Lunyungu
JF-Expert Member
- Aug 7, 2006
- 8,873
- 1,898
Sitta: Sikukejeli vielelezo vya Dk Slaa kuhusu BoT
*Asema hakuvionyesha vyote kwenye televisheni
*Ataka wabunge watoe hoja hata kama ushahidi wao si asilimia 100
*Slaa asema propaganda za Spika, Makada wa CCM zimewaumbua
*Serikali yajikanganya kuhusu kurejeshwa Daudi Ballali
Na Joyce Mmasi
SPIKA wa Bunge, Samuel Sitta, ameibuka na kupinga madai yanayoelekezwa kwake kuwa alivikejeli vielelezo vya Mbunge wa Karatu (Chadema), Dk Wilbrod Slaa kuhusu tuhuma za ufisadi katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Vielelezo hivyo viliwasilishwa na Dk Slaa bungeni alipowasilisha hoja binafsi ya kutaka iundwe kamati ya bunge kukagua mahesabu ya BoT na baadaye kuiondoa baada ya kuhisi kwamba hatatendewa haki. Akizungumza na gazeti hili jana, Sitta alikana akisema kuwa tatizo hapo ni waandishi wa habari wenye tabia ya kuchonganisha watu.
"Hapa tatizo lipo kwa waandishi wa habari, wanakuwa na kitu kama kuchonganisha, wanapenda kuandika kile wanachoamini, wanachosikia au kupenda wao," alisema Sitta. Alipotakiwa kufafanua msimamo wake wa wakati huo, hasa baada ya kubainika kuwa baadhi ya hoja za Dk Slaa zimebainika ni za kweli, Sitta alisema; Mimi sikuwa nazungumzia ukweli au uongo wa hoja ya Dk Slaa, nilizungumzia kuhusu utaratibu wa kuziwasilisha hoja bungeni," alisema na kuongeza; "Kwa mfano, Dk Slaa alipeleka vielelezo vyenye kurasa 1,000, barua na vielelezo vingi kutoka kwenye mitandao ya komputa.
Haikuwa rahisi kwangu kuweza kuvipitia kwa wakati huo, hivyo niliomba nipatiwe muda zaidi ili niweze kuviangalia na kujiridhisha na niweze kutenda haki. "Naomba ifahamike tu kuwa, si kazi ya mbunge kupeleka hoja yenye uhakika kwa asilimia 100, ni hoja yoyote yenye mashaka juu ya jambo fulani, lakini tunachozungumzia hapa ni muda wa kuifanyia kazi.
"Mfano, moja ya kielelezo kilimtaja waziri mmoja kwa jina kuwa alitaka kupewa mgawo wake na mambo mengine ambayo mimi niliona hayana haja kuwepo kwenye vielelezo vile, nikamwambia Dk Slaa si lazima vielelezo vyote viende, sasa kama barua moja ilitiliwa mashaka haimaanishi kuwa tulitilia mashaka vielelezo vyote," alisema Sitta.
Spika huyo aliongeza kuwa, kama Slaa angepeleka au kuacha hoja yake kwa ajili ya kikao kingine cha bunge, yeye angeifanyia kazi na si kuitupa kapuni. Lakini pia Sitta alieleza kushangazwa kwake kusikia hoja hiyo ikizungumziwa mahali pengine nje ya bunge. Sitta aliongeza kuwa baada ya kupokea vielelezo vya Dk Slaa alikuwa amejiandaa kuvipeleka kwa wataalam wa kuvichunguza, jambo ambalo hakulifanya baada ya hoja hiyo kuondolewa bungeni.
Dk Slaa aliamua kuichomoa hoja yake baada ya kupata taarifa kuwa kulikuwa na mpango wa kumdhibiti kama ilivyofanyika kwa Mbunge mwenzake wa Chadema, Zitto Kabwe, ambaye alisimamishwa kazi za bunge kwa kuwasilisha hoja binafsi dhidi ya Waziri Nazir Karamagi kuhusu utiaji saini mkataba wa Mgodi wa Buzwagi.
Baada ya Dk Slaa kuchomoa hoja hiyo, aliamua kuitangaza kwa umma kupitia mikutano ya hadhara, huku Spika Sitta akionekana hadharani kwenye moja ya vipindi vya Televisheni ya Taifa akionyesha baadhi ya vielelezo vya hoja hiyo na kuviponda kuwa ni vya kibabaishaji na kuahidi kuvipeleka polisi kuchunguzwa.
Akizungumzia suala hilo, Dk Slaa alisema hana mpango wowote wa kumchukulia hatua Spika Sitta na badala yake wananchi ndio watakaoamua baada ya kuona ukweli wa hoja yake dhidi ya kauli za propaganda zilizokuwa zikitolewa na Sitta na viongozi wengine wa Chama Cha Mapinduzi. "Nitamshitaki kwa wananchi, na si yeye tu hata Makamba (Katibu Mkuu wa CCM), Aggrey Mwanri na Seif Khatib.
Wote hawa walionekana kutetea ufisadi ule na kutangaza propaganda za chama chao, lakini sasa wanaona aibu kutokana na ukweli kuwekwa hadharani," alisema Dk Slaa. Mbunge huyo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), aliongeza kuwa anachokiona sasa ni umuhimu wa kuitazama upya nafasi ya Spika kwa kuwa inahitaji kushikiliwa na mtu asiye na masilahi na chama chochote cha siasa.
"Spika wetu anafanya kazi kwa masilahi ya CCM kutokana na yeye kuwa kada wa chama hicho. Tunachotaka sasa ni kuwa mtu akichaguliwa kuwa Spika hata kama alitokana na chama fulani asiruhusiswe tena kufungamana na kazi za chama ili awe huru. Hii itasaidia kumpa nafasi ya kutokuwa na upande kama ilivyo sasa ambapo Spika anaonekana kuwa upande wa CCM na serikali yake hata kama inakosea."
Alisema, Spika amekuwa shabiki wa CCM na amekuwa akipeleka hoja zinazojadiliwa na wabunge kwenye vikao vya CCM na hali hiyo akaifananisha na kuwa mwamuzi anayependelea upande mmoja wa timu huku akitaka kuonyesha haki katika kuchezesha mchezo.
Wakati huo huo; hatima ya kurejeshwa nchini kwa Gavana wa Benki Kuu (BoT) aliyetimuliwa, Daud Ballali ambaye inasemekana yuko Marekani kwa matibabu bado ni kitendawili baada ya watendaji kutupiana mpira kuhusu nani anahusika kutoa amri hiyo.
Awali, ilielezwa kuwa, vyombo vya kiintelejentsia vilipewa agizo na Rais Jakaya Kikwete kumrejesha Ballali nchini kufuatia wananchi kutaka kumwona, lakini vyombo hivyo vikashindwa kutekeleza agizo hilo kwa kile kilichoelezwa kuwa amri hiyo haikufuata taratibu.
Vyombo hivyo vilielezwa kuwa mtoaji agizo angekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utawala Bora, Philip Marmo na si Rais mwenyewe, lakini Marmo alipoulizwa kuhusu taarifa hizo akasisitiza kuwa hafahamu lolote na hana taarifa kuhusu alipo Ballali. "Mimi nasikia tu kama wewe, sijui yuko wapi na kwa kweli niko safarini, sasa na sina taarifa ya kwamba natakiwa kutoa agizo hilo," Marmo aliliambia gazeti hili jana.
Jitihada za gazeti hili kubaini kama kuna jitihada zozote zilizokuwa zikifanywa na serikali kuhusu kurejeshwa kwa Ballali nchini, zilionyesha kuwa, kuna kazi iliyokuwa imeanza, lakini ikakosa baraka kufuatia kuwepo vyombo vingi vinavyotakiwa kujumuishwa kabla ya kufikia uamuzi wa ama kumrejesha au kumuacha huko aliko.
"Unajua Ballali ana mambo mengi sana ambayo hata sisi tunamtaka atusaidie, hivyo basi akipatikana mambo mengi zaidi yatawekwa hadharani," chanzo chetu kimoja kilieleza na kuongeza kuwa; "Kutokuwepo kwake hapa nchini, inaonyesha kama anageuzwa jalala la kila uchafu. Kila aliyefanya uchafu katika masuala ya fedha katika Benki Kuu anaelekeza shutuma kwake."
Aidha, taarifa zinaeleza kuwa, ujio wa Ballali utasaidia kutoa taarifa za kweli kuhusu kilichobainishwa na ukaguzi wa Kampuni ya Ernest and Young iliyofanya uhakiki wa hesabu za BoT katika Akaunti ya Malipo ya Nje (EPA) na kubaini upotevu wa Sh133 bilioni.
Taarifa hizo zinaongeza kuwa, mbali na kuwasaidia kupata taarifa zinazohitajika, Ballali anatakiwa kuwekwa katika ulinzi ili asije akadhuriwa na hao waliohusika katika upotevu huo wa Sh133 bilioni pamoja na zile ambazo hazijakaguliwa, ambao wamekuwa wakimtupia lawama au kuhofu kuwa anaweza kuwachifua. "Unajua 'brother' hawa jamaa wanaweza kumfanyia lolote Ballali kabla sisi hatujapata lolote katika mambo yetu, hivyo anahitaji kuwa katika mikono yetu salama," alisema.
Chanzo chetu kingine kilieleza kuwa, mmoja wa wahusika katika kundi linalotakiwa kutoa maamuzi ya ama Ballali arejeshwe au kuachwa ni Kamishna wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Robert Manumba. Kamishna huyo alipoulizwa kuhusu nafasi yake na maamuzi aliyokwisha kuyafikia alisema; "Muulize mwenyekiti ambaye ni Mwanasheria Mkuu, ndiye mwenyekiti wa Kamati, hebu muulize huyo ndiye msemaji."
Hata hivyo, Johnson Mwanyika ambaye ni Mwanasheria Mkuu hakuweza kupatikana jana kufuatia kuwepo taarifa kuwa yuko likizo na pia simu yake kubakia kuita bila kupokewa.. Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali, Ludovick Utoh, alipoulizwa kama mmoja wa wajumbe waliokabidhiwa jukumu la kuhakikisha wanawafuatilia waliohusika na ubadhirifu wa fedha za BoT, jukumu walilopewa na Rais Kikwete alisema; "Mimi si mjumbe wa kamati, kama suala ni kutazama kuhusu kamati inayohusika na jambo hili la BoT tafadhali jaribu kuwatafuta wajumbe wengine waliomo katika kamati hiyo."
Utoh alitangazwa kuwa mjumbe wa kamati hiyo na Katibu Mkuu Kiongozi, Phillemon Luhanjo. Wajumbe wengine walitajwa ni; Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hosea, Inspekta Jenerali wa Polisi, Said Mwema na Johson Mwanyika. Kamati hii ilipewa miezi sita ya kukamilisha zoezi zima la kufuatilia waliohusika na utafunaji huo mkubwa wa fedha za umma.
Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na taarifa tata hasa kutoka kwa viongozi wa upinzani zikieleza kuwa, Ballali amehama kutoka Boston, Marekani kwenda katika visiwa vya Malta. Taarifa hiyo ilitolewa siku moja baada ya kuelezwa na Marekani kuwa imefuta viza ya Ballali huku msemaji wa masuala ya Habari wa Ubalozi wa Marekani nchini, Jaffery Salaiz, akieleza kuwa hana uhakika wa alipo Ballali.
Kwa mujibu wa taratibu za Marekani, Idara ya Mambo ya Nje ndiyo inayohusika na masuala ya viza na mtu anapoingia ndani ya nchi hiyo hubakia chini ya Wizara ya Ulinzi wa Ndani na anaweza kutolewa humo kama idara hizo mbili zimehusishwa kwa pamoja na sio moja peke yake .