Simulizi: The Blood at Midnight(Damu usiku wa manane)

Simulizi: The Blood at Midnight(Damu usiku wa manane)

Kanungila Karim

JF-Expert Member
Joined
Apr 29, 2016
Posts
20,745
Reaction score
25,676
Mtunzi:Erick Shigongo



Mawingu yalikuwa yametanda katika anga lote la jiji la Dar es Salaam, haikuwa kawaida kwani jiji hilo lilisifika kwa joto kali. Manyunyu ya mvua yalikuwa yakidondoka taratibu baada ya mvua kubwa kuwa imekatika kama nusu saa hivi kabla. Barabarani kulikuwa na msongamano mkubwa mno wa magari, hali iliyojitokeza kila mara mvua iliponyesha. Pamoja na mawingu hayo, si watu wengi sana waliovaa makoti kwa madai kuwa hali ya hewa ya Dar es Salaam ilikuwa haitabiriki, wakati wowote jua lingechomoza na joto kupanda.

Kwenye kiti cha nyuma cha moja ya mabasi yafanyayo safari kati ya Kariakoo na Mwenge, ambayo wengi huyaita daladala, waliketi wasichana wawili warembo kupindukia, wote wakiwa wamevaa miwani ya jua ingawa halikuwepo. Kwa kuwatazama tu mtu yeyote angejua aidha walikuwa wafanyakazi mahali fulani au wanafunzi wa Chuo Kikuu. Haukuwa uongo, Katarina na Deborah walikuwa ni wanafunzi wa Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ‘Mlimani’, walipanda basi hilo kuelekea Mwenge ambako wangechukua basi jingine dogo la kuwapeleka hadi chuoni kwao.

“Umekisoma kitabu hiki?” Katarina alimuuliza rafiki yake.
“Kitabu gani?”
“The Blood at Midnight?”
“Kimetungwa na nani?”

“James Mwang’amba”
“Yule Mwandishi maarufu wa vitabu duniani?”
“Ndiyo”
“Hebu, wewe umekisoma?”
“Nimekimaliza leo”
“Kinaeleza juu ya nini?”

“Juu ya mwanamke aitwaye Judith Mchome”
“Judith Mchome yupi? Rais wa Jamhuri ya Kasomeko?”
“Ndiyo!”
“Anaelezea nini?”
“Historia yake, jinsi alivyoanza safari yake kuelekea Ikulu akiwa kahaba, akiuza mwili wake mtaani hatimaye akafanikiwa kuingia Ikulu na kuwa Rais wa nchi, kinatia moyo sana, huwezi kuamini kina kurasa mia tano na ishirini lakini nimekisoma siku tatu tu! Usiku wa kuamkia leo sijalala, ukishakishika huwezi kukiweka chini!”

“Kweli?”
“Kabisa, niazime basi na mimi nikisome!”
“Chukua, ila ukitunze, maana ninyi waswahili mkiazimishwa vitabu huwa hamjui kurudisha, ukikipoteza tu tutagombana”
“Nitakitunza shosti”
“Haya chukua” Katarina alisema akimkabidhi Deborah kitabu hicho.

Bila kupoteza wakati, basi likiwa limefika maeneo ya Moroco likikata kona kuelekea Mwenge, Deborah alikifunua kitabu hicho ukurasa wa kwanza na kusoma maandishi yaliyoandikwa, “Chapter one, From a hooker to President” moyo wake ukapiga, maneno hayo peke yake yalitosha kabisa kumfanya asinyanyue kichwa chake kuangalia nje, akitaka kujua nini kilitokea mpaka kahaba huyo muuza mwili kujikuta amekuwa Rais wa nchi.

***
“Baba yetu uliye mbinguni, jina lako litukuzwe, ufalme wako ufike, utakalo lifanyike duniani kama mbinguni, utupe leo riziki yetu ya kila siku…utusamehe makosa yetu…” Ilikuwa ni sauti ya Daniel Mchome, ambaye pamoja na kuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Jamhuri ya Kasomeko, alikuwa mcha Mungu kupita kiasi, ndivyo alivyoelelewa na alitaka arithishe tabia hiyo kwa watoto wake wawili, Judith mwenye umri wa miaka kumi na John mwenye umri wa miaka mitano.
Walipomaliza kusali tu, Judith aliaga na kuondoka kuelekea chumbani kulala, alikuwa amechoka baada ya kufanya kazi za shule na asubuhi sana dereva angefika kumchukua ili waende shuleni. Alikuwa mwanafunzi wa darasa la tano katika shule ya msingi ya kimataifa ya Martin Luther King, iliyokuwa katikati ya jiji la Nyamadoke, makao makuu ya nchi ya Kasomeko.

Daniel na mke wake Anastazia waalibaki sebuleni pamoja na mtoto wao John, aliyekuwa amejilaza miguuni kwa mama yake, akiwa katikati ya usingizi. Walikuwa wakiongea hili na lile kuhusu nchi yao, Daniel akimweleza mke wake jinsi hali ilivyokuwa tete, wananchi wakiandaa maandamano ya kupinga serikali yao kwa madai kuwa ilikuwa ikiendeshwa bila kujali maslahi ya wengi, ufisadi ulikuwa umeongezeka, kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya maendeleo ya nchi ziligawanwa na wachache huku mamilioni ya watu masikini nchini humo wakiteseka na kufa hata kwa magonjwa yaliyoweza kuzuilika.
“Lakini kweli ninyi viongozi mnakula? Mbona mimi sijawahi kuona umeleta fedha hapa nyumbani? Huwa unapeleka wapi? Au una nyumba ndogo Daniel?”

“Acha utani mke wangu, unajua siwezi kufanya hivyo, hakuna kinachoniudhi duniani kama wizi na dhuluma ya mali ya Umma, niliingia katika siasa kuwatumikia wananchi si kwa lengo la kujitajirisha, lengo langu lingekuwa hilo tusingeishi maisha hay…” Alisema Daniel lakini hakumalizia sentensi yake baada yakusikia milio mingi ya risasi nje ya nyumba yake.
Alipochungulia kupitia dirishani alishuhudia lango kuu likivunjwa, walinzi wakapigwa risasi na kuanguka chini! Walikuwa ni wananchi wa jiji la Nyamadoke waliovamia nyumba yake, wakiimba nyimbo za kimapinduzi na kusema “Wafe, wafe na familia zao, tutokomeze utawala wa kidhalimu na kuingiza madarakani utawala wa watu”

“Mke wangu, tumevamiwa, sidhani kama tutapona! Bila shaka huu ndiyo mwisho wetu, watu hawa hawatatuacha hai” Daniel aliongea, kabla hajafanya lolote mlango ulipigwa risasi na kufunguka, watu zaidi ya hamsini wakaingia hadi sebuleni na kuanza kumimina risasi nyingi.
 
SEHEMU YA 02


Daniel Mchome ni Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje katika serikali ya Jamhuri ya Kasomeko, baba wa watoto wawili (Alice na John), mume wa mwanamke mrembo aitwaye Anastazia. Ni kijana mwenye matarajio makubwa maishani mwake, akiamini siku moja angeweza kuwa Rais wa Jamhuri hiyo ambayo hivi sasa imegubikwa na suala la ufisadi, viongozi wachache walioko madarakani wakijitajirisha na kuwasahau walio wengi ambao ni wananchi masikini wa nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa madini na maliasili.


Daniel ni kiongozi muadilifu, hajawahi kula rushwa maishani mwake, anaamini yeye ni mtumishi wa watu ingawa anaponzwa na viongozi wenzake sababu ya ule msemo usemao Samaki mmoja akioza wote wameoza. Mke wake hajawahi kumwona na fedha zozote nyingi nyumbani, waliishi kwenye nyumba ya serikali wakiwa bado hawajajenga hata kibanda.

Kwa muda mrefu wananchi wa Kasomeko waliishi hivyo, wakiumia tu ndani ya mioyo yao, wakiwa wamejawa na hofu na kushindwa kufungua midomo yao kuongea chochote wakiamini wangeuawa au kufungwa na watawala. Lakini siku hiyo Daniel akiwa ndani ya nyumba yake, baada ya ibada kabla hawajaenda kulala, Alice peke yake ndiye akiwa ameondoka na kuwaacha wazazi wake pamoja na mdogo wake John wakiongea, kelele zilisikika nje ya nyumba yao.

Daniel alipochungulia nje kupitia dirishani aliona makundi ya watu wenye silaha za jadi pamoja na bunduki, wakiimba nyimbo za kimapinduzi na kutamka maneno kama “Wafe, wafe na familia zao” hofu nyingi ikamwingia, akajua tayari wananchi walikuwa wameamua kuchukua sheria mkononi na kufanya mapinduzi ya kiraia. Akamgeukia mke wake, huku akiwa na wasiwasi mwingi na kumweleza kuwa huenda huo ndio ungekuwa mwisho wao.
Kabla hawajafanya lolote mlango ulipigwa risasi, ukafunguka na kundi la watu wengi kuingia ndani.
Je, nini kitafuata? SONGA NAYO…


Wote walikuwa wakitetemeka wakiwa wamechuchumaa mbele ya watu wakatili, ambao nguo zao zilijaa damu kuonyesha kuwa huko walipotoka walikuwa wameua watu wengi mno. Daniel alijaribu kuwaomba wasimuue kwa sababu yeye hakuwahi kufanya jambo lolote baya, alikuwa masikini kama wao sababu ya kuwatumikia wananchi. Hakuna aliyemsikiliza, mmoja wa watu hao akamsogelea mke wake akamnyang’anya mtoto na kumtupa pembeni bila huruma, mtoto akaanza kulia lakini hakuna aliyemjali.
“Vua nguo zako zote!”
“Mimi?” mke wake Daniel aliuliza.
“Naongea na nani?”
“Mimi?”
“Vua, au unataka nikumiminie risasi?”

Anastazia akamwangalia Daniel kwa macho ya huruma kama vile alikuwa akiomba kibali cha kuvua nguo, Daniel hakusema chochote, alikuwa na uwezo wa kumwambia avue lakini hakutaka kufungua mdomo wake akielewa kabisa kitu ambacho wauaji hao walitaka kufanya mbele ya macho yake. Mwisho akatingisha kichwa kwa ishara ya kukataa mkewe asivue nguo zake, hapo ndipo kiongozi wa watu hao akawaamuru vijana wake wamvue kwa nguvu, nguo zote zikachanwa ndani ya dakika mbili tu, Anastazia alikuwa uchi wa mnyama. Huku akilia Daniel alinyanyuka mahali alipoketi, akapigwa na kitako cha bunduki na kurudi chini, hata hivyo, akivuja damu nyingi kutoka upande wa kulia wa jicho, aliweza kunyanyuka tena na kutembea akimfuata kiongozi wa watu hao.
“Brigedia Kachenje!” akaita.

“Toka hapa! Vitu vizuri mnataka mle peke yenu?” alifoka kipande cha mtu aliyekuwa na bunduki aina ya AK47 iliyojazwa risasi za kutosha, akimtisha nayo Daniel.
“Niliapa mbele ya Padri nitamlinda mke wangu, katu sitakuruhusu umwingilie mbele ya macho yangu nikiwa hai, naomba niwe wa kwanza kufa ndio mfanye mambo mnayotaka kumfanyia mke wangu!” Daniel aliongea huku akibubujikwa na machozi, dunia ilikuwa imebadilika, mtu ambaye siku zote aliishi vizuri akiwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje ndiye aliyekuwa akilia mbele ya kiongozi wa Jeshi.

“Mwondoeni hapa huyu!” Brigedia Kachenje alisema, Daniel akakamatwa na kuanza kuvutwa huku akimwona Brigedia Kachenje akifungua vishikizo vya suruali yake, akaivua na kuitupa pembeni kisha kupiga magoti katikati ya miguu ya Anastazia.
“NOOOO!NOOOO!” Daniel alipiga kelele na kunyanyuka kwa nguvu akiwasukuma watu waliomshikilia, pamoja na kuwa Waziri, alikuwa ni mtu wa mazoezi kupita kiasi, mwili wake ulikuwa umekaa vizuri kwa mapambano! Akawaangusha wote na kuanza kukimbia kumfuata Brigedia Kachenje, ambaye tayari alishalala juu ya kifua cha Anastazia, kabla hajamfikia, risasi ilimpenya shingoni, akaanguka chini akivuja damu nyingi, hapo hapo akatulia. Kilichofuata baada ya hapo yeye hakukielewa.

Milio ya risasi ilimshtua Alice usingizini, akanyanyuka na kunyata kutoka chumbani akielekea sebuleni, hakujua kama risasi hizo zilikuwa zikilia ndani ya nyumba yao! Akawaona watu wengi wamesimama wakiwa wamemzunguka mama yake aliyelala chini, kulikuwa na kitu kilichoendelea kwenye mduara huo ambao hakutaka kabisa kukubali kwamba kilikuwa kikitokea. Akarejea ndani haraka akilia na kufungua sanduku la nguo, akatoa nguo zote na kuzitupa kitandani kisha yeye kuingia ndani yake na kujifunika, akiacha sehemu ndogo tu ya kupumulia.

Ndani ya sanduku hilo aliendelea kulia huku akimwomba Mungu atende muujiza, alifundishwa kusali kila alipokuwa na tatizo ili apate msaada wa Mungu. Machozi yalikuwa yakimbubujika, hakujua mahali baba yake alipokuwa na pia hakuelewa ni nini kilikuwa kimetokea. Baadaye watu hao waliingia mpaka chumbani, akasikia wakifunua magodoro na kuangalia uvunguni, wakilipita sanduku bila kujua ndani yake kulikuwa na mtu, ilionekana wazi hawakuwa na shida na nguo.

Walipomaliza upekuzi walitoka nje na kumwacha Alice akiwa ndani ya sanduku, bila kuamini kama alinusurika. Hakutoka humo mpaka saa nzima baadaye ndipo akajitokeza, baada ya kusikia sauti ya mdogo wake akilia. Fikra zake zikamtuma kuamini huenda wazazi wake walikuwepo sebuleni, akatoka na kunyata taratibu hadi sebuleni. Alichokiona, hakika aliapa kutokisahau maishani; wazazi wake walikuwa wamelala sakafuni wakivuja damu nyingi, mdogo wake John aliketi katikati yao, kwa umri mdogo waliokuwa nao hakuelewa kilichotokea.
“Baba!Baba!Babaa!” aliita akimtingisha baba yake.
“Mwa…nangu na…kufa…lete kalamu na kara…tasi, niku..pe majina ya watu waliof…anya hivi, fan…ya har…aka!” Aliongea kwa taabu kubwa Daniel na Alice akanyanyuka na kukimbia hadi chumbani kwake, akimwacha mdogo wake John analia.

Aliporejea alikuwa na kalamu na karatasi, akaketi kando ya baba yake ambaye bado alikuwa akihangaikia hewa, akitupa kichwa chake huku na kule kama mtu aliyekuwa akikata roho.
“Andika Bri…gedia Kache…..nje, Meja Jenerali Paul Lugazi, Kanali Emmanuel Ntemin….yanda na Brig…edia Bashw…eka Kaj…igiri, mwa…nangu hawa ndio walio…fanya uka….tili huu, ukifan…..ikiwa maish…..ani mwako kuf…ika juu, kama hawa…..takuua basi uta….jua cha kufan…..ya mwa….nangu, umenisikia mwanangu?”
“Ndiyo baba!”
“Mtunze md….ogo w…ako, mimi na mama yenu tunata…ngulia…ikiwezekana torokeni muende Tanz….ania, hu…ko ku…na usal…ama,” Daniel alimaliza na shingo yake kuanguka upande.

Alice alilia mbele ya maiti za wazazi wake, kwa mara ya kwanza ndiyo alikuwa ameona mtu akiwa amekufa tena kifo cha kikatili. Roho ilimuuma mno, kuondokewa na wazazi ni kitu ambacho hakuwahi kufikiri kinaweza kutokea kwake. Kwenye umri wa miaka kumi alikuwa na uwezo wa kuelewa umuhimu wa wazazi katika maisha. Alichofanya ni kutoka ndani ya nyumba yao, kwenda kugonga nyumba ya jirani akiomba msaada, hawakuwa tayari kumfungulia, risasi zilikuwa bado zikiunguruma.

Akalazimika kurejea tena ndani ya nyumba yao kujificha mpaka siku iliyofuata asubuhi, akimwomba Mungu na kuangalia kwenye luninga ambako ilitangazwa kuwa serikali ya Jamhuri ya Kasomeko ilikuwa imepinduliwa na wananchi wa nchi hiyo ambao kwa pamoja waliamua kumweka Brigedia Kachenje madarakani ili aiongoze nchi hiyo mpaka utakapoitishwa Uchaguzi Mkuu. Alice akiwa na maumivu makali moyoni, aliichukua karatasi aliyoandika majina ambayo baba yake alimtajia, akaliona jina la Brigedia Kachenje likiwa juu kabisa.

“Mwa…nangu na…kufa…lete kalamu na kara…tasi, niku..pe majina ya watu waliof…anya hivi, fan…ya har…aka!”
Maneno hayo yakajirudia kichwani mwake, ingawa alikuwa mdogo tena mtoto wa kike alielewa jambo ambalo baba yake alimtaka afanye akikua. Moyoni akaukubali wajibu huo. Vyombo vya habari vilitangaza kuwa asilimia sabini ya mawaziri karibu wote wa serikali ya Rais Christopher Chambo, walikuwa wameuawa katika mapinduzi hayo, Rais alifanikiwa kutoroka kwenda nchini Tanzania. Neno hilo Tanzania likawa limejirudia kichwani mwa Alice, hata baba yake alimtaka yeye na ndugu yake waende huko.

Maiti zote zilikusanywa na kuzikwa kwenye makaburi ya viongozi katikati ya jiji la Nyamadoke, maelfu ya watu wakiwa wamehudhuria. Wengi wakiwa hawajafurahia kitendo kilichofanyika, ikathibitika wazi kuwa kundi fulani la wanajeshi liliamua kuwatumia wananchi kufanya ukatili huo.
Alice hakushuhudia mazishi ya baba yake, alikuwa ndani ya lori lililokuwa likielekea mpakani mwa Kasomeko na Tanzania, kwenye kijiji cha Nyantakubwa ambako alijua angevuka mpaka kuingia Tanzania. Hakuwa yeye tu ndani ya gari hilo bali pia watoto wengi ambao wazazi wao waliuawa, mwenye gari aliamua kuwapa msaada akiamini mauaji yangeweza kutokea tena.
 
SEHEMU YA 03


Daniel Mchome ni Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje katika Jamhuri ya Nchi ya Kasomeko, iliyo jirani kabisa na nchi ya Tanzania. Amemuoa Anastazia na pamoja wana watoto wawili ambao ni Alice mwenye umri wa miaka kumi na John mwenye umri wa miaka mitano.
Ni familia yenye furaha na matarajio makubwa maishani, katika nchi ambayo ufisadi umeshamiri, viongozi wengi wakijitajirisha huku wananchi wao wakiteseka. Daniel si miongoni mwao, ni kijana muadilifu asiyejihusisha na ufisadi, akiamini yeye ni kiongozi wa watu.

Ghafla mambo yanabadilika, wananchi wa Kasomeko wamechoshwa na ufisadi pamoja na ubadhirifu wa mali ya umma na kuamua kuingia mitaani kupindua serikali wakishirikiana na Jeshi. Ni heri wangepindua tu, lakini wamewaua pia viongozi wengi wa serikali iliyoondolewa madarakani, akiwemo Daniel na mke wake.
Watoto peke yake ndio wamenusurika, hivi sasa wapo ndani ya gari la msamaria mwema wakielekea mpakani mwa Kasomeko na Tanzania, wanaamini nchini Tanzania watakuwa salama. Gari limepakia watoto wengi.
Je, watafika salama? Nini kitaendelea katika maisha ya Alice na mdogo wake John, ikiwa Alice alitajiwa na baba yake kabla ya kukata roho, majina ya watu waliomuua yeye na mke wake? SONGA NAYO…


Hali ilikuwa imechafuka nchini Kasomeko, ambako siku zote watu walizoea kuishi na amani wakidhani ingedumu milele. Wananchi wa nchi hiyo walikuwa wamegawanyika makundi mawili, waliopinga serikali ambao waliungana na Jeshi na kufanya mapinduzi ya aina yake, mamia ya watu walikuwa wamekufa katika mapambano kati ya kundi lililopinga serikali na jingine lililounga mkono serikali iliyopinduliwa, hali ilikuwa tete. Hakuna aliyejua kilichokuwa kikija mbele. Asilimia kubwa ya viongozi wa serikali iliyopinduliwa walikuwa wameuawa, ingawa Rais alifanikiwa kutoroka kabla hajakamatwa.

Hayo yakiendelea, Alice na mdogo wake John walikuwa ndani ya lori la msamaria mwema aliyejitolea kusaidia watoto waliozagaa mitaani wakiwemo wa viongozi wa nchi hiyo waliouawa, kuwapeleka mpakani mwa nchi ya Kasomeko na Tanzania, lengo lake likiwa ni kuwaingiza upande wa pili kulikokuwa na amani. Wakati akiwapakia watoto hao, mfanyabiashara huyo maarufu katika mji mkuu wa Kasomeko, hakujua kwamba kulikuwa na watu waliomwona ambao walimfahamu vizuri Alice na mdogo wake.

Saa nzima baada ya gari hilo kuondoka, taarifa zilipelekwa kwa Brigedia Kachenje ambaye aliagiza mara moja gari hilo lifuatiliwe, pia kwenye eneo la mpaka pawekwe kizuizi na litakapofika watoto wote washushwe na kuuawa bila huruma. Gari la jeshi likaondoka Ikulu likiwa na wanajeshi kumi wenye silaha, ambao vichwani mwao waliwaza jambo moja tu; kuwaua watoto wote ndani ya gari walilokuwa wakilifuata.

“Aichi, tuakwenda mjini? Mbona chichi acha mama na baba lala chini?” mtoto John mwenye umri wa miaka mitano alisema akimwambia dada yake Alice ambaye alikuwa amembeba miguuni, akifikiria mambo yote yaliyokuwa yakitokea, John hakuelewa kilichokuwa kikiendelea, fikra zake zilikuwa yeye na dada yake walikuwa wakienda mjini lakini waliwaacha wazazi wao wamelala chini, hakujua kabisa kwamba sasa alikuwa yatima.

Alice alimwangalia mdogo waka na kuzidi kububujikwa na machozi, John akanyoosha mikono na kuanza kumpangusa huku akimbembeleza dada yake asilie, “Nani akupiga? Tema hapa tumchape!” John alimwambia dada yake, maneno ambayo mama yake kila siku alimwambia alipokuwa akilia. Badala ya kunyamaza Alice alizidi kububujikwa na machozi, uchungu aliokuwa nao moyoni mwake haukuwa na kipimo.
“Mbona alia?” John alizidi kumuuliza.

“Hapana silii!”
“Mbona machozi yanatoka?”
“Mafua!”
“Tuwarudie baba na mama, twende nao mjini.”
“Tutawarudia baadaye, haya weka kichwa hapa,” Alice aliongea akilaza kichwa cha mdogo wake kifuani, kisha kuendelea kulia kwa nguvu zake zote bila kutoa sauti.
Moyo ulikuwa umejaa hasira, akaichomoa karatasi yenye majina ambayo baba yake alimtajia na kuanza kuyapitia jina moja baada ya jingine. Hasira ikazidi kuongezeka, hasa alipowakumbuka wazazi wake walivyolala sakafuni wakivuja damu, mama akiwa kimya na baadaye baba kunyamaza pia.

Aliifahamu kazi aliyokuwa ameachiwa, cha muhimu kwake ilikuwa ni kuingia nchini Tanzania ambako angejificha na kubadilisha jina, kisha kujipanga vizuri na maisha ili akirejea Kasomeko aweze kuwa na uwezo mzuri wa kulipa kisasi.
“Nitakutunza John mpaka ukue, nitafanya kila kinachowezekana kuhakikisha unapata elimu bora, mimi ni mdogo lakini naahidi, kwani kazi hiyo baba aliniachia!” Alice aliwaza akimwangalia mdogo wake, machozi yakawa yanadondoka na kumlowanisha John.

Ghafla mvua ilianza kunyesha, ilikuwa kubwa na ya mawe iliyowalowanisha wote sababu hawakuwa na kitu cha kujifunika na kasi ya gari ikapungua taratibu, baadaye dereva akaegesha kando na kuchungulia nyuma. Akawataka watoto wote walale chini, kwani walikuwa wamekaribia kufika mpakani ambako mara nyingi kulikuwa na kizuizi cha askari waliokagua kila gari lililopita.
“Msiogope maji, laleni tu, sitaki kabisa maaskari wawaone, hatuwezi kujua ni kitu gani wanachokifikiria.”
“Sawaaaa!” watoto wote zaidi ya kumi na tano waliitikia, Alice akamlaza mdogo wake na yeye kulala pembeni mwake, wote wakakaa kimya na safari ikaendelea.

Hawakwenda umbali mrefu sana, muungurumo wa gari jingine likija kwa nyuma ukasikika, lakini hawakujali sana. Dereva akazidi kuongeza kasi, hasa baada ya kuchungulia kwenye kioo na kuona gari lililokuwa likiwafuata lilikuwa ni la jeshi. Kitu fulani kikamwambia moyoni mwake, hakuelewa kilitokea wapi, lakini alisikia tu sauti ikisema “Ongeza kasi, watu hao wanawafuata ninyi.”

Akaitii sauti hiyo na kuzidi kukanyaga mafuta, kwani zilikuwa zimebaki kilometa chache sana kabla ya kufika mpakani. Kilometa kama mbili hivi, macho yake yakakiona kizuizi, katika hali ya kushangaza zaidi siku hiyo idadi ya maaskari ilikuwa imeongezeka, tena walikuwa ni wanajeshi wenye silaha kali. Halikuwa jambo la kawaida, siku zote kulikuwa na askari mmoja au wawili, lakini siku hiyo walikuwepo zaidi ya kumi. Akajipa moyo na kuzidi kuendesha gari lake, akiamini pengine ni kutokana na machafuko, hakuwa na habari kabisa kwamba tayari taarifa zake zilishafika mpakani.

“Jamani habari zenu?” aliwasalimia maaskari akijichangamsha ili kuwafanya waamini hakuwa na hofu, wakati moyo wake ulikuwa ukidunda kupita kiasi chini ya shati na jasho likimtoka.
“Una nini?” badala ya kuitikia salamu yake, maaskari walimuuliza juu ya kitu alichobeba kwenye gari.
“Hakuna kitu jamani, nawahi mpakani kupokea mzigo.”
“Weka gari kando.”
“Kando?”
“Ndio.”

“Afande naomba tuzungumze kidogo,” alisema dereva akiwa na lengo la kumshawishi mmoja wa maaskari hao aliyeonekana kiongozi, apokee rushwa ili yeye aachiwe kuendelea mbele.
“Nasema weka gari pembeni.”
“Afande…”
“Hivi husikii? Nasema weka gari pembeni!”
Alice aliyasikia mazungumzo yote hayo, akiwa amelala kifudifudi, mkono wa kushoto umemkumbatia mdogo wake. Mwili wote ulikuwa ukitetemeka, hakutaka kabisa maaskari wakague nyuma ya gari jambo ambalo lazima lingewasababisha hatari watoto wote waliobebwa ndani ya gari hilo.

Ghafla gari lililokuwa likija kwa nyuma nalo likafunga breki, wanajeshi wenye bunduki zilizowekwa tayari wakashuka na kumfuata dereva, mlango ukafunguliwa, akavutwa na kutolewa nje ya gari kisha kusukumwa na kuanguka chali ardhini, kilichofuata hapo ni milio ya risasi nyingi! Zote zikazama mwilini mwake na kumuua hapo hapo.
“Washusheni hao watoto, wapate haki yao!” mmoja wa wanajeshi waliokuja na gari alisema.

Wanajeshi watano wakapanda juu na kuanza kuwashusha watoto hao kwa nguvu nyingi, Alice alikuwa bado amemshikilia mdogo wake. Wote wakaamuriwa walale kifudifudi juu ya ardhi, macho yao yakiwa yameelekezwa chini. Bado Alice alikuwa amemkumbatia mdogo wake John, wote wakilia.
“Paa!Paa!Paaa! Paaaa!” ilikuwa ni milio ya risasi ikifyatuliwa kwa watoto wasio na hatia waliolala kifudifudi ardhini.
 
SEHEMU YA 4


Ni usiku wa damu.
Hali katika jamhuri ya watu wa Kasomeko imebadilika ghafla, wananchi waliodharauliwa na viongozi wao wameamua kutumia nguvu yao kuiangusha serikali ya Rais Christopher Chambo wakishirikiana na baadhi ya wakuu katika jeshi la wananchi wa nchi hiyo wakiwemo Brigedia Kachenje, Meja Jenerali Paul Lugazi, Kanali Emmanuel Nteminyanda na Brigedia Bashweka Kajigiri.

Machafuko makubwa sana yanatokea, watu wengi wameuawa, likiwemo karibu baraza lote la Mawaziri la serikali ya Rais Christopher Chambo ambaye peke yake amefanikiwa kutoroka kwa helkopta kwenda nchini Tanzania. Daniel Mchome, alikuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje katika serikali hiyo, yeye na mke wake pamoja na watoto wao wawili walikuwa nyumbani walipovamiwa na wanajeshi wakiwa na wananchi na kuuawa kikatili.

Alice, mtoto wao mkubwa alikuwa chumbani wakati unyama huo unafanyika, akajitokeza baada ya wauaji kuondoka na kukuta mama amekwishakufa lakini baba akiwa katika dakika za mwisho! Alichofanya Daniel ni kumtajia majina ya watu waliofanya unyama huo, akamkabidhi pia mdogo wake (John) ili atoroke naye kwenda nchini Tanzania kulikokuwa na usalama, akimtaka amtunze na kumsomesha katika maisha yake.

Huku akilia machozi, Alice aliondoka usiku huo huo mdogo wake mkononi, mbele alipata msaada wa lifti ya gari ya mfanyabiashara mmoja maarufu katika jiji la Nyamadoke, aliyejitolea kuwasaidia watoto waliofiwa na wazazi wao, lengo lake likiwa ni kuwavusha mpaka na kuwaingiza Tanzania. Hakujua kama wakati anawapakia Alice na John alionekana, taarifa zikatolewa kwa Brigedia Kachenje aliyetangazwa kama kiongozi wa Kijeshi wa nchi hiyo , yeye aliamuru gari hilo lifuatiliwe mpaka lipatikane na watoto wote kuuawa.

Tajiri mwenye gari aliendesha bila kufahamu kilichokuwa kikiendelea, mbele akiwa amebakiza kilometa chache tu kabla ya kufika mpakani, gari lake lilisimaishwa kwenye kizuizi. Akawaamuru watoto wote walale chini ili wasionekane, maaskari wakaanza kumhoji alikuwa amebeba nini, alijaribu kudanganya lakini haikusaidia kwani muda mfupi tu baadaye gari lililokuwa likija nyuma lilifika na maaskari wenye bunduki, watoto wote wakashushwa chini na kulazwa kifudifudi.

“Paaa!Paaa!Paaa!” ilikuwa ni milio ya risasi ikiwapenya watoto wasio na hatia baada ya dereva kuuawa.
Je, nini kitafuata? SONGA NAYO…

Damu zilikuwa zimetapakaa kila mahali, askari hao hawakujali kabisa kama waliokuwa wamewaua ni binadamu wenzao. Ilikuwa ni sawa na mtu anavyopuliza dawa ya mbu ndani ya chumba chake, huwa haelewi kabisa kuwa mbu anaowaua ni viumbe wenye familia na wanaopendwa na watoto wao. Hivyo ndivyo ilivyotokea kwa wanajeshi hao, hawakujali kabisa.

Vifo vya watoto hao wasio na hatia wala havikuwaumiza mioyo, walikuwa wakitekeleza agizo la Brigedia Kachenje, aliyedai kuwaacha watoto hao wavuke mpaka na kuingia nchini Tanzania ilikuwa sana na kwenda kuanzisha kikundi cha waasi ambao baadaye wangerejea na kulipa kisasi.
“Tuwafanye nini sasa?”

“Hatuwezi kuacha maiti hapa njiani, wapakieni.”
“Tuwapeleke wapi?”
“Tukawatupe porini wawe chakula cha ndege.”
“Sawa.”

Wanajeshi wote walikubaliana, miili hiyo ya watoto zaidi ya kumi na tano ikapakiwa ndani ya magari mawili kama magunia na kuondolewa eneo hilo, magari yakiendeshwa kwa kasi kufuata barabara iliyoingia ndani ya pori kukifuata kibao kilichoandikwa Lukulumilo Mission Hospital, mbele kidogo walikata kushoto wakifuata njia ya ng’ombe na kuzidi kuzama porini. Kilometa kumi na tano wakasimama kando ya barabara na kukubaliana kuitupa miili maeneo hayo ambako hapakuwa na binadamu kabisa.

“Hapa panafaa!”
“Sana!”
“Basi tuishusheni!”

Kwa pamoja maaskari hao wakaanza kuibeba miili hiyo mmoja baada ya mwingine na kwenda kuitupa katikati ya nyasi kama lundo la magunia, walipomaliza walirejea kama mashujaa kwenye magari yao na kuondoka kwa kasi kurejea barabarani, mikono yao ikiwa imelowa damu lakini hawakujali. Mioyo yao ilishachafuka, kazi ilikuwa imekamilika, Alice na wenzake wote walikuwa marehemu.

***
Padri Stansleus Stein alikuwa Mmisionari wa shirika la Kitawa la Moyo Safi wa Kristo ambalo makao yake makuu yalikuwa nchini Berlin, aliingia Jamhuri ya Kasomeko miaka miwili kabla ya uhuru wa nchi hiyo uliopatikana mwaka 1956 na kuanza kazi ya kuhubiri Injili. Baadaye alitulia katika pori la Lukulumilo ambako alianzisha Parishi yake na baadaye zahanati ndogo ambayo kwa misaada ya wahisani kutoka Ujerumani ilikua na kuwa hospitali kubwa iliyohudumia watu wengi wa maeneo ya Kaskazini mwa nchi hiyo, karibu na mpaka wake na nchi ya Tanzania.

Pamoja na kuhubiri injili, Padri Stansleus alipenda sana uwindaji. Kila katikati ya wiki alipokuwa hana kazi nyingi za kufanya, alichukua bunduki yake aina ya Shortgun na kuongozana na msaizidi wa Parishi aliyeitwa Makoye, kwenda porini kuwinda wakiwa na mbwa wakali kumi aliowafuga Padri Stansleus kwa ajili ya kazi hiyo.

Siku hiyo ya Jumatano walikuwa katikati ya pori bila kuelewa kwamba jana yake yalitokea machafuko makubwa katika mji Mkuu wa Jamhuri ya Kasomeko, ambako wananchi waliamua kuuondoa utawala madarakani, Padri Stansleus hakujua hilo kwa sababu hakuwa mfuatiliaji sana wa taarifa za habari. Walizunguka huku na kule porini wakiua swala na Makoye kuwapakia kwenye gari lao.

Mara ghafla mbwa wao walianza kukimbia kwenda mbele wakinusa chini, huku wakitoa mlio usio wa kawaida, Padri akaiweka bunduki yake tayari akiamini kulikuwa na hatari ikija. Wakaanza kukimbia wakiwafuata mbwa wao na kuwakuta wakibweka sehemu kulikokuwa na nyasi nyingi, wakapunguza mwendo na kuchungulia katikati ya nyasi hizo, hawakuamini walichokiona!

“Maiti za watoto, Mungu wangu! Kitu gani hiki? Lazima kuna muuaji maeneo haya!”
“Tuondoke haraka sana Padri.”
“Hapana, nahitaji kufahamu, tena nasikia hapa ndani kama kuna sauti ya mtoto analalamika!”

“Hata mimi nasikia.”
“Sogea karibu Makoye, jikaze, anza kupangua mwili mmoja baada ya mwingine huku mimi nikiwa nalinda na bunduki, sawa?”
“Sawa Padri.”

Msaidizi aliitikia na kuanza kupangua maiti moja baada ya nyingine wakijaribu kutafuta iliyokuwa ikilalamika, damu ilikuwa nyingi mno ikiwa imeganda, Makoye alikuwa amejitoa mhanga bila kuogopa virusi vya Ukimwi ili mradi amwokoe mtoto aliyekuwa akilalamika.
“Huyu hapa!” Alipiga kelele baada ya kuwa amepangua kama maiti nane hivi.
“Hebu mlete,” Padri alisema.

Makoye akatembea na mwili wa mtoto huyo, akaulaza mbele ya Padri alipomfikia. Hakuwa amepigwa risasi shingoni na nyama kusambaa kabisa, moyo wake ulikuwa bado ukipiga na alihema kwa mbali. Padri akamwomba Makoye ambebe, wote wakaanza kukimbia kuelekea mahali walipoliacha gari lao, shughuli ya uwindaji ilikuwa imefika mwisho. Makoye akampakia mtoto huyo nyuma ya gari kulikokuwa na swala, Padri akaingia mbele na kuwasha gari, bila kupoteza wakati akaondoka kwa kasi isiyokuwa ya mtumishi wa Mungu, bali mwendesha gari la mashindano.
“Anaendeleaje?” Padri aliuliza.

“Anahema, lakini kwa taabu.”
“Mpigepige kwenye moyo, ili usisimame.”
“Sawa Padri.”

Gari lilizidi kwenda kwenye mabonde likiruka vibaya, dakika arobaini na tano baadaye liliegesha idara ya mapokezi katika hospitali ya Lukulumilo, wauguzi wakafika wakikimbia na machela yao baada ya kuliona gari la Padri Stansleus. Walishindwa kuamini walichokiona, wakambeba mtoto huyo juu ya machela kumkimbiza chumba cha daktari ambaye alipomwona tu aliamuru apelekwe chumba cha upasuaji haraka.

“Atapona?” Padri aliuliza.
“Sijui Padri, wacha tujitahidi.”

“Sijui nani kafanya ukatili huu, tumeacha maiti nyingi sana!”
“Najua ni kwa sababu ya machafuko!”
“Machafuko gani?”

“Huna habari Padri?”
“Sina habari kabisa.”
“Serikali imepinduliwa, watu wengi sana wamekufa katika mapigano huko Nyamadoke.”
“Kweli?”

“Acha niingie chumba cha upasuaji kwanza Padri, nijaribu kuokoa maisha ya huyu mtoto.”
“Sawa, fanya kadri uwezavyo na Mungu atakusaidia angalau tuweze kuokoa maisha ya mtoto mmoja kati ya waliokufa!”
“Ahsante Padri,” daktari alisema maneno hayo na kuondoka huku akikimbia.

Je, mtoto huyu ni nani? Atapona? Nini kitatokea zaidi huko Jamhuri ya Kasomeko? Ndio mwisho wa familia ya
 
SEHEMU YA 05


Orodha hiyo Alice aliiweka mfukoni mwake na kumbeba mdogo wake John hadi mahali ambako walipakiwa ndani ya gari la msamaria mwema wakiwa na watoto wengine kwa lengo la kuwakimbiza mpakani ambako wangevuka na kuingia Tanzania.
Hawakuweza kuvuka, kwani walikutana na kizuizi na ni hapo kwenye kizuizi ndipo gari jingine lililotumwa na Brigedia Kachenje, kiongozi mpya wa kijeshi kwa lengo la kwenda kuwaua watoto hao, lilifika na wote wakashushwa na kulazwa ardhini! Risasi zikaanza kuwamiminikia mmoja baada ya mwingine.

Wauaji wakiamini wamekufa, waliwabeba na kwenda kuwatupa katikati ya pori ambako Padri Stansleus Stein ambaye pia ni mwindaji aliiona miili hiyo na kugundua mmoja alikuwa hajafa ndipo akamchukua mpaka kwenye hospitali ya Lukulumilo ambako mtoto huyo alipokelewa na kukimbizwa chumba cha upasuaji.
Je, nini kitaendelea? SONGA NAYO…


Ndani ya chumba cha upasuaji cha hospitali ya Lukulumilo, madaktari na wauguzi walikuwa wakitembea huku na kule kwa haraka wakifanya maandalizi ya mwisho kabla hawajaanza kumrekebisha Alice sehemu aliyofumuliwa na risasi. Mpaka wakati huo hapakuwa na mmoja kati yao aliyeelewa ni kitu gani kilitokea mtoto huyo akawa hai ingawa alikuwa amejeruhiwa vibaya mno.

Wote walikuwa na habari juu ya mambo yaliyotokea nchini mwao, walifuatilia vizuri kupitia vyombo vya habari, lakini hawakuwa na wasiwasi mwingi wakijua hakuwepo mtu wa kuwavamia kijijini walikoishi, waliamini machafuko yangeendelea kubaki mjini peke yake.
“Tumfanyie hivyo hivyo?” Mmoja wa madaktari aliuliza baada ya kumwona Alice akiwa bado hana fahamu.
“Hapana anaweza kuzinduka katikati ya shughuli halafu ikawa ngumu kuendelea, nashauri achomwe Ether!” Dk. Prepo Mangwasha, bingwa wa upasuaji katika hospitali hiyo alisema, yeye ndiye aliyetegemewa kuiendesha kazi hiyo.

Mtaalam wa dawa za usingizi akasogea karibu na kumchoma Alice sindano moja kwenye mshipa kisha kufunika pua zake na kifaa maalum na kumshuhudia akihema kwa kuvuta hewa kutoka kwenye kifaa hicho. Kazi hiyo ilipokamilika, madaktari walijipanga vizuri kuanza kazi ya kurekebisha shingo yake kuanzia mishipa ya damu mpaka misuli iliyokuwa imesambaratishwa, walishangaa kukuta mshipa mkubwa ambao hupeleka damu kichwani ukiwa haujaguswa.

“Huu ni muujiza!”
“Kwanini daktari?”
“Yaani risasi ipite hapa, halafu Jugular isiguswe? Sijawahi kuona!” Dk. Prepo aliongea akiendelea kurekebisha sehemu mbalimbali za shingo ya Alice zilizokuwa zimeharibiwa.
Tofauti na masaa matatu waliyotarajia kuukamilisha upasuaji huo, walikwenda mpaka saa ya nne wakiwa bado wanaendelea. Hofu yao kubwa ikawa ni dawa ya usingizi kumaliza nguvu kabla hawajamaliza kazi, hata hivyo sehemu ndogo sana ilikuwa imebaki, wakajipa matumaini na kuendelea.

***
Nikiwa katikati ya kutokuwa na kumbukumbu na kuwa nazo, nilisikia sauti za watu wakiongea, ilikuwa ni kwa mbali kidogo lakini sauti zao ziliambatana na maumivu makali shingoni. Taswira za baba na mama yangu zikanijia, si wao tu bali pia mdogo wangu John. Wazazi wangu walikuwa wakicheka na kutabasamu, lakini ghafla nikaiona miili yao ikiwa imelala chini, imesambazwa kwa risasi, damu nyingi zikimwagika. Ni ndoto? Nilijiuliza, lakini sikupata jibu nikabaki njia panda nikijaribu kufikiria kilichokuwa kimetokea. Hofu nyingi ikaniingia, macho yakapatwa na giza. Ghafla tu nikawa sina fahamu kabla sijapata majibu ya maswali yangu.

Nilipofumbua macho nilijikuta nimelala kitandani, nikayazungusha macho yangu huku na kule chumbani nikijaribu kutafakari juu ya mahali nilipokuwa bila kupata majibu. Mashuka niliyofunikwa yalikuwa ya rangi nyeupe, kwa juu yakiwa yameandikwa neno Health, ambayo kwa kumbukumbu zangu ingawa hazikuwa nzuri sana, yalimaanisha neno ‘Afya’. Tayari nikaelewa kwamba mahali nilipokuwa ni hospitali.

Mh! Nimefikaje hapa? Nilijiuliza nikiendelea kuzungusha macho yangu, sekunde hizo hizo niligundua shingo yangu ilikuwa nzito na mwili wangu haukuwa na nguvu. Nikauvuta mkono wangu wa kuume na kujigusa shingoni, kiganja kikakutana na bendeji. Maswali yasiyo na majibu yakazidi kuongezeka. Nikiwa katika hisia hizo, mlango ulifunguliwa, mzee mwenye ndevu nyingi nyeupe akaingia. Nilichokiona baada ya sura yake ni msalaba mkubwa ulioning’inia kifuani kwake, mkononi akiwa na kitabu cheusi ambacho kwa kumbukumbu zangu nilikifananisha na kile kiitwacho Biblia.

“Ha!” mzee huyo aliongea kwa mshangao, nami nikamwangalia katika hali ya kutokuamini.
“Babu vipi?” nilijikakamua nikamuuliza.
“Umeamka? Kweli Mungu ni mwema,” jibu lake likazidi kunichanganya huku kichwani nikijaribu kupiga picha na kujiuliza juu ya kilichonitokea bila kukumbuka.
“Wewe ni nani? Na nimefikaje hapa?” Pamoja na umri wangu mdogo niliuliza maswali mfululizo kabla hata ya salamu huku nikimshuhudia namna mzee huyo alivyokuwa ametokwa na macho, akapiga magoti chini na kuanza kusali akimshukuru Mungu.

Mungu nakushukuru,
Nimeamini wewe ni Mungu wa kweli,
Kama umeweza kumwokoa binti huyu kati ya wote waliokufa,
Ahsante Mungu,
Nakushukuru baba,
Najua una makusudi naye,
Basi naomba ukayatimize.

“Mamaaaa!Mamaaaa!Mamaaaa!” Nilipiga kelele kwa nguvu nyingi kupita kiasi, maombi ya mzee huyo yalikuwa yamenikumbusha kila kitu, unyama waliofanywiwa wazazi wangu na tulivyolazwa chini na watoto wenzangu kisha mmoja baada ya mwingine kuanza kumiminiwa risasi tukiwa tumelala ardhini kifudifudi, kumbukumbu zangu zikanirejesha kwa John mdogo wangu. Sikuwa na uhakika kama alikuwa hai.

Kelele zangu ndizo zilizofanya madaktari na wauguzi wakimbilie wodini, baada ya kuzisikia wakiwa kwenye ofisi yao. Chumba kikajaa watu wengi wakiwa wamevalia nguo nyeupe, magauni pamoja na makoti. Walikuwa madaktari na wauguzi. Wote wakaonyesha mshangao. Nilichojifunza kutoka kwenye macho yao ni kwamba, walikuwa watu waliokuwa wamekata tamaa kabisa kwamba ningeishi tena.

“Pole!” mmoja wao aliyevaa nguo za bluu alisema.
“Ahsante, John yuko wapi?”
“John ndio nani?”
“Mdogo wangu.”
“Tulia kwanza mjukuu, utibiwe upone halafu Padri Stansleus atakusimulia kila kitu kilichotokea!”
“Simfahamu Padri.”

“Huyu hapa,” alisema akimsonta mzee aliyeingia mwanzo, mwenye msalaba kifuani, nikagundua alikuwa ni kiongozi wa Kanisa Katoliki lakini sikuelewa ni kwanini yeye ndiye alipendekezwa kunieleza kilichotokea.
Kwa wiki mbili mfululizo nilibaki wodini nikimlilia John, sikujua mahali alikokuwa na kwa sababu mimi nilikuwa hai, nilijua lazima naye alikuwepo mahali fulani ambako ningeonyeshwa baada ya kuruhusiwa. Wiki ya tatu nikiwa nimeshatolewa bendeji na kidonda kuonyesha maendeleo, niliruhusiwa kutoka hospitali na Padri Stansleus akanichukua kunipeleka kwenye jumba la Mapadri ambako ningeishi na kuhudumiwa kila kitu.

“Padri naomba unieleze ukweli wa kilichotokea.”
“Unataka kufahamu?”
“Ndiyo.”
Padri aliketi vizuri kitini na kuanza kunieleza kila kitu kilichotokea siku aliponiokota porini akiwinda na mbwa wake, nililia sana, mwisho nikamshukuru na kumuuliza mahali mdogo wangu alipokuwa. Bila kuficha kitu Padri Stansleus alinieleza wazi kwamba, lazima John alikuwa marehemu. Nikarejea kwenye kulia tena ingawa machozi yangu yalishaanza kukauka na kazi ya Padri ikawa ni kunibembeleza kwa saa mbili ndipo nikatulia.

“Usijali, ndiyo dunia, naweza kukufahamu sasa?” Padri aliniuliza.
“Mimi?”
“Ndiyo.”
“Naitwa Alice Daniel Mchome!” nikamjibu.
“Mchome?”
“Ndiyo.”
“Mchome yupi? Waziri?”
“Ndiyo.”
“Kweli?”
“Kabisa.”
“Yuko wapi?”

