TEMBELE LA UWANI
SEHEMU YA THELATHINI NA TATU
MTUNZI
Mbogo EDGAR
ILIPO ISHIA SEHEMU YA THELATHINI NA MBILI: Wakati mzee Mahamud anatoka ndani ndio muda ambao alisikia simu yake inaita, alipotazama akaona kuwa mpigaji alikuwa ni bwana Mahadhi, kwanza akamtazama mke wake ambae alikuwa anaongozana nae kutoka nje, “Mahadhi huyo anapiga simu” alisema Mahamud kwa sauti ya kuhitaji ushauri, “pokea msikilize anataka kusema nini, mimi nilitaka tumfumanie huko huko msikitini” alisema mama Soraya, ambao sasa walikuwa wametokea nje na kuwakuta wakina Talib wakiwa wana subiria kuingia kwenye gari……… SONGA NAYO SASA
Mzee Mahamud akapokea simu ile na kuiweka sikioni, huku anasogea pembeni akipishana na Soraya aliekuwa anakuja toka ndani, akiwa amependeza kweli kweli kwa gauni lake refu la kijivu na shungi (kilemba) cheupe na niqab ya kijivu aliyoishia mikononi, viatu leo alivaa vya kudumbukiza vyeusi, lakini vya chini, “hallow assalam alaykum” alisalimia bwana Mahamud, kwa sauti nzito na tulivu, “waalaykum salaam bwana Mahamud, kwanza uniwie radhi mzee mwenzangu, maana muda unapiga simu nilikuwa nimeisahau nyumbani nahangaika mitaani kumtafuta Idd, maana alikumbwa na balaa kubwa” alisema bwana Mahadhi, huku akijichekesha chekesha, hapo Mahamud akakunja sura kwa mshangao, “balaa lipi bwana Mahadhi zaidi ya lile alilomsababishia binti yangu?” alisikika akiuliza bwana Mahamud kwa sauti ya ukali kiasi cha watu wote kugeuka kumtazama kwa mshangao, maana walizoea kumuona mzee huyu akiongea kwa sauti ya upole siku zote, “ukisema alimsababishia utakuwa umekosea mzee mwenzangu, kama mwanao alipata tatizo, basi hilo tatizo limewakuta wote wawili” alisema Mahadhi kwa sauti ya upole, lakini hakuacha kujichekesha kidogo, “ni matatizo gani aliyapata kijana wako bwana Mahadhi?” bado sauti ya Mahamud ilikuwa ni ile iliyojaa hasira, “kwa kweli ni hatari ndugu yangu, kijana wangu jana alishindwa hata kurudi nyumbani, aliokotwa asubuhi akiwa amelala kwenye gari hajitambui hata kidogo, anasema jana walienda sehemu kununua Juice ya mabungo kwaajili ya huyo mwenzie Soraya na yeye akanunua maji, kumbe walitegeshewa vilevi kwenye juice na maji, yeye akajikuta amelewa na kukimbilia kwenye gari, hakujuwa Soraya ameenda wapi, hivyo nikasema nikupigie simu ili nijuwe na yeye ilikuwaje?” aliuliza Mahadhi kwa sauti ya upole kama vile ana masikitiko fulani, hapo Mahamud alishusha pumzi kidogo kama ile pumzi ya kushusha hasira, “nadhani tukutane baada ya swala ili tuongee vizuri, lakini kwa kifupi na yeye aligundua kuwa juice alieyoletewa ilikuwa na kilevi” alisema Mahamud na wakakubaliana hivyo.
Naam Mahamud na familia yake iliingia kwenye gari ambalo lilikuwa linaendeshwa na Soraya, huku safari ikaanza kuelekea msikitini, wakiburudishwa na qaswida, huku Mahamud aliekaa mbele akimsimulia mke wake pamoja na mwanae Soraya aliokuwa nao kule mbele ya gari, kilicho tokea kwa Idd jana jioni, “lakini baba mbona ile harufu ya pombe ilikuwa ni kali sana, ina maana hakuisikia hata kidogo mpaka anywe na alewe?” alisema Soraya akipingana na utetezi wa bwana Mahadhi, yaani baba yake Idd, ok! wacha nikawasikilize kwanza” alisema Mahamud, ambae alionekana kuwa hasira zimesha muondoka, “lakini hata kama watasema nini ukaribu na mwanangu sihitaji tena”, alisisitiza mama Soraya.******
Kwa upande wa Higgno leo yeye ndie alieenda nyumbani kwao, maana toka jana hakuwahi kuonana na baba yake, ni baada ya kutembea kwenye mitego michache ya wanyama wa porini, akaona ni bora akienda kwanza kwa baba yake kisha akirudi aende kutazama mitego ya kanga kwale na samaki, Higgno alifika nyumbani kwao akiwa amebeba nyama ya wanyama kama Sungura na digi digi, ikiwa ni moja ya vitu ambavyo mzee Frank alijivunia kutokana na mwanae kukaa kule shambani, maana alisha sahau mambo ya kwenda buchani kununua nyama au utumbo, “mwanangu afadhali umekuja, maana umenipunguzia safari ya kuja huko” alisema bwana Frank mara baada ya kusalimiana na mwanae Higgno, “niliona kuna umuhimu wa kuja kuonana leo, kwasababu kesho nitakuwa na kazi ya kumalizia sehemu fulani pale shambani, jumapili nitakuwa nafua nguo kwa maandalizi ya kwenda kwenye kuomba kazi kule mjini” alisema Higgno, “basi umefanya vyema, ila kwa kifupi nadhani umejionea mwenyewe hali halisi kwa yaliyo tokea jana kule kwa shangazi yako?” alisema mzee Frank kwa mtindo wa kuuliza, na Higgno akaitikia kwa kichwa kukubali kuwa ameshuhudia mwenyewe, “sasa mimi nakuomba wewe jitahidi utafute mwanamke, ujue katika jamii yetu haipendezi kijana mkubwa kama wewe uonekane hauna mwanamke hata wakuongozana nae” aliongea mzee Frank kwa sauti ya chini na tulivu, huku Higgno akimsikiliza kwa umakini mkubwa, “kuna kitu hujui Higgno, unajua hawa wakina mama inafikia wakati wanapenda kuona au kusikia kesi ndogo ndogo toka kwa wenzao wakilalamika kuhusu mabinti zao” alisema bwana Frank na kuendelea kumsisitiza mwanae, “hivyo Higgno wewe tafuta mwanamke hata kama ukiona umependa mwanamke fulani na unashindwa la kufanya njoo uniambie” alisema mzee Frank, kwa sauti ya chini iliyojaa msisitizo, “lakini baba wanawake wanapenda hela mi naona nisubiri kwanza nipate kazi, nikiwa na hela nguo nzuri viatu vizuri lazima watanipenda wenyewe”alisema Higgno, akionekana kukatishwa tamaa na maisha ya wanawake aliowahi kuwaona kwa macho yake mfano Hilda.
Hapo baba yake Higgno alitabasamu kidogo, “Higgno kama ulikuwa hujui basi wacha nikueleze na unisikilize kwa umakini” alisema mzee Frank kwa sauti iliyojaa umakini mkubwa, Higgno nae akaongeaza umakini kumsikiliza baba yake, “najuwa kama asilimia kubwa ya wanawake hasa wale wenye maisha ya chini wanapenda kuishi au kuwa na mwanaume mwenye fedha na uwezo mkubwa ili watatue shida walizoshindwa kuzitatua, japo kuna wengine hupanda kuishi maisha ambayo wamekuwa wakiya shuhudia kwa wenzao” alisema baba Higgno ikiwa ni mwanzo wa maelezo yake, lakini pia wapo wanawake haijalishi ni kutoka kwenye familia za hali ya chini kama zetu au kutoka kwenye maisha bora wao hupenda mwanaume mwenye mapenzi ya kweli, japo asilimia kubwa ni huwa wale wenye maisha mazuri” alisema baba Higgno akimpa somo kijana wake aliekuwa anamsikiliza kwa umakini mkubwa, “cha kuzingatia kwanza usitumie kitu kumpata mwanamke, hilo litakusumbua sana maishani, hasa utakapo kosa kuwa na kitu, pili hakikisha unamuonyesha upendo mwanamke wako, mchukulie kama rafiki na mwenzako, sio adui au kijakazi wako pale nyumbani, ujuwe siku zote wanawake wanapenda sana kuonyeshwa upendo, kudekezwa kama wao wanavyo wadekeza watoto” alimaliza kueleza baba Higgno na hapo ni kama somo lilimuingia Higgno, “sasa baba nitaanzaje kumuonyesha mwanamke kuwa nampenda, si mpaka anipe nafasi ya kuwa karibu yake na mimi niweze kumuambia?” aliuliza Higgno na kumfanya baba yake acheke kidogo, tena kicheko cha huzuni, “ina maana huwezi kumueleza mwanamke unachotaka kwake?” aliuliza kwa mshangao mzee Frank, na Higgno akatulia kimya, “ok! kwanza kabisa lazima utambue kuwa penzi halijifichi, na huwa linakuja lenyewe, asilimia themanini na tano ya mwanamke unae mtongoza tayari anakuwa amesha kuandalia jibu kabla huja mueleza chochote, (sijui kama mzee Frank alikuwa sahihi) iwe mwenye mapenzi juu ya wewe ulivyo au mwenye mapenzi juu ya fedha au ulicho nacho, ukweli anakupenda au kukuchukia mara tu baada ya kukufahamu, cha msingi weka hisia zako wazi” alisema mzee Frank, na hapo Higgno akakubaliana nae kwa kutikisa kichwa juu chini, akionyesha ameleewa alichoambiwa.********
Wakati huo huku mjini, tayari ibada ilishamalizika kwenye msikiti wa mkoa wa Ruvuma, Mahamud akiwa nje ya msikiti anatazama kama angemuona bwana Mahadhi na kumkaba maswali juu ya kitendo cha jana, mara akamuona kijana mmoja ambae hujihusisha na kufundisha mafundisho ya dini kwa watoto wadogo na wakubwa wasio na ufahamu wa dini, yaani madrasa, akimjia na kumueleza kuwa anaitwa kwenye ofisi ya baraza la wazee pale pale msikitini, hapo Mahamud ambae hakutegemea kuwa atamkuta bwana Mahadhi akiwa na wazee wengi namna ile, maana licha ya kuwa pamoja na kijana wake Idd pia alikuwa pamoja na wazee wengine watano, akaingia ofisini na kukaa kitako kwenye mazuria mazuri ambayo baadhi yake alinunua yeye mwenyewe.
Naam baada ya kusalimiana maongezi yakaanza, na mwanzilishi alikuwa ni bwana Mahadhi, “samahani wazee wenzangu, kuna jambo ambalo limetokea jana jioni baina ya vijana wetu wawili, yaani kijana wangu Idd, na binti wa bwana Mahamud” hapo kila mmoja akaonekana kumtazama mwenzie, wakionyesha kuwa walijawa na maswali vichwani mwao juu ya jambo ambalo bwana Mahadhi alitaka kuwaeleza, jambo ambalo limemfanya awakusanye mahali hapa, “kifupi nimeona kuwa endapo nitaongea na bwana Mahamud tukiwa wawili peke yetu haita kuwa vyema, yaani pengine asingeweza kunielewa kutokana na mazingira ya tukio lenyewe ambalo naimani kwa upande wa mwenzangu hakukuwa na madhara makubwa kama ilivyokuwa kwangu” alieleza bwana Mahadhi, ambae alianza kwa kueleza kama alivyo mueleza bwana Mahamud kuwa kijana wake alitoka na Soraya kwenda sehemu aliyowatuma, lengo likiwa ni kuwa weka vijana hawa karibu ikibidi watengeneze urafiki ambao utawaweka kwenye ndoa, “lakini kwa bahati mbaya katika matembezi yao wakajikuta wameingia kwenye mitengo ya kuwekewa kilevi kwenye vinywaji vyao” alieleza bwana Mahadhi, ambae alidai kuwa pengine lengo la watu hao lilikuwa ni kuwaibia, “lakini bahati nzuri Soraya aliwahi kuondoka, naimani alifika salama nyumbani kama nilivyo muona leo amehudhuria ibada vizuri kabisa, na kijana wangu Idd aliwahi kujifungia kwenye gari ambapo aliokoa vitu vyao vyote ikiwa na bengi la Soraya, hivyo naomba ifahamike kuwa hawakuwa wametumia kilevi kwa makusudi, isipokuwa waliwekewa kilevi bila wao kujuwa” alimaliza bwana Mahadhi kueleza simulizi ambayo alikuwa ameibadilisha maudhui kidogo kwa lengo la kuficha uovu wa mwanae Idd, “mh! nadhani wote tumesikia jamani, kwa upande wangu naona ni kisa cha kusikitisha kwa kweli, pole kwa vijana wetu kwa mtihani uliowafika” alisema mmoja wa wazee ambae ndie mwenyekiti wa baraza lile kwa mkoa wa Ruvuma, huku wenzie wakimuunga mkono kwa kuonyesha masikitiko yao kwa kilicho watokea Idd na Soraya wakiamini kuwa waliwekewa vilevi kwaajili ya kuibiwa, “kijana hii songea ni mpya sio ile uliyoiacha miaka ile” alisema mmoja wa wazee wale akimtazama Idd, ambae muda wote alikuwa anakenua meno kwa tabasamu, “sijui bwana Mahamud kama umeelewa alichokueleza mzee mwenzio?” aliuliza yule mzee wa kwanza huku anamtazama bwana Mahamud, “kiukweli mimi bado nina utata na maelezo ya bwana Mahadhi, Soraya anasema baada ya kuanza kulewa huyu Idd aliondoka pale mezani, na yeye akaona bora anywe maji haraka ili aondoe ulevi ule aliowekewa kwenye juice na maji ya haraka yalikuwa ni yale aliyokuwa anakunywa Idd, lakini alipoyafungua na kuyasogeza mdomoni akagunduwa kuwa ni pombe tena ilikuwa na harufu mbaya, sasa Idd alishindwa vipi kujuwa kama wametegeshewa kilevi?” aliuliza bwana Mahmudu akionyesha kuwa hakuwa na imani na Idd, “lakini kama mwanao hakuweza kusikia harufu Idd angewezaje bwana Mahamud, tusimhukumu kijana pasipo ukweli” alishauri yule mzee na wengine wakiendelea kuchangia maoni yao, wakimtetea Idd kuwa hakufanya hivyo, na kama angefanya hivyo basi wasingekuja kufafanua mbele ya baraza la wazee, wengine wakawalaumu wazee hawa wawili kwa mpango wao mbaya, “halafu kwa upande mwingine nyie ndio mlikosea hamuwezi kufanya hivyo, ni sawa na kukaribisha zinaa kwa vijana wetu, mlichotakiwa kufanya ni kuwaita wazee waende pale kwa Mahamud kutoa barua ya posa, ndivyo wazee wetu walivyofanya, sasa nyie mnafanya mambo ya wapi?” aliongea yule mwekiti na hapo wote wakakaa kimya, ikiwa ni pamoja na wakina Mahadhi na mwanae Idd na bwana Mahamud, kila mmoja akilitafakari kwa namna yake swala lile, wakati bwana Mahamud akiona kuwa ni jambo la kweli kabisa, maana hata baadhi ya hadithi kwenye vitabu vya dini vimesimulia hivyo.
Tofauti na upande wa Mahadhi na mwanae, walifurahia mioyoni mwao kwa kuona kuwa mwenyekiti ana warahisishia mipango yao ya kumnasa Soraya kuwa mke wa Idd, na mwisho wao ndio wawe watawala wa mali za Mahamud, “tena nilicho wasifu hamja angalia hali ya mtu zaidi ya kuangalia kuwa kijana ni mcha mungu na binti ni mchamungu, kwakweli juu ya swala hilo ninawaunga mkono” alisema mwenyekiti, akionyesha ana maanisha anachokisema, na amekiunga mkono kwa moyo wake wote.
Hapo Mahamud akahisi kijasho chembamba kina churuzika kwenye paji la uso wake, kwanza ataanzaje kumueleza mwanae Soraya mpaka amuelewe pia mke wake atamuelezaje, “ok! kama ni kweli alichoeleza bwana Mahadhi, mimi sina neno juu ya wazo lenu” alisema bwana Mahamud, huku kila mmoja anasikiliza kwa umakini, “ila kwa kweli nisiwafiche ndugu zangu sina uwezo wa kuileza familia yangu hasa Soraya mwenyewe juu ya jambo la ndoa kati yake na Idd na akanielewa, kama kweli mtaweza kumshawishi Soraya kwa namna yoyote mimi sina maneno” alisema Mahamud na wakakubaliana kuwa siku ya jumapili saa saba mchana baada ya swala kuna wazee wataenda nyumbani kwa bwana Mahamud ili kufikisha ujumbe wa uchumba, wakipanga kuwa iwe ni jambo la kushtukiza………… ITAENDELEA