SIYO Jukumu la CHADEMA kuikosoa CCM ili ijisahihishe na kutawala Vizuri

CCM wanajua fika kwamba kinachowabakisha madarakani ni mfumo wa ovyo wa kisiasa na sio utashi wa wananchi. Katika hali ya kawaida, na kwa kuzingatia kwamba wana namba bungeni, watahakikisha katiba yeyote ijayo haiharibu mazingira yao kisiasa. Mimi binafsi nipo cynical and skeptical na zoezi zima la katiba mpya kusimamiwa na CCM. Mswada huu uliopo ni ushahidi mdogo tu kwamba inawezekana tutakapata katiba mpya lakini itakuwa ni mbovu kuliko hii iliyopo.

Mimi ninaamini kabisa kuwa pakiwepo juhudi zaidi, mshikamano zaidi na akili zaidi, CCM inashindika hata kwa mazingira haya tuliyo nayo. Mazingira ya kuishinda CCM ni mazuri kuliko yaliyokuwepo Kenya kuiondoa KANU. Lakini bado kuna kitu kinakosekana. Vyama vyetu vya upinzani bado vinategemea makosa ya CCM ili viweze kufanya siasa na kupata umaarufu. Ndio kusema CCM wangekuwa smart wakafanikiwa kuweka mambo yao sawa na kupata watu smart katika safu yao ya uongozi, upinzani ungeweza kupwaya ghafla.

Tunahitaji twende mbele zaidi. Ifike mahala watu waone kwamba CDM, kwa mfano, ni zaidi ya chama cha upinzani. Waone kwamba ni chama kinachosubiri kuunda serikali. Inabidi tuwafikishe wananchi mahala ambapo watakosa imani na CCM in totatilty kiasi kwamba hata wamuweke nani na hata waje na sera gani, bado wananchi washindwe kurudisha imani nao. Hatujawafikisha hapo bado. Ukiona watu wanaongelea kwa kusifia kwamba upinzani mzuri unaona wanavyochachafya CCM ujue bado. Lengo la upinzani sio kuichachafya CCM; ni kuiondoa madarakani ili upinzani wapate fursa ya kutekeleza dira, falsafa na sera zao. We are on the right track, but we need to work a bit harder especially in shaping and redirecting our people's attitudes!
Muda unaenda kasi sana.
 
Ahaa Mzee.katika ubora wake Miaka Kumi iliyopita!
Na. M. M. Mwanakijiji

SIYO jukumu la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kukikosoa Chama cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake ili vijirekebishe na hatimaye viweze kutekeleza majukumu yao vizuri. Siyo kazi ya CHADEMA kuwa mkosoaji mkuu wa serikali ili serikali iweze kujisahihisha na kufanya kazi yake vizuri ya kuwahudumia wananchi. Kwa hakika kabisa siyo jukumu la upinzani nchini kuipatia CCM na serikali iliyoko madarakani mawazo mapya ya mambo ya kufanya ili mambo hayo yafanywe na kila mtu awe na furaha. Ni makosa ya kifikra na kutoelewa siasa kudhania au kukubali kuwa upinzani jukumu lake ni "kuikosoa serikali".

Fikra potofu za lengo na nafasi ya Upinzani nchini
Kwa muda mrefu sasa kuna watu ambao wanataka tuamini kuwa jukumu kubwa la upinzani ni kuwa wapinzani wa kudumu. Watu wenye fikra hizi wamekuwa wakirudia na kutukumbusha kuwa wapinzani wanatakiwa waseme hili au watoe mawazo yale ilimradi yasikike kuwa yametolewa na ni jukumu la serikali "kuyafanyia kazi" mapendekezo au mawazo hayo. Ndugu zetu wenye mawazo haya wengine ni watu wenye madaraka makubwa serikalini, kwenye CCM na hata kwenye vyombo vingine vya umma au binafsi.

Hawa wanaamini Chama Kikuu cha Upinzani nchini Chadema kinatakiwa kiwe ndiye mkosoaji mkuu wa kisiasa nchini ili "kuisaidia serikali" iliyoko madarakani kujitambua madhaifu yake na kujisahihisha. Hivyo, mara nyingi ukiwasikiliza watu hawa utaona kuwa wanatukumbusha kuwa upinzani lengo lake ni "kuikosoa serikali". Mara kwa mara Watanzania hawa wenzetu utaona wanakubali kabisa kuwa upinzani una nafasi nchini lakini ukiwauliza ni nafasi gani utasikia wanatuambia kuwa ni "kuikosoa" serikali.

Wengine huenda mbali zaidi kama tulivyoona siku za karibuni baada ya uchaguzi mkuu kwa kutaka upinzani utoe mawazo mbadala ili kusaidia serikali. Huja na hoja za kutaka kujua msimamo wa "CHADEMA" ni nini au wanauliza wapinzani kwanini hawatoi hoja zenye mshiko ili kuisaidia serikali kujisahihisha. Baadhi ya maswali huulizwa ili kuweza kuona kama wapinzani wana mawazo tofauti. Utaona kuwa wapinzani wanadaiwa watoe mawazo fulani fulani Bungeni ili au sehemu mbali mbali ili CCM iweze kuyafanyia kazi kwa sababu "ndio chama kilichoko madarakani".

Jambo la kusikitisha zaidi ni kuwa wapo wapinzani na baadhi ni viongozi wakubwa tu ambao wanakubali nafasi hii ya kuwa "wapinzani wa kudumu". Wapinzani hawa huamini kuwa ni jukumu lao kuitaarifu serikali ili ijisahihishe na kuipatia mawazo bora ili iyafanyie kazi. Wapinzani hawa na mashabiki wengine wa fikra hizi za "upinzani wa kudumu" huamini kabisa na kutetea kuwa upinzani lengo lake ni "kuikosoa serikali" na ni jukumu la serikali kuyafanyia kazi mapendekezo hayo mazuri.

Matokeo yake ni kuwa wapinzani hawa hujitahidi sana kuisaidia serikali au chama tawala kuona mapungufu mbalimbali kwa ajili ya maslahi ya kile wanachokiita ni "taifa". Hivyo utaona kuwa wapinzani hawa wakudumu wanakuja na mawazo mazuri sana na kuyafikisha kwa furaha kwa viongozi wa serikali au wa chama tawala na watawala hao huwapa mikono ya pongezi na kuwagongagonga migongoni kwa kuwatia moyo kuwa hao viongozi au wapinzani wa kudumu wanajua kuweka "maslahi ya taifa mbele".

Na kama ni Bungeni au hata kwenye vyombo vingine vya kusimamia serikali madiwani kwa mfano, wale wenye fikra za upinzani wa kudumu utawasikia wanajitahidi sana kuisii serikali na kuishauri serikali ili ifanye mambo fulani fulani. Hapa bila ya shaka nisipuuzie jukumu la mbunge kwa mfano toka chama cha upinzani ambaye anajukumu la kuisimamia na kuishauri serikali. Jukumu hili ni la Kikatiba lakini halimlazimishi Mbunge kuwa mpinzani wa kudumu.

Hivyo, kutokuelewa jukumu la upinzani na katika mazingira yetu jukumu la Chadema ni kutokuwa na uelewa wa nafasi na lengo la upinzani ni nini hasa. Kama lengo siyo kuwa mkosoaji mkuu wa serikali ili kuisaidia serikali kuona madudu yake na kujisahihisha swali inabidi liulizwe - jukumu la upinzani ni nini basi? Na linaloendana na hilo ni jukumu la CHADEMA kama chama kikuu cha upinzani nchini ni nini basi?

Jukumu la Chama cha Upinzani

Jukumu la upinzani Tanzania ni kuidhoofisha serikali iliyoko madarakani, kuifanya ionekane isiyo na u wezo wa kuongoza au kutawala ili hatimaye serikali hiyo aidha ikubali kuwa imepoteza imani ya wananchi na kujiuzulu au serikali nzima iamue kuwapa nafasi wananchi kuithibitisha tena au kuiondoa hata kabla ya uchaguzi mkuu mwingine.

Naomba nilirudie wazo hilo hapo juu tena ili kusiwe na utata nimesema kitu gani: Jukumu la upinzani Tanzania ni kuidhoofisha serikali iliyoko madarakani, kuifanya ionekane isiyo na u wezo wa kuongoza au kutawala ili hatimaye serikali hiyo aidha ikubali kuwa imepoteza imani ya wananchi na kujiuzulu au serikali nzima iamue kuwapa nafasi wananchi kuithibitisha tena au kuiondoa hata kabla ya uchaguzi mkuu mwingine.

Maana yake nini?
Kimsingi, chama cha upinzani kinatakiwa kitumie nafasi yake ya upinzani kudhoofisha chama kilichoko madarakani ili wananchi waweze kuona tumaini nje ya chama tawala na kukumbatia chama cha upinzani ili katika mazingira ya kawaida itakapofika wakati wa uchaguzi basi wachague chama hicho cha upinzani. Hivyo, hakuna kitu kama "upinzani wa kudumu" bali wapo "watawala watarajiwa". Chama cha Upinzani kinapokuwa nje ya madaraka kinatumia nafasi mbalimbali ili kukikosoa chama cha upinzani si kwa ajili ya kukisafisha au kukisaidia kutawala bali kwa ajili ya kuonesha ubovu wake ili hatimaye chama hicho kiwe dhaifu madarakani na kulazimisha mabadiliko makubwa ikiwemo kuitishwa kwa uchaguzi kabla ya kipindi cha uchaguzi au kuweza kusababisha chama kilicho tawala kinafanya vibaya sana na hatimaye kusababisha chama cha upinzani kuindia madarakani.

Maana ya kuidhoofisha serikali iliyoko madarakani ni nini?
Utaona kuwa sijasema kuwa ni jukumu la chama cha upinzani kuiondoa serikali iliyoko madarakani kwa nguvu. Huo utakuwa ni uhaini hasa katika mazingira ambapo kuna utaratibu wa kuondoa serikali iliyoko madarakani hata wakati ambapo si wa uchaguzi mkuu. Maana ya kuidhoofisha serikali maana yake ni kutumia mbinu na nyezo za kisiasa ambazo zitaifanya serikali iliyoko madarakani kuonekana kuwa haiwezi kutawala, inaboronga na kutokupendwa na wananchi wake.
Mbinu hizi ziko nyingi na katika nchi ya kwetu au zile ambazo hazina kawaida ya kuwa na uchaguzi kabla ya uchaguzi mkuu (snap election) hutumika ili kukidhoofisha chama tawala kwa lengo la kukiweka katika mazingira magumu ya kushinda uchaguzi mkuu.

Kukidhoofisha chama tawala maana yake ni kujiwekea mazingira ya chama cha upinzani kuweza kufanya vizuri zaidi katika uchaguzi mkuu na kushika madaraka. Kumbe basi lengo lote la chama cha upinzani ni kujijengea mazingira ya kukubalika zaidi na wananchi na hatimaye kufanya vizuri kwenye uchaguzi na kushika madaraka. Siyo lengo la chama cha upinzani kukisaidia chama tawala kutawala au kukifanya kitawala kwa muda mrefu zaidi. Ni lengo la chama cha upinzani kukiondoa chama tawala madarakani kwa njia za kukidhoofisha na kukibomoa kisayansi kwa kukipatia upinzani madhubuti. Lengo la CHADEMA kama chama kikuu cha upinzani ni kusababisha CCM kama chama tawala hatimaye kuondolewa madarakani.

Ili kuelewa uzito wa kauli hii labda niioneshe kwa kinyume chake. SIYO jukumu la Chama tawala kuboresha upinzani ili upinzani uweze kushika madaraka badala yake. Ni jukumu la chama tawala kutumia mbinu mbalimbali za kisayansi kuudumaza upinzani na kuhakikisha hawapati nafasi ya kutawala. Kwa maneno mengine CCM haina jukumu la kuisaidia CHADEMA iimarike. Jukumu la CCM ni kuivuruga Chadema, kuidhoofisha na kuhakikisha ukifika uchaguzi mkuu au mwingine wowote inafanya vibaya kuliko uchaguzi wa kabla yake.

Ndio maana ninawashangaa sana watu wanaiangalia CCM na kuibembeleza itengeneze sheria na kusaidia vyama vya upinzani!

Hakuna chama chenye haki ya kutawala
Vyama vinapewa nafasi ya kutawala kwa muda fulani tu. Havina haki ya kudai kutawala daima. Kukidhoofisha chama kilichoko madarakani siyo kukiondolea haki ya kutawala. Kuna watu ambao wanataka Watanzania ama wapinzani wajisikie vibaya wanapojitahidi kukikosoa Chama cha Mapinduzi kwa minajili ya kukidhoofisha kisiasa kiasi kwamba waonekane kama wanakinyang'anya haki yake ya kutawala.

Na wapo wana CCM ambao wamejiaminisha kuwa wao ndio wenye haki ya kuitawala Tanzania na hivyo jaribio lolote la kukidhoofisha hukutana na maneno makali kiasi cha kuita wanaharakati "wahaini" au "wakoloni mambo leo" au "wanatumiwa na mataifa ya nje". Siyo wana CCM tu wapo hata wapinzani na Watanzania wengine ambao wanaamini kuwa "bila CCM" nchi haiwezi kutawalika na hivyo wameweka maslahi yao kuwa ni pamoja na maslahi ya CCM. Hawa huamini kabisa kuwa CCM na serikali wana haki ya kutawala na hakuna chama kingine.

Jambo la hatari ni kuwa wapo wapinzani kama nilivyodokeza hapo juu ambao na wenyewe wanatenda na kufikiri kwa misingi hiyo hiyo - kuwa CCM ndio wana haki ya kutawala. Ninapozungumzia haki ya kutawala si maanishi madaraka ya kutawala. Madaraka ya kutawala yanatolewa na wananchi. CCM ina madaraka na nafasi ya kutawala. Lakini madaraka haya yanaweza kuondolewa na wananchi na ni jukumu la wapinzani kushawishi wananchi kwa njia mbalimbali kuiona CCM kuwa ni chama kisichofaa kuendelea kuongoza.

Wakati njia za Chama tawala kuvuruga upinzani ni nyingi njia za upinzani kuvuruga chama tawala kisayansi ni nyingi vile vile. Ukiondoa njia kama maandamano na kutajana majina kuna njia sa kisasa za kuvurugana kati ya wapinzani na watawala. Chama tawala kinaweza kutumia njia zifuatazo* kuuvuruga upinzani:


  1. [censored]
  2. [censored]
  3. [censored]
  4. [censored]
  5. [censored]
  6. [censored]
  7. [censored]

Kwa vyama vya upinzani kama Chadema ambavyo vinatambua hasa lengo lake ni kushika madaraka ya nchi siyo kuwa na wabunge wengi zaidi tu na wala siyo kujijengea umaarufu wa baadhi ya wabunge basi vinajiwekea lengo la wazi la kutaka kushika madaraka na hutumia mbinu mbalimbali kudhoofisha chama tawala. Ukiondoa migomo na maandamano au mikutano ya waandishi wa habari yenye kuonesha maovu au udhaifu wa chama tawala na kukidhoofisha mbele ya wananchi kuna mbinu nyingine nyingi za kisasa zenye kufuata saikolojia ya siasa (political psychology) au nadharia ya kisiasa (political theory) ambazo husaidia kuweza kujenga chama cha kisasa. Mbinu hizo ni kama mbinu za kivita (war tactics) ambavyo vyama vikiwa vinawatala zinatumia kudhoofisha upinzani na vikiwa upinzani vinatumia kudhoofisha chama tawala.

CHADEMA kama kweli kinataka kuja kushika madaraka ni lazima kitambue na kianze kufikiri nakutenda kama chama kinachotaka kutawala. Viongozi na wanachama wake, mashabiki na wapenzi wake ni lazima wawe na fikra kama waliyonayo wana CCM na viongozi wao. CCM imejenga imani ndani ya wanachama wake kuwa kinataka kutawala na kitatumia mbinu zozote zile kujikita zaidi madarakani.

Kwa baadhi yetu tunaelewa kile kinachoitwa "kujivua gamba" kama mbinu tu ya kisiasa ya kuweza kujijenga zaidi ili kuwa madarakani. Kujivua gamba kulikofanyika hakuna lengo jingine zaidi ya kuwafanya watu wabadili mawazo juu ya CCM na kukiona kuwa ni chama ambacho kinastahili kupewa madaraka ya kutawala zaidi. Kujivua gamba hakukuwa kamwe kwa ajili ya nchi bali ni kwa ajili ya CCM na nafasi yake. CCM imetishwa na baada ya kutishika imetoa majibu. Swali ni je CHADEM inaweza kudhoofisha CCM?

Binafsi ninaamini lakini inawezekana kwa kutumia mbinu za kisayansi na siyo kubahatisha au kujaribu. Katika siasa huwezi kutegemea upepo wa kisiasa kupeleka ngalawa yako kule unakotaka. Upepo wa kisiasa unapokoma au unapobadilika ni jukumu lako kuanza kutumia kasia. Upepo wa kisiasa nchini unaelekea kubadilika na kukipa nguvu CCM, lakini ina maana Chadema na wapinzani wengine wakae pembeni na kuangalia CCM ikifanya vitu vyake?

Binafsi ninaamini kuwa Chadema kinaweza kutumia mbinu zifuatazo kuanza kudhoofisha CCM zaidi na zaidi na kujibu mapigo ya mashambuli ya kisayansi ambayo yameanza na ambayo kwa mtu ambaye anajua jinsi ya kufanya siasa anaweza kuyatabiri. Kama watu wanafikiria kujivua gamba kutaishia hapa basi hawajawasoma wanamikakati wa CCM ambao wengi wanatumia mbinu ambazo zimejaribiwa na kuonesha matokeo mazuri sehemu nyingine duniani kwa vyama vikongwe kujifanyia mabadiliko na kujaribuu kujidumisha madarakani.

Baadhi ya mbinu hizo kwa wakati huu ni hizi zifuatazo*:


  1. [censored]
  2. [censored]
  3. [censored]
  4. [censored]
  5. [censored]
  6. [censored]
  7. [censored]
  8. [censored]
  9. [censored]
  10. [censored]
  11. [censored]
  12. [censored]
  13. [censored]
  14. [censored]


Mbinu hizi zote zikitumiwa kitaalamu na watu ambao wanajua nafasi yao na wako tayari kujijenga kuelekea kutawala zinasababisha udhaifu ndani ya chama tawala na kukitisa. Badala ya kutumia trekta kung'oa mbuyu na kutumia mafuta na nguvu nyingi basi mbinu hizi nyingi ni za kutumia mchwa kula mizizi na nyingi ni za kutumia watutu kula majani ya juu na kuukausha mbuyu huku ukiwa bado umesimama.

Chama cha upinzani hakiwezi kuzitumia mbinu hizi vizuri bila ya kujiweka katika mkao wa kupigana. Bila kujijua uko kwenye mapambano au kama unafikiria kuwa jukumu lako ni kusaidia kukikosoa chama tawala huwezi kuzitumia mbinu hizi ili kukidhoofisha ili hatimaye wewe uweze kuingia madarakani.

Hivyo basi, tunapoangalia bahari ya kisiasa nchini ilivyo na vyombo vilivyoko majini hatuna budi kuangalia kwa umakini ni jinsi gani upinzani unatumia nafasi yake sawasaawa. Tunaweza kuyageuza maneno ya Baba wa Taifa ambayo wana CCM wanayatumia kama halali yao ya kuendelea kutawala kuwa "Bila CCM madhubuti nchi yetu itayumba". Binafsi naamini "Bila upinzani madhubuti, nchi yetu inayumba".

Tukumbuke, siyo jukumu la upinzani kuimarisha chama tawala wala serikali yake, bali kuviidhofisha kwa mbinu, nguvu, na njia zote zinazokubalika kisiasa.

MWISHO

NB: * Zimeachwa bila kujazwa kwa makusudi.
 
Watu mnapenda kufukuaaa
Lakini Mzee wewe si wa kukaa kimyaa kipindi Moto Kama hiki ...Nini kimekukuta ,ukosoaji wote uliofqnya kwa CCM na majisifu yote kwa JPM,!
Tunahitaji neno kutoka moyoni mwako!
Ibuka tujadili Siasa za 2020 !
Usisubiri mshindi uanze kuchambua!
 
Back
Top Bottom