Dr.slaa kila anapoenda akiulizwa kipaumbele cha kwanza cha CHADEMA anasema ni elimu.Kipaumbele hiki mwanzilishi wake ni mwana CCM Edward Lowasa ambaye wimbo wake ulikuwa elimu kwanza na alianza kuimba kabla Slaa hajaanza.Hata iliposemwa kilimo kwanza Lowasa alisema Elimu kwanza .
CHADEMA walikuwa hawana kipaumbele wamepora kipaumbele cha elimu kwanza toka kwa mwana-CCM lowasa bila hata kumnukuu.CHADEMA mfilisi wa sera hata hiyo ya elimu kwanza wizi mtupu wamemwibia LOWASA.
SURA YA PILI
2. FURSA KWA KILA MTOTO WA KITANZANIA KUPATA ELIMU BORA
2.1 Utangulizi
CHADEMA inaamini kuwa elimu ndio nguzo kuu ya maendeleo na nyenzo ya haraka na ya uhakika zaidi ya kujenga taifa la kisasa. Wananchi wasio na elimu au wenye elimu hafifu hawawezi kupata fursa za kumiliki na kuendesha uchumi, hawawezi kuiwajibisha serikali yao na hawawezi kuwajibika. Kwa hivyo kutoa fursa katika kupata elimu bora ni hatua ya kwanza na ya msingi katika kujenga taifa linalojitegemea na lenye uchumi imara na maendeleo endelevu.
2.2 Hali halisi kuhusu elimu hapa nchini
2.2.1 Kuna matatizo mawili ya msingi kuhusu elimu hapa nchini. Tatizo la kwanza ni uduni wa elimu inayotolewa katika shule zetu, na hasa shule za umma. Ukiwauliza CCM kuhusu elimu wanakujibu kuwa Taifa limepiga hatua kubwa ya upanuzi wa fursa za elimu hapa nchini, hasa elimu ya sekondari kufuatia kuanzishwa kwa Mpango wa Elimu ya Sekondari (MES). Hii ni kweli kwa upande mmoja. Mfano mzuri ni kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaojiunga na shule za sekondari, hasa za kata, kutoka wanafunzi 345,441 mwaka 2003 hadi kufikia wanafunzi 1,466,402 mwaka 2009.
2.2.2 Hata hivyo, Serikali ya CCM iliahidi kupitia Mpango wa Elimu ya Sekondari (MES) kuongeza kiwango cha kufaulu katika madaraja ya I, II na III toka asilimia 37.8 mwaka 2004 hadi kufikia asilimia 70 mwaka 2009. Lakini, pamoja na kwamba Serikali ya CCM kwa msaada wa mashirika ya kimataifa imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 200 chini ya Mpango wa Elimu ya Sekondari, kiwango cha kufaulu katika madaraja haya kimeshuka. Kwa mfano, kwa mujibu wa takwimu za Baraza la Mitihani la Taifa na Kijitabu cha Takwimu cha Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, idadi ya wanafunzi wanaofaulu katika madaraja ya I, II na III kimeshuka kutoka asilimia 37.8 mwaka 2004 hadi asilimia 17.8 tu mwaka 2009. Aidha, idadi ya wanafunzi wanaofeli kwa kupata Daraja la 0 (Division 0) imeongezeka kutoka asilimia 8.5 mwaka 2004 hadi kufikia asilimia 27.49 mwaka 2009. Asilimia 54.66 ya watahiniwa wote wa Kidato cha Nne mwaka 2007 walifaulu kwa kiwango cha Daraja la IV, ambalo kimsingi ni sawa na kufeli.
2.2.3 Chanzo kikubwa cha tatizo la uduni wa elimu yetu ni sera mbovu za elimu na uongozi legelege katika Wizara ya Elimu na Serikali ya CCM kwa ujumla. Sera za CCM kuhusu elimu ni bora elimu; kwao wingi wa mashule ndio elimu yenyewe bila kujali wanachokipata wahitimu wa mashule hiyo. Kwa miaka nenda wameendelea kutuhubiria juu ya kuboresha elimu huku wakitekeleza sera ya kubabaisha elimu Serikali ya CHADEMA itatilia mkazo elimu bora na hiki ndicho kitakachokuwa kipaumbele cha kwanza katika sera ya elimu.
