwa hajapata taarifa kamili ambazo zingemsaidia katika kukamilisha faili la upelelezi na kukomesha tishio jipya la uhalifu lililoanza kuibuka jijini Dar es Salaam?

Jioni ya siku iliyotangulia alikuwa ameitwa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kwenye kikao cha dharura na kutakiwa kutoa maelezo mbele ya wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, Mawaziri wa Mambo ya Ndani na wa Ulinzi na Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani.

Ingawa alikuwa na taarifa za awali za upelelezi wa kesi ile zilizoonesha kuwa kwa kiasi fulani mwenendo wa kesi ile, taarifa zile alikuwa ameziwasilisha kishujaa kwenye kile kikao cha wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama huku moyo wake ukidunda kwa hofu, alijua kuwa hakuwa tayari kuyajibu maswali yao mengi ili kuwaridhisha. Jasho jembamba lilimtoka baada ya kutupiwa lawama kuwa yeye na vijana wake wote walionekana kutumia mbinu za kizamani katika kukabiliana na wahalifu walioonekana kuwa mbele yao.

Wale wakuu walimtaka Naibu Kamishna Mamboleo awape maelezo ambayo yangewaridhisha iwapo alidhani alikuwa bado anatosha kuendelea kushika nafasi ile ya Ukamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam. Wale wakuu walimkumbusha kuwa yeye na vijana wake walipaswa kuwa makini muda wote kwani walikuwa wamefundishwa mbinu zote za kuwawezesha kung’amua viashiria vyovyote vya uhalifu kabla havijatokea na kwamba uhai wa jiji zima la Dar es Salaam ulikuwa ukiwategemea wao.

Nusura Naibu Kamishna Mamboleo apate hasira kwa lawama zilizokuwa zikielekezwa kwake ambazo hakuona kama zilimstahili. Ilibaki kidogo tu atangaze kujiuzulu nafasi hiyo, lakini hakuweza kufanya hivyo baada ya kukumbuka kuwa jambo lolote la kihalifu ambalo lingetokea katika Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ni yeye ndiye aliyestahili kupewa lawama zile, kwani kufanya kazi ni kupata matokeo mazuri ya kazi hiyo na kama hakuna matokeo basi hiyo haiwezi kuitwa kazi.

Naibu Kamishna Mamboleo alikuwa amedhamiria kupata matokeo mazuri ya kazi na kulifunga jalada la kesi ile haraka iwezekanavyo ndani ya wiki ile, lakini muda ule alikuwa amepata taarifa mbaya sana zilizoonesha kumchangaya zaidi. Taarifa kuhusu ajali ya gari na kuumia kwa Inspekta Abel wakati akiwa katika majukumu yake ya upelelezi, na ilionesha wazi kuwa ilikuwa ni ajali ya kupangwa, baada ya kugundulika kuwa gari lililosababisha ajali hiyo aina ya Tata Daewoo lilikuwa limeibiwa mahali na dereva wake kupewa kiwango kikubwa cha dawa za kumpumbaza akili.

Kwa vyovyote mtu au watu waliofanya tukio lile walikuwa watu makini sana katika kazi yao kwa kuwa hawakuwa wameacha alama zozote ambazo zingewawezesha polisi kuwatambua. Tayari mahabusu ya Kituo Kikuu cha Polisi yalikuwa yamejaa washukiwa ambao walihojiwa kwa maneno na vitendo. Wale walioonekana kuwa hawana tatizo waliachiwa, walioonekana kutiliwa shaka, japo kidogo, waliandaliwa mashtaka. Hata hivyo, hakuna hata mtu mmoja ambaye alielekea kujua mengi ambayo yangeweza kuwasaidia katika kesi ile.

* * * * *

Saa sita mchana, Tunu na Bob walikuwa peke yao kwenye sebule kubwa ya kifahari iliyo katika mazingira ya upweke, eneo la Kinyerezi. Muda ule Tom na Dumba walikuwa wametoka kwenda mjini, ambako walikusudia kupeleka taarifa za siri kwa Solomon Zirro, Inspekta Jenerali wa Polisi na kwa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Naibu Kamishna Mamboleo. Pia walikusudia kufikisha salamu kwa Kamishna Omalla, Mkuu wa Kamisheni ya Intelijensia wa Jeshi la Polisi na kwa Mr. Oduya mwenyewe.

Inaendelea...

CC the_legend Norshad bobefu zoefu Pablo PAKAYA Ibney blackstarline Bryece Tater Bigjahman moneytalk marybaby nipo2 ram kisukari Smart911 Madame S carbamazepine Astelia culture gal Prisoner of hope Mine eyes kuku mweus Thad hearly Shunie Tumosa Mine eyes Kudo swahiba92 ludist Toyota escudo Clkey macson3 boga la kiangazi LEGE Smart911 Richard irakunda skfull popie Krizy Beat hearly nipo2 MWINDAJI HARAMU kakhulu Katavi Norami mbududa iron2012 popie Bughy Harry Mlenge Kacheda mjasiliamali Laki Si Pesa cocochanel kinusikwetu big jambo mludego Shupavu Kacheda mjasiliamali Mweweso Songa Heri esiankiki mnadhimu mkuu wa jf red apple the-sniper MR KUO dan oseko Jackal kuku mweus mtugani wa wapi huyo chiqutitta ndukulusudicho ADK aggyd BAHARI J

NB: Litro 👩
 
Taxi - (154)

Taarifa na salamu hizo zilikuwa zimebebwa kwenye nakala kadhaa za CD maalumu zilizorudufiwa na kuhifadhi sauti na video kuhusiana na mauaji ya Jaji Mkuu, Sylvester Lutego. Tom na Dumba walipoondoka, Tunu alimtaka Bob ampeleke Kurasini ili akaonane na Victoria. Hivyo aliingia chumbani akajiandaa kwa ajili ya safari ya kuelekea Kurasini.

Baada ya dakika chache Tunu alitoka chumbani akiwa amebadilisha nguo na sasa alikuwa amevaa suruali ya Jamsuit ya rangi ya bluu iliyolionesha vyema umbo lake refu maridadi lenye minofu ya mapaja iliyokaza kutokana na mazoezi ya kila siku. Miguuni alikuwa amevaa viatu vya mchumumio vye visigino virefu vya rangi nyeusi na kujipulizia manukato ghali mwilini yaliyofanya harufu yake itamalaki sebule yote na kuzifanya pua za Bob zipate uhai mpya.

Muda huo huo wakaisikia sauti ya kengele iliyokuwa imewekwa getini ikiita kwa fujo. Tunu na Bob wakatazamana kwa makini katika namna ya kuulizana “huyo atakuwa nani?” huku wakijitahidi kusikiliza kwa makini. Kengele ile iliendelea kuita kwa fujo.

Mlango wa hisia ya sita katika ubongo wa Tunu ulifunguka, ilikuwa ni hisia iliyomfahamisha kuwa yeyote aliyekuwa pale nje anabonyeza ile kengele hakuwa amefika pale kwa jambo la heri. Tunu alikumbuka katika mafunzo ya ushushushu nchini Israel, maendeleo ya hisia ya sita yalikuwa yanapewa uzito mkubwa kwa wanafunzi wa ushushushu, na kadri yalivyosisitizwa ndivyo ambavyo yalimjenga Tunu kutambua umuhimu wa nyenzo hiyo muhimu.

Kwa mara ya kwanza tangu apate sehemu ya maficho katika eneo lile la Kinyerezi alijikuta akigundua kuwa alikuwa amekosea sana kuwadharau watu wa Mr. Oduya kiasi hicho. Mwanzoni aliamini kuwa wasingeweza kugundua uwepo wake katika nyumba ile. Hata hivyo, hakutaka kumfanya mtu yeyote aliyepo nje ya ile nyumba ahisi kuwa alikuwa amegundulika na watu waliokuwemo mle ndani, hivyo akamtumia Bob jicho ambalo lilibeba ujumbe wote, ujumbe ambao masikioni mwa Bob ulijieleza waziwazi “Kazi kwako, mzee!”

Papo hapo Bob akanyanyuka na kutoka nje kisha akaelekea getini huku akiwa makini sana kama mbwa awindaye. Alipolifikia geti akaufungua mlango mdogo uliokuwa pembeni ya lile geti kubwa. Kama walivyotegemea, aliwaona wanaume wawili warefu wenye miili iliyojengeka wakiwa wamesimama nje ya lile geti, wote walikuwa makini sana. Macho yao tu yalitosha kumfahamisha Bob kuwa wale watu walikuwa wazee wa kazi.

“Samahani sana, bro,” mwanamume mmoja alianza kujieleza mbele ya Bob. “Tumelazimika kukusumbua kidogo. Nadhani utatuwia radhi. Mimi ni mwenyekiti wa mtaa huu na huyu ni mjumbe wa eneo hili, nadhani wewe ndiye mwenye nyumba hii?”

Bob aliwatazama kwa makini na kutaka kucheka, lakini hakuweza kufanya hivyo, kwani alishaelewa wale walikuwa kina nani na kwa nini walikuwa pale. Hata hivyo, aliitikia kwa kubetua kichwa chake huku akiendelea kujifanya mjinga aone nini walitaka kufanya. Wakati huo mkono wake wa kulia aliupeleka kiunoni na kuigusa bastola yake, mwili wake ukasisimka.

“Nyumba hii imeonekana kutokaliwa na mtu tangu ikamilike, hivyo tupo katika ziara ya kutembelea wakazi ambao bado ni wageni katika mtaa wetu huu ili kujua mambo mawili matatu ambayo nadhani utatujibu. Uisijali, ni mzunguko wa kawaida tu kwa wakazi wote wageni ili kufahamiana. Samahani kama tutakuwa tumekusumbua kidogo, kwa kawaida hapa mtaani kwetu hatupendi kusumbua wakazi wetu,” yule mwanamume mwingine alidakia.

“Bila samahani, mnakaribishwa sana,” Bob aliitikia, “Karibuni basi ndani,” akasema na kuwapisha ili waingie kisha aliwaongozana kuelekea sebuleni.

“Sijui mwenzetu unaitwa nani?” mwanaume mmoja alimuuliza Bob wakati wakielekea kwenye mlango wa kuingilia ndani.

“Godwin Tyson,” Bob alijibu mara moja pasipo hata kufikiria.

“Wewe ni mwenyeji wa wapi?”

“Hapa hapa Dar es Salaam.”

“Umeoa?”

“Nina mke na mtoto mmoja,” Bob alijibu huku akiufungua mlango na kuwaruhusu waingine ndani.

“Nao wanaishi hapa hapa?”

“Kumbe ulitaka wakaishi wapi?” Bob aliuliza kwa mshangao huku akimtazama yule mwanamume aliyekuwa akimuuliza maswali, kisha akawapisha wale wanaume waingie ndani.

“Sahamani, bwana mkubwa, kama nimekukwaza kwa maswali yangu, nilimaanisha wapo ndani?”

“Wala usijali, ukihitaji kuwaona utawaona tu,” Bob alijibu huku akianza kushindwa kuzizuia hasira zake.

Walipoingia tu sebuleni Bob aliufungua ule mlango wa ufunguo kisha akauchomoa ule ufunguo na kuuweka mfukoni, wale watu wakashtuka na kugeuka haraka kumtazama kwa mshangao, na hapo wakakutana na mtutu ukiwaelekea, lakini ni kama walikuwa wamejiandaa kwa jambo hilo. Walijigawa na kuruka juu huku wakiachia mapigo ya haraka kumwelekea Bob lakini mapigo yao hayakutimiza wajibu wake ingawa walifanikiwa kuidondosha bastola ya Bob iliyokuwa mkononi huku Bob akifanikiwa kuyakwepa mapigo hayo na kujiweka sawa.

Kabla hawajafanya jambo jingine lolote walishtukia wakimwona Tunu akiibuka toka kusikojulikana na kuruka juu huku akijipindua hewani akiwa ametanua miguu yake na kuutanguliza mguu wake wa kushoto usiokuwa na jeraha, ukifuatiwa na mguu wa kulia. Mwanamume mmoja aliyekuwa karibu na Tunu akafanya jitihada za kujikinga na shambulizi hilo huku akiwa tayari amechomoa bastola yake.

Tunu alikiwa bado hewani aliachia pigo moja matata lililomfanya mwanamume yule na kumfanya apepesuke na kugonga kichwa chake kwenye ukuta. Bastola iliyokuwa mkononi mwake ilimtoka na kuanguka kando. Kabla Tunu hajatua sakafuni akampa pigo jingine la judo ambalo lilitua ubavuni mwake na kumlegeza kabisa. Pigo lililofuata lilimlazimisha yule mwanamume kuanguka sakafuni akiwa hana fahamu.

Wakati hayo yakiendelea yule mwanamume wa pili alijikuta akikabiliwa na Bob aliyeachia pigo maridadi lakini yule mwanamume aliliona na kuinua mkono wake juu kulikinga huku mkono wake wa pili ukijiandaa kubonyeza kitufe cha bastola yake. Bob hakuruhusu mkono huo ufanikiwe kuifyatua ile bastola. Aliruka akampiga kichwa kikavu kilichompa kisurisuri na kufanya ateremke sakafuni bila ubishi na kupoteza kabisa fahamu.

Mpambano unazidi kupamba 🔥🔥🔥. Je, baada ya kufahamika kwa maficho hayo Tunu na Bob watafanikiwa kutoka salama ndani ya nyumba hiyo? Endelea kusafiri nami katika safari hii ya kusisimua ndani ya 🚖🚖 hadi mwisho...

NB: Litro 👩
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom