MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Geita, Joseph Msukuma amesema ana siri kubwa ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuhamia Chadema na kupewa nafasi ya kugombea urais akiwakilisha vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Msukuma alisema yeye alikuwa miongoni mwa timu ya watu 11 iliyokuwa na mkakati wa kumsaidia Lowassa kushinda katika kura za maoni za kuomba kuteuliwa kugombea urais ndani ya CCM, ambapo alikatwa na kuhamia Chadema.
Alitoa kauli hiyo kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni za mgombea ubunge wa Jimbo la Geita Mjini, Costantine Kanyasu uliofanyika juzi kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Nyankumbu.
Alidai kuwa baada ya Lowassa kukatwa wananchi wengi walianza kusema ana mpango wa kuhamia Chadema ili kumfuata, lakini alisisitiza kwamba hana mpango huo kwani ana siri nzito kuhusu mgombea huyo wa Ukawa.
Msukuma ambaye ni mgombea wa CCM Jimbo la Geita Vijijini, alidai kuwa hadi sasa mpango wa Lowassa kama atashinda kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kumteua Waziri Mkuu mstaafu aliyehamia Chadema, Frederick Sumaye kuwa waziri mkuu katika serikali yake.
Alisema mpango wake mwingine ni kumteua Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe kuwa Waziri wa Fedha, vyeo ambavyo alidai ni kugawiana kutokana na ukanda ili waunde Serikali.
Mimi nilizunguka nchi nzima na Lowassa, nikiwa miongoni mwa timu ya watu 11 iliyokuwa ikimpigia debe ashinde, najua mipango yake mingi, namsubiri aje Geita aropoke hapo ndiyo atamjua Msukuma ni nani, nitatoa siri zake zote, alisema Msukuma huku akishangiliwa na wananchi.
Aliwataka wananchi kumpuuza mgombea huyo wa Ukawa na badala yake wananchi waelekeze nguvu zao kumchagua mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli huku akisisitiza kuwa ni muda wa Kanda ya Ziwa kumtoa rais.
Matata
Aliyewahi kuwa Meya wa Jiji la Mwanza kupitia Chadema, Henry Matata naye ametoboa siri baada ya kudai alijiunga na chama hicho akiwa pandikizi kutoka CCM na kwamba alichokipata kinatosha.
Mimi nilikuwa pandikizi wa CCM ndani ya Chadema, baada ya kuona Mbowe natekeleza Ilani ya CCM katika kipindi changu cha Uongozi wakanifukuza, alidai Matata.
Aliongeza kuwa akiwa Chadema amekaa humo na kujua matatizo na siri zote za chama hicho pamoja na matatizo yote ya Mbowe.
Hata hivyo, aliwataka wanachama wa CCM Wilaya ya Geita ambao bado wamegawanyika kutokana na makovu ya uchaguzi wa kura za maoni kuvunja makambi ili kujihakikishia ushindi katika jimbo hilo la Geita.
Mgombea
Mgombea ubunge wa Jimbo la Geita, Costantine Kanyasu alisema akichaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Geita atahakikisha makapi ya mawe yanayosadikika kuwa na dhahabu katika Mgodi wa Geita maarufu kwa jina la Magwangala yanatolewa kwa wananchi.
Alisema kilio kikubwa cha wananchi wa Geita hasa vijana wachimbaji wadogo ni Magwangala na kuahidi kama atapata ridhaa hiyo atapambana kufa au kupona ili kuhakikisha mawe hayo yanatolewa kama inavyofanyika katika migodi ya Kahama na Nyamongo.
Kanyasu alisema kero kubwa kwa wananchi wa Geita ni tatizo la maji ambalo limekuwepo kwa kipindi kirefu na kudai kwamba kabla ya kuomba ridhaa alikuwa anafuatilia tatizo hilo ambalo limeanza kutatuliwa na Serikali.
Mimi mkinipa nafasi hii nitahakikisha stendi inakuwa ya kisasa..ni muda mrefu stendi yetu mmekuwa mkiilalamikia
mvua zikinyesha yanakuwa majaluba ya mpunga..nawaahidi nitahakikisha tunakuwa na stendi inayoendana na hadhi ya mkoa wetu, alisema.
Aliongeza kuwa atahakikisha Kituo cha Afya Nyankumbu kinapatiwa gari la wagonjwa ili kuondoa kero ya kutegemea gari la Hospitali ya Wilaya ya Geita hali inayochagia vifo kwa wagonjwa.
Aliwaomba wananchi wamchague yeye pamoja na mgombea urais, Dk. Magufuli ambaye anaamini kwa uchapakazi wake Geita itabadilika na kuwa mkoa unaofanana na rasilimali iliyopo.
Dk Slaa
Katika hatua nyingine, aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya za Same, Magu na Misenyi, Mhandisi Elias Maarugu (70) amemlipua aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa kuwa si msafi wala mwadilifu akisema asiwadanganye Watanzania.
Alidai kuwa Dk. Slaa hana tofauti na dikiteta na kwamba alikuwa mzigo kwa chama hivyo wananchi wapuuze kauli zake ambazo amezitoa hivi karibuni kuhusu Lowassa.
Slaa si mwadilifu. Ameendesha chama kwa mabavu kwa sababu alikuwa hatoi nafasi kwa wanachama kujitetea ambayo ni haki ya mtu kufanya hivyo, alidai Maarugu wakati akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Bukoba na kuongeza;
Alinisingizia kuwa nimehongwa fedha na kunitaka nitoe majibu ndani ya wiki mbili nilifanya hivyo lakini alinijibu kwamba suala langu linashughulikiwa na sekretarieti ya chama kumbe ulikuwa uongo mtupu. Ni muongo na hana uadilifu wowote, alidai.
Chanzo: Jambo leo