Chachasteven
JF-Expert Member
- Jul 4, 2014
- 1,878
- 1,849
SEHEMU YA 1
Nilikamatwa na maaskari majira ya saa sita mchana kwenye mgahawa wa ENO. Nilikuwa nakula mayai huku nikinywa kahawa. Unaweza kuita kifungua kinywa kilichochelewa, kwa sababu ndiyo kwanza nilikuwa natia kitu mdomoni kwa hivyo sio sahihi kusema ni chakula cha mchana. Nilikuwa nimelowa tepe tepe na mchovu baada ya kutembea kwa mwendo mrefu kwenye mvua kubwa nikitokea kati kati ya mji hadi nje kidogo ya jiji.
Mgahawa wenyewe ulikuwa mdogo, lakini mwanga uliokuwa mule ndani ulipafanya pang’ae na kupendeza. Nilikadiria ungekuwa umejengwa muda sio mrefu sana. Meza za kulia vyakula vikiwa mbele, pembeni kulia na kushoto na jiko likiwa kwa nyuma.
Mimi nilikuwa nimekaa dirishani kushoto, nikisoma gazeti nililolikuta pale mezani kipindi naingia lililokuwa likinadi kampeni za Rais ambaye sikumpigia kura wakati wa uchaguzi mkuu uliopita na sikuwa na mpango wa kumpigia kura wakati huu pia. Nje, mvua ilikuwa tayari imeshakata ila vioo vilikuwa vimefunikwa na manyunyu na ukungu kiasi lakini haikuzuia macho yangu kuziona gari mbili za polisi zilipowasili mgahawani hapo na kuegeshwa. Muda kidogo tu baada ya gari hizo za polisi kuegeshwa, milango ikafunguka na polisi wawili wawili wakatoka kwenye kila gari kwa kasi na wepesi huku silaha zao zikiwa tayari. Bunduki mbili kubwa mkononi, bunduki mbili ndogo mkononi. Hizi zilikuwa ni silaha nzito ukiniuliza. Mwenye bunduki ndogo mmoja akajiunga na mwenye bunduki kubwa mmoja wakakimbilia upande wa mlango wa nyuma wa Mgahawa.
Nikabaki nimekaa nawatazama tu. Nilikuwa najua kila aliyekuwemo Mgahawani mule. Mpishi mmoja nyuma jikoni. Wahudumu wa kike wawili. Wazee wawili. Na mimi. Hivyo ilikuwa wazi kuwa Operesheni ambayo ilikuwa ifanyike na maaskari hawa Mgahawani hapo haikuwa ya mtu mwingine bali ya kwangu. Ni mimi ndiye nilikuwa nimeingia hapo Mgahawani muda sio mrefu nikitokea mjini. Hawa wengine, pengine nusu ya uhai wao wameitumia wakiwa ndani ya mgahawa huu na kama Askari polisi wangekuwa na shida na mmoja kati yao, basi ujio wa askari ungekuwa ni ule wa kistaarabu na upole. Wasingekuja wamebeba mabunduki. Wangekuja wakamchukuwa yule ambaye wanamuhitaji kimya kimya bila silaha. Kwa hivyo zile kasi za wale askari na mabunduki vilikuwa ni kwaajili yangu. Hilo lilikuwa halina ubishi.
Nilichukua yai langu lililokuwa limebaki nikalibugia lote mdomoni halafu nikatoa noti ya shilingi elfu 5 nikaiweka mezani. Nikalikunja kunja lile gazeti nililokuwa nalisoma nikalidumbukiza kwenye mfuko wa jaketi langu. Niliinywa kahawa iliyokuwa imebaki kwenye kikombe changu halafu nikaweka mikono yangu juu ya meza.
Wale askari wawili waliopitia mlango wa mbele wakagawana majukumu. Yule mwenye bunduki kubwa akasimama mlangoni. Akaielekeza bunduki yake usawa wa kichwa changu.Yule mwenye bunduki ndogo akawa ananisogelea karibu. Kimuonekano walionekana ni wazee wa kazi. Na nyendo zao zilikuwa makini kama tu inavyoelekezwa kwenye vitabu vya mafunzo ya mapigano na matumizi ya silaha. Ile bunduki ya mlangoni ingeweza kuhakikisha inapiga popote ndani ya kile chumba cha mgahawani. Na ile ambayo ilikuwa inakuja karibu yangu ingeweza kusanisambaratisha ubongo wangu ukatapakaa kwenye vioo vya madirisha ya mgahawani humo. Pia upande wa nyuma usingekuwa sahihi kutumia ili kukimbia. Lingekuwa ni kosa. Ile bunduki ndogo ingenikosa lakini bunduki kubwa isingeniacha salama, risasi moja tu ingeua watu wawili. Mimi na yule afisa aliyesogea kuniweka chini ya ulinzi. Mpaka hapo walikuwa wanafanya vizuri. Hakuna ubishi juu ya hilo. Bahati ilikuwa upande wao. Hakuna ubishi juu ya hilo pia. Udogo wa ule mgahawa haukuwa unaniruhusu kufanya jambo lolote hivyo niliituliza mikono yangu mezani. Yule askari alikuwa amefika karibu yangu.
