TEMBELE LA UWANI
SEHEMU YA NNE
MTUNZI
Mbogo EDGAR
ILIPO ISHIA SEHEMU YA TATU : “nimeiona baskeri yako uligongwa na gari au uliingia shimoni?” aliuliza tena baba yake Higgno na ndio wakati ambao Higgno aligundu kuwa mama yake alikuwa nyuma ya baba yake, “yani ndio hivyo hivyo wala hajibu, mimi namfikiria Hilda sijui ana hali gani huko aliko, wacha niende nikaulizie” alisema mama Higgno akitaka kuondoka, lakini mume wake akamzuia, “hebu! subiri kwanza tuongee na Higgno, we ukienda huko utauliza nini?” alizuia baba Frank, kisha akamgeukia Higgno, “wewe! hebu amka ukaoge kisha uje dukani” alisema mzee Frank, kisha akatoka na kuelekea dukani…………..ENDELEA……………
Nusu saa baadae Higgno alitoka bafuni alikokuwa anaoga, ambako muda wote alikuwa anajiuliza atamueleza nini baba yake, ambae kiukweli ni kama rafiki yake, maana siku zote humuelewesha jambo kwa upole na busara, sio kwa bakora kama vijana wengi walivyofanyiwa na wazazi wao enzi hizo, baada ya kujiandaa vizuri Higgno alienda dukani kama alivyo agizwa na baba yake, ambapo mida hii ya saa mbili bado wateja huwa ni wengi lakini sio sana.
Hivyo Higgno akamsimulia mkasa mzima baba yake, kuanzia alipo wakuta Hilda na wenzake waliokataa kumpisha, na yeye kuingia mtaroni, na wale wenzake na Hilda kumshushia kipigo akija okolewa na askar wa jeshi la wananchi waliokuwa wanatokea kambini, “hebu nikuulize, inamaana urafiki wako na Hilda umeisha?” aliuliza mzee Frank, kwa sauti fulani ya mshangao, “mbona toka siku nyingi tu! Hilda amepata marafiki wengine” alijibu Higgno, kwa sauti ya upole, “ina maana ulishindwa hata kujitetea kidogo?” aliuliza mzee Frank, “mh! hao watu wenyewe ni form four, tena wanasifika kwa fujo na utemi” alijibu Higgno na kumfanya baba yake atabasamu kidogo, “we unahisi ni kwanini wame kufanyia vile, au wamekupiga bila sababu yoyote” hapo ndipo palikuwa pagumu, lakini Higgno hakuwa na jinsi zaidi ya kueleza ukweli, “ni kwaajili ya Hilda” alisema Higgno na kumsimulia toka siku ile alipo mueleza kuwa lazima atembea na Hilda na mpaka alipowakuta wana zini, na pia alimsimulia mabadiliko ya tabia ya Hilda yakuto kuwa nae jirani, “namimi nikaamua kukaa mbali na Hilda, kwasababu hiyo Talib ana sifa ya kuwa mvuta bangi, niliogopa haya yaliyonikuta leo” alisema Higgno japo alificha mengi katika simulizi ile, kama vile Hilda kufumaniwa mara kwa mara ana zini kwenye vichaka na Talib, pia tabia mpya ya uvutaji wa bangi wa mschana huyu rafiki yake wa zamani, nayo hakumueleza baba yake, “ok! kwahiyo siku hizi Hilda sio rafiki yako kama zamani” aliuliza kwa mara nyinge baba Higgno, hapo Higgno akaitikia kwa kichwa kukubali kuwa Hilda sio rafiki yake tena, hapo mzee frank akatulia kidogo kama vile anatafakari, kisha akamtazama mwanae, yaani Higgno, “sikia Higgno, kwa sasa wewe ni kijana mkubwa, umesha balehe, na unapata hisia za kuwa na mpenzi, japo sio sahihi kwa wewe kuwa na rafiki wa kike kutokana na kuwa wewe bado mwanafunzi, najua ni machungu kiasi gani unayapata kwa sasa juu ya Hilda, lakini ukweli huyo sio mwanamke sahihi kwako, achana nae na uwe makini sana, wakati mwingine unapoingia kwenye urafiki” alisema baba Higgno, wakiwa wanahitimisha maongezi yao na kujiandaa kufunga duka.*****
Yap leo wana jamii forums twendeni nyumbani kwa mzee Komba, lilikuwa ni eneo kubwa kiasi lenye nyumba moja ya tofari za udongo zilizo chomwa na kuezekwa kwa nyasi kama vibanda viwili vidogo vilivyo pembeni ya nyumba hii, ambavyo vilikuwa kushoto na kulia mwa nyumba, kibanda cha kushoto kikiwa ni bafu na choo, na kile cha kulia kilikuwa ni kibanda cha jiko, ambako mama Hilda alikuwa anatoka huku amebeba sinia lililofunikwa na sufulia jeusi lililokuwa lina fuka moshi kwa mbali, ulioambatana na harufu ya ugali, anatoka jikoni na kuelekea kwenye mkeka uliokuwepo nje ya nyumba yao pembezoni mwa ukuta, ambapo alikuwepo mzee Komba, alie kuwa amekaa kwenye kiti kifupi (kigoda), pembeni ya mkeka huo, sijui kwa lugha gani lakini wakati mwingine walikuwa wanauita mpasa, “shida hii, jamani, mpaka koroboi zita ota kutu kwa kukosa mafuta” alilalamika mama Hilda mke wa mzee Komba, huku anaweka sinia lile mkekani akisaidiwa na mwanga wa mbala mwezi, “subiri mwanao amalize shule akuwekee umeme, si unaona anavyosoma kwa bidii” alisema mzee Komba, na hapo mke wake akacheka kidogo, kicheko cha matumaini, “yaani sipati picha nitakavyo kuwa navaa nguo mpya kila sikukuu” alisema mama Hilda huku anarudi jikoni, “ila usiku huu inabidi wawe waangalifu sana huko njiani, maana baskeri ya Higgy sijui kama ina taa” alisema Mzee Komba akimaanisha kuwa mwanae Hilda alikuwa bado hajarudi na alikuwa na Higgno, “huyooo hatajwi” alisikika mama Hilda akisema wakati ana toka jikoni na sufuria dogo jeusi, mkononi sufuria lililo toa siri kuwa lilikuwa linapikiwa kwenye jiko la kuni.
Mzee Komba akainua uso wake kutazama njia ya kuingilia pale nyumbani, akamuona mwanae Hilda akiwa anaingia pale nyumbani kwa mwendo wa kichovu huku ameshika kipande cha gazeti kilicho viligwa nakuacha vijiti vyembamba vya mianzi vikichungulia, mkono mwingine alikuwa amebeba, kitabu kimoja tu mkononi, na kwa kukuibia siri ni kwamba kitabu hicho sio cha masomo, kilikuwa ni kitabu cha simulizi ya UMEKOSEA LAKINI TAMU, toka kwa
Mbogo Edgar, “hooo! msomi wangu huyooo” alisema mzee Komba, kwa sauti ya kushangilia, “shikamoo baba” alisalimia Hilda, huku akivua viatu vyake na kujikalisha mkekani kivivu, akisababisha kiskert chake kupanda juu kutokana na ufupi wake, akishindwa kukiweka vizuri, “marahaba msomi wangu, naona umebanwa sana na masomo” aliitikia mzee Komba na wakati huo mama yake alikuwa anawekasufuria kwenye mkeka, “afadhari umewahi mwanangu, maana hawa kauzu (dagaa) wenyewe wa shilingi hamasini tu, sijui tunge gawanaje” alisema mama Hilda huku anaenda kuchukua maji ya kunawa, “si nimekuja na mishikaki ya pale kilabuni” alisema Hilda kwa sauti ya kivivu iliyoonyesha ametumia bangi muda sio mrefu, huku anafungua kipande cha gazeti, na kutoa mishikaki kumi akaiweka pembeni ya sinia ambalo bado lilikuwa lime funikwa na sufuria, mishakaki hiyo ilikuwa inauzwa shilingi kumi kila mmoja, “haaaa! hapo ndipo ulipokosea, si unge niletea hela nikanywe ulanzi” alilalamika baba Hilda yani mzee Komba, “ona sasa we mzee akili zako zilivyo, yaani unaona bora ukanywe ulanzi kuliko kula vizuri, ulanzi wenyewe unaumalizia huko huko kilabuni” alisema mama Hilda akimzodoa mume wake, “nyie wazee acheni kusemana nitawapa mia mbili mkanunue ulanzi” alisema Hilda kwa sauti ile ile ya kivivu, “hayo ndiyo mambo sasa, wacha nile haraka nikachukuwe ulanzi” alisema mzee Komba, wakati huo mke wake alie kuja na maji ya kunawa akiweka vizuri vyakula tayari kwa kuanza kuliwa.
Wakati wanakula ndipo mama yake Hilda nikama alikumbuka jambo, “mbona siku hizi, sikuoni na Higgy, au ndio kubanwa na masomo?” aliuliza mama Hilda, wakiendelea kula, “haaa! mama mambo gani hayo ya kunitajia huyo zoba” alisema Hilda kwa sauti ya kivivu akionekana hata lugha zake zimebadilika sana na kuwashangaza wazazi wake, “inamaana ume gombana na rafiki yako?” aluliza mama Hilda kwa sauti ya mshangao, “mama bwana, nimesema achana nae huyo lofa, tena leo alituletea ubwege wake wakina Talib wakampiga mpaka amekoma” alisema Hilda kwa sauti ya kivivu, japo ilikuwa ya majigambo, “kwanini sasa umeacha wanampiga rafiki yako?” aliuliza mama Hilda kwa sauti ya mshangao, lakini alionyesha kuwa hakujutia kitendo kile cha mwanae, “tatizo Higgy ana wivu, yeye ameona mimi nimepata marafiki matajiri ndio ananifanyia visa kila siku, leo ndio wamemkomesha” alisema Hilda, “huyu mtoto mbaya sana, ndio maana toka mwanzo sikutaka kabisa we karibu na mwanangu” alisema mama Hilda kwa sauti iliyojaa chuki, “unadhani nitawaacha hivi hivi, lazima nikawape ukweli wao, tatizo bwana Frank na kijana wake wanajiona wao ndio matajiri pekee hapa mtaani hivyo Higgy anavyoona mwenzie amepata marafiki matajiri, anamuonea wivu” alisema mzee Komba kwa sauti iliyoonyesha wazi kujawa na chuki na hasira, huku akipanga ataenda kesho asubuhi nyumbani kwa mzee Frank, maana usiku huu alipanga akanunue ulanzi anywe na mke wake, utakuwa umefanya jambo la mbolea” alisifia mama Hilda.*****
Siku ya pili asubuhi ya saa moja, ndio muda ambao Higgno alishtuka toka usingizini, huku akihisi maumivu katika baadhi ya sehemu zake za mwili kutokana na kipigo cha jana kule pacha nne, wakati ana jiinua kitandani ndipo aliposikia mtu anapiga hodi kwa fujo, na aliposikiliza vizuri alikuwa ni mzee Komba, yani baba yake Hilda, “ina maana humu ndani hakuna watu au kiburi tu!” aliuliza mzee Komba baada ya kubisha hodi mara mbili.
Higgno alitaka kwenda kufungua mlango, lakini akasikia mlango unafunguliwa, “vipi mzee mwenzangu, umetisha sana, utadhania mgambo anafuata kodi ya kichwa” alisema bwana Frank, kwa sauti iliyo jaa utani, japo mwenzie alionekana kuwa, hakuwa katika hali ya utani, “sikia bwana Frank, mkanye mwanao aache matumizi ya bangi, kama ukishindwa kumueleza hilo basi usijisumbue kulipa elfu themanini yako kwaajili ya ada, kwa maana una msomesha mfungwa mtarajiwa, ambae hatokusaidia kwa lolote” alisema kwa hasira mzee Komba, “mzee mwenzangu maneno gani hayo tuna watia laana watoto, hebu temea mate chini” alisema mzee Frank, ambae bado alionekana kuchukulia kama utani juu ya maongezi yale, “we fanya mzaha bwana Frank, lakini chonde chonde, mueleze mwanao aache kuvuta bangi” alisema tena mzee Komba, kwa sauti ile ile ya jazba, “taratibu basi mzee mwenzangu, hebu tulia unieleze Higgy amefanya nini” Higgno akiwa ndani aliweza kumskia baba yake akiongea kwa upole, “sikia bwana Frank, unajua kwa sasa huyu mwanao ameanza tabia fulani za ajabu” alisema mzee Komba, na kutulia kidogo….. Higgy wizzy anazidi kupewa kashafa, ilikujuwa ilikuwaje, tuonane tena hapa hapa Jamii Forums.