2.2.4 Tatizo la pili la msingi linahusu mfumo wa elimu hapa nchini. Mfumo wetu wa elimu haumfanyi mhitimu aweze kujitegemea. Ni mfumo unaotaalumisha bila kutalaamisha. Hii inafanya vijana wanaohitimu masomo yao wasiweze kujitegemea kikamilifu nje ya mfumo rasmi wa ajira.
2.2.5 Pamoja na matatizo haya ya msingi, kuna matatizo sita mahususi katika elimu yetu ambayo CHADEMA itakabiliana nayo mara baada ya kuunda serikali.
i. Matabaka katika elimu na kutelekezwa kwa shule za umma
Serikali ya CCM imezitekeleza shule za umma. Shule nyingi za serikali zimechakaa kimajengo, hazina madawati, vitabu, maabara na vifaa muhimu vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia. Watoto wanaosoma katika shule za serikali wanasoma katika mazingira magumu sana. Kwenye shule kadha wa kadha za bweni na za kutwa lishe bado ni tatizo na ni duni. Matokeo yake wazazi wenye uwezo wanalazimika kuwapeleka watoto wao katika shule za binafsi, ambazo ni chache na ghali. Matokeo yake tumetengeneza ubaguzi katika mfumo wa elimu kati ya shule binafsi na za serikali. Hali hii ni hatari kwa mustakabali wa taifa kwa muda mrefu ujao.
ii. Kudhalilishwa kwa taaluma ya ualimu kiujira na kitaaluma: Walimu wa shule za serikali wametelekezwa kwa kulipwa mishara midogo na wanafanya kazi katika mazingira magumu na ya kudhalilishwa. Matokeo yake, walimu walio wengi wamekata tamaa, na wakipata mwanya wa kazi nyingine huacha ualimu mara moja. Bado walimu ndio viongozi wa awali kabisa ambao watoto wetu wanakutana nao katika makuzi yao na ni kutoka kwao ndio wanajifunza tunu mbalimbali za maisha. Kutotengeneza mazingira na mfumo mzuri wenye kujali maisha na kazi ya ualimu ni kuweka msingi mbaya kwa wanafunzi wao kujifunza kutoka kwao na kuwaiga.
iii. Watoto wa kitanzania kutojengewa msingi mzuri wa lugha ya taifa na za kimataifa hasa Kiingereza. Katika ukanda wa Afrika Mashariki (EAC) na Kusini mwa Afrika (SADC), ni watoto wa kitanzania pekee wasiofundishwa lugha ya kiingereza kwa ufasaha. Matokeo yake, ili mtoto ajifunze lugha kama ya Kiingereza vizuri ni lazima apelekwe kwenye shule binafsi za international. Wale wasio na nafasi hizo wanajikuta katika hali ngumu ya kujifunza katika ngazi za juu za elimu ambazo zinahitaji ufasaha mkubwa wa lugha ya Kiingereza kuweza kuelewa na kujieleza. Kumudu lugha hii si kwa ajili ya ajira tu bali kwa ajili ya kujenga uwezo wao kuhusiana na kushirikiana katika ngazi mbalimbali za maisha na watu wengine ambao lugha inayowaunganisha ni ya Kiingereza au Kifaransa.
iv. Utoro na Watoto wa kike kuacha shule kwa sababu ya mimba Moja ya tatizo linaloikabili elimu yetu ni utoro wa wanafunzi. Takwimu za elimu zinaonyesha kuwa utoro wa wanafunzi wa shule za msingi umefikia kiwango cha asilimia 35.5, na baadhi ya mikoa na wilaya hadi asilimia 56.7. Takwimu zinaonyesha pia kwamba mimba za utotoni ni moja ya sababu kubwa za watoto wa kike kuacha shule, ambapo asilimia zaidi ya 15 ya watoto wote walioacha shule mwaka 2009 ilisababishwa na mimba za utotoni.
Kinachoshangaza zaidi ni kwamba Rais Kikwete, badala ya kuja na suluhu ya tatizo, anawalaumu watoto wanaopata mimba kwa kuwaambia kuwa wanapata mimba kwa sababu ya kiherehere chao (Nipashe, Jumatatu, 07 Juni 2010). Tunahitaji ufumbuzi wa haraka na wa kudumu wa tatizo la watoto wetu wa kike kuacha shuke kwa sababu ya mimba.
Serikali ya CHADEMA itaweka utaratibu ili kuhakikisha kuwa wanafunzi ambao wanajikuta wanalazimika kukatisha masomo kwa sababu ya ujauzito wanaruhusiwa kuendelea na masomo mara baada ya kujifungua bila kulazimika kuhama maeneo yao kwa sababu ya unyanyapaa. Tanzania imepoteza mabinti wengi walioachishwa shule kwa sababu ya ujauzito ambao kama wangepata nafasi ya kuendelea na shule wangeweza kutoa mchango kwa taifa
Pamoja na hilo, Serikali ya CHADEMA itahakikisha kuwa wale wote wanaowapatia wanafunzi mimba wanawajibishwa kisheria pamoja na kulazimishwa kulipia gharama yote ya kukatisha masomo na malezi ya mtoto hadi mtoto afikapo miaka 18. Na wale ambao wanafanya vitendo hivyo kwa mabinti wa chini ya miaka 18 watashtakiwa kwa mujibu wa sheria kwa makosa ya ubakaji (statutory rape).
v. Kufifishwa kwa shule za kitaifa Serikali ya CCM imeondoa shule za kitaifa ambazo zilikuwa ni muhimu katika kujenga moyo wa utaifa miongoni mwa vijana na wananchi kwa ujumla kwa kuwapokea wanafunzi kutoka sehemu kila pembe ya nchi. Matokeo yake kuna watoto wanaoanza shule katika kata na wilaya moja kuanzia shule ya awali hadi kidato cha sita na kuna baadhi wana hatari ya kusoma hadi chuo kikuu katika wilaya moja. Hii si hali nzuri kitaifa kwa sababu inawafanya vijana wawe na mawazo finyu na kutokutambua hali halisi ya nchi yao, na hivyo hubomoa mshikamano wa kitaifa.
vi. Mfumo usio wa uhakika wa kugharamia elimu ya juu. Serikali ya CCM imeshindwa kubuni njia endelevu za kugharamia elimu, na hasa elimu ya juu. Kukosekana kwa njia za uhakika za kugharamia elimu ya juu kumesabisha matatizo mengi katika sekta ya elimu ya juu ikiwemo:
o Vyuo vikuu na taasisi nyingine za elimu ya juu kukabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha kunakopelekea vishindwe kutimiza majukumu yao ya msingi kikamilifu. Kwa mfano, katika mwaka wa fedha wa 2009/2010, baadhi ya vyuo vikuu vilipata asilimia 30 tu ya bajeti ilivyopangiwa.
o Kushindwa kwa Serikali ya CCM kugharamia tafiti zinazofanywa katika vyuo vyetu, na tafiti chache zinazofanywa zinagharamiwa na wafadhili wa nje. Ni wazi kuwa tafiti za namna hii haziwezi kuwa na ajenda endelevu ya kujibu matatizo ya nchi kwani wanaofadhili tafiti wana ajenda zao ambazo wangependa zitimizwe
o Kushindwa kuwa na mfumo endelevu wa kufadhili au kuwapa mikopo wanafunzi katika vyuo vikuu. Mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu inatolewa kimatabaka, kwa usumbufu mkubwa, na mara nyingine wanapata wasiotahiki na wanaostahiki hawapati.
o Vyuo vikuu kupoteza uhuru kamili wa kufanya kazi za kitaaluma na kitaalamu kunakosababishwa na kuingiliwa na wanasiasa. Imefika mahala hata ajira za vyuo vikuu sasa hivi zinaamuliwa na wanasiasa badala ya mabaraza ya vyuo hivyo kwa kuzingatia sifa zao za kitaalma na kimaadili.
o Kasi ndogo ya maendeleo katika sekta ya sayansi na teknolojia kunakosababishwa na uwekezaji mdogo katika sekta hii na kutowajali wana sayansi kimaslahi, hasa walio katika sekta ya umma.
2.3 CHADEMA itafanya nini?
CHADEMA inaamini kuwa kuwekeza katika elimu ndio nyenzo kuu ya kukabiliana na matatizo yote yanayoikabili nchi yetu, ikiwemo umaskini. Tukifanikiwa kuwa na elimu bora tutakuwa tumejipatia silaha muhimu ya kukabiliana na maadui ujinga na maradhi na nyenzo muhimu ya kukuza uchumi imara na shirikishi. Hivyo basi, Serikali ya CHADEMA itatilia mkazo sana ubora wa elimu badala ya bora elimu.
Katika kuinua ubora wa elimu CHADEMA inaamini kuwa Elimu bora ni walimu bora. Hivyo basi, CHADEMA itaweka mkazo katika kuwapatia walimu mafunzo bora na ujira stahiki ili waweze kuwa na maarifa ya kutosha na kutulia mashuleni. Tutaweka mkazo katika kuwapatia watoto wa shule kiwango cha juu katika elimu kuanzia chekechea hadi chuo kikuu. Mkazo utawekwa katika kuhakikisha kuwa shule na taasisi zote za elimu zinatoa elimu inayochochea fikra, udadisi, maarifa na ugunduzi na inayoibua vipaji. Lengo ni kuhakikisha kuwa kila hatua ya kielimu inamuwezesha mhitimu kujitegemea na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya nchi na jamii aliyomo.
Katika kutekeleza haya, serikali ya CHADEMA itachukua hatua zifuatazo:
2.3.1 Kuhusu Elimu ya Msingi na Sekondari
Lengo la Serikali ya CHADEMA ni kubadili mfumo wa elimu ya msingi ili iweze kujitoshekeza kwa kuhakikisha kuwa wahitimu wanapata maarifa na stadi za maisha zitakazowawezesha kujitegemea kimaisha. Ili kufikia adhima hii, tutafanya mabadiliko yafuatayo:
o Muda wa elimu ya msingi utaongezwa kutoka miaka saba (7) hadi miaka kumi. Hii inamaanisha kuwa watoto watamaliza shule wakiwa na umri wa miaka 16/17, umri unaomwezesha kuanza maisha ya kazi kwa mujibu wa sheria za nchi na kimataifa
o Mtaala wa elimu ya msingi utapanuliwa kwa kuingiza muhtasari wa kidato cha kwanza na cha pili cha sasa kuwa sehemu ya elimu ya msingi
Elimu ya Sekondari itabadilishwa kutoka miaka sita (6) hadi minne (4) kwa kuunganisha mihtasari ya kidato cha tatu,nne, tano na sita kuwa muhtasari mmoja wa elimu ya sekondari. Hii itasaidia sana kuongeza idadi ya wanafunzi wanaopata sifa za kujiunga na elimu ya sekondari.
Kuimarisha shule za umma ili zitoe elimu bora. Hili litafanywa kwa kuanzisha kampeni ya kujenga upya, kukarabati na kuzipatia shule zote nchini huduma muhimu za jamii hasa maji safi na umeme.
Kuhakikisha kuwa ndani ya miaka mitano ya utawala wa Serikali ya CHADEMA kila mtoto mwenye umri kati ya miaka 4 na 5 anahudhuria elimu ya awali kabla ya kuanza elimu ya msingi. Hii ni hatua muhimu kwa kuwa tafiti zinaonyesha kuwa watoto waliohudhuria elimu ya awali huanza shule ya msingi wakiwa na msingi bora zaidi kuliko wale ambao hawakupitia elimu hiyo.
Kuimarisha ufundishaji wa Lugha ya Kiingereza. Hili litafanywa kwa kuboresha mazingira mazuri ya kujifunzia lugha ya Kiingereza, ikiwemo kuzipatia shule walimu wenye ujuzi wa kufundisha lugha ya Kiingereza. Lengo likiwa ni kuhakikisha mwanafunzi anapoingia kidato cha pili anafahamu lugha ya kiingereza katika kuelewa, kuandika, kusema na kujieleza.
Kuimarisha ufundishwaji wa lugha ya Kiswahili. Pamoja na mkazo wa lugha ya Kiingereza, Serikali ya CHADEMA itaweka msisitizo wa pekee wa kuifahamu lugha ya Kiswahili pamoja na Kiingereza. Wanafunzi wa kitanzania ni lazima waimudu lugha yao ya taifa bila kujiona duni na wakati huo huo wakijiimarisha katika lugha ya Kiingereza.
Kuimarisha ufundishaji wa Sayansi na Hisabati kwa kuandaa walimu wa masomo hayo kwa uhakika, kujenga maabara za masomo hayo zenye vifaa vyote vya msingi pamoja na kemikali vinavyohitajika. Kwa upande wa somo la elimu viumbe, shule zitaweka utaratibu wa kufuga wanyama wadogo wadogo na kutunza mimea ya aina mbalimbali kwa ajili ya kufundishia. Ufundishaji wa Hisabati utaboreshwa ili uendane na misingi yake ambayo inazingatia sayansi ya kimantiki inayojengeka hatua kwa hatua ili kuondokana na tatizo la kukaririshwa, na hivyo kuinua kiwango cha kufaulu katika somo hili.
Kuinua ujira wa walimu kwa kuangalia upya viwango vyao vya mishahara na kuimarisha mazingira ya kazi na kimakazi. Katika kuboresha mishahara ya walimu, na wafanyakazi wengine wote katika sekta ya umma, tutaweka fomula ya kupandisha mishahara kwa kadri mfumuko wa bei na gharama za maisha zinavyopanda kwa kutumia mpango wa Scala Mobile, ambayo ndio inayotumika katika nchi nyingi duniani. Hii ndio kusema kila mara ambapo mfumuko wa bei utapanda na hivyo gharama za maisha kupanda, mshahara nao utapanda. Hii ni hatua muhimu katika kuhakikisha kuwa wafanyakazi wanamudu gharama za maisha ya kawaida ili waweze kuwekeza muda na utaalamu wao katika kulitumikia taifa. Utaratibu huu pia utaondoa umuhimu wa migongano baina ya Serikali na vyama vya wafanyakazi.
Sambamba na kuboresha mishahara ya wafanyakazi kwa ujumla, Serikali ya CHADEMA itarudisha posho ya mazingira magumu kwa walimu wanaofundisha maeneo magumu ya vijijini hasa katika mikoa inayotambulika kuwa ni ya pembezoni.
Kupitia upya mfumo na mtaala wa elimu ili:
o Kuhakikisha kuwa, pamoja na taaluma, wahitimu wanapata utaalamu na stadi sahihi za kujitegemea. Serikali ya CHADEMA itabadili kabisa mfumo wa sasa wa elimu ili kutoa fursa kwa vijana walio wengi wapate utaalamu na stadi za kujitegemea mapema.
o Kuhimiza ufundishwaji wa stadi za maisha na TEKINOHAMA kwa kuhakikisha kuwa matumizi ya teknolojia ya kisasa yanaanza mapema kwa wanafunzi wetu ili kuweza kuwaleta katika kiwango cha kimataifa cha elimu na ujuzi mapema inavyowezekana.
Kuingiza katika mitaala elimu ya uzazi na mahusiano kuwiana na umri wa wanafunzi. Ufundishwaji wa somo hili litawapatia vijana wa kike stadi za kuweza kujikinga na tatizo la kuanza ngono katika umri mdogo. Nchi nyingi zilizofanikiwa kupunguza au kumaliza tatizo la mimba utotoni ni zile zinazozingatia utolewaji wa elimu ya uzazi na mahusiano mashuleni. Elimu hii itazingatia uelewa wa kisayansi kuhusu maisha ya watu, lakini vile vile utazingatia umuhimu wa kulinda familia na maamuzi ya wazazi juu ya watoto wao kwa kuhakikisha elimu inayotolewa ni ile yenye kuzingatia heshima, kujiamini na kujilinda katika mahusiano ya kijinsia.
Elimu ya ngazi ya msingi na sekondari itagharamiwa na serikali kuu pamoja na serikali za mitaa. Lengo ni kuhakikisha kuwa elimu hii ya msingi kabisa inakuwa ni haki kwa kila mtoto wa Kitanzania na kiwango cha ubora kinalingana kwa nchi nzima.
Ili kukabiliana na wimbi la utoro na usinziaji darasani kwa sababu ya njaa miongoni mwa watoto wa shule, Serikali ya CHADEMA itarudisha utaratibu wa kutoa chakula cha mchana mashuleni, ambayo kitagharamiwa na serikali za halmashauri za miji na
wilaya pamoja na serikali za mitaa na vijiji, kwani mtoto mwenye njaa au asiye na uhakika wa lishe hawezi kuzingatia elimu.
Tutazihuisha na kuanzisha shule mpya za kitaifa za bweni za sekondari. Shule hizi zitachukua wanafunzi wote waliofanya vizuri zaidi katika mitihani yao ya mwisho ya elimu ya msingi. Katika kila mkoa kutakuwa na angalau shule moja ya kitaifa itakayochukua wanafunzi kutoka katika mikoa mingine kwa lengo la kujenga utaifa na uzalendo miongoni mwa wanafunzi, na CHADEMA itarejesha utaratibu wa usafiri wa Warrant kwa wanafunzi hao ili kuondoa makali ya gharama za nauli kwa wazazi. Ni wazi kuwa utaratibu huu ni ghali, lakini kuua utaifa ni ghali zaidi!
2.3.2 Kuhusu Elimu ya Juu na Vyuo Vikuu
CHADEMA kina lengo la kubadilisha na kuboresha sekta ya elimu ya juu ili iweze kuwa ya kisasa zaidi na inayomuandaa msomi wa Tanzania kushiriki katika kutumia elimu yake kuiletea maendeleo Tanzania na vile vile kumpa nyenzo za kisasa za kielimu kuweza kumuandaa na maisha ya ulimwengu wa kisasa. Lengo ni kuhakikisha kuwa elimu ya juu inapatikana kwa kila kijana wa Kitanzania anayetaka elimu hiyo, ni ya kisasa, na inamuandaa msomi kurudisha katika jamii ujuzi alioupata chuoni.
Katika kupanua wigo na kuboresha elimu ya juu, Serikali ya CHADEMA itachukua hatua zifuatazo:
Serikali ya CHADEMA itaanzisha mfuko wa elimu uitwao Uhuru Scholarship Fund kwa ajili ya kugharamia masomo katika chuo kikuu cha umma kwa wanafunzi wanaofaulu katika kiwango cha Daraja la I na II. Huu hautakuwa mkopo kwa kijana yeyote ila atalipiwa Chuo kwa kadiri ya kwamba anaendelea kufikia viwango vya juu vya kitaaluma kwa mujibu wa taratibu kwa muda wote atakaokuwa chuoni.
Kwa wanafunzi ambao watafaulu madaraja mengine (daraja la tatu na la nne) mfumo mpya wa kugharimia elimu ya juu utawekwa ili kuhakikisha kuwa gharama ya elimu ya juu haiwi kizuizi kwa kijana yeyote anayetaka elimu ya Chuo Kikuu. Katika
kutimiza adhima hii, Serikali ya CHADEMA itahakikisha kila mkoa unaanzisha mifuko ya elimu ya Juu kwa ajili ya vijana wake, taasisi za dini na watu binafsi watawekewa utaratibu wa kisheria ili waweze kuanzisha mifuko ya elimu hasa inayotoa fedha zisizo mikopo (grants) kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kwa kuzingatia vigezo mbalimbali.
Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu itavunjwa kutokana na uendeshaji mbovu, mfumo wake mbovu wa kisheria, na uongozi ambao umeshindwa kufanya elimu ya juu ipatikane kwa kila kijana na ambayo kutokana na uongozi usiofaa imeshindwa kukusanya madeni toka kwa wakopaji. Uchunguzi huru utafanyika wa fedha zote zilizotumika hadi hivi sasa na kuangalia kama waliopewa dhamana hawakutumia nafasi zao kujinufaisha. Miezi sita baada ya uchunguzi kufanyika ripoti itawekwa hadharani na mapendekezo yake kuanza kufanyiwa kazi mara moja.
Serikali ya CHADEMA itaunda chombo kipya cha utoaji na usimamizi wa mikopo ya elimu ya juu ambacho kitajulikana kama Mamlaka ya Taifa ya Kugharimia Elimu ya Juu (Tanzanian Higher Education Financing Authority - TAHEFA). Hiki ndicho kitakuwa ni chombo cha kifedha ambacho kitachukua majukumu yote ya Bodi ya Mikopo ya sasa chini ya muundo mpya na sheria mpya itakayoweka utaratibu mpya na wa kisasa kutoa mikopo ya elimu ya juu na kuhakikisha hakuna kijana wa Kitanzania anayetaka elimu ya juu ambaye ataikosa.
Vyuo vikuu vitapewa fursa ya kujiendesha, kuanzia utawala hadi kitaaluma bila kuingiliwa na serikali. Vyuo vikuu vitakuwa na fursa kamili ya kuchagua viongozi wao bila kuingiliwa na serikali. Kazi kuu ya serikali itakuwa ni kutunga sera za jumla za kuendeleza na kulinda ubora wa elimu ya juu, kuhakikisha rasilimali muhimu zinapatikana lakini uendeshaji wa vyuo vikuu utaachwa mikononi mwa mabaraza ya vyuo vikuu.
Serikali ya CHADEMA itarejesha na kuruhusu uwepo wa siasa katika vyuo vikuu vyote nchini kama shughuli ambazo ni nje ya masomo. Hii itasaidia kujenga uwanja wa demokrasia katika serikali za vyuo na vile vile itasaidia katika kuweka mazingira
ambapo wasomi wetu wanaanza kujifunza mbinu na utendaji wa kisiasa katika mazingira ya elimu ili waweze kujifunza kuishi pamoja, kupingana kwa hoja na kujua jinsi ya kuvumiliana katika mazingira ya tofauti mbalimbali za kiitikadi, imani, na mtazamo. Uamuzi wa kufanya hivi utachukuliwa ndani ya siku mia moja za kwanza za utawala wa serikali ya CHADEMA. Utawekwa utaratibu mzuri ili shughuli za kisiasa zisiingiliane na zile za kitaaluma.
Ili kuchochea ubunifu na kuviweka vyuo vyetu vikuu katika Nyanja za kimataifa, Serikali ya CHADEMA itaanzisha Baraza la Taifa la Utafiti (National Research Council) ambalo pamoja na jukumu lake la kuratibu na kusimamia tafiti mbalimbali za kisayansi na teknolojia, kazi yake mojawapo itakuwa ni kutoa fedha kwa vyuo vikuu kwa njia ya kuvipatia uwezo vyuo hivyo kufanya tafiti mbalimbali ambazo matokeo yake yanakoleza matumizi ya sayansi na teknolojia nchini. Vile vile baraza hilo litasimamia mashindano ya changamoto za kisayansi ili kuchochea utafiti na ubunifu. Kila mwaka zawadi nono ya fedha taslimu itatolewa kwa Chuo Kikuu na wabunifu mbalimbali wa vitu ambavyo havijabuniwa sehemu nyingine duniani. Uundwaji wa baraza hili utaenda sambamba na uunganishwaji wa baadhi ya taasisi mbalimbali za utafiti nchini chini ya baraza hili moja huku zikiendelea kuwa huru kiutendaji, lakini zikiweza kushirikiana na kutegemeana katika kufanya utafiti na kusimamia matumizi ya tafiti hizo.
Ili kuchochea kasi ya ukuaji wa sayansi na teknolojia, Serikali ya CHADEMA itabadilisha vyuo viwili vya sasa ili viwe viwe vyuo vikuu vya Teknolojia. Vyuo hivyo ni Mbeya Instute of Science and Techonology ili kiwe Mbeya University of Science and Technology MUST pamoja na Chuo cha Ufundi Tanga kuwa Chuo Kikuu Kishiri cha MUST.
Pamoja na kutoa elimu ya Chuo Kikuu na Shahada, Serikali ya CHADEMA itaanzisha utaratibu wa kuwa na Vyuo Vya Kati vya Jumuiya ambavyo vitatoa elimu sawa na inayotolewa katika miaka miwili ya kwanza ya Chuo Kikuu. Lengo ni kuanza kutengeneza kundi la wasomi wa elimu ya kati ambao kutokana na sababu mbalimbali wasingeweza kupata elimu kamili ya chuo Kikuu. Vyuo hivi vya Jumuiya
(Community Colleges) vitakuwa ni kiunganisha kati ya elimu ya Sekondari na Elimu ya Vyuo Vikuu na vitakuwa na uwezo wa kutoa Shahada Shirikishi (Associate Degrees). Mwanafunzi anayemaliza vyuo hivyo akitaka baadaye anaweza kuendelea na Elimu ya Chuo Kikuu katika taaluma yake kwa kuendeleza pale alipoachia na siyo kuanza kama mwanafunzi wa mwaka wa kwanza. Baadhi ya vyuo mbalimbali vya jamii vilivyopo sasa vitapandishwa ngazi na kuwa Vyuo Vikuu vya Jumuiya.
Serikali ya CHADEMA itafufua Huduma ya Maktaba kwa kuhakikisha kuwa kila Halmashauri ya Mji inakuwa na mfumo wa Huduma ya Maktaba. Maktaba hizi zitatakiwa kuwa ziwe kwenye bajeti zote za kwanza za Serikali ya CHADEMA na ufikapo mwaka wa pili asilimia 50 ya Halmashauri zote nchini ziwe zimekamilisha ujenzi wa Maktaba za kisasa. Utakapofika mwisho wa ngwe ya kwanza ya serikali ya CHADEMA, asilimia 100 ya Halmashauri zote ziwe na mtandao wa Huduma za kisasa za Maktaba. Viongozi wa kisiasa na jamii watahimizwa kuonesha mfano wa kupenda kujisomea ili kuchochea moyo wa kujisomea kwa vijana na watoto wetu. Ili kuonesha mfano na umuhimu wa kujisomea Rais Dr. Slaa atakuwa na utaratibu wa kusoma na watoto wetu katika mojawapo ya maktaba nchini mara kwa mara.
Ili kurudisha mori wa utumishi miongoni mwa wahadhiri wa vyuo vikuu, Serikali ya CHADEMA itahakikisha kuwa katika bajeti yake ya kwanza, madeni yote ya wanataaluma ya posho ya pango kwa wanaostahili yanalipwa na mpango wa kuboresha mafao ya uzeeni unatekelezwa kikamilifu. Tunataka wasomi wetu wasiwe na hofu ya maisha ya kila siku na wajikite kweli katika kutoa elimu, utafiti na ushauri wa kitaalam.
Ili kuendelea kutumia utaalamu na uzoefu wa maprofesa hapa nchini katika kuwanoa vijana wetu vyuo vikuu, Serikali ya CHADEMA itajadiliana na wanataaluma pamoja na Mabaraza ya Chuo na Senate zao kuona uwezekano wa kuongeza umri wa kustaafu kwa maprofesa kamili kutoka miaka 60 70, maadamu chuo husika kitakuwa kimejiridhisha kuwa maprofesa husika bado ni wataaluma kikamilifu.