SIYO Jukumu la CHADEMA kuikosoa CCM ili ijisahihishe na kutawala Vizuri | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

SIYO Jukumu la CHADEMA kuikosoa CCM ili ijisahihishe na kutawala Vizuri

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Mzee Mwanakijiji, Apr 18, 2011.

 1. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #1
  Apr 18, 2011
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,362
  Likes Received: 6,393
  Trophy Points: 280
  Na. M. M. Mwanakijiji

  SIYO jukumu la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kukikosoa Chama cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake ili vijirekebishe na hatimaye viweze kutekeleza majukumu yao vizuri. Siyo kazi ya CHADEMA kuwa mkosoaji mkuu wa serikali ili serikali iweze kujisahihisha na kufanya kazi yake vizuri ya kuwahudumia wananchi. Kwa hakika kabisa siyo jukumu la upinzani nchini kuipatia CCM na serikali iliyoko madarakani mawazo mapya ya mambo ya kufanya ili mambo hayo yafanywe na kila mtu awe na furaha. Ni makosa ya kifikra na kutoelewa siasa kudhania au kukubali kuwa upinzani jukumu lake ni "kuikosoa serikali".

  Fikra potofu za lengo na nafasi ya Upinzani nchini
  Kwa muda mrefu sasa kuna watu ambao wanataka tuamini kuwa jukumu kubwa la upinzani ni kuwa wapinzani wa kudumu. Watu wenye fikra hizi wamekuwa wakirudia na kutukumbusha kuwa wapinzani wanatakiwa waseme hili au watoe mawazo yale ilimradi yasikike kuwa yametolewa na ni jukumu la serikali "kuyafanyia kazi" mapendekezo au mawazo hayo. Ndugu zetu wenye mawazo haya wengine ni watu wenye madaraka makubwa serikalini, kwenye CCM na hata kwenye vyombo vingine vya umma au binafsi.

  Hawa wanaamini Chama Kikuu cha Upinzani nchini Chadema kinatakiwa kiwe ndiye mkosoaji mkuu wa kisiasa nchini ili "kuisaidia serikali" iliyoko madarakani kujitambua madhaifu yake na kujisahihisha. Hivyo, mara nyingi ukiwasikiliza watu hawa utaona kuwa wanatukumbusha kuwa upinzani lengo lake ni "kuikosoa serikali". Mara kwa mara Watanzania hawa wenzetu utaona wanakubali kabisa kuwa upinzani una nafasi nchini lakini ukiwauliza ni nafasi gani utasikia wanatuambia kuwa ni "kuikosoa" serikali.

  Wengine huenda mbali zaidi kama tulivyoona siku za karibuni baada ya uchaguzi mkuu kwa kutaka upinzani utoe mawazo mbadala ili kusaidia serikali. Huja na hoja za kutaka kujua msimamo wa "CHADEMA" ni nini au wanauliza wapinzani kwanini hawatoi hoja zenye mshiko ili kuisaidia serikali kujisahihisha. Baadhi ya maswali huulizwa ili kuweza kuona kama wapinzani wana mawazo tofauti. Utaona kuwa wapinzani wanadaiwa watoe mawazo fulani fulani Bungeni ili au sehemu mbali mbali ili CCM iweze kuyafanyia kazi kwa sababu "ndio chama kilichoko madarakani".

  Jambo la kusikitisha zaidi ni kuwa wapo wapinzani na baadhi ni viongozi wakubwa tu ambao wanakubali nafasi hii ya kuwa "wapinzani wa kudumu". Wapinzani hawa huamini kuwa ni jukumu lao kuitaarifu serikali ili ijisahihishe na kuipatia mawazo bora ili iyafanyie kazi. Wapinzani hawa na mashabiki wengine wa fikra hizi za "upinzani wa kudumu" huamini kabisa na kutetea kuwa upinzani lengo lake ni "kuikosoa serikali" na ni jukumu la serikali kuyafanyia kazi mapendekezo hayo mazuri.

  Matokeo yake ni kuwa wapinzani hawa hujitahidi sana kuisaidia serikali au chama tawala kuona mapungufu mbalimbali kwa ajili ya maslahi ya kile wanachokiita ni "taifa". Hivyo utaona kuwa wapinzani hawa wakudumu wanakuja na mawazo mazuri sana na kuyafikisha kwa furaha kwa viongozi wa serikali au wa chama tawala na watawala hao huwapa mikono ya pongezi na kuwagongagonga migongoni kwa kuwatia moyo kuwa hao viongozi au wapinzani wa kudumu wanajua kuweka "maslahi ya taifa mbele".

  Na kama ni Bungeni au hata kwenye vyombo vingine vya kusimamia serikali madiwani kwa mfano, wale wenye fikra za upinzani wa kudumu utawasikia wanajitahidi sana kuisii serikali na kuishauri serikali ili ifanye mambo fulani fulani. Hapa bila ya shaka nisipuuzie jukumu la mbunge kwa mfano toka chama cha upinzani ambaye anajukumu la kuisimamia na kuishauri serikali. Jukumu hili ni la Kikatiba lakini halimlazimishi Mbunge kuwa mpinzani wa kudumu.

  Hivyo, kutokuelewa jukumu la upinzani na katika mazingira yetu jukumu la Chadema ni kutokuwa na uelewa wa nafasi na lengo la upinzani ni nini hasa. Kama lengo siyo kuwa mkosoaji mkuu wa serikali ili kuisaidia serikali kuona madudu yake na kujisahihisha swali inabidi liulizwe - jukumu la upinzani ni nini basi? Na linaloendana na hilo ni jukumu la CHADEMA kama chama kikuu cha upinzani nchini ni nini basi?

  Jukumu la Chama cha Upinzani


  Jukumu la upinzani Tanzania ni kuidhoofisha serikali iliyoko madarakani, kuifanya ionekane isiyo na u wezo wa kuongoza au kutawala ili hatimaye serikali hiyo aidha ikubali kuwa imepoteza imani ya wananchi na kujiuzulu au serikali nzima iamue kuwapa nafasi wananchi kuithibitisha tena au kuiondoa hata kabla ya uchaguzi mkuu mwingine.

  Naomba nilirudie wazo hilo hapo juu tena ili kusiwe na utata nimesema kitu gani: Jukumu la upinzani Tanzania ni kuidhoofisha serikali iliyoko madarakani, kuifanya ionekane isiyo na u wezo wa kuongoza au kutawala ili hatimaye serikali hiyo aidha ikubali kuwa imepoteza imani ya wananchi na kujiuzulu au serikali nzima iamue kuwapa nafasi wananchi kuithibitisha tena au kuiondoa hata kabla ya uchaguzi mkuu mwingine.

  Maana yake nini?
  Kimsingi, chama cha upinzani kinatakiwa kitumie nafasi yake ya upinzani kudhoofisha chama kilichoko madarakani ili wananchi waweze kuona tumaini nje ya chama tawala na kukumbatia chama cha upinzani ili katika mazingira ya kawaida itakapofika wakati wa uchaguzi basi wachague chama hicho cha upinzani. Hivyo, hakuna kitu kama "upinzani wa kudumu" bali wapo "watawala watarajiwa". Chama cha Upinzani kinapokuwa nje ya madaraka kinatumia nafasi mbalimbali ili kukikosoa chama cha upinzani si kwa ajili ya kukisafisha au kukisaidia kutawala bali kwa ajili ya kuonesha ubovu wake ili hatimaye chama hicho kiwe dhaifu madarakani na kulazimisha mabadiliko makubwa ikiwemo kuitishwa kwa uchaguzi kabla ya kipindi cha uchaguzi au kuweza kusababisha chama kilicho tawala kinafanya vibaya sana na hatimaye kusababisha chama cha upinzani kuindia madarakani.

  Maana ya kuidhoofisha serikali iliyoko madarakani ni nini?

  Utaona kuwa sijasema kuwa ni jukumu la chama cha upinzani kuiondoa serikali iliyoko madarakani kwa nguvu. Huo utakuwa ni uhaini hasa katika mazingira ambapo kuna utaratibu wa kuondoa serikali iliyoko madarakani hata wakati ambapo si wa uchaguzi mkuu. Maana ya kuidhoofisha serikali maana yake ni kutumia mbinu na nyezo za kisiasa ambazo zitaifanya serikali iliyoko madarakani kuonekana kuwa haiwezi kutawala, inaboronga na kutokupendwa na wananchi wake.
  Mbinu hizi ziko nyingi na katika nchi ya kwetu au zile ambazo hazina kawaida ya kuwa na uchaguzi kabla ya uchaguzi mkuu (snap election) hutumika ili kukidhoofisha chama tawala kwa lengo la kukiweka katika mazingira magumu ya kushinda uchaguzi mkuu.

  Kukidhoofisha chama tawala maana yake ni kujiwekea mazingira ya chama cha upinzani kuweza kufanya vizuri zaidi katika uchaguzi mkuu na kushika madaraka. Kumbe basi lengo lote la chama cha upinzani ni kujijengea mazingira ya kukubalika zaidi na wananchi na hatimaye kufanya vizuri kwenye uchaguzi na kushika madaraka. Siyo lengo la chama cha upinzani kukisaidia chama tawala kutawala au kukifanya kitawala kwa muda mrefu zaidi. Ni lengo la chama cha upinzani kukiondoa chama tawala madarakani kwa njia za kukidhoofisha na kukibomoa kisayansi kwa kukipatia upinzani madhubuti. Lengo la CHADEMA kama chama kikuu cha upinzani ni kusababisha CCM kama chama tawala hatimaye kuondolewa madarakani.

  Ili kuelewa uzito wa kauli hii labda niioneshe kwa kinyume chake. SIYO jukumu la Chama tawala kuboresha upinzani ili upinzani uweze kushika madaraka badala yake. Ni jukumu la chama tawala kutumia mbinu mbalimbali za kisayansi kuudumaza upinzani na kuhakikisha hawapati nafasi ya kutawala. Kwa maneno mengine CCM haina jukumu la kuisaidia CHADEMA iimarike. Jukumu la CCM ni kuivuruga Chadema, kuidhoofisha na kuhakikisha ukifika uchaguzi mkuu au mwingine wowote inafanya vibaya kuliko uchaguzi wa kabla yake.

  Ndio maana ninawashangaa sana watu wanaiangalia CCM na kuibembeleza itengeneze sheria na kusaidia vyama vya upinzani!

  Hakuna chama chenye haki ya kutawala

  Vyama vinapewa nafasi ya kutawala kwa muda fulani tu. Havina haki ya kudai kutawala daima. Kukidhoofisha chama kilichoko madarakani siyo kukiondolea haki ya kutawala. Kuna watu ambao wanataka Watanzania ama wapinzani wajisikie vibaya wanapojitahidi kukikosoa Chama cha Mapinduzi kwa minajili ya kukidhoofisha kisiasa kiasi kwamba waonekane kama wanakinyang'anya haki yake ya kutawala.

  Na wapo wana CCM ambao wamejiaminisha kuwa wao ndio wenye haki ya kuitawala Tanzania na hivyo jaribio lolote la kukidhoofisha hukutana na maneno makali kiasi cha kuita wanaharakati "wahaini" au "wakoloni mambo leo" au "wanatumiwa na mataifa ya nje". Siyo wana CCM tu wapo hata wapinzani na Watanzania wengine ambao wanaamini kuwa "bila CCM" nchi haiwezi kutawalika na hivyo wameweka maslahi yao kuwa ni pamoja na maslahi ya CCM. Hawa huamini kabisa kuwa CCM na serikali wana haki ya kutawala na hakuna chama kingine.

  Jambo la hatari ni kuwa wapo wapinzani kama nilivyodokeza hapo juu ambao na wenyewe wanatenda na kufikiri kwa misingi hiyo hiyo - kuwa CCM ndio wana haki ya kutawala. Ninapozungumzia haki ya kutawala si maanishi madaraka ya kutawala. Madaraka ya kutawala yanatolewa na wananchi. CCM ina madaraka na nafasi ya kutawala. Lakini madaraka haya yanaweza kuondolewa na wananchi na ni jukumu la wapinzani kushawishi wananchi kwa njia mbalimbali kuiona CCM kuwa ni chama kisichofaa kuendelea kuongoza.

  Wakati njia za Chama tawala kuvuruga upinzani ni nyingi njia za upinzani kuvuruga chama tawala kisayansi ni nyingi vile vile. Ukiondoa njia kama maandamano na kutajana majina kuna njia sa kisasa za kuvurugana kati ya wapinzani na watawala. Chama tawala kinaweza kutumia njia zifuatazo* kuuvuruga upinzani:


  1. [censored]
  2. [censored]
  3. [censored]
  4. [censored]
  5. [censored]
  6. [censored]
  7. [censored]

  Kwa vyama vya upinzani kama Chadema ambavyo vinatambua hasa lengo lake ni kushika madaraka ya nchi siyo kuwa na wabunge wengi zaidi tu na wala siyo kujijengea umaarufu wa baadhi ya wabunge basi vinajiwekea lengo la wazi la kutaka kushika madaraka na hutumia mbinu mbalimbali kudhoofisha chama tawala. Ukiondoa migomo na maandamano au mikutano ya waandishi wa habari yenye kuonesha maovu au udhaifu wa chama tawala na kukidhoofisha mbele ya wananchi kuna mbinu nyingine nyingi za kisasa zenye kufuata saikolojia ya siasa (political psychology) au nadharia ya kisiasa (political theory) ambazo husaidia kuweza kujenga chama cha kisasa. Mbinu hizo ni kama mbinu za kivita (war tactics) ambavyo vyama vikiwa vinawatala zinatumia kudhoofisha upinzani na vikiwa upinzani vinatumia kudhoofisha chama tawala.

  CHADEMA kama kweli kinataka kuja kushika madaraka ni lazima kitambue na kianze kufikiri nakutenda kama chama kinachotaka kutawala. Viongozi na wanachama wake, mashabiki na wapenzi wake ni lazima wawe na fikra kama waliyonayo wana CCM na viongozi wao. CCM imejenga imani ndani ya wanachama wake kuwa kinataka kutawala na kitatumia mbinu zozote zile kujikita zaidi madarakani.

  Kwa baadhi yetu tunaelewa kile kinachoitwa "kujivua gamba" kama mbinu tu ya kisiasa ya kuweza kujijenga zaidi ili kuwa madarakani. Kujivua gamba kulikofanyika hakuna lengo jingine zaidi ya kuwafanya watu wabadili mawazo juu ya CCM na kukiona kuwa ni chama ambacho kinastahili kupewa madaraka ya kutawala zaidi. Kujivua gamba hakukuwa kamwe kwa ajili ya nchi bali ni kwa ajili ya CCM na nafasi yake. CCM imetishwa na baada ya kutishika imetoa majibu. Swali ni je CHADEM inaweza kudhoofisha CCM?

  Binafsi ninaamini lakini inawezekana kwa kutumia mbinu za kisayansi na siyo kubahatisha au kujaribu. Katika siasa huwezi kutegemea upepo wa kisiasa kupeleka ngalawa yako kule unakotaka. Upepo wa kisiasa unapokoma au unapobadilika ni jukumu lako kuanza kutumia kasia. Upepo wa kisiasa nchini unaelekea kubadilika na kukipa nguvu CCM, lakini ina maana Chadema na wapinzani wengine wakae pembeni na kuangalia CCM ikifanya vitu vyake?

  Binafsi ninaamini kuwa Chadema kinaweza kutumia mbinu zifuatazo kuanza kudhoofisha CCM zaidi na zaidi na kujibu mapigo ya mashambuli ya kisayansi ambayo yameanza na ambayo kwa mtu ambaye anajua jinsi ya kufanya siasa anaweza kuyatabiri. Kama watu wanafikiria kujivua gamba kutaishia hapa basi hawajawasoma wanamikakati wa CCM ambao wengi wanatumia mbinu ambazo zimejaribiwa na kuonesha matokeo mazuri sehemu nyingine duniani kwa vyama vikongwe kujifanyia mabadiliko na kujaribuu kujidumisha madarakani.

  Baadhi ya mbinu hizo kwa wakati huu ni hizi zifuatazo*:


  1. [censored]
  2. [censored]
  3. [censored]
  4. [censored]
  5. [censored]
  6. [censored]
  7. [censored]
  8. [censored]
  9. [censored]
  10. [censored]
  11. [censored]
  12. [censored]
  13. [censored]
  14. [censored]


  Mbinu hizi zote zikitumiwa kitaalamu na watu ambao wanajua nafasi yao na wako tayari kujijenga kuelekea kutawala zinasababisha udhaifu ndani ya chama tawala na kukitisa. Badala ya kutumia trekta kung'oa mbuyu na kutumia mafuta na nguvu nyingi basi mbinu hizi nyingi ni za kutumia mchwa kula mizizi na nyingi ni za kutumia watutu kula majani ya juu na kuukausha mbuyu huku ukiwa bado umesimama.

  Chama cha upinzani hakiwezi kuzitumia mbinu hizi vizuri bila ya kujiweka katika mkao wa kupigana. Bila kujijua uko kwenye mapambano au kama unafikiria kuwa jukumu lako ni kusaidia kukikosoa chama tawala huwezi kuzitumia mbinu hizi ili kukidhoofisha ili hatimaye wewe uweze kuingia madarakani.

  Hivyo basi, tunapoangalia bahari ya kisiasa nchini ilivyo na vyombo vilivyoko majini hatuna budi kuangalia kwa umakini ni jinsi gani upinzani unatumia nafasi yake sawasaawa. Tunaweza kuyageuza maneno ya Baba wa Taifa ambayo wana CCM wanayatumia kama halali yao ya kuendelea kutawala kuwa "Bila CCM madhubuti nchi yetu itayumba". Binafsi naamini "Bila upinzani madhubuti, nchi yetu inayumba".

  Tukumbuke, siyo jukumu la upinzani kuimarisha chama tawala wala serikali yake, bali kuviidhofisha kwa mbinu, nguvu, na njia zote zinazokubalika kisiasa.

  MWISHO

  NB: * Zimeachwa bila kujazwa kwa makusudi.
   
 2. Shalom

  Shalom JF-Expert Member

  #2
  Apr 18, 2011
  Joined: Jun 17, 2007
  Messages: 1,315
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 135
  Mwanakijiji bwana hata kazi hazifanyiki. Uliyoyasema nikweli tupu na nadhani umewasaidia watu wa type ya Waberoya ( najua kwa busara zako huwezi kumtaja mkuu ila hili tuachie sisi) kuja kupoteza muda wao hapa kila siku chadema haijafanya hiki au kile. Message sent!
   
 3. Wizzo

  Wizzo JF-Expert Member

  #3
  Apr 18, 2011
  Joined: Nov 28, 2010
  Messages: 696
  Likes Received: 82
  Trophy Points: 45
  nmekukubali m.m
   
 4. koo

  koo JF-Expert Member

  #4
  Apr 18, 2011
  Joined: Mar 9, 2011
  Messages: 258
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 35
  Ujumbe umefika nashukuru kwa hekima zako mungu akuzidishie
   
 5. zumbemkuu

  zumbemkuu JF Bronze Member

  #5
  Apr 18, 2011
  Joined: Sep 11, 2010
  Messages: 9,004
  Likes Received: 585
  Trophy Points: 280
  Hapo patamu, lakin mmmh!!! hapo kwenye * usisite kuwapa CDM km bado hawazijui ili nao watumie makasia badala yakutegemea upepo, au ya yaliyojiri tabora ndo mwanzo wakutumia makasia nini?
   
 6. tanga kwetu

  tanga kwetu JF-Expert Member

  #6
  Apr 18, 2011
  Joined: May 12, 2010
  Messages: 2,165
  Likes Received: 1,125
  Trophy Points: 280
  ..another shule from Mwanakijiji. Bravo,mkuu!! ngoja nikugongee senksi
   
 7. U

  Uswe JF-Expert Member

  #7
  Apr 18, 2011
  Joined: Nov 1, 2010
  Messages: 2,201
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 135
  asante ila hizo censored. . . mwaga mambo hadharani bana!
   
 8. zumbemkuu

  zumbemkuu JF Bronze Member

  #8
  Apr 18, 2011
  Joined: Sep 11, 2010
  Messages: 9,004
  Likes Received: 585
  Trophy Points: 280
  hapana, sishauri afanye hivyo, atazidi kuzidisha mapambano kwa team pinzani, ngoja ibaki hivyo ili adui asijipange kivingine.
   
 9. kilimasera

  kilimasera JF-Expert Member

  #9
  Apr 18, 2011
  Joined: Dec 2, 2009
  Messages: 3,073
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 135
  mimi naona kama CCM wana uweazo mdogo sana wa kufikiri imefika wakati kila kitu mpaka kitoke upinzani wao ndio watekeleze mfano mambo ya dowans,fedha za eppa mafisadi na kadharika ni vitu ambavyo vilianzia upinzani ila wao walitakiwa mapema sana waanze kuwawajibisha watu sijui wanaogopana,au ndio kuleana kwenyewe kweli inasikitisha sana kwa sasa watu hawafanyi kazi kabisa nchi imefika wakati inakopa hadi mishahara ya watumishi wake!
   
 10. W

  WildCard JF-Expert Member

  #10
  Apr 18, 2011
  Joined: Apr 22, 2008
  Messages: 7,477
  Likes Received: 70
  Trophy Points: 145
  Kwa mtazamo wangu ni kwamba CHADEMA hawaikosoi CCM bali wanaanika UOZO wa baadhi ya watu wa CCM. Mbinu ambayo imewapatia kura si haba mwaka jana. Ukimsoma vizuri Dr Slaa na wenzake wao hawadili na CCM, wanahangaika na watu ndani ya CCM.
   
 11. Wambandwa

  Wambandwa JF-Expert Member

  #11
  Apr 18, 2011
  Joined: Dec 3, 2006
  Messages: 2,240
  Likes Received: 337
  Trophy Points: 180
  MM, sioni kitufe cha 'Thanks', naomba uipokee hata hivyo.
  Chama tawala na chama pinzani kwa hiyo vinategemeana / vinategeana ili maendeleo ya nchi na wananchi kwa ujumla yapatikane.
  Hayo mapendekezo yaliyo 'censered' yangemaliza kiu yangu / yetu zaidi.
   
 12. S

  Sheba JF-Expert Member

  #12
  Apr 18, 2011
  Joined: May 14, 2009
  Messages: 210
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  Mwanakijiji.

  Asante kwa post hii yenye kuelimisha. Nakubaliana na wewe kwa kiasi kikubwa. Ningependa kuchangia na kutoa maoni yangu juu ya masuala machache kati ya mengi uliyoyaainisha:

  1. Awali, majukumu ya msingi ya Chama chochote cha siasa ni mawili yaani kukusanya maoni na maslahi ya wananchi (Interest aggregation); pili, kuyaoanisha maoni hayo na kuyatafsiri katika Sera/ Ilani na kuyasimamia (Interests articulation). Hivyo, naanza kwa kusema kuwa jukumu la Chama cha siasa sio kudhoofisha Chama kingine, hili la kudhoofishana linaweza kuwa suala la mkakati, yena mkakati mchafu, na ndio maana hufanywa siri. Mfano, katika kutekeleza Mkakati mchafu wa kudhoofisha upinzani, CCM itajificha katika 'kupokea viongozi wa upinzani wanaohama vyama vyao' na CHADEMA kitaitisha maandamano ya kitaifa kikidai kinataka kuwakilisha kilio cha wananchi juu ya kupanda kwa gharama za maisha na bei ya sukari.

  2. Naomba kutofautiana na wewe kuwa kazi ya 'Vyama Mbadala' ni kudhoofisha Chama Tawala na Serikali yake. Kudhoofisha Chama Tawala na Serikali yake hakuna tofauti kubwa sana na 'Uhaini' na vitendo vya kudhoofisha vinatoa mwanya mzuri kwa Chama kinachotawala kutafsiri na kuhalalisha kuwa ' Vyama vya upinzani' vinataka kufanya uhaini. Kazi ya 'Vyama vya Upinzani' ni kujiandaa kukamata dola kwa kuainisha na kushawishi wananchi wakubali sera na mipango mbadala wakati wa uchaguzi; na kuendelea kushawishi na kuthibitisha kwa wananchi kupitia taasisi na majukwaa halali kuwa Sera zao Mbadala zingezaa matunda zaidi ya hizo za Chama tawala zinazotekelezwa. Hii dhana ndio ambayo inatumika na wale walioanzisha demokrasia za mabunge. Kudhoofisha Serikali ni ku 'Weaken' au 'undermine' Serikali iliyo madarakani kiasi cha kuifanya ishindwe kutawala, hilo naamini sio lengo la upinzani maana halina tofauti na kuchukua silaha na kuanzisha civil war. Aidha katika Demokrasia iliyokomaa, 'Vyama vya Upinzani' havifanyi kazi ya kudhoofisha Chama Tawala na Serikali kwa kuepuka kuanzisha mzunguko (Vicious Cycle) wa kudhoofishana na hatimaye lengo kuu la kuleta maendeleo ya nchi (prospertity) kutofikiwa kwa kutumia nguvu nyingi kudhoofishana. Wenzetu ukiwa nje ya Serikali ni kipindi cha kujifunza na kutafakari namna ya kuenenda na kuleta tofauti pale unapopata fursa ya kushika dola.

  3. Aidha katika muktadha huo huo, jukumu la Chama Tawala sio kudhoofisha upinzani wala kuujenga. Jukumu lao ni kutawala na kulinda katiba inayotoa fursa na wigo kwa 'vyama vya upinzani' kufanya majukumu yake sambamba na lengo kuu la 'prosperity' ya nchi.

  Majumuisho yangu ni kuwa,Neno 'Upinzani' halina maana ya moja kwa moja ya 'Opposition' kama linavyomaanisha katika kiingereza na pia katika muktadha (Context) wa historia ya demokrasia katika nchi za magharibi. Neno 'Upinzani' kama ambavyo limekuwa likitumika kwetu lina maana ya ' Resistance' na si 'Opposition'. Naamini 'wapinzani' nchini kwetu waliingizwa mkenge na kukubali jina hili ambalo linamaanisha kuwa ni watu 'wanaopinga' Chama Tawala na si 'Vyama Mbadala' yaani ' alternative parties'. Matokeo yake katika tafsiri ya siasa zetu, vyama vya upinzani, vinapinga juhudi za chama tawala katika kusukuma maendeleo, kujenga umoja wa kitaifa na kusimamia amani ya nchi (kwa ujumla Ustawi). Jina hili 'wapinzani' limewatafuna sana 'vyama mbadala' na kwa kiasi kikubwa wananchi wengi bado hawajaelewa dhana hii.  lengo la nchi (Purpose of the State/Nation) sio kufanya siasa, ni kuhakikisha ustawi (prosperity). Ndio maana pale Ubelgiji kuna 'Care Taker Goverment' kwa zaidi ya mwaka sasa lakini nchi inakwenda na inaendelea, pale Japan hali kadhalika, katika kpindi cha miaka miwili, kumebadilishwa Serikali zaidi ya mara tatu lakini nchi inaendelea na inastawi pamoja na majanga ya Tsunami. Kwa upande wetu, bahati mbaya tumedandia dhana ya demokrasia ya uwakilishi tofauti na wenzetu ambao dhana hii imetokana na migongano ya kihistoria ya ndani ya jamii zao. Matokeo yake, tumelazimika kuazima dhana (Concepts) na wakati mwingine kuzitumia kuhalalisha nafasi zetu, kama ambavyo Chama Tawala kilivyo 'coin' neno 'Upinzani' kwa faida yake. Naendelea kuamini kuwa, Lengo/ Sababu ya Taifa letu si kudhoofishana, ni kuhakikisha ustawi wa taifa letu na vizazi vyake. Hili la kudhoofishana halikuwahi kuwa moja ya sababu za kupigania uhuru wetu bali ustawi wa watu wetu ambao ulikuwa unakandamizwa. Tunaweza kutofautiana juu ya njia za kufikia ustawi huo lakini sio lengo. Vyama vinafanya kazi ya kuhamasisha umma kukubaliana na mawazo yake mbadala juu ya namna ya kufikia ustawi wa taifa na kuomba ridhaa yao, huo ndio msingi wa demokrasia ya vyama vingi na si kudhoofishana.

  Pengine, tatizo langu ni matumizi ya neno 'kudhoofisha'. Kimsingi nakubaliana na mawazo yako kwa kiasi kikubwa.
   
 13. Johnsecond

  Johnsecond JF-Expert Member

  #13
  Apr 18, 2011
  Joined: May 4, 2010
  Messages: 1,077
  Likes Received: 7
  Trophy Points: 0
  Umezunguka hapo hapo mwanangu
   
 14. nsimba

  nsimba JF-Expert Member

  #14
  Apr 18, 2011
  Joined: Oct 7, 2010
  Messages: 785
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 33
  hongera mkuu,umesomeka vema. Nashauri uruhusu viongozi CDM wa ku-PM ili uwepe utamu wa kwenye *cencered; ili wafuate vema kuwavyoofisha ccm kwa maandalizi nyoofu ya kutawala 2014 (serikali za mitaa) na hatimaye 2015
   
 15. Edson

  Edson JF-Expert Member

  #15
  Apr 18, 2011
  Joined: Mar 7, 2009
  Messages: 9,202
  Likes Received: 721
  Trophy Points: 280
  NB: * Zimeachwa bila kujazwa kwa makusudi.


  usiwe na shida tunaozijua tunazijua mkuu..........mpaka sasa mkuu mchwa wametafuna mizizi ya mbuyu na nusu ya mizizi imetafunywa...tatizo walipofika mchwa kuna mwamba na mizizi imejichimbia ndani ya hiyo miamba ndio maana inakuwa ngumu mizizi kutafunwa.............majani yameachwa kwa makusudi ili kama mchwa wakifanikiwa mbuyu utaanguka hivyo hivyo...........hata hivyo upande uliotafunwa na mchwa majani yake yameanza kuwa na rangi ya njano.........yanaelekea kunyauka
   
 16. W

  WildCard JF-Expert Member

  #16
  Apr 18, 2011
  Joined: Apr 22, 2008
  Messages: 7,477
  Likes Received: 70
  Trophy Points: 145
  Hapana. Nisome vizuri tu. CCM wanayo ILANI yao ya UCHAGUZI. Dr Slaa na wenzake hawaiongelei hiyo. Badala yake wanahangaika na Maghufuli kauza nyumba za serikali. Malecela kaandika vimemo vya EPA na mambo mengine kama hayo ambayo yalipaswa kufanywa na vyombo vya habari za uchunguzi.
   
 17. e

  ejogo JF-Expert Member

  #17
  Apr 18, 2011
  Joined: Dec 19, 2009
  Messages: 994
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 35
  Thanks mwanakijiji kwa shule nzuri. Ni kama ile principle ya kuhubiri dini kwani you must condemn the devil and praise God.
   
 18. lukindo

  lukindo JF-Expert Member

  #18
  Apr 18, 2011
  Joined: Mar 20, 2010
  Messages: 7,891
  Likes Received: 6,086
  Trophy Points: 280
  kwenye red, kuwa wazi tu. Tatizo hakuna kuogopana ila "Mwajibishaji" anawaogopa "Wawajibishwaji".
   
 19. Mfamaji

  Mfamaji JF-Expert Member

  #19
  Apr 18, 2011
  Joined: Nov 6, 2007
  Messages: 6,525
  Likes Received: 556
  Trophy Points: 280
  Mimi Nafahamu kuwa jukumu la chama pinzani ni kushika madaraka next. Kwa hiyo wana kila sababu ya kufichua uovu wa chama tawala ila kutoa solutions kwa maana ya kuwasaidia ni kupoteza mabomu au risasi vitani. Kwanza hata wakikosolewa na wakapewa lililojema hawataki . CCM imekuwa ikiendeshwa na vilaza miaka yote, Imagine hadi Mwanasheria Mkuu wa serikali hajui sheria hadi kuumbuliwa na wanasheria wa CDM?

  Nawashauri viongozi wa CDM mkiona uchafu semeni sisi tujue , wala msitake warekebishe maana kama walishindwa kufanya hivyo kwa miaka 50 watawezaje leo.? Do not wake them up!!!!!
   
 20. NewDawnTz

  NewDawnTz JF-Expert Member

  #20
  Apr 18, 2011
  Joined: Nov 15, 2010
  Messages: 1,675
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 0
  Mzee MM uko sawa kabisa..........

  Mara nyingi nimekuwa nikijiuliza hili swali, ni kweli kazi ya upinzani ni kuipa serikali njia mbadala za kutawala? Hakika ndiyo CDM wafanyavyo kama ulivyobainisha kwenye post yako

  But nikigeuka upande wa pili naona kama vile let them do otherwise we will be doomed.........

  kwa nini nasema hivi.....kama unaserikali ya watu ambao hawajui kuwaza and they do not use their faculty of thinking katika kupanga mambo sahihi na vipaumbele vya kufanya, na kama wakiwaza wanakuja na approach ambayo matokeo yake baada ya kutekeleza ni mabaya zaidi ya kutekeleza, kwa nini wasisaidiwe kufikiri na wanaojua kufikiri vizuri?....that still remain as a challenge, Je wawashauri (zingatia wako kwenye dola) ili kupata mbinu mbadala za kuongoza taifa au wawaaache waendelea kuboronga kwa kufikiri kinyume nyume tuendelee kuumia?

  Hapa ni sisi watanzania kusoma alama za nyakati na kufahamu kuwa CCM imefika mwisho wa kufikiri na wanahitaji watu wengine kuwafikiria....hili litoshe kutuambia kuwa hatuhitaji chama kinachofikiriwa na wengine bali chama chenye hazina ya kufikiri ambacho chama tawala huiga mawazo, mbinu na mikakati ya kuitawala kutoka kwacho....otherwis
  e :sleepy:
   
Loading...