“Tulia! Polisi!” Aling’aka.
Alikuwa ni kama anaepiga kelele kwa nguvu kadri alivyoweza. Nadhani ili kuondoa uwoga ndani yake na kwa wakati huo huo kunitishia nishtuke. Miondoko ya kwenye vitabu. Kelele nyingi ili umtulize na kumtisha mhalifu. Nilinyoosha mikono yangu juu. Yule askari akasogea karibu. Karibu sana. Kosa lao la kwanza. Kama ningetaka, Ningempiga mkono na kuuelekeza juu. Risasi moja ingepiga ceiling board halafu akiwa anazubaa ningemchapa kiwiko cha uso, kufumba na kufumbua bunduki yake ingekuwa mikononi mwangu. Yule askari wa mlangoni asingefanya chochote kwa sababu alikuwa ameshusha kidogo bunduki yake kwa hivyo hata ningefanya hayo yote asingeruhusu risasi itoke kwenye bunduki yake kwani ingeishia tu kumdunda mwenzie. Siku yao ingeisha vibaya sana. Lakini licha ya hayo yote, nilikaa tu hapo nikiwa nimenyoosha mikono juu. Huyu jamaa mwenye bunduki ndogo alikuwa bado anapiga makelele yake.
“Inuka ulale sakafuni” Alinishtua.
Nilitoka taratibu nilipokuwa nimekaa nikainyoosha mikono yangu kuelekea alipo. Sikuwa tayari kulala chini tena mbele ya viaskari polisi. Isingetokea kwa bahati mbaya hata kama wangekuja na idara yao nzima ya mapigano na mabunduki juu.
Jamaa alielewa, hivyo akaichomoa pingu iliyokuwa kwenye mkanda wake akanifunga mikono. Wale askari wawili waliokuwa nyuma wakaingia ndani punde tu baada ya mimi kufungwa pingu. Wakatembea hadi nyuma yangu na kuanza kunipiga parapata. Nikamuona Askari aliyenifunga pingu akitingisha kichwa kama kukubaliana nao jambo kuwa sikuwa na silaha. Akili yangu ikaniambia Askari yule ndiye alikuwa kiongozi wao.
Alikuwa fiti. Umri kama wa kwangu. Baji aliyokuwa amevaa kwenye shati yake ilimtambulisha kwa jina la PUGU. Alinizunguka halafu akanitazama machoni.
“Upo chini ya ulinzi kwa kosa la mauaji,” Aliniambia “Unayo haki ya kubaki kimya. Jambo lolote utakalolisema linaweza likatumika kama ushahidi dhidi yako. Pia unayo haki ya wakili. Kama utashindwa kumudu gharama za wakili binafsi, serikali itakupatia mmoja wa kukuwakilisha bila ya gharama zozote. Umenielewa??”
Njia nzuri ya kufikisha ujumbe. Aliongea kwa ufasaha. Hakuwa anayasoma maneno hayo kutoka kwenye karatasi. Aliyaongea ni kama mtu aliyekuwa anajua anamaanisha nini na yana umuhimu kwa kiasi gani kwake na kwangu. Sikujibu chochote.
“Umezielewa haki zako?” Alirudia tena kuuliza.
Kama mwanzo, Mimi pia sikujibu chochote. Uzoefu wa muda mrefu ulikuwa umenifundisha kitu muhimu sana maishani. Ukimya ndiyo njia sahihi. Ropoka jambo, watu wanaweza wakusikie vibaya. Usieleweke. Utafsiriwe ndivyo sivyo. Inaweza ikufanye uonekane una hatia. Na mbaya zaidi inaweza ikasababisha ukauliwa. Hata hivyo, kukaa kimya huwa kunawakera sana askari. Ni wajibu wake kukuambia kuwa unayo haki ya kukaa kimya lakini anachukia pindi unapoitumia hiyo haki yako. Mimi nilikuwa nimewekwa chini ya ulinzi kwa kosa la mauaji lakini sikuwa tayari kusema chochote.
“Unazielewa haki zako?” jamaa mwenye jina la Pugu aliniuliza tena. “Unaongea Kiswahili?”
Sikusema chochote. Akatulia. Alitulia kama mtu ambaye wakati wake wa hatari ulikuwa umekwisha kupita. Kwanza kwanini ajali, maana angenipakia kwenye gari tukaenda kituoni halafu nikawa mzigo wa mtu mwingine. Aliwaangalia wenzie.
“OK, andika hajasema chochote,” Alilalama. “tuondoke”.
Tulianza kutembea kuelekea ulipokuwa mlango. Tuliunda mstari mmoja ili tupite vizuri kulingana na udogo wa mlango. Alianza Pugu. Halafu jamaa mwenye bunduki kubwa, akawa anatembea kinyume nyume huku bunduki yake akiwa kaiweka tayari kunifyatua kichwa. Baji yake ilimtambulisha kama Stevenson. Alikuwa fiti. Mweupe. Nyuma yangu walisimama wale askari wawili waliokuwa nyuma ya mgahawa. Ghafla nikasukumwa kwa nguvu kutoka nje ya mlango.
Nje, eneo la maegesho joto lilikuwa juu. Lazima mvua ingekuwa imenyesha usiku wote na asubuhi yote. Ni sasa hivi jua ndiyo lilikuwa linachomoza na ardhi ilikuwa inatoa mvuke. Kikawaida, hapa pangekuwa na vumbi sana. Lakini leo palikuwa panatoa mvuke baada ya mvua kunyesha na kusafisha mazingira na kuyafanya yawe ya kuvutia sana. Nililiangalia jua halafu nikavuta hewa nyingi sana kwenda ndani. Nilijisikia vizuri. Kumuona Stevenson bado yupo mbele yangu na bunduki yake kuliirejesha akili yangu kwenye tukio lililokuwa mbele yangu. Nilishtukia kichwa changu kinabonyezwa kwenda ndani ya mlango wa gari wa nyuma halafu nikasukumwa kuingia ndani. Miondoko ya kwenye vitabu. Si ajabu sana kwa sababu kwenye mji ulio mbali na sehemu yoyote ya mjini, unategemea kuona nini zaidi ya nadharia nyingi kuliko vitendo.?
Milango ililokiwa nikawa mwenyewe nyuma ya gari. Pugu na Stevenson walikuwa siti za mbele. Stevenson akageuka ili kunitazama kwa ukaribu. Hakuna aliyemuongelesha mwenzake. Pugu alianza kuendesha gari. Nyuma yetu gari la wale askari wengine wawili nao walianza kutufuata. Gari zilikuwa mpya. Safi na nzuri kwa ndani. Hakukuwa na alama au viashiria kuwa watu wengi sana walikuwa wamekwishaipanda na kukalia kiti nilichokuwa nimekalia.
Niliangalia nje ya dirisha. Geita. Niliiona ardhi tajiri. Ardhi nyekundu iliyozungukwa na vichaka na miti miti kama katani. Yalikuwa mananasi au majaruba ya mchele labda. Si mengi sana, ila naamini yana manufaa sana kwa mpandaji au mmiliki. Ni watu ndiyo walikuwa wamiliki halali wa ardhi? Au makampuni? Sijui.
Safari yetu haikuwa ndefu sana kuelekea mjini. Baada ya dakika kama 20 nilianza kuona majengo mawili makubwa mapya. Moja likiwa ni kituo cha polisi na lile la pili likiwa ni makao makuu ya zima moto kwa mkoa. Yalikuwa yanavutia. Majengo mazuri katika bajeti ndogo. Bara bara zilikuwa zinavutia. Takribani kama hatua thelathini kusini niliona jengo jeupe kama kanisa kwa sababu lilikuwa na msalaba kwa juu. Nyuma yake kulikwa na majengo kadhaa. Kila kitu kilivutia kutazama. Jamii iliyoendelea iliyojengwa kutokana na kodi za wananchi. Safi.
Stevenson alikuwa bado ananiangalia kipindi ambacho Pugu alikuwa analiingiza gari kwenye maegesho ya kituoni hapo. Niliangalia kushoto nikaona ubao mpana uliosomeka : Kituo Kikuu Cha Polisi Geita. Nikajikuta nawaza: Hivi natakiwa kuogopa? Nipo chini ya ulinzi kwenye mji ambao sijawahi kuwepo hapo kabla katika maisha yangu yote. Tena kwa kosa la mauaji. Ila nikiwa nawaza nikajifariji tena. Kwanza, hawawezi kuthibitisha kuwa jambo limetokea na wakati halijatokea. Na pili, Sikuwa nimeua mtu kwa muda mrefu sasa.
Kusoma sehemu ya pili bonyeza HAPA.