Analyse
JF-Expert Member
- Jan 19, 2014
- 17,641
- 47,660
MUAFAKA -1
Wakati Edward anafika kwenye kituo cha mabasi yanayotoka Arusha kwenda Dar es Salaam, basi lililokuwepo tayari kwa safari ni moja, mengine yote yalikwishaondoka. Hakuwa na wasiwasi, kwani alikuwa tayari amekwishakata tiketi yake tangu siku iliyopita. Wapiga debe walimzogoma kwa kuwahi wamkatie tiketi.
Aliwajulisha kuwa yeye tayari amekwisha kata. Mkononi mwake alinyanyua sanduku la wastani lenye-mabaka mabaka.
Aliingia ndani ya gari taratibu na kutafuta nafasi iliyokuwa tupu kwenye sehemu za kuwekea mizigo na kupandisha sanduku lake, Kisha akatia mkono
kwenye mfuko wa shati, akatoa tiketi yake na kuiangalia.
Kiti chake kilikuwa na nambari 30 upande wa dirishani.
Gari hili lilikuwa aina ya viti viwili viwili kila pande.
Akaangaza macho huku na huko, kwa madhumuni ya kukiona kiti nambari 30, na tegemeo ni kukiona kiti hicho kitupu, hakikukaliwa na mtu sababu kiti chenye nambari hiyo ni chake yeye. Lakini badala yake tayari kiti hicho kilikuwa kimekaliwa na msichana mmoja mrembo.
Aliangalia tena tiketi yake aliyokuwa nayo mkononi kuhakikisha kuwa nambari 30 ni yake kweli.
Akaona ni kweli yake. Alimwendea yule msichana na kumuomba radhi ampishe kwenye kiti chake.
"
Samahani dada, naona kiti hiki ni changu." Edward aliomba kwa heshima na unyenyekevu.
"Kiti hiki ni changu kaka, angalia vizuri tiketi yako"
Msichana yule alijibu bila wasiwasi na kuendelea kujiweka vizuri juu ya kiti.
Edward aliangalia tena tiketi yake na kwa hilo hakuwa na shaka yeyote kuwa tiketi nambari 30 na kiti chenye nambari hiyo ni chake. Kwa hiyo, aliitoa ile tiketi yake na kumkabidhi yule msichana huku akisema: "Hebu tafadhali dada nisaidie kuisoma hii tiketi, huenda nimekosea. Hiyo siyo nambari 30?"
Msichana yule aliipokea na kuisoma, kisha naye akatoa yake na kumkabidhi Edward huku naye akisema:
"Hebu na mimi isome hii yangu kama sikukosea ni nambari 30 nayo pia…Mimi ndio nimekwishakaa hivi, sasa wewe ni bora umtafute kondakta akutafutie kiti cha kukaa kabla gari halijaondoka"
Yule msichana alimshauri Edward.
Edward alimtafuta kondakta na kumueleza hali halisi ilivyo kati ya yeye na yule msichana, na kuhusu kukatiwa tiketi nambari ya kiti kimoja.
Kondakta yule alikuja mpaka pale karibu na viti alipokaa yule msichana. Akaomba aoneshwe tiketi zote mbili. Baada ya kuzikagua na kulinganisha na karatasi ya orodha ya majina ya abiria aliyokuwa nayo, aligundua kuwa tiketi nambari 30 ni ya Edward, na yule msichana alikatiwa tiketi nambari hiyo kwa makosa.
Baada ya mjadala mrefu, Edward alikubali kumwachia yule msichana kiti na yeye atafutiwe kingine. Edward alipatiwa kiti nambari 31, ambacho ni ubavuni mwa yule msichana.
Kwa hiyo walikaa pamoja, lakini kila mtu na kiti chake.
* * * *
Edward ni mtoto pekee wa Bwana na Bibi Jonathan Oloi.
Ni kijana mrefu wa kimo, maji ya kunde na mwenye sura jamali. Ni mcheshi sana pale panapo stahili na ni mkimya mno pale ambapo hastahili kusema.
Ana umri wa miaka 27. amemaliza elimu ya sekondari kidato cha sita, na baada ya hapo alipata nafasi ya kwenda Australia.
Huko alijiunga na chuo cha taaluma ya upigaji picha, Utengenezaji na uhariri wa filamu fupi za matangazo ya biashara.Alichukua taaluma hiyo kwa muda wa miaka mitatu.
Baada ya kurudi, aliajiriwa na shirika la kigeni kwa muda wa miaka minne.Mkataba wa shirika hili ulikwisha na baada ya kukaa bila kazi kwa takribanimiezi sita.
Sasa amepata ajira nyingine ambayo makao yake makuu ni Dar es Salaam.
Kwa hiyo siku hiyo alikuwa anasafiri kutoka Arusha ambako ndio kwao, na kuelekea Dar es Salaam kwa ajili ya ajira hiyo.Mzee Jonathan Oloi, baba yake Edward hakuwa mchache wa fedha.
Alikuwa anazo biashara zake ndogo ndogo. Anayo mashamba makubwa ya kahawa, na mifugo ya kutosha.
Kwa kuwa mtoto wake alikuwa ni huyo huyo mmoja tu, hivyo (Edward au Edo) walikuwa naye karibu wakati wote.
Mzee Oloi hakupendelea suala la kijana wake kufanya kazi za kuajiriwa. Lakini Edo mwenyewe alikuwa anapenda mno kazi yake ya kupiga picha za filamu fupi za matangazo ya biashara. Zaidi ya yote hayo, Bwana Jonathan Oloi na mkewe walikuwa wanataka mno mtoto wao wa pekee aoe, waliweza
kumtafutia mchumba ambaye waliona kuwa atafaa.
Kwa kuwa wazazi wa binti huyo hawakuwa na uhusiano wa mbali na familia ya marehemu baba yake Mzee Oloi, mazungumzo yalifanywa na wazazi wa pande zote mbili, tangu Edo alipokuwa Australia na walikubaliana.
Baada ya Edo kurudi toka ngámbo, kabla hata hajaanza kazi, alijulishwa habari hizo. Edo alikataa na kutaka afanye kazi kwanza.Ajira yake ya kwanza ilipokwisha alikaa nyumbani kwa muda wa miezi sita.
Suala la yeye kuoa lilizungumzwa tena na akatakiwa na wazazi wake akubali mchumba aliyechaguliwa na afunge ndoa. Lakini Edo alikataa kabisa na kusema,
"Sikilizeni wazee wangu, mimi bado sijawa mkubwa wa kukimbilia kufunga ndoa hilo mosi. Pili, hata kama naamua kuoa basi nitaoa mke niliye mchagua mimi mwenyewe niliye mpenda.
Sintaoa mwanamke ambae hata hatujajuana, ni wazazi tu wamekaa na kupanga. Nitatafuta mwenyewe mke wa kuoa."
Kwa vile ni mtoto pekee, Edo alikuwa na sauti sana kwa wazazi wake, isitoshe walimlea ki ujukuu. Baba yake Edo alimwambia mwanae,
"Edo mwanangu, ingawa wewe mwenyewe unajiona u mdogo, bado hujawa wa kuoa, lakini sisi wazazi wako tunajiona kuwa tu wakubwa sasa, tuna hamu na wajukuu. Kwa kuwa mtoto wetu ni wewe tu, basi ndio maana tungependa uoe kabla Mungu hajamchukua hata mmoja wetu."
Mama yake Edo naye alimrai mwanae pia kwa kusema,
"Edward fahamu sisi ni wazazi wako, isitoshe wewe uko pekee yako, hivyo pendo letu lote lipo kwako. Unadhani sisi tunaweza kukupa chochote kilicho kibaya kwako.Haiwezekani hivyo basi mchumba tulie kutafutia, tunaamini atakufaa na anatoka katika familia inayofanana na yako. Ukoo huo kwa mbali unahusiana na babu zako. Mwanangu fikiri sana jambo hili."
Edo aliwasikiliza wazazi wake kwa makini kisha naye akatoa rai zake pamoja na maombi kwa kusema.
"
Baba na mama wapendwa, kwa kuwa furaha yenu ni kuniona mimi nimo ndani ya furaha, hilo ninalikubali wala sina shaka nalo. Na mchumba mlie mtafuta kwa ajili yangu naamini mmefikiria sana mpaka kumpata. Na ninyi na wazazi wake mkaamua mpange mpango wa mimi na huyu binti tuoane, vema. Lakini je mmepata kusikia kauli yeyote ya huyo binti kuhusu mpango huu?".
"Hapana" Walijibu kwa pamoja.
"Kwa hiyo hamuoni wazazi wangu kuwa ninaweza nisiwe na furaha katika ndoa yangu endapo huyu binti atakubali tu kuolewa kwa kuwaridhisha wazee wake? Huenda asinipende kama mnavyotaka ninyi. Kwa nini nisipewe nafasi ya kuchagua mchumba mimi mwenyewe? Iwapo furaha yenu ndio yangu,
basi tafadhali naomba mnipe muda, angalau wa miezi michache nitafute mchumba mimi mwenyewe."
"Ina maana ukatafute huko Dar es Salaam uliko pata kazi?" Baba yake aliuliza.
"Popote pale katika ulimwengu huu baba, mradi tu mwanamke huyo aniridhi nafsi yangu"
Wazazi wake Edo walitulia kimya, baadaye kidogo mzee Oloi alimwambia mwanawe,"Kama hivi tunavyosema, tulikwisha panga na tunajua linalokufaa ni nini.
Hivyo basi tunakupa nafasi hiyo ya kuchagua mchumba atakae kufaa mwenyewe, lakini itakapotimu miezi sita, kama bado hujapata wa kumuoa, basi rudi uje uoe huyu tuliye kuchagulia, sababu sintavunja uchumba huu mpaka wewe umeoa."
"Sawasawa baba nimesikia."Hayo yalikuwa ni mazungumzo ya mwisho kati ya Edward na baba yake na mama yake, kabla ya kuondoka Arusha kuelekea Dar es Salaam.
* * * *
Gari lilianza kuondoshwa taratibu kutoka stendi ya mabasi ya Arusha. Kilometa chache baada ya kutoka hapo, walifika Usa River. Edo baada ya kuhakikisha kuwa sasa hana wasiwasi hapo alipokaa aligeuza kcihwa chake kumuangalia msichana aliyekaa naye karibu.Kwa mara ya kwanza alitambua kuwa ni mzuri, kwa hali halisi ya uzuri utakikanavyo, hasa wa kisasa.
Pamoja na kuwa msichana huyu alikuwa amekaa juu ya kiti cha basi, alionyesha dhahiri kuwa ni mrefu, alikuwa mwembamba, mweusi wa wastani na nywele zake zilizotengenezwa ki unadhifu zilikuwa zimeteremka hadi mabegani kwake.
Edo alishikwa na hamu ya kutaka kumjua zaidi.
Msichana huyo aliyekuwa kiti cha dirishani, alionekana kupendezewa zaidi na yanayopitwa na gari huko nje, kuliko mvulana aliyekaa naye karibu. Edo alijikohoza kidogo na kusema,
"Samahani dada, ni vizuri tukafahamiana, kwa vile tunasafiri pamoja. Mimi jina langu ni Edo Oloi, ni mwenyeji wa Arusha, na ninaelekea Dar es Salaam."
Alitoa tabasamu kubwa wakati akisema hivi, na yule msichana aligeuza uso kumtazama, alitabasamu naye pia, akajibu,
"Mimi jina langu ninaitwa Lulu Frank, naelekea Dar"
"Vizuri sana, inaonekana tutakuwa pamoja safari yote"
"Mungu akipenda"alijibu Lulu kwa ufupi.
Baada ya hapo walikaa kimya kipindi kirefu, gari ikiwa inakata mbuga tu. Waliwasili Moshi. Baada ya muda mchache safari ilianza tena.
"Bi Lulu, Dar es Salaam ndiko unakoishi?"
"Ndio, ninafanya kazi, au tuseme ninakwenda kuanza kazi."
"Ahaa, hali kadhalika na mimi, ninakwenda kuanza kazi."
Walinyamaza tena kimya, baadae kidogo, Edo alianza kusema kwa hamu kubwa ya kutaka kumfahamu zaidi Lulu, kwa kumwambia,
"Lulu naomba unisamehe tafadhali, kabla sijakuuliza swali ambalo ni la kibinafsi kabisa."
Lulu alimtazama Edo kwa sura iliyojaa wasiwasi baada ya kusikia hivyo ilibidi amuulize Edo,
"Ni swali gani hilo? Mbona unanitisha!!"
"Hapana, usiogope kabisa, swali lenyewe ni la kawaida sana, lakini ni kwa watu wanaojuana, kwa wasiojuana kama hivi mimi na wewe, ni lazima tuombane radhi kwanza"
" Sawa, Bwana Edward, niko radhi, niulize tu."
Edo kusikia hivyo alitulia kidogo na kuinamisha uso wake chini kama vile amesahau swali alilokuwa anataka kumuuliza Lulu, kIsha kwa ghafla alimtazama usoni na kumuuliza,
"Hivi Lulu umekwisha olewa? Au tusemee… una mume? Au mchumba?."
Lulu alitoa tabasamu kubwa lililomfanya aonekane mrembo zaidi na kujibu,
"Hapana, bado sijaolewa. Sina mume wala mwanaume na… pia sina mchumba."
"Je una umri gani?"
"Miaka ishirini na mbili, kwa nini? Mbona unaniuliza umri wangu?"
"Sababu, jinsi ulivyo. Nina maana umbo lako zuri, sura yako nzuri, haiyumkini msichana kama wewe kuwa huna mume, mwanaume wala mchumba mpaka wakati huu."
"Basi nisemayo ni yakini, sina uhusiano wa kimapenzi na mwanamume yeyote."
"Kwa kukosa au kwa kupenda?"
"Kukosa ni vipi na kupenda ni vipi?" Lulu aliuliza swali hili huku akicheka cheka."Kukosa ni kuwa hakuna mtu aliyewahi kukutaka kama rafiki yake, nina maana hakuna mwanamme. Kupenda nako ni kuwa unatakiwa na wavulana lakini wewe hutaki…huwataki kwa urafiki, mapenzi na wala kuoana nao."
Lulu aliangua kicheko akacheka sana, kiasi cha kumpa tamaa Edo hata akaona sasa amekwisha upata mwanzo wa uzoefu na Lulu, jambo ambalo amelidhamiria. Lulu alimtazama Edo na kusema,
"Unasikia Edo, ni kweli sina mvulana yeyote kwa kukosa."
"Siyo kweli! Una maana hujawahi kutakiwa na mvulana yeyote maishani mwako!!"
"Ndiyo ninatakiwa takriban kila siku ya maisha yangu, tangu nipate fahamu, lakini hao wavulana wanaonitaka sio kwa dhati ya urafiki au kunioa, bali dhamira zao kwangu ni kuchezeana tu, jambo ambalo siko tayari nalo…Mmoja kati ya walionitaka, alikuwa na dhamira ya kunioa, lakini kwa kupitia kwa wazazi wake yaani ndoa ya kupangiwa; na mimi ningependa kuolewa na mvulana ambaye ninampenda. Bahati mbaya sijawahi kupenda mvulana yeyote kimapenzi hasa kama msichana na mvulana.
Nadhani nimejieleza vya kutosha!"
Lulu alimalizia kwa kutabasamu huku akimuangalia Edward ambaye wakati huu alikuwa ametulia na kumsikiliza Lulu kwa makini sana kama vile mjukuu anayesikiliza hadithi aipendayo toka kwa bibi yake.
"Kiasi umejieleza. Hujawahi kupenda… kama mimi. Hupendi ndoa za kupangiwa… pia kama mimi, na umepewa nambari ya kiti cha gari nambari 30, vilevile kama mimi! Sijui ni lipi jingine?"
Edo alisema maneno haya kwa sauti ya uchovu na kujaribu kumfanya Lulu aamini kuwa mambo yao mengi yanafanana.
"Ina maana wewe pia Edo hujawahi kupenda?"
"Hapana, kabisa… sijapenda mtu."
"Na… pia hupendi ndoa za kupangiwa!!" Sauti ya chini ilisikika iliyokuwa na mchanganyiko wa maelezo na swali.
"Hivi nisemavyo, nimetoka kumkatalia baba yangu na mama yangu walionizaa kunioza mke waliyemchagua wao."
"Na kwa nini katika umri ulio nao bado hujapenda msichana tu."
"Kwa sababu bado sijakutana na msichana ambaye… tunapendana."
"Mungu atakupa."
"Aamen."
* * ***
Safari ya MUAFAKA imeanzia hapa……..TUKUTANE tena kesho