Sikuweza kulijibu swali hilo, badala yake nikaangua kilio kikubwa zaidi! Ilibidi Padri Stansleus anisogelee karibu na kuanza kunibembeleza mpaka nilipotulia tena ndipo nikaendelea kuelezea historia ya maisha yangu, namna wazazi wangu walivyouawa kikatili siku ya mapinduzi. Mwisho nikaeleza nia yangu ya kuondoka nchini Kasomeko kwenda kujificha nchini Tanzania kama alivyoagiza baba yangu, ingawa sikuieleza nia yangu ya kurejea tena nchini Kasomeko kulipa kisasi wa wabaya wa wazazi wangu.

“Lakini kabla sijaondoka, nitakuomba unipeleke sehemu tulipokuwa tumelundikwa nikauangalie mwili wa mdogo wangu, inawezekana?” Nilimuuliza.
“Inawezekana kabisa.”
“Lini?”
“Wewe kuondoka hapa kwenda Tanzania lini?”
“Kesho kutwa.”

“Basi nitakupeleka kesho.”
“Lakini kitu kimoja nataka niseme kwako Padri, ukweli ni kwamba nakushukuru sana, umekuwa mtu mwema mno kwangu, sitakusahau maisha yangu yote yaliyobaki!”
“Amina! Tumshukuru Mungu, nilichokuwa nafanya ni kumwakilisha yeye duniani!”
Siku hiyo usiku mzima sikupata usingizi, nikiifikiria siku iliyokuwa ikija mbele, kulipokucha nilijiandaa kwa ajili ya safari ya kwenda porini. Saa nne na nusu ndipo nikakutanishwa na Makoye, msaidizi wa Padri Stansleus sote tukaingia ndani ya gari na safari ya kwenda porini ikaanza.

Saa mbili baadaye wakiwa katikati ya pori, gari liliegeshwa, tukashuka Padri Stansleus akiwa mbele na bunduki yake na kuanza kutembea kwa miguu kuingia porini zaidi, kadri tulivyosonga ndivyo harufu ilivyozidi kuongezeka, sikuelewa ilikuwa ni harufu ya nini mpaka alipoambiwa neno “NI HAPA”.
Nikatupa macho yangu na kuona mabaki ya watu yaliyolundikana, roho ikaniuma kupita kiasi, machozi yakabubujika kama chemchemi.

Hata hivyo nilijipa moyo na kusogea kwenye lundo la miili iliyoharibika, haikuwa rahisi kumtambua yeyote kwani nyama zilishaporomoka na kubaki mifupa! Kando kukiwa na ndege wakubwa waliogeuza miili hiyo kitoweo. Nikaangaza macho yangu ndani nikimtafuta John, sikumwona, kwa ujasiri wa ajabu ilibidi nianze kupangua mwili mmoja baada ya mwingine kwa kutumia mti, huku harufu ikinitesa. Padri Stansleus na msaidizi wake wakinisaidia.
“Huyu hapa!” nilisema baada ya kuziona nguo za John na kulia kwa uchungu.
 
SEHEMU YA 06


Machafuko yametokea nchini Kasomeko, serikali ya Rais Christopher Chambo imeondolewa madarakani na wananchi wakiongozwa na baadhi ya viongozi katika jeshi. Brigedia Kachenje ndiye ametangazwa kuwa Rais wa Kijeshi wa nchi hiyo. Watu wengi wameuawa wakiwemo baadhi ya Mawaziri.

Daniel Mchome, alikuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje katika serikali hiyo, kijana tu, baba wa watoto wawili na mume wa mwanamke mrembo aitwaye Anastazia. Wote wameuawa, watoto wao tu ndio wamenusurika na mkubwa (Alice) mwenye umri wa miaka kumi anafanikiwa kutoroka akiwa na mdogo wake (John) kwenda mpakani mwa nchi hiyo na Tanzania wakiwa ndani ya lori lililotolewa na mfanyabiashara mmoja mwenye huruma.

Mbele wakiwa wamekaribia mpakani, gari lilifika kwenye kizuizi, dereva akauawa na watoto wote kulazwa chini kisha kufyatuliwa risasi bila huruma. Baada ya zoezi hilo la kinyama miili yote ilichukuliwa kwenda kutupwa porini ambako Padri Stansleus Stein, mpenda kuwinda, aliigundua na kumchukua mtoto mmoja aliyekuwa hai kwenda hospitali ambako alitibiwa mpaka akapona.

Huyu ni Alice, kitu cha kwanza alichoulizia ni mdogo wake John na Padri ambaye alishakubali kumtorosha Alice kwenda mpakani ili avuke kuingia Tanzania, aliamua kumpeleka porini alikomwokota ili akaone maiti ya mdogo wake. Baada ya kupekua katikati ya maiti hizo akitumia mti kwa msaada wa Padri, Alice huku akilia alisema “Huyu hapa” Je, nini kitaendelea? SONGA NAYO…

Zilikuwa ni nguo zile zile ambazo John aliondoka nazo nyumbani, zikiwa zimejaa damu nyingi. Baba alimnunulia John nguo hizo wakati wa sikukuu ya Kristmasi kabla hatujaondoka kwenda kijijini kwa babu mapumziko. John alikuwa mifupa tupu, kichwa kikiwa kimebaki fuvu lakini ndani ya nguo zake. Nikageuka kuwaangalia ndege waliokuwa jirani, hasira zikanishika, kwani hao ndio walikuwa wamekula nyama za ndugu yangu. Machozi yalinibubujika, Padri Stansleus akiwa amenikumbatia.

“Padri!” Nikaita.
“Naam Alice.”
“Ningependa kumzika ndugu yangu kwa heshima zote.”
“Inawezekana.”

“Utamfanyia Ibada ya maziko?”
“Sawa.”
“Ahsante Padri, tutachimbaje kaburi?”

“Bila shaka kwenye gari letu lipo jembe na koleo.”
“Tunaweza kuvipata?”
“Makoye! Hebu nenda kwenye gari chukua jembe na koleo ulete hapa.”

“Sawa ba…ba Pa…dri” aliitikia kijana huyo, pia machozi yakimbubujika, lundo la watu waliokufa hakika haikuwa picha nzuri sana kuishuhudia hata kama hawakuwa ndugu zake. Akajitahidi na kutembea mpaka kwenye gari kuchukua jembe na koleo, kisha akarudi mpaka mahali ambako mimi na Padri tulikuwa tumesimama akiwa bado amenikumbatia kama njia ya kunipa faraja.

Sote tukasogea kando, kwenye sehemu iliyokuwa wazi na Makoye akaanza kuchimba kaburi, alipochoka Padri alichukua jembe na koleo na kuendelea huku mimi nikiangalia. Ardhi ilikuwa laini isiyokuwa na mawe, hivyo ndani ya saa moja na nusu walishafikisha kaburi viunoni, wote wakatoka nje na kusimama kando, mimi nikishuhudia, muda wote machozi yakinibubujika, fikra zangu zote zikiwa kwa jambo lililokuwa limetokea. Nilikuwa mtoto mdogo, lakini ilitosha kabisa kuelewa kilichofanyika ni unyama na kwamba tangu siku hiyo nisingekuwa na baba, mama wala mdogo wangu tena.

Padri na Makoye wakasogelea lundo la maiti tayari kwa kubeba mifupa ya John! Kabla hawajafanya hivyo, Padri alishtuka, akamwomba Makoye arejee tena kwenye gari kuchukua mifuko ya nailoni iliyokuwemo, akafanya hivyo na kuileta ndipo wote wakajifunga mikononi na kuitumia kuichomoa mifupa ya John kutoka katikati ya mabaki ya marehemu wengine. Pamoja wakaubeba mpaka kando ya kaburi.
“Padri!” nikaita.
“Naam.”

“Naomba nguo za John.”
“Nguo za John?”
“Ndiyo.”

“Za kazi gani?”
“Ndio kumbukumbu pekee nitakayobaki nayo.”
“Hazitakuwa zinakuumiza moyo?”

“Ndio vizuri, sitaki kumsahau John maisha yangu yote, sitazipoteza wala kuzigawa,” aliongea Alice, Padri akamwangalia kwa mshangao, alikuwa mtoto mdogo mno kufahamu mambo yote aliyokuwa akiyazungumza, hakika hakulingana nayo.

“Mungu akusaidie katika maisha yako yote Alice, damu ya Bwana ikufunike kokote utakakokwenda, ili siku moja upate kutimiza makusudi ya kuzaliwa kwako.”
“Amina.”

Mabaki ya John yaliingizwa kaburini nikishuhudia, kisha Padri akaniomba nichukue mchanga kidogo na kumwaga kaburini kama ishara ya kumuaga ndugu yangu. Kisha akaanza kuendesha Ibada ya watu watatu tu tukimwombea John apumzike kwa amani, nilikuwa na uhakika kabisa moyoni kwamba alikuwa amekwenda si sehemu nyingine bali Mbinguni. Hilo lilinifariji na kufanya machozi yangu yakauke.

“Usilie sana Alice, John amekwenda kwa Baba, ipo siku tutakutana naye tena kwenye ulimwengu ujao, jambo jema ni sisi tuliobaki tuishi maisha ya kumpendeza Mungu, unasikia?”

“Ndio Padri,” nilijibu lakini kichwani mwangu likaingia wazo la orodha ya majina ambayo baba alinikabidhi kabla ya kifo chake, watu walioua wazazi wangu na kusambaratisha familia kisha kunifanya mimi kuwa mtu wa kutapatapa duniani.

Machozi yalikuwa yakinibubujika, mashavu yote yalikuwa yamelowa. Halikuwa jambo rahisi kuliamini hasa nilpofikiria historia ya maisha yangu, nikiwa mtoto niliyezaliwa kwenye familia ya wasomi na wenye mamlaka, sasa nilikuwa nashuhudia mdogo wangu kipenzi akifukiwa kwa udongo katikati ya pori mahali ambako hakika nisingepakumbuka bila kuweka alama. Nikawakumbuka pia baba na mama yangu na uchungu kuzidi kuongezeka, hapo hapo nikawalaani waliosababisha machafuko, moyoni nikadhamiria kulipa kisasi nikitimiza umri wa kufanya hivyo ingawa Padri alisisitiza juu ya mimi kutenda mema ili niwe na sifa za kukutana na John katika ulimwengu ujao, taswira ya wazazi wangu chumbani wakiwa wamekufa, ndio ilinifanya nisikubaliane na Padri Stansleus.
“Padri naomba unisaidie kuweka lile jiwe hapa ili niweze kukumbuka siku nitakaporejea.”
“Sawa.”

Padri aliitikia na yeye na Makoye wakatembea hadi kando palipokuwa na jiwe kubwa, wakalisukuma mpaka juu ya kaburi. Nikaangaza macho yangu huku na kule nikijaribu kupiga picha ya eneo hilo, moyoni nikiamini lazima ningerudi kupaona mahali nilipomzika kaka yangu. Shughuli hiyo ilipomalizika, tulitembea kuelekea kwenye gari, nikageuka nyuma kila baada ya hatua chache kuliangalia kaburi la John, hasira ikazidi kupanda.
“Hawa! Hawa tu, lazima siku moja wajue walifanya kosa…” nilijisemea moyoni nikiiangalia orodha kwenye karatasi yangu.

Kwenye gari tuliingia, Padri akawasha na kuanza kuendesha kwa kasi tukielekea mpakani, uamuzi ulikuwa ni kunifikisha mimi huko ili nivuke na kuingia nchini Tanzania. Hakuwepo mtu mwenye uhakika tungefika salama,

kwani machafuko yalikuwa yamezidi kuongezeka. Padri alisimamisha gari na kunipa moyo kisha kuniomba nizunguke sehemu ya nyuma ambako nilifungwa kwenye turubai kama mzigo ndipo safari ikaendelea, alifanya hivyo akiamini mbele lazima kungekuwa na vizuizi na kama wauaji wangeniona ni lazima wangenipiga risasi na kunimalizia.

Safari ikaendelea, kila baada ya kama dakika ishirini hivi gari lilisimama, nikasikia mazungumzo yakiendelea kati ya Padri na watu ambao niliamini kwamba ni maaskari, nilitetemeka mno nikijua yamenikuta kwa mara nyingine. Padri alipojitambulisha tu kuwa yeye ni Mtawa kutoka Lukulumilo hospitali, hakuna aliyemzuia, aliheshimiwa sababu ya msaada alioutoa nchini Kasomeko. Hivyo hivyo hatimaye tukafika mpakani, ambako Padri alivuka hadi upande wa Tanzania na kunishusha.

