Sitasahau Christmas ya mwaka 2016. Nikiwa na rafiki yangu asubuhi kunakucha hatuna hili wala lile tunajipa moyo na kusogea gengeni kulikuwa na mama mmoja alikuwa anatuuzia mboga, ndani tulikuwa na mia 3 ila unga tulikuwa nao tatizo kubwa lilikuwa ni mboga, safari ya kwenda gengeni ikaanza taratibu huku tukiwa na matumaini ya kumkuta mama dah! Kufika tunakuta wapo tu wauza nyanya hapo tuna njaa ya ya siku moja maana usiku hatukula, ikabidi tupumzike pale gengeni tukawa tunasubiri labda mama angekuja atupatie mboga ila wapi.
Dakika chache nikamuona mpenzi wangu na rafiki yake wanatoka salon kutengeneza nywele, alishangaa mimi kuwa pale akauliza vipi huko kwenu sikukuu vipi nikamwambia poa tu hapa tumekuja kuchukua nyanya tukapike karibuni wakasema asante. Nikamuuliza wapi mbona mmetoka salon akasema tunajiandaa kutoka (nikajua tayari naenda kugongewa) nikamwambia kila la kheri uwe makini wakaanza safari ya kwenda huko kwenye mtoko wao.
Basi jamaa yangu akaniambia twende kwa shangazi yupo hapa mjini najua tutakula na kurudi home tukiwa vizuri bhana safari ya kwenda kwa shangazi ikaanza wakati huo nilikuwa nina jipu kwenye paja yaani maumivu ya jipu njaa na hela hakuna nilikuwa naona kama maisha yanatutania sana, basi tukafika kwa shangazi tulikuta kuna foleni ya watu maana wengi walikuja pale pia kujumuika nao hvyo msosi wetu ukawa haupo kwenye mahesabu wakaugawanya gawanya hatimaye na sisi tukapata kidogo tukala na jioni tukarudi nyumbani.
Ile tunafika tukakuta majirani wanapika pilau kuku aisee nikaingia ndani nikamwambia mshikaji mimi nalala (tulikuwa vyumba tofauti) kabla sijasinzia akaja kugonga mlango akaniomba sufuria kubwa nikampa baada ya muda akaja na pilau limejaa sufuria likiwa na nyama aisee tulikula siku 2 pilau haliishi hadi tukamwaga.
Siku hiyo niliamini Mungu ndiye anajua nini utakula hata kama huna pesa. MUNGU ATUFANIKISHE SANA.