Josh Michael
JF-Expert Member
- Jun 12, 2009
- 2,523
- 77
- Kauli zake zaivuruga CCM, Kamati ya Mwinyi
MWENENDO na kauli zinazotolewa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Samuel Sitta, zimekivuruga Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuipa kazi ya ziada kamati ya usuluhishi wa mgogoro kati yake na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa.
Kauli hizo za Sitta zinakwenda sambamba na msimamo wake wa kugoma kumwomba radhi Lowassa, badala yake anataka mbunge huyo wa Monduli ndiyo awaombe radhi Watanzania.
Hivi karibuni, wakati wa hafla ya uzinduzi wa albamu ya kwaya ya Kanisa Katoliki la Mtakatifu Michael, Parokia ya Mtakatifu Xavery, Chang'ombe, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Sitta alisema ujasiri wake unatokana na nguvu za Mungu.
Alisema nguvu hizo zimekuwa zikimwezesha kutekeleza wajibu wake kwa uhakika bila kuyumbishwa wala kuogopa kitu chochote.
Sitta ambaye siku za hivi karibuni amekuwa akishambuliwa kwamba amewasaliti Watanzania kutokana na kuufunga mjadala wa kashfa ya Richmond, juzi akiwa mjini Songea, alikaririwa akisema alinusurika kuvuliwa uanachama CCM kutokana na ujasiri wake wa kusimamia ukweli.
Kauli hizo zimeonekana kuivuruga zaidi CCM na kamati inayongozwa na Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi inayorusha karata ya mwisho kuwasuluhisha Sitta na Lowassa.
Wajumbe wengine wa kamati hiyo ambayo imeongezewa muda wa mwezi mmoja kusuluhisha mgogoro huo, ni Makamu Mwenyekiti wa CCM taifa, Pius Msekwa na Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho, Abdulrahman Kinana.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Kapteni John Chiligati, aliiambia Tanzania Daima jana kuwa, CCM imeshangazwa na kauli za Sitta wakati anapaswa kujiandaa kwa usuluhishi.
Chiligati ambaye pia ni Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, alisema kwa kawaida vikao vya NEC na CC ni vya siri na mjumbe yeyote hapaswi kutoa siri za vikao hivyo.
"Ndugu yangu kweli nimemsikia, inasikitisha sana, lakini sina cha kusema na nakuomba uandike hivi kwamba Chiligati hana cha kusema kuhusu kauli za Sitta," alisema Chiligati.
Alipoulizwa kama Sitta anaweza kuchukuliwa hatua kwa kauli hizo, Chiligati alisisitiza kuwa hawezi kusema chochote kuhusu hilo.
Kwa upande wa Kamati ya Mzee Mwinyi, kauli hizo zimezidi kuwaweka katika wakati mgumu na huenda wakarejesha ripoti katika muda uliopangwa bila kupata suluhu kati ya watu hao.
Akizungumzia kauli za Sitta, Msekwa kama ilivyokuwa kwa Chiligati, alisema hawezi kusema chochote kwani kamati hiyo ni ya CCM na inafanya kazi za CCM na si za CHADEMA.
"Hii kamati ni ya CCM, si ya CHADEMA, ninyi watu wa CHADEMA mnaitakia nini? Hata kama Sitta anatoa kauli tata si kazi yetu, tuacheni jamani, mnaitakia nini CCM?" alilalama Msekwa na kukata simu.
Kwa upande wake, Sitta ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Mashariki, aliliambia Tanzania Daima Jumatano kuwa siku zote anasimamia katika ukweli na kuzingatia maadili.
Alisema kauli kwamba alitaka kupokonywa kadi ya CCM kwenye vikao vya NEC mwaka jana na mwaka huu mjini Dodoma ni ya ukweli na kila mtu anajua.
"Huo ni ukweli wenyewe, tatizo liko wapi? Maana kila mtu anajua, mimi sioni kama kuna siri hapa, na hili nitaendelea kulisema hata kama wenzangu hawataki," alisema Sitta.
Akizungumzia hoja kwamba kundi lake linaandaa mgombea urais, Sitta alisema katika mzozo wake na Lowassa hapendi kuzungumzia vyeo kwani msimamo wake ni kusimamia maadili.
"Mimi sipendi kuzungumzia vyeo sijui urais au sijui nini, ila nasimamia kwenye maadili na ndiyo maana tunausubiri kwa hamu muswada wa sheria wa kutenganisha siasa na biashara. Haiwezekani mtu umeingia kwenye siasa masikini, unatoka tajiri," alisema.
Sitta alilazimika kuzungumzia suala la urais baada ya kuwapo taarifa kuwa siri ya ugomvi wake na Lowassa ni kinyang'anyiro cha urais mwaka 2015.
Kwa mujibu wa habari hizo, Sitta na Lowassa ambao hadi sasa wameligawa Bunge na chama kwa misimamo yao, kila mmoja anataka rais ajae baada ya Rais Jakaya Kikwete kumaliza muda wake, kama si yeye, atoke kwenye kundi lake.
Kwa hali jinsi ilivyo kuhusu mzozo wa vingunge hao, Kamati ya Mzee Mwinyi ambayo inajipanga kuwakutanisha vigogo hao, inaweza kugonga mwamba kutokana na msimamo wa Sitta na kauli anazozitoa hivi sasa tangu kumalizika kwa kikao cha NEC mjini Dodoma.
Mbali ya kuifanya kazi ya Kamati ya Mwinyi kuwa ngumu, msimamo huo wa Sitta unamweka pabaya Mwenyekiti wa CCM taifa, Rais Jakaya Kikwete kufanya maamuzi magumu.
Tangu kuibuka kwa sakata la mkataba wa kifisadi kati ya Kampuni ya Richmond na TANESCO, uliosainiwa Juni 23, 2006, kisha kusababisha Lowassa kujiuzulu Uwaziri Mkuu na Rais Kikwete kuvunja baraza la mawaziri, CCM na Bunge hata serikali vimejikuta vikiingia katika mgawanyiko mkubwa.
Kundi la Lowassa ambalo linaundwa na watu wenye nguvu ya fedha, limekuwa na ushawishi mkubwa ndani ya CCM na hata bungeni, lakini Spika Sitta akiwa na kundi dogo la watu majasiri wanaojiita wapambanaji wa ufisadi wamesababisha msuguano ndani ya CCM na Bunge ambalo asilimia kubwa ya wabunge ni wa chama hicho tawala.
Mgawanyiko huo ndiyo ulioifanya NEC kuunda Kamati ya Mwinyi kutafuta suluhu. Hata hivyo, kamati hiyo iliyoanza kazi Agosti mwaka jana ilishindwa kumaliza tatizo hilo baada ya Spika kukataa suluhu na Lowassa.
Licha ya Spika kukubali kuizika hoja ya Richmond bungeni, bado msuguano uliendelea ndani ya chama na hivyo mkutano wa NEC uliofanyika hivi karibuni uliamua kuiongezea muda Kamati ya Mwinyi kwa kuitaka ichunguze kiini cha tatizo.