“Mwanangu! Hapa ndipo zinapokomea juhudi zangu, enenda kwa amani na Mungu akusaidie, chukua na hii itakusaidia!” Padri Stansleus aliongea akinikabidhi noti ya dola mia moja, nikasomgelea akaninyanyua na kunikumbatia, machoni nikamwona hata yeye akilengwalengwa na machozi, hakuwa na uhakika kama kweli nilikokuwa nikielekea ningekuwa salama.

Akiwa bado amenikumbatia lori kubwa lilionekana likivuka mpaka, akamtuma Makoye akalisimamishe na kuuliza kama walikuwa wakielekea Dar es Salaam. Lilikuwa ni lori aina ya Leyland lililobeba magunia mengi ya mahindi. Liliposimama Makoye alionekana akizumgumza na dereva kisha kukimbia tena mahali tuliposimama.

“Vipi?” Padri aliuliza.
“Wamekubali lakini atapanda huko nyuma.”
“Hakuna tatizo.”

“Umewaelezaje?”
“Ni mtoto amenusurika kwenye mauaji na anachohitaji ni kufika Dar es Salaam, huko atapata kila kitu.”
“Hakuna shida, wameonyesha wasiwasi?”

“Hapana, wanachohitaji wao ni fedha tu.”
“Shilingi ngapi?”
“Elfu kumi na tano.”

“Sawa, twende tumpeleke basi,” Padri aliongea na kwa pamoja tukaanza kutembea kuelekea kwenye lori hilo ambako nilipandishwa na Padri kutoa noti ya dola ishirini nikishuhudia, akamkabidhi dereva.
“Dola tena?”

“Ndiyo niliyonayo, ni zaidi ya ulichoomba lakini chukua tu ili mradi umfikishe huyu mtoto Dar es Salaam.”
“Ana ndugu?”

“Hapana ni mkimbizi, wewe mshushe popote pale mkishafika, utakuwa ni msaada mkubwa sana.”
“Nitafanya hivyo.”

Maongezi hayo niliyasikia nikiwa chini ya turubai, juu kabisa ya gari hilo. Hakuwepo mtu mwingine tena isipokuwa mimi, hofu haikuwemo moyoni mwangu, nilifurahi kuingia Tanzania, nchi iliyosifika kwa amani. Safari ikaanza nikiendelea kulia na kuwafikiria wazazi na mdogo wangu na hata babu na bibi yangu walioishi kijiji cha Chenzuga, kilometa ishirini na tano kutoka mjini Nyamadoke. Sikuwa na uhakika kama nao walikuwa hai,

ingawa hisia zangu zilinituma kuamini nilikuwa nimebaki peke yangu duniani.
 
SEHEMU YA 08


Mambo yameharibika nchini Kasomeko, serikali ya nchi hiyo iliyoongozwa na Rais Christopher Chambo imepinduliwa na wananchi kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi katika Jeshi. Rais ametoroka lakini baadhi ya Mawaziri wake wamekamatwa na kuuawa kikatili, miongoni mwao akiwemo Waziri wa mambo ya Nje Daniel Mchome, yeye na mke wake wamechinjwa kama kuku.
Mtoto wao Alice akiwa amembeba mdogo wake John ndio wananusurika na msamaria mwema amewapakia ndani ya gari ili awakimbize mpakani wakiwa na watoto wengine wa viongozi waliouawa, gari hilo halikufanikiwa kuvuka mpaka, kwani lilizuiwa kwenye kizuizi na watoto wote kushushwa na kupigwa risasi.


Alice akanusurika kifo kwani risasi ilipita pembeni mwa shingo yake, Padri mmoja Mwindaji ndiye aliyemwokoa porini na kumpeleka hospitali ambako alitibiwa mpaka kupona kisha kumsimulia Padri huyo historia ya jambo lililotokea na kumwomba amsaidie kuondoka Jamhuri ya Kasomeko ndipo Padri akamvusha mpaka kuingia Tanzania ambako alimtafutia usafiri wa lori, Alice akimlilia mdogo wake pamoja na wazazi wake, akasafiri mpaka jiji la Dar es Salaam, huko akajikuta uwanja wa Fisi, eneo baya la Ukahaba.

Msichana mmoja aitwaye Levina, aliyefanya shughuli za Ukahaba katika eneo hilo, alimwona na kumchukua hadi nyumbani kwake ambako alimlea kama mdogo wake mpaka akatimiza umri wa miaka kumi na mbili na kupendeza! Hapo ndipo akaeleza nini lilikuwa lengo la msaada wake, alitaka Alice akue ili aanze kumuuza jambo ambalo Alice hakukubaliana nalo, ndipo Levina akanyanyua simu yake na kumpigia mwanaume mwenye misuli aliyewasili muda mfupi baadaye na kumpatia kiasi cha shilingi elfu tano, akiahidi kumwongezea Bia mbili baadaye. Levina akaondoka chumbani na kuwaacha wawili.
Je, nini kitaendelea? SONGA NAYO…

Alice akiwa amejilaza kitandani bila kuelewa ambacho kingefuata, alimshuhudia mwanaume huyo mwenye misuli akinyanyuka baada ya Levina kutoka na kufunga mlango. Akatembea hadi kitandani na kuketi kando yake, kwa umri mwanaume huyo alilingana kabisa na baba yake mzazi, hakika, kama mzazi hakutakiwa kumfanyia unyama na alijua wazi nyumbani kwake lazima alikuwa na binti mwenye umri kama wake.

“Vipi mpenzi?” Mwanaume huyo akasema.
“Shikamoo”

“Unaniamkia? Kwani unataka kuninyima kitu gani?”
“Ah!Ah!” Wewe ni sawa na baba yangu, mimi kama mtoto nimefundishwa kuheshimu wakubwa.
“Mtoto wa mwenzio mkubwa mwenzio, hebu njoo hapa!” Mwanaume huyo aliongea akimvuta Alice amsogelee.

“Unataka kufanya nini baba?”
“Kwani bosi wako hajakueleza?”
“Bosi wangu nani?”

“Aliyeondoka, au hukuona wakati nampa elfu tano yangu?”
“Si umempa yeye, sasa kwanini unataka kunionea mimi?”
“Nimekununua, usinizidishie maneno, vua!”

“Naomba uniache, mimi ni sawa kabisa na mwanao”
“Nimekwishakueleza mtoto wa mwenzio mkubwa mwenzio, kama hutaki kuvua basi mimi nakuvulisha, usinipotezee wakati wangu,” mwanaume huyo aliongea kwa ukali.

Alice akidhani angeonewa huruma, alimshuhudia mwanaume huyo akinyanyuka na kusimama wima mbele yake. Katika hali ya kushangaza alimwona akifungua vifungo vya shati lake kisha kulivua na kulitundika kwenye msumari uliogongwa ukutani. Alipomaliza kuvua shati, bila kujali alikuwa amesimama mbele ya mtoto mdogo, mwanaume huyo aliikamata suruali na kufungua vifungo kisha kuishusha pamoja na nguo ya ndani, maumbile yake ya kiume yakaonekana.

“Mama yanguuu!” Alice alitamka maneno hayo ndani ya kifua chake, tangu kuzaliwa kwake hakuwahi kuona maumbile makubwa kiasi hicho, alizoea kuona watoto wadogo tu chini ya umri wake wakipita bila kuvaa nguo au wakati wa kuogeshwa.


“Fumbua macho, unaogopa nini?”
“Siwezi! Siwezi kukuangalia, wewe ni sawa na baba yangu mzazi!”
“Baba yako nani? Hebu njoo” mwanaume huyo alifoka akimnyanyua Alice na kumsimamisha wima, akaanza kumvua nguo zote kwa nguvu.

Alice alijaribu kupiga kelele na kuzuia asivuliwe lakini haikusaidia, zote zikachanwa na kujikuta amebaki kama alivyozaliwa. Hapo ndipo alielewa kweli mwanaume huyo alikuwa amedhamiria kumwingilia kimwili kwa nguvu.

Levina ambaye siku zote alijifanya msamaria mwema, ndiye alikuwa amemuuza, kumbe wema wake wote ulikuwa na lengo kama hilo siku moja. Machozi yakamtoka wakati mwanaume huyo akimbeba na kumtupa kitandani, akamgandamiza kwenye godoro akiwa chali, yeye akaja kwa juu yake!

“Mungu wangu weee! Nisaidie!” Alilia Alice kwa nguvu zake zote mpaka mwanaume huyo akamwachia na kutembea hadi ukutani ambako alitungua shati lake na kurejea nalo kitandani, nusu ya shati hilo likashindiliwa mdomoni mwa Alice na kufanya sauti yake isitoke tena ndipo kwa mara ya pili akagandamizwa kitandani akiwa chali na mwanaume huyo mwenye uzito usiopungua kilo mia moja na ishirini akamwangukia kama gunia la mchele.

Kilichofuata hapo hakielezeki, ulikuwa ni unyama uliokithiri. Alice alilia kwa nguvu zake zote sababu ya maumivu makali yaliyompata lakini haikusaidia, bila huruma yoyote mwanaume huyo aliendelea kumwingilia, akifurahi kitendo cha yeye kukutana na mtoto bikra. Damu nyingi zilimwagika na kuchafua kabisa shuka na godoro, haja yake ilipomalizika, Alice akiwa hajitambui, mwanaume huyo aliruka kitandani akidhani amekufa na kuvaa nguo zake haraka kisha kutoka chumbani na kupotelea gizani.

Saa nzima baadaye fahamu zilimrejea Alice na kujikuta amelala katikati ya dimbwi la damu, sehemu zake za siri zikimuuma kupita maelezo. Akakumbuka picha nzima ya tukio na kuanza kulia, akimtupia lawama zote Levina, lakini zaidi sana alizitupa kwa Brigedia Kachenje na wenzake, hao ndio waliovuruga maisha kwa kuwaua wazazi wake kikatili. Akanyanyuka na kutembea taratibu mpaka kwenye sanduku lake la nguo, akalifungua na kutoa suruali moja ambayo aliivaa kwa taabu kubwa, akachukua pia fulana ya rangi nyeusi na kuvaa kisha kwenda tena kwenye suruali yake iliyochanwa, akaingiza mkono ndani ya mfuko mmoja na kutoa karatasi ndogo, akaikunjua na kuanza kuisoma.

Brigedia Kachenje,
Meja Jenerali Paul Lugazi,
Kanali Emmanuel Nteminyanda
Brigedia Bashweka Kajigiri.

Aliyasoma majina hayo machozi yakimbubujika, hasira ikazidi kumpanda, akawaona baba na mama yake wakiwa sakafuni wote wamekufa, halafu akamwona mdogo wake John mwili wake ukiwa umebaki mifupa tupu, akamzika na kuweka alama juu ya kaburi lake, akiahidi iko siku angerudi. Sauti ya baba yake ikasikika ikimweleza juu ya nini cha kufanya kwa majina hayo, mara moja akatembea miguu yake ikiwa imetandazwa sababu ya maumivu makali hadi kwenye mlango, akafungua na kutoka nje. Muda huo huo mvua kubwa ikaanza kunyesha.

Bila kuelewa ilikuwa ni saa ngapi katikati ya usiku, Alice alitembea peke yake kwa taabu akipita kwenye madimbwi ya maji huku akiteseka kwa maumivu mpaka kufika uwanja wa Fisi. Akamshukuru Mungu kufika bila kukutana na vijana wahuni wa maeneo hayo waliobaka wanawake.

Akajificha kwenye kona ya nyumba moja iliyokuwa na klabu, hapo ndipo akaanza kufikiria kuhusu maisha yake, hofu ya kifo kwa ugonjwa wa Ukimwi ikamwingia, kwani mwanaume huyo alikuwa amemwingilia bila kutumia kinga yoyote. Mawazo hayo yalimfanya apandwe na hasira na kuzidi kulia, hakujua ni kitu gani angemfanyia Levina kwa ukatili huo.

Hakupata hata lepe la usingizi mpaka saa kumi na mbili asubuhi, akiwa hataki kabisa kukutana na Levina aliamua kuondoka kuelekea katikati ya jiji ambako alitaka kutafuta namna nyingine ya kuishi. Kwenye stendi ya barabara ya Manzese darajani, alimwomba mmoja wa makondakta msaada, bila kuuliza maswali mengi, kondakta huyo alimruhusu kupanda na basi likaondoka kuelekea mjini ambako tangu aingie Tanzania hakuwahi kufika katika eneo hilo.

