HEKAHEKA! 1
Na Bishop Hiluka
DAR ES SALAAM, SAA 12:30 JIONI.
SAUTI laini ya mwanadada mrembo mhudumu wa ndege aina ya Airbus A340-600 ya shirika la ndege la Uholanzi la KLM tuliyoiabiri, ilinizindua kutoka usingizini.
Sauti ile ilikuwa ikiwatangazia abiria wote kufunga mikanda ya siti zao tayari kwa kujiandaa na tukio la kutua kwa ndege hiyo katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Kiwanja cha ndege cha Julius Nyerere kipo umbali wa kilomita 12 kusini magharibi mwa jiji hilo la Dar es Salaam ambalo ni jiji kubwa zaidi nchini Tanzania.
Usingizi ukiwa haujaniisha sawasawa niliyafumbua macho yangu taratibu, kisha nikayatembeza taratibu mle ndani ya ndege nikitazama huku na kule, na kwa kufanya vile, nikagundua kuwa abiria wenzangu wote mle ndani ya ndege walikuwa macho na tayari walikwisha funga mikanda ya siti zao tayari kwa tukio lile la kutua kwa ndege.
Niliwatazama haraka haraka na hapo nikajua kuwa ni mimi tu ndiye ambaye nilikuwa nimepitiwa na usingizi wakati yule mwanadada mrembo mhudumu wa ndege ile alipokuwa akitutangazia abiria wote kufunga mikanda kabla ya tukio la kutua kwa ndege.
Tulikuwa tumesafiri tukiwa angani kwa takribani saa nzima tangu ndege yetu iliporuka katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Jomo Kenyatta jijini Nairobi nchini Kenya hadi Dar es Salaam.
Kupitia ukuta msafi ya vioo vya dirisha la ile ndege niliweza kuona sehemu kubwa ya bahari ya Hindi, barabara zote kuu zilizokuwa zinaingia na kutoka katikati ya jiji la Dar es Salaam, makazi ya watu na hata eneo la Mto Msimbazi uliokuwa ukitapisha maji yake katika pwani ya Bahari ya Hindi.
Kiujumla sehemu kubwa ya mandhari ya jiji la Dar es Salaam ilinivutia sana kwa uoto wake wa asili wa kijani kibichi kama ilivyokuwa katika nchi nzima ya Tanzania iliyo na mito mingi yenye maji ya kutosha.
Nilipiga mwayo mrefu wa uchovu huku nikiendelea kustaajabu maendeleo makubwa niliyokuwa nikiyashuhudia katika jiji la Dar es Salaam yaliyofikiwa katika kipindi kifupi tu cha miaka kumi.
“Aisee! Ni bahati iliyoje kurudi tena katika nchi yangu nzuri na tajiri kama hii, I real love my country,” (Naipenda nchi yangu) nikanong’ona nikiiambia nafsi yangu mwenyewe.
Usingizi wa takribani saa nzima safarini, tangu tuliporuka kutoka kiwanja cha ndege cha Jomo Kenyatta jijini Nairobi hadi Dar es Salaam, ulikuwa umenipunguzia kwa kiasi kikubwa uchovu wa safari ndefu ya kutoka katika jiji la Amsterdam nchini Netherland (au huitwa Uholanzi) nilikokuwa nikiishi.
Wakati ndege yetu ikizunguka angani kutafuta uelekeo mzuri wa kutua, nikatumia nafasi ile kutazama nje, kupitia ukuta msafi wa vioo vya dirisha nikayaona machweajua yakiwa yamepaka rangi ya damu huku jua lenye kutua likijificha nyuma ya wingu, ati kutughilibu tusilione wakati linaingia upande wa pili wa dunia.
Kisha niliyahamisha macho yangu kutoka kule na kuyaangalia mandhari ya kupendeza ya eneo lililozunguka kiwanja cha ndege cha Julius Nyerere kupitia ukuta msafi wa vioo vya dirisha pale nilipokuwa nimeketi.
Nilitazama nje nikiyastaajabia mandhari ya kupendeza ya eneo lile la uwanja wa ndege, nikajiuliza kama ni kweli kile kilikuwa ni kiwanja cha ndege cha Julius Nyerere cha jijini Dar es Salaam au labda rubani alikosea, kwani nilichokuwa nakishuhudia ilikuwa ni kiwanja kikubwa, kizuri na chenye majengo ya kisasa.
Kudhihirisha mshangao wangu, niliivua miwani yangu myeusi mikubwa niliyokuwa nimeivaa muda wote wa safari yangu ikifunika macho yangu, na hapo nikaangalia vizuri kule nje.
Hapo ndipo nilipoyaona vizuri zaidi mandhari ya kupendeza ya uwanja ule yaliyonivutia kwa mpangilio wake mzuri wa majengo, hasa lile jengo kubwa lililokuwa bado jipya la kituo nambari tatu cha uwanja wa ndege, maarufu kama ‘terminal 3’.
Jengo lile la kituo nambari tatu lilikuwa kubwa na refu zaidi kuliko yale majengo mengine ya vituo nambari moja na nambari mbili, na lilikuwa lina migahawa na maduka ya kisasa, na ofisi mbalimbali za utawala zikiwemo ofisi za uhamiaji za nchi ya Tanzania kwa ajili ya wageni waliokuwa wakifika nchini kupitia ule uwanja wa ndege.
Nikakumbuka kuwa nilisoma kwenye mtandao wa intaneti mara kadhaa kuwa lile jengo lilikuwa na uwezo wa kuruhusu ndege kubwa 24 kwa wakati mmoja na abiria milioni 6 kwa mwaka, pale nilipokuwa natafuta habari kuhusu maendeleo ya nchi yangu, na nilipokuwa najiandaa kuja Dar es Salaam.
Niliachia yowe dogo la mshangao nikizidi kuajabia maendeleo yale ya haraka yaliyofikiwa, kwani nilipokuwa naondoka nchini miaka kumi na mbili iliyopita kwenda Ulaya hali ya ule uwanja haikuwa kama nilivyokuwa nikiishuhudia sasa.
Niliporidhika kuyatazama mandhari ya eneo lile nikageuza shingo yangu kuwatazama abiria wenzangu wawili waliokuwa wameketi kwa utulivu jirani yangu na macho yangu yakaangukia kwenye uso wa abiria mwanamke aliyekuwa ameketi pembeni yangu kwenye siti ya katikati.
Mara tu macho yetu yalipogongana, tukajikuta wote wawili tukiachia tabasamu bashasha.
Abiria yule alikuwa ni mwanadada chotara aliyekuwa mchanganyiko wa Mswahili na mzungu, nadhani kutoka Ulaya mashariki, kama si Mgiriki basi Mturuki. Kwa mwonekano wa haraka tu niliweza kugundua kuwa alikuwa na umri wa miaka kati ya therathini na therathini na mbili.
Mwanadada yule alikuwa ameketi na mtoto mmoja wa kike aliyeonekana kuwa na miaka mitatu. Wakati huo yule mtoto alikuwa amepitiwa na usingizi huku akiwa amezuiliwa vyema na mkanda wa siti ya ndege ile.
Kwa uzoefu wangu kwa wadada warembo, haraka niliweza kugundua kuwa abiria yule alikuwa na umbo la kuvutia la kimiss, mwenye weupe wa asili na hakuwa mwanamke wa kumtizama mara moja tu ukamwacha.
Mwonekano wake ulinitanabaisha kuwa alikuwa mrefu kiasi na mwenye haiba ya kuvutia sana, alikuwa na mashavu mfano wa chungwa na nywele zake zilikuwa ndefu zilizokuwa nyeusi tii za kichotara ambazo alikuwa amezisuka mtindo wa mkia wa pweza.
Niliweza kuziona vyema nywele zake zilizokuwa zimeangukia mgongoni kwani alikuwa amezifunika kwa mtandio mwepesi wa rangi ya njano uliozifanya zionekane vyema.
Nyusi zake alikuwa amezitinda vizuri na kuzipaka wanja, na kope zake zilikuwa zimerembwa vyema na hivyo kuyafanya macho yake makubwa kidogo na legevu yenye kung’ara kama nuru yaonekane vizuri na kupendeza.
Alivaa gauni fupi jepesi la rangi ya pinki lililohifadhi vyema umbile lake na ndani ya lile gauni alikuwa amevaa suruali ya jeans ya bluu.
Miguuni alikuwa amevaa sendozi ngumu za kike zilizotengenezwa kwa ngozi imara ya mamba.
Nilipomtazama kwa makini nikagundua kuwa sikuwa nimemchanganyia macho vizuri kabla ya hapo, japo tulikuwa tumeketi katika siti zilizokuwa jirani, na tulisafiri pamoja muda wote tangu ndege yetu iliporuka kutoka katika kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Jomo Kenyatta, jijini Nairobi ambako ndiko alikokuwa amepandia.
Itaendelea...