Siku hiyo ndiyo alipata nafasi ya kuiona Dar es Salaam vizuri, akiwa kiti cha nyuma kabisa alishangaa majumba marefu yaliyowaka taa nzuri. Yalimsahaulisha kidogo maumivu makali aliyokuwa nayo mpaka wakafika Posta ya Zamani na gari kusimama, watu wote wakashuka na kumwacha Alice peke yake.
“Wee mtoto unakwenda wapi?”

“Mjini”
“Mjini sehemu gani?”
“Mjini katikati”
“Hapa ndiyo mjini na mwisho wa safari yetu, shuka!”

Alice akanyanyuka kitini na kuanza kutembea kwenda nje ya gari ambako alishuka na kushuhudia likiondoka kwa kasi. Hapakuwa na mtu hata mmoja asubuhi hiyo kituoni na manyunyu ya mvua yalikuwa bado yakidondoka, gari likaondoka na kumwacha amesimama huku akitetemeka mwili mzima sababu ya baridi.
 
SEHEMU YA 09


Wananchi kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wa jeshi wameipundua serikali ya Rais Christopher Chambo na Rais huyo ametoroka, baadhi ya viongozi katika serikali yake wameuawa kikatili, akiwemo waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Jamhuri hiyo, Daniel Mchome ambaye yeye pamoja na mke wake wameuawa kwa kukatwa mapanga.

Mtoto wao mwenye umri wa miaka kumi, Alice, ndiye alinusurika akiwa amembeba mdogo wake wa kiume (John) mwenye umri wa miaka mitano na kwa msaada wa gari la msamaria mwema aliyejitolea kuwaokoa watoto hao wanasafirishwa hadi karibu kabisa na mpaka wa Tanzania na Kasomeko, lengo ni kuwaingiza nchini Tanzania ambako kuna amani ya kutosha.
Gari hilo lilizuiliwa kwenye kizuizi kabla ya kufika mpakani, dereva akapigwa risasi na watoto wote wakalazwa chini kisha kumiminiwa risasi wakiwa wamelazwa kifudifudi! Maiti zao zikabebwa kwenda kutupwa porini na kuachwa ziwe chakula cha ndege. Bahati nzuri, risasi hazikumpata vizuri Alice, siku chache baadaye alizinduka na kujikuta yuko hospitalini.

Kando ya kitanda chake akiwepo Padri ambaye alimsimulia namna alivyomwokoa, Alice huku akilia akamweleza Padri historia yake na kumtaka amwondoe nchini Kasomeko na kumpeleka Tanzania lakini kabla ya kufanya hivyo apelekwe kwanza mahali kulikokuwa na miili iliyotupwa ili akauone mwili wa mdogo wake. Hilo lilifanyika, Alice akamzika mdogo wake na baadaye kuvushwa kuingia nchini Tanzania hadi Dar es Salaam ambako alifikia uwanja wa Fisi, eneo la ukahaba.

Msichana mmoja akamwona na kumhifadhi nyumbani kwake akawa anamhudumia kila kitu kama mdogo wake, Alice akaamini yuko mikononi mwa Msamaria, jambo ambalo halikuwa kweli. Miaka miwili baadaye msichana huyo alimweleza ukweli kuwa, siku zote alikuwa akiwekeza kwake kwa kumhudumia na sasa ulikuwa umefika muda wa kumtumia katika biashara ya ngono, jambo ambalo Alice hakulikubali.

Pamoja na kukataa kwake, aliuzwa kwa nguvu, akabakwa na mwanaume mkubwa kama baba yake na kuachwa katika maumivu makali damu nyingi zikimtoka. Hakuona tena sababu ya kuishi nyumbani kwa msichana huyo aliyeitwa Levina, akatoroka alfajiri na kwenda mpaka stendi ambako alipanda basi lililompeleka mpaka katikati ya Jiji la Dar es Salaam eneo la Posta ambako ilishuka mvua kubwa akajibanza kando ya jengo la Benki ya NBC, muda mfupi baadaye askari alimfuata na kuanza kumuuliza maswali, badala ya kujibu, Alice akiwa na hofu alikimbia.
Je, nini kitafuata katika maisha ya mtoto huyu? SONGA NAYO…


Huku akitetemeka na kunyeshewa na mvua, Alice alikimbia akikatisha katikati ya bustani iliyopandwa maeneo hayo, hakujali maumivu aliyokuwa nayo sehemu za siri, ilikuwa ni bora aumie lakini asiingie mikononi mwa askari huyo ambaye lazima angetaka kudadisi alitokea wapi na mwisho angeweza kugundua hakuwa Mtanzania, jambo ambalo lazima lingemwingiza matatizoni kama sheria za Uhamiaji zingetumika. Aliiogopa jela.

Upande wa pili wa barabara alizidi kuporomoka hadi ufukweni mwa Bahari ya Hindi, akaanza kuambaa kando kando kwenye mchanga mpaka sehemu fulani karibu na boti nyingi mbovu. Akawaona watoto wa kike wa umri wake wakinawa nyuso zao kwa kutumia maji ya bahari, wote walipogeuka kumwangalia nyuso zao zilitabasamu, bila kutarajia Alice naye akajikuta akifanya hivyo hivyo. Huo ndiyo ukawa mwanzo wa urafiki wao, kitu kama sumaku kikamvuta kuwasogelea.

“Mambo?” Mmoja wa watoto hao alimwambia.
“Poa!” Alice alijibu, ingawa hakuelewa vizuri lugha ya Kiswahili bado.
“Unakwenda wapi?”
“Natembea.”
“Kwenu wapi?”

“Kuleee Manzese! Ninyi?”
“Hapa hapa”
“Mnakaa hapa?”
“Ndiyo.”
“Wazazi wenu?”
“Walishakufa”

Maneno hayo yalimfanya Alice ajisikie yuko na watu wa kundi lake, moyoni akahisi usalama, hao ndiyo wangemwonyesha jinsi ya kuishi jijini mpaka atakapotimiza umri wa kuanza kutekeleza maagizo ya baba yake. Wakamkaribisha kwenye boti moja mbovu na kumwonyesha mahali walipolala, alishangazwa na ukarimu wao, ingawa walikuwa na muda mfupi tu tangu wakutane, ilionekana kama walishakutana miaka mingi kabla.
“Huyu hapa ni Tatu, yule Mwasiti, mimi Irene na yule kwenye kona ni Joyce, wewe ni nani?”
“Alice.”

“Wazazi wako wako wapi?”
“Walishakufa.”
“Kwa hiyo unafanana na sisi?”
“Ndiyo.”
“Walifia wapi?”
“Mmh!Mmh!Manzese!” Alice alidanganya, asingeweza kutaja Kasomeko, swali kama hilo peke yake lilimkumbusha siku wazazi wake walipouawa kikatili, akili ikahama ndani ya boti na kurejea Kasomeko, haraka akakichomoa kiratasi kidogo alichokiandika siku hiyo na kukikunjua, akaanza kukipitia akiyasoma majina bila kujali mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea.

“Brigedia Kachenje…” alirudia tena kulisoma jina hilo, akauma midomo yake ya chini.
“Mbona umehuzunika, utaishi tu hapa mtaani, mambo safi, waungwana wako wengi tutakuonyesha jinsi ya kufanya.”
“Ahsanteni”

Majira ya kama saa mbili hivi asubuhi wasichana hao ambao umri wao ulilingana kabisa na wake, isipokuwa Mwasiti aliyeonekana mkubwa kidogo na huyo ndiye alikuwa kiongozi, walimchukua mpaka eneo la Feri, wakamnunulia chai na mkate. Alice akanywa akiwa na mawazo mengi, aliifikiria sana dunia na mambo iliyokuwa ikimtendea, aliamini hakustahili kabisa ukatili wote huo na alishindwa kukubali kama kweli Mungu alikuwepo. “Kwanini kama yupo, anaruhusu nipate shida hizi bila hatia?” alijiliza lakini muda huo huo akakumbuka fungu ambalo baba yake alimsomea kwenye Biblia siku moja wakiwa nyumbani katika Kutoka 20, “Nami nawapatiliza wana maovu za baba zao..”

“Kwanini niadhibiwe mimi kwa makosa ambayo sijayafanya?” alijiuliza Alice akinywa chai.
Saa nzima baadaye walipomaliza, kundi lote la wasichana hao liliondoka kwa miguu mpaka kwenye taa za kuongozea magari zilipo karibu kabisa na hoteli ya Royal Palm, hapo ndipo walisimama kando na kuanza kumwelewesha Alice jinsi walivyojipatia fedha kwa kuombaomba kwenye magari yaliyosimama eneo hilo kusubiri taa ziruhusu yapite. Alielewa vizuri lakini alikuwa na aibu, kila gari lilipokuja na kusimama walimwambia “Nenda!Nenda!Nenda” naye akatii.

Kila gari alilosimama kando yake kuomba, dereva alifungua dirisha na kumpa chochote alichokuwa nacho, tofauti kabisa na watoto wengine na baadhi ya madereva walionekana wakiongea jambo fulani kumhusu yeye kabla ya kumpa fedha au chakula. Haikuwa bure, pamoja na kuwa na umri mdogo, Alice tayari alishaanza kuvutia, uzuri wake ulionekana waziwazi, alikuwa mtoto aliyeonekana angekuwa mrefu, rangi ya ngozi yake ilikuwa ya Kahawia, akiwa na pua pamoja na shingo ndefu.

Ingawa alivaa suruali pana, bado ndani yake kulionekana kuwa na ‘kitu’ hasa sehemu za nyuma ambacho kama angeendelea kukua na kuongezeka uzito, kingewapagawisha wanaume wenye tamaa. Kifua chake kilikuwa kimebinuka na kulikuwa na Chuchu zilizochomoza. Hii ndiyo ilikuwa sababu kubwa ya watu kumjadili na kumpa fedha kila aliposimama kwenye dirisha kuomba, rafiki zake walilielewa hilo na walimtumia kama mradi maana baada ya shughuli ilikuwa ni lazima waketi chini na kugawana walichopata sawa kwa sawa ingawa Alice alikusanya fedha nyingi zaidi. Hayo ndiyo yakawa maisha kila siku mpaka mwaka ukaisha.

“Wewe mtoto!” Ilikuwa ni sauti ya mwanamke mmoja ndani ya gari aina ya Landcruiser akimwita Alice asogee, huyo alikuwa miongoni mwa watu waliompa Alice fedha kila siku walipopita na magari yao.
“Shikamoo!” Aliamkia alipofika kwenye dirisha huku akipiga magoti mpaka chini jambo nadra kabisa kufanyika mjini.
“Marahaba, unaitwa nani?”
“Alice.”
“Kila siku nakuona hapa, unaishi wapi?”
“Mimi?”

“Ndiyo.”
“Kuleee!”
“Wapi?”
“Feri.”
“Na nani?”

“Na hawa wenzangu.”
“Wazazi wako wako wapi?”
“Walishakufa”
“Mh! Kweli?”
“Ndiyo.”
“Hebu ingia kwenye gari.”

Alice akazunguka upande wa pili na kufungua mlango kisha kuingia kwenye gari hilo na kuketi, sekunde chache baadaye taa ya kijana ikawaka na gari likaondoka akionekana mwenye wasiwasi mwingi kwani hakujua ni wapi walikokuwa wakielekea. Mbele kidogo mwanamke huyo alisimamisha gari hilo la thamani kubwa kando ya barabara na kuendelea kumuuliza Alice maswali mengi akitaka kumfahamu, yote aliyajibu lakini hakudiriki kueleza ukweli kuhusu ni wapi alikotokea.
“Twende nyumbani kwangu”
“Nyumbani kwako?”

“Ndiyo.”
“Kufanya nini?”
Mwanamke huyo alichelewa kujibu.
 
SEHEMU YA 10


Mtoto wao mdogo wa kike (Alice) amenusurika na kuondoka na mdogo wake kwa msaada wa msamaria mwema kuelekea mpakani, lengo ni kuingia Tanzania kulikojaa amani. Jambo hili halikutimia, kwani kabla ya kufika mpakani gari lilifika kwenye kizuizi na maaskari wakawashusha watoto wote na kuwapiga risasi, dereva akiwa ameuawa kabla yao. Miili yao ikabebwa na kwenda kutupwa porini.
Siku chache baadaye Padri mmoja akiwinda aliiona miili hiyo na kugundua kuwa mmoja kati yake, ulikuwa wa mtu aliye hai ingawa alikuwa amejeruhiwa shingoni. Akiwa na msaidizi wake walimbeba mtoto huyo na kumpeleka hospitali ambako alitibiwa na kupona ndipo akataja jina lake kwamba ni Alice.

Akamwomba Padri amwondoe Jamhuri ya Kasomeko ili kuokoa maisha yake, lakini kabla ya kufanya hivyo kwanza ampeleke mahali iliko miili ya wenzake, akautafuta mwili wa mdogo wake na kuuzika kwa heshima ndipo akavuka kuingia Tanzania kwenye Jiji la Dar es Salaam.

Alifikia eneo la Uwanja wa Fisi ambako alipokelewa na msichana aitwaye Levina, huyo alimtunza kwa miaka miwili bila kuelewa alitokea wapi, lengo lake likiwa ni kumtumia kwenye biashara ya ngono akikua. Jambo hili la kikatili lilipotokea, Alice aliamua kutoroka na kuingia katikati ya jiji ambako aliishi kwenye boti mbovu akifanya kazi ya kuombaomba mitaani akiwa na wasichana wenzake, kazi hiyo akaifanya kwa muda mpaka alipokutana na mwanamke mwenye gari zuri, ambaye alimpakia na kumpeleka mbele, kisha kuanza kumdadisi, mwisho akamtaka waende nyumbani kwake.
Je, nini kitaendelea? Kuna usalama kwa Alice? SONGA NAYO…

Bibi Chausiku Shomari, alikuwa ni mfanyabiashara maarufu sana nchini Tanzania, akiishi jijini Dar es Salaam. Biashara yake kubwa ilikuwa ni vinyago, akiwa na maduka makubwa katika miji ya NewYork, Washington, London, Mumbai ambako alisafirisha kontena nyingi za vinyago kila mwaka. Alikuwa ni mwanamke mwenye mafanikio makubwa sana.
Pamoja na mafanikio hayo mwanamke huyu tajiri alikuwa na tatizo moja tu lililomfanya akose furaha ya maisha yake; Watoto. Hakuwa na mtoto hata mmoja ambaye angetegemewa kuwa mrithi wa utajiri wote aliokuwa nao atakapokufa. Ndugu zake wengi ndio waliotupia macho utajiri wake, wakiamini siku akifa wangegawana kila kitu.

Kila siku alipopita kwenye taa za kuendeshea magari za Royal Palm, alimwona mtoto mdogo mzuri akiombaomba, alifungua dirisha lake na kumwita kisha kumpa kiasi kikubwa cha fedha ambacho aligawana na wenzake. Kwa karibu wiki mbili alifanya hivyo, hatimaye akaamua kumwita binti huyo na kumpandisha ndani ya gari lake na kuendesha hadi mbele ambako aliegesha na kufanya naye mazungumzo.
Alimshawishi sana wakubali kwenda nyumbani kwake lakini binti huyo alikataa, ikabidi ashuke na kurejea kwenye taa kuendelea kuomba. Siku iliyofuata walikutana tena na kama kawaida binti huyo alikimbilia tena kwenye gari na akaruhusiwa kupanda, taa ziliporuhusu gari liliendeshwa mpaka sehemu ile ile ya jana yake ambako liliegeshwa na mazungumza kuendelea, mama huyo akijaribu kumshawishi binti akubali kwenda nyumbani kwake.

“Nilisahau kukuuliza jina lako, unaitwa nani kweli?”
“Alice!”
“Alice twende nyumbani kwangu, utaishi vizuri na nitakufanyia kila kitu ikiwa ni pamoja na kukusomesha, huhitaji kuteseka hivyo barabarani wakati kuna watu tunatafuta watoto, kama una wasiwasi wowote twende Kituo cha Polisi nikatoe maelezo kabla hatujaondoka kwenda kwangu ili uwe na uhakika utakuwa salama.”
“Sawa, kama ni hivyo sawa, nilikuwa naogopa!”

Gari likawashwa na kugeuzwa kisha kuelekezwa moja kwa moja Kituo Kikuu cha Polisi (Central)ambako walishuka na kuingia kituoni, maaskari wote waliokutana nao wakawa wanamsalimia bibi Chausiku kwa heshima kubwa na mmoja wao kujitolea kumpeleka moja kwa moja hadi ofisini kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dar es Salaam ambako Bibi Chausiku alieleza nia yake ya kumchukua Alice kwenda kumlea.
“Wee mtoto unakataa bahati? Unamjua huyu mama?”
“Hapana!”
“Usipoteze bahati yako, huyu mama ni tajiri kupita kiasi na atakuelea vizuri kama mwanaye, chukua bahati hiyo na sisi polisi tunamtetea maana si mtu mhalifu hata kidogo!”

“Sawa baba nimeleewa!”
“Wewe ni mtu wa wapi?”
“Manzese.”
“Wazazi wako?”
“Walishafariki.”
“Nakuunga mkono bibi Chausiku, huyu mtoto ninavyomwona ukimwacha mtaani, muda si mrefu kesi itafunguliwa hapa amebakwa na wanaume, bora umwondoe.”

“Kabisa.”
“Yule mtoto mwingine uliyekuwa ukimlea yuko wapi?”
“Bahati mbaya alifariki, nilisafiri naye kwenda Brazil kwa likizo fupi, akapata ajali ya gari na kufa huko huko, nikasafirisha mwili kuuleta hapa nyumbani kwa mazishi!”
“Pole sana, bora uchukue huyu angalau atakupunguzia machungu, sawa binti?”

“Nimesikia baba!” Alice aliitikia moyo wake ukiwa umejawa na furaha, kila alipomwangalia bibi Chausiku usoni mwake alijifunza kwamba mwanamke huyo alikuwa mtu mwaminifu aliyestahili kuaminiwa.
Dakika kumi na tano baadaye walikuwa ndani ya gari kwenye Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, walipopita kwenye taa za Royal Palm, Alice aliwaona rafiki zake na kuwapungia mkono, wakamwangalia kwa huzuni. Kuondoka kwake ilikuwa ni sawa na kunyang’anywa mradi, kwani yeye ndiye aliyefanya wapate fedha nyingi katika kazi yao ya kuombaomba.

Safari yao iliishia eneo la ufukweni mwa bahari ya Hindi liitwalo Coco, ambako gari la kifahari lilikatisha kulia, lango kubwa likafunguka baada ya bibi Chausiku kubonyeza kitufe fulani ndani ya gari lake, wakaingia kwenye ngome kubwa iliyozungushiwa nyaya za umeme kujikinga na wezi ambayo ilitawaliwa na ukimya wa ajabu.
Wakiwa ndani ya ngome hiyo, bibi Chausiku alibonyeza tena kitufe kingine na lango jingine lililokuwa mbele yao likafunguka na gari likaingia ndani ya nyumba ambako wote wawili walishuka na kuanza kupandisha juu kwa kutumia ngazi zilizowekewa marumaru za kung’ara ambazo kwa kuziangalia tu zilionekana wazi ni za thamani kubwa.
Walikwenda mpaka juu kabisa kwenye ghorofa ya tatu ambako bibi Chausiku alianza kumzungusha Alice sehemu mbalimbali za jumba hilo kubwa, moyoni mwake Alice alikiri hakuwahi kuingia kwenye nyumba ya kifahari kiasi hicho.

“Hapa ndio kwenye bwawa la kuogelea ambako huwa nakaa na kupumzika!” Aliongea mwanamke huyo wakiwa ghorofa ya tatu, walipotoka hapo alimwingiza kwenye chumba chake cha kulala, kitanda kiling’ara mithili ya kilichopakwa madini ya almasi.
“Hapa ndio huwa nalala! Njoo nikuonyeshe chumba ambacho wewe utakuwa unatumia.”

Alice akamfuata nyuma nyuma akitetemeka, moyo wake ulijaa hofu, kuna hisia ilimwambia alikuwa mahali pasipo salama na lolote baya lingeweza kumtokea lakini akazibeza hisia hizo na kuziita za kijinga zilizotokana na kumbukumbu ya nyuma ya maisha yake. Chumba cha kulala alichoonyeshwa, hakikuwa tofauti sana cha bibi Chausiku, kitanda pia kiling’ara na ukutani kulikuwa na runinga kubwa bapa ya inchi arobaini na mbili, iliyounganishwa chaneli zote muhimu, bafu lilikuwa zuri mno lenye vigae vya kung’ara kiasi cha mtu kujiona kutokea chini.

“Utalala hapa siku zote, wewe sasa ni mwanangu, utanifariji katika shida na raha, hutakiwi kuteseka mtaani kiasi hiki!”
“Mh! Mama, kwanini unifanyia wema wote huu?”
“Sina mtoto Alice, lakini nina utajiri mkubwa mno, ni bora wewe uishi hapa na mimi kama mwanangu, nitakutunza na kukufanyia kila kitu ikiwa ni pamoja na kukusomesha Shule ya Kimataifa, umesoma mpaka darasa la ngapi?”
“Ni kama sijasoma tu!”

“Kwanini?”
“Nilisoma kidogo, baadaye sikuendelea, wazazi wangu walikufa!”
“Pole sana, yasahau yote hayo, tutafidia!”
“Mh! Kwanini wema wote huu?” Alice alizidi kuuliza.
“Ni upendo tu, hakuna kitu kingine!”
“Kweli?”
“Kabisa!”
“Haya!” Alice aliitikia kwa shingo upande.

“Mbona unaonekana kuwa na wasiwasi?”
“Ah! Ah!”
“Uliza tu!”
“Unaishi na nani hapa?”
“Peke yangu!”
“Nyumba yote hii?”
“Sipendi kuishi na watu.”
“Hauna ndugu?”
“Ninao wengi!”
“Haya!”

Kilichofanyika ni Alice kuingizwa bafuni na kufundishwa jinsi ya kuoga kutumia mabomba yaliyokuwemo, bibi Chausiku alikuwepo kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa. Alipomaliza alifungwa kwenye taulo safi nyeupe na kurejeshwa chumbani kwake, bibi Chausiku akampa mafuta yake mwenyewe pamoja na manukato akapaka na kumtaka atulie chumbani wakati yeye akitoka kidogo.
“Unakwenda wapi?”
“Nakuja sasa hivi!”
“Mimi naogopa!”

“Wala usiwe na wasiwasi, narudi baada ya muda mfupi!”
“Haya!” Kama kawaida yake, Alice akaitikia kwa shingo upande, kichwani mwake akiwaza kwamba duniani hapakuwa na wema wa bure, lazima kuna malipo angetakiwa kuyafanya, akamkumbuka Levina na unyama aliomtendea, hisia zikamfanya aamini kuna kitu cha hatari ambacho bibi Chausiku alikuwa amekwenda kukifuata.
“Hapana, hanikuti!” Akasema na kunyanyuka kuufuata mlango, ulikuwa umefungwa kwa nje, hofu ikaongezeka na kujikuta analia.

Je, nini kitaendelea? Bibi Chausiku amekwenda wapi? Kufanya nini? Je, Alice ameingia kwenye tatizo jingine?
 
Hapana mkuu usifanye hivyo loooh .. wafuatiliaji wa simulizi wako wengi so maoni yangu peke yangu hayapaswi kuwanyima watu wengine haki ya kufuatilia kile wanacho kipenda ..... then najua maneno yangu yatakuwa yame kuvunja nguvu I'm so sorry ...

Ni wazi mimi sivutiwi na simulizi za shigongo lakini hii haimaanishi kwamba watu wote wana mtazamo kama wangu dhidi yake
Basi siendelezi mzee

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Hapana mkuu usifanye hivyo loooh .. wafuatiliaji wa simulizi wako wengi so maoni yangu peke yangu hayapaswi kuwanyima watu wengine haki ya kufuatilia kile wanacho kipenda ..... then najua maneno yangu yatakuwa yame kuvunja nguvu I'm so sorry ...

Ni wazi mimi sivutiwi na simulizi za shigongo lakini hii haimaanishi kwamba watu wote wana mtazamo kama wangu dhidi yake

Sent using Jamii Forums mobile app
Sehemu nayoCOPY imeishia sehemu ya